KUNA kitu Bruno Fernandes ameongeza Manchester United tangu atue Old Trafford akitokea Sporting Lisbon wakati wa usajili wa Januari - nacho si kingine, bali ni ubunifu na hamu ya kushinda mechi.
Lakini, wakati Fernandes akiendele kuifanya Man United kuwa bora, bado mashabiki wa timu hiyo wanajiuliza swali hili, je, itakuwaje siku Paul Pogba akirudi uwanjani baada ya kupona majeraha ya enka yaliyokuwa yanamsumbua? Balaa.
Maana kurudi kwa Pogba kutamaanisha kuwa safu ya kiungo ya Man United itakuwa na mafundi wawili kwa wakati mmoja, kitu kitakachozidisha ufundi katikati ya uwanja kwenye kikosi cha Ole Gunnar Solskjaer.
Ila kama unajiuliza wote wawili watatumikaje kwa wakati mmoja, basi jibu lako liko kwenye mifumo hii inayotoa picha ya jinsi gani Pogba na Fernandes watakichafua pamoja.
Mfumo wa 4-3-3
Golini kama kawaida anaanza David De Gea, ukuta utakuwa na Aaron Wan-Bissaka, Victor Lindelof, Harry Maguire na Luke Shaw kama majeraha hayatasumbua, kisha mbele yao kutakuwa na viungo watatu.
Katika mfumo huu wa 4-3-3 ni wazi kuwa Fred ataanza huku Scott McTominay na Nemanja Matic wakisugua benchi katika nafasi ya kiungo wa kati, kisha upande wake wa kushoto atasimama Fernandes na kulia atasimama Pogba.
Kama Frank Lampard alivyowatumia Ross Barkley na Mason Mount dhidi ya Everton, inawezekana kucheza na viungo washambuliaji wawili katika hizo nafasi mbili, lakini kikubwa waridhie kushuka chini kukaba.
Mfumo wa 4-2-3-1
Solskjaer anaweza kuamua kutumia viungo wawili wa chini katika mfumo wa 4-2-3-1, hivyo eneo hilo anaweza kumtumia McTominay na Pogba.
Hii itamruhusu Pogba kuchezesha timu kutokea chini wakati Fernandes atapewa ruhusa ya kutembea juu na kucheza huru huku akiwa na jukumu la kutengeneza nafasi akitokea shimoni.
Kulia na kushoto kwa Fernandes katika mfumo huu wanaweza kutumiwa kina Daniel James na Anthony Martial, huku kinda Mason Greenwood akisimama mbele peke yake kuongoza mashambulizi.
4-1-2-1-2
Katika mfumo huu, Solskjaer anaweza kutumia mfumo wa Diamond katika eneo la kiungo. Mfumo huu tayari Man United imeshautumia katika siku za karibuni na kuleta matokeo chanya.
Fred atacheza kama kiungo wa chini, kisha mbele yake kulia na kushoto watakuwa McTominay na Pogba mbele yao atasimama Fernandes ambaye atakuwa nyuma ya washambuliaji wawili akiwa na jukumu la kuwalisha.
Mbele kabisa Martial anaweza kuanza sambamba na mmoja kati ya Greenwood, Daniel James au hata Odion Ighalo.
Mfumo wa 3-4-2-1
Man United ya Solskjaer imekuwa na utamaduni wa kubadilikabadilika katika mifumo ambayo inatumia hasa kutokana na aina ya wapinzani. Kuna wakati wamekuwa wakitumia mabeki watatu au watano kama ambavyo walifanya katika mechi dhidi ya Manchester City.
Lindelof, Maguire na Shaw watacheza kama mabeki watatu wa kati katika mfumo huu, kisha Wan-Bissaka na Brandon Williams watacheza kama ‘mawing-backs’ wa kulia na kushoto.
Fred na McTominay wanaweza kucheza kama viungo wa chini huku Pogba na Fernandes wakisogea juu kidogo na kutanua uwanja kulia na kushoto ambapo Martial ataongoza mashambulizi.
Mfumo wa 5-3-2
Mwisho kabisa utatu wa eneo la kiungo wa Fernandes, Fred na Pogba utajaziliziwa pembeni na Wan-Bissaka na Williams, huku mbele kukiwa na watu wawili ambao ni Martial atakayecheza na Greenwood, James au Ighalo.
Katika mfumo huu mabeki wa kati wataziba nafasi ambazo zitaachwa na Pogba na Fernandes pindi wakiwa wamepanda mbele kushambulia.
Sent using
Jamii Forums mobile app