KAMA kuna usajili ulisubiriwa kwa hamu na mashabiki wa Manchester United basi ni huu wa Bruno Fernandes aliyetua Old Trafford juzi akitokea Sporting Lisbon, kulekule walikowachukua Luis Nani na Cristiano Ronaldo enzi zile za Sir Alex Ferguson.
Baada ya kumkosa wakati wa usajili wa kiangazi, Man United imetumia sehemu kubwa ya dirisha dogo la usajili kupambana kunasa saini ya kiungo huyo na hatimaye siku chache kabla usajili kufungwa alitua Trafford.
Kwa nini watu wengi wanaamini Fernandes atakuwa suluhisho katika safu ya kiungo ya Man United? Ametoka wapi? Ni ipi historia yake? Na kipi ataongeza? Ni baadhi ya maswali ambayo yatajibiwa na makala haya;-
Ni nani?
Jina lake kamili ni Bruno Miguel Borges Fernandes, alizaliwa Septemba 8, 1994, katika kitongoji Maia, Porto, nchini Ureno, alianzia kucheza soka katika klabu ya Novara inayoshiriki Ligi Daraja la Pili nchini Italia, kabla ya kutua Udinese, kisha Sampdoria zote za Serie A.
Mwaka 2017, alijiunga na Sporting Lisbon ambako alijenga jina lake na kuibuka kuwa mmoja kati ya wachezaji tishio zaidi wa kiungo barani Ulaya, akishinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Ureno katika misimu ya 2017–18 na 2018–19. Januari 2020, Man United ilimnasa kwa dau la awali la Pauni 47 milioni.
Frank Lampard wa Kireno
Fernandes, 25, anajulikana kama Lampard wa Kireno kutokana na aina yake ya uchezaji ambayo imetawaliwa na kufunga mabao mengi akitokea kwenye eneo la kiungo.
Kama ilivyokuwa kwa Lampard ambaye enzi zake uwanjani alisifika kwa kuwa kiungo mwenye mabao mengi, huku akifunga sana kwa mashuti makali ya mbali na Fernandes pia ni hatari sana akiwa katikati ya Uwanja.
Wakati Lampard akifunga mabao 27 kutokea katikati ya Uwanja katika msimu wa 2009-10, Fernandes aliweka rekodi ya kuwa kiungo mwenye mabao mengi zaidi msimu uliopita kutokana na kufunga mabao 32 katika mechi 50.
Mbali na kufunga Fernandes pia anajua sana kupiga pasi za mwisho, katika mechi 134 alizocheza akiwa na kikosi cha Sporting Lisbon amefunga mabao 63 na kupiga pasi za mabao 42 hii inanyesha jinsi gani staa huyu anakuja na mabao Old Trafford.
Fundi mwenye jicho la tatu
Huyu jamaa anajulikana kwa jina la Fundi Mwenye Jicho la Tatu au ‘The Three-Eyed Maestro’ kama ambavyo amekuwa akiitwa huko kwao kutokana na aina yake ya uchezaji.
Pale timu yake inapopoteza mpira hukabia juu akiwa na straika ili kuwapa wakati mgumu mabeki wa kati wa timu pinzani, wapinzani wakifanikiwa kuondoa mpira katika eneo lao la hatari na yeye hushuka chini kabisa kucheza kama kiungo wa chini.
Timu yake ikiwa inashambulia hupenda kupandisha timu juu au kucheza pembeni ya mshambuliaji na kusubiri kugongeana naye haraka na kuwazuru wapinzani. Mashabiki wake pale Sporting walikuwa wanamuita ‘Three-Eyed Maestro’ wakimaanisha kiungo fundi mwenye jicho la tatu jina hili lilikuja kutokana na uwezo wake mkubwa sana wa kupiga pasi kwa wenzake hata katika mazingira magumu.
Fernandes ana uwezo wa kupiga chenga, kukokota mpira na miguu yote miwili, mzuri kwenye mipira ya kichwa anajua kupiga mipira iliyokufa ana mashuti makali sana na ni aina ya kiungo ambaye hukaa nje ya boksi kusubiri mipira ianguke na kumuadhibu mpinzani.
Jezi namba 10
Fernandes anajiamini sana akiwa na miaka 21 alienda Sampdoria akitokea Udinese na baada ya kufika pale akadai kuwa anaitaka jezi namba 10 ya timu hiyo, jezi ambayo inaheshimika sana ndani ya klabu hiyo kutokana na kuvaliwa na magwiji kama Roberto Mancini, hii iliwashangaza wengi, lakini huyo ndiye Bruno ambaye haogopi presha ya mashabiki.
Soka la kimataifa
Wakati akiwa Italia hakuwahi kuitwa kwenye timu ya taifa ya Ureno, kwa mara ya kwanza Fernandes alichaguliwa kujiunga na timu yake ya taifa Agosti 28, 2017 akichukua nafasi ya Pizzi ambaye aliumia kuelekea mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Visiwa vya Faroe, lakini hakucheza mechi hiyo.
Fernandes alichezea timu ya taifa ya Ureno chini ya miaka 23 katika michuano ya Olimpiki mwaka 2016, na kwa mara ya kwanza alichezea timu ya taifa ya wakubwa Novemba 10, 2017 akiingia kuchukua nafasi ya Manuel Fernandes katika mechi ya kirafiki ambayo timu yake ilishinda 3-0 dhidi ya Saudi Arabia.
Alifunga bao lake la kwanza akiwa na kikosi cha Ureno, Juni 7 mwaka 2018 katika mechi ya mwisho ya kujiandaa na fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Algeria ambayo timu yake ilishinda kwa mabao 3-0.
Sent using
Jamii Forums mobile app