USAJILI WA MAN U HUU HAPA
UNAMTAKA supastaa kama Neymar na Philippe Coutinho kwenye kikosi chako? Kama wewe ni shabiki wa Manchester United basi hii inakuhusu zaidi.
Kocha Ole Gunnar Solskjaer amesema hivi anataka kusitisha mpango wa Man United kusajili wachezaji kwa pesa nyingi na kwamba anachotaka ni kunasa wachezaji wa kawaida tu kwa gharama ndogo.
Kocha huyo amedai anataka kuijenga Man United mpya bila ya kusajili wachezaji wenye majina makubwa na badala yake anahitaji kunasa wachezaji wenye vipaji na makinda.
Kocha, Solskjaer ataingia sokoni kufanya usajili mwishoni mwa msimu huu huku akilenga kuleta wachezaji makinda zaidi wenye faida kwenye timu kuliko kunasa wachezaji waliokomaa kwa pesa nyingi na kisha hawana maajabu.
Miaka ya karibuni, Man United imekuwa ikitumia pesa nyingi sana kwenye usajili kama ilivyomnasa Paul Pogba kwa Pauni 89 milioni, Angel Di Maria kwa Pauni 59.7 milioni na Romelu Lukaku kwa Pauni 75 milioni na wote hao wamekuwa hasara tu kwenye timu.
Lakini, Solskjaer anataka kufuata nyayo za Mauricio Pochettino wa Tottenham za kusajili wachezaji wenye vipaji kwa gharama nafuu na wenye umri mdogo. Mchezaji aliyesajiliwa pesa nyingi Spurs ni beki Davinson Sanchez, aliyenaswa kwa Pauni 42 milioni kutoka Ajax na umri wake ni miaka 21.
Solskjaer sasa anataka kunasa makinda matata wenye vipaji kama Jadon Sancho, Matthijs de Ligt, Declan Rice, Aaron Wan-Bissaka na makinda wengine wenye umri wa miaka 20 mwanzoni.
Ripoti zinadai wachezaji kama Pogba, Lukaku wanaweza kufunguliwa mlango wa kutoka huku Ander Herrera akijiandaa kuondoka mwisho wa msimu.
Gwiji wa Man United, Gary Neville alisema Solskjaer anahitaji kusajili makinda wenye uwezo kama anataka kurudisha timu kwenye Top Four akisema: Lile kundi la wachezaji waliopo kwa sasa, silipendi. Ole anachopaswa kukifanya cha kwanza ni kusafisha nyumba yake.”