Manchester United imemtangaza aliyekuwa mshambuliaji wake wa zamani raia wa Norway, Ole Gunnar Solskjaer kuwa kaimu kocha mkuu wa klabu hiyo kumrithi Jose Mourinho.
Klabu hiyo jana asubuhi ilimfukuza kazi Mourinho baada ya kuiongoza kwa karibu miaka miwili ambapo alianza vizuri lakini baadaye mambo yalibadilika na msimu huu alikuwa katika kipindi kigumu akipata.
Taarifa za kuteuliwa kwa Solskjaer, zilithibitishwa na tovuti ya klabu hiyo yenye maskani yake Old Trafford lakini hakukuwa na maelezo yoyote zaidi ya ufafanuzi.
Solskjaer mwenye miaka 45, aliifungia Man United mabao 126 katika misimu 11 aliyoitumikia chini ya kocha Sir Alex Ferguson.
Kabla ya kuteuliwa kuinoa Man United, Solskjaer alikuwa akiinoa klabu ya Molde ya nchini Norway kuanzia mwaka 2015 hadi Machi mwaka huu alipojiweka kando lakini akaombwa na kuridhia kusaini mkataba mpya mwanzoni mwa mwezi huu.
Waziri Mkuu wa Norway, Erna Solberg, amempongeza nguli huyo wa soka akisema uteuzi wake kuinoa klabu hiyo maarufu duniani kote ni heshima kwa Taifa.
Solskjaer mfungaji wa bao lililoipa Man United taji la Ligi Mabingwa Ulaya dhidi ya Bayern Munich mwaka 1999, mechi yake ya kwanza akiwa kocha itakuwa Jumamosi hii dhidi ya Cardiff City.
Iwapo atafanikiwa kufanya vizuri katika mechi atakazoiongoza Man United, pengine akathibitishwa kuwa kocha wa kudumu wa timu hiyo ambayo imepanga kumtangaza kocha wa kudumu baada ya kumalizika kwa msimu huu.
Akiwa mchezaji wa Man United, alitwaa mataji sita ya Ligi Kuu England, mawili ya FA na lile la Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Anatwaa mikoba hiyo wakati Man United ipo nafasi ya sita katika msimamo ikiwa na pointi 26, ambazo ni 19 nyuma ya vinara Liverpool ambayo Jumapili iliyopita iliwalaza kwa mabao 3-1 ambayo yalichangia kwa kiasi kikubwa kutimuliwa kwa Mourinho.