Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu atapokewa kwa mila za kabila la Kinyaturu kwa nguo zake alizopigwa nazo risasi kutolewa rasmi, kufuliwa na kupewa wazee kwa ajili ya kuzivaa.
Akizungumza na Mwananchi, Katibu wa Chadema Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, Ibrahim Saidi alisema mkutano wa leo utakuwa na ajenda kadhaa, lakini kubwa ni mapokezi ya Lissu kurudi nyumbani.
Alisema nguo za Lissu, zikiwamo shati, suruali, koti, viatu na soksi ambavyo vilihifadhiwa vikiwa na damu vitatolewa siku ya Jumatatu (kesho) kwa ajili ya kumwagiwa mafuta aina ya samli na baadaye zitafuliwa na watapewa wazee wazivae hadi zitakapochakaa.
Lissu alikuwa mbunge wa Singida Mashariki tangu mwaka 2010, alivuliwa ubunge Juni 28, 2019 akiwa kwenye matibabu nchini Ubelgiji kwa madai ya kutoonekana bungeni bila Spika kuwa na taarifa ya maandishi na kutojaza fomu ya tamko la mali na madeni.
Mwanasiasa huyo alikumbwa na mkasa wa kupigwa risasi zaidi 30 Septemba 7, 2017 na kujeruhiwa akiwa kwenye gari nyumbani kwake Area D, mjini Dodoma alipotoka kuhudhuria vikao vya Bunge.