WAKALA WA POGBA AFUNGIWA DUNIA NZIMA
Wakala wa wachezaji mashuhuri barani Ulaya, Mino Raiola amefungiwa kufanya shughuli zake kwenye mataifa yote duniani.
Awali, Raiola alikuwa amefungiwa kwa muda wa miezi mitatu katika taifa la Italia pekee lakini Kamati ya Maadili ya FIFA imeongeza adhabu hiyo na kumzuia kufanya shughuli zake dunia nzima kwa kipindi hicho hicho cha miezi mitatu.
Chama cha Soka nchini Italia (FIGC) hakikuweka bayana sababu za kumfungia wakala huyo wa wachezaji wakubwa akiwemo Paul Pogba, Matthijs de Light, Zlatan Ibrahimovic, Henrikh Mkhitaryan, Marco Verratti, Gianluigi Donnarumma na Mario Balotelli.
Hata hivyo Mino alinukuliwa akisema kuwa FIGC ilimuhukumu kwa madai ya uongo na alipanga kukata rufaa akisema “adhabu hii haishangazi wala si bahati mbaya, ni adhabu ambayo imegubikwa na utashi wa kisiasa bila kujali haki”
Mino aliongeza “Nafikiri FIGC haijanisamehe pale nilipowakosoa kwa kuwa sababu ya anguko la soka la Italia pamoja na kuendelea kuwepo kwa tatizo la ubaguzi wa rangi kwenye soka nchini la nchi hiyo”