Serikali inatarajia kutumia Tsh. Trilioni 9.59 katika Mikopo kwenye Bajeti ya 2024/25

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,376
8,118
Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. @mwigulunchemba (Mb), amesema kuwa Tanzania ni nchi ya mfano Afrika kwa kutimiza viashiria vya Malengo ya Milenia ambapo imefanya vizuri katika sekta za Afya, Elimu, Maji.

Dkt. Nchemba alitoa ufafanuzi huo wa ukomo wa Bajeti kwa mwaka 2024/25, wakati alipokuwa akiweka jiwe la msingi katika jengo la Taaluma la Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), jijini Dodoma.

Alisema kuwa katika makadirio yaliyowasilishwa bungeni Serikali inatarajia kutumia kiasi cha shilingi trilioni 49.34 ambapo fedha za maendeleo zilizotengwa ni kiasi cha shilingi trilioni 16.

‘‘Fedha za maendeleo ni trilioni 16, fedha hizi zinatarajiwa kutumika katika Miradi ya Kilimo cha Umwagiliaji, Elimu ya Msingi na Elimu ya Juu, Ujenzi wa Barabara, Maji, Umeme Miradi ya Afya pamoja na ukamilishaji wa Bwawa la umeme la Mwalimu Nyerere’’, alifafanua Dkt. Nchemba.

Alisema kiasi cha fedha kinachotarajiwa kutumika katika uchaguzi ni shilingi bilioni 600 kwa mwaka unaofuata na kwa mwaka huu ni Shilingi bilioni 300 inayoenda kwenye uchaguzi.

‘‘Uchaguzi ni matakwa la kikatiba sio maamuzi ya Serikali bali ni kuhakikisha kuwa matakwa ya kikatiba yanatimizwa hivyo katika bajeti ya Sh. trilioni 49 kiasi kitakachoitumika katika kuendesha uchaguzi kwa mwaka ujao ni shilingi bilioni 300, alifafanua Dkt. Nchemba.

Akifafanua kuhusu fedha zinazotarajiwa kutumika katika maandalizi ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 linalotarajiwa kufanyika Tanzania Dkt. Nchemba alisema kuwa Tanzania kuwa mwenyeji wa AFCON ni suala la kujivunia kwani ni heshima kwa Taifa ambapo kiasi kilichotengwa ni Sh. bilioni 200 tu katika bajeti ya shilingi. trilioni 49.

Akizungumza kuhusu ugharamiaji wa Deni la Taifa Dkt. Nchemba alisema kuwa katika sh. trilioni 49, deni halisi ni shilingi trilioni tano (5) pamoja na riba ambayo haitazidi kiasi cha shilingi trilioni 10.

‘'Deni lenyewe ni miradi ya maendeleo inayoonekana kama ni ujenzi wa reli ya kisasa, kivuko cha Kigongo Busisi Mwanza, ujenzi wa mabweni ya shule, tumejenga mabweni ya vyuo vikuu karibu kila chuo kimepata kwa mradi mkubwa wa fedha za Benki ya Dunia"alifafanua Dkt. Nchemba.

WIZARA YA FEDHA TANZANIA

1710420037902.png

SERIKALI imeweka wazi mfumo na ukomo wa bajeti yake kwa mwaka 2024/25, ikitaja maeneo manane ya kipaumbele ikiwamo Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024, Uchaguzi Mkuu 2025 na ujenzi na ukarabati wa viwanja kwa ajili ya michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.

Kwa mujibu wa Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, serikali katika mwaka ujao wa fedha inatarajiwa kukusanya na kutumia Sh. trilioni 49.34.

Waziri huyo amebainisha kuwa misaada na mikopo kutoka kwa washirika wa maendeleo itapungua kwa asilimia 6.1 kutoka Sh. trilioni 5.4 mwaka 2023/24 hadi Sh. trilioni 5.1.

Akiwasilisha kwenye mkutano wa wabunge jijini hapa mapendekezo ya mfumo na ukomo wa bajeti ya serikali kwa mwaka 2024/25, Waziri Mwigulu amesema mapendekezo hayo ya bajeti ni sawa na ongezeko la asilimia 11.2 kulinganishwa na bajeti ya mwaka 2023/24 ya Sh. trilioni 44.38.

Amesema makadirio ya mapato kwa mwaka 2024/25 yamezingatia vigezo mbalimbali ikiwamo mwenendo halisi wa ukusanyaji wa mapato; mwenendo wa viashiria vya uchumi jumla; na jitihada zinazoendelea kuchukuliwa na serikali katika kuboresha mifumo ya ukusanyaji mapato ya ndani.

Waziri Mwigulu amesema sehemu kubwa ya bajeti (asilimia 70.1) itagharamiwa na mapato ya ndani ambayo yanatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 10 mwaka 2024/25.

“Serikali itaendelea kuweka msukumo na jitihada za kuimarisha ukusanyaji mapato ya ndani kwa kuwa ndicho chanzo chenye uhakika na kisicho na masharti hasi katika kugharamia bajeti ya serikali,” amesema .

Waziri huyo amesema kwa mwaka huo, serikali inakadiria kukopa Sh. trilioni 6. 61 kutoka soko la ndani na Sh. trilioni 2.98 kutoka soko la nje kwa masharti ya kibiashara kwa ajili ya kugharamia utekelezaji miradi ya ujenzi wa miundombinu.

“Serikali itaendelea kuhakikisha fedha za mikopo zinaelekezwa kwenye miradi ya kimkakati yenye matokeo ya haraka na manufaa mapana kwa taifa ikiwamo kuongeza fursa za ajira na wigo wa mapato ya serikali na kuhakikisha kuwa miradi inakamilika kwa wakati,” amesema.

MIKOPO YA ELIMU

Katika mwaka 2024/25, Dk. Mwigulu amesema Sh. trilioni 33.55 zitatumika kwa matumizi ya kawaida na Sh. trilioni 15.78 kwa ajili ya matumizi ya maendeleo sawa na ongezeko la asilimia 3.8.

Pia amesema fedha za maendeleo zinajumuisha ruzuku ya maendeleo ya Sh. trilioni 1.23 kwa ajili ya kugharamia mikopo ya wanafunzi wa elimu ya kati na ya juu pamoja na programu ya elimumsingi na sekondari bila ada, maarufu elimu bure.

Amefafanua kuwa sehemu kubwa ya matumizi itaelekezwa katika kugharamia Deni la Serikali, mishahara ya watumishi wa umma, Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024, maandalizi ya Uchaguzi Mkuu 2025, ulipaji hati za madai na ujenzi na ukarabati wa viwanja kwa ajili ya AFCON 2027, huduma za jamii na sekta za uzalishaji.

Waziri huyo amesema utengaji fedha za maendeleo umezingatia miradi inayoendelea ikiwamo miradi ya kimkakati na ya kielelezo pamoja na utekelezaji miradi kupitia utaratibu wa ubia kati ya serikali na sekta binafsi (PPP) ili kuipunguzia serikali mzigo wa kugharamia miradi ya maendeleo kwa utaratibu uliozoeleka.

Ili kufikia malengo na shabaha za utekelezaji bajeti ya 2024/25, Dk. Mwigulu amesema sera za mapato na hatua za kiutawala kwa mwaka 2024/25 zitalenga kuongeza makusanyo ya mapato kwa kuendelea kuimarisha na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini ikiwa ni pamoja na kuwianisha, kufuta au kupunguza viwango vya kodi, tozo na ada zinazoonekana kuwa kero.

Amesema wataboresha pia mazingira ya ulipaji kodi kwa hiari, kuongeza wigo wa kodi, kuimarisha usimamizi wa sheria za kodi ili kutatua changamoto za ukwepaji kodi na kupunguza upotevu wa mapato na kuimarisha na kuhimiza matumizi sahihi ya mifumo ya TEHAMA ya ukusanyaji mapato, hususan kodi ya ardhi na pango.

Katika mwaka 2024/25, Dk. Mwigulu amesema serikali itaendelea kusimamia nidhamu ya matumizi ya fedha za umma kwa kuzingatia Sheria ya Bajeti, Sura 439, Sheria ya Fedha za Umma, Sura 348, Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa, Sura 290 na Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sura 410 ili kuimarisha usimamizi wa fedha za umma na kugharamia mahitaji yasiyoepukika ikijumuisha mishahara na Deni la Serikali.

Pia amesema serikali itaendelea kugharamia matumizi ya maendeleo yenye vyanzo mahsusi kwa ajili ya uwekezaji katika maeneo maalum yenye maslahi mapana kwa taifa kama vile Mfuko wa Barabara, Mfuko wa Reli, Mfuko wa Umeme Vijijini na Mfuko wa Maji na Wakala wa Maji Vijijini.

Vilevile, amesema serikali itaendelea kuhakiki, kulipa na kuzuia ongezeko la malimbikizo ya madai pamoja na kufanya maboresho katika mfumo wa ununuzi wa umma ili kuhakikisha ununuzi wa umma unakuwa wenye tija na kuendana na thamani ya fedha.

BAJETI 2023/24

Akizungumzia tathmini ya bajeti ya mwaka 2023/24, Dk. Mwigulu amesema katika kipindi cha Julai 2023 hadi Januari 2024, mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa yalifikia Sh. trilioni 17.18 sawa na asilimia 95.9 ya lengo la kukusanya Sh. trilioni 17.92 kulinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2022/23, sawa na ukuaji wa asilimia 10.

Amesema kati ya mapato yaliyokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yalikuwa Sh. trilioni 15.15 sawa na asilimia 97.9 ya lengo la kukusanya Sh. trilioni 15.49; mapato yaliyokusanywa na wizara, idara zinazojitegemea, wakala na taasisi za serikali yalikuwa Sh. trilioni 1.37 na mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa yalifikia Sh. bilioni 654.1.

NIPASHE
 
Back
Top Bottom