Waziri wa TAMISEMI Ummy Mwalimu amemshukuru Rais Samia Suluhu kwa kuonesha kwa vitendo dhamira yake ya kujenga barabara Vijijini kwa kuongeza bajeti kutoka Tshs bilioni 273 mwaka 2020/21 hadi kufikia shilingi bilioni 966.43 mwaka huu wa fedha 2021/22.
Itakumbukwa jana Waziri Ummy alizindua Mpango Mkakati wa Pili wa Miaka Mitano wa Wakala wa Barabara Vijiji na Mjini(TARURA) na kaulimbiu isemayo 'TARURA tunakufungulia barabara, kufika kusipofikika'.
Akizungumza kwenye uzinduzi huo Waziri Ummy alisema———“Kauli mbiu hii isiwe kwenye makaratasi na mwaka huu ndio wa kuwapima, matarajio ya Serikali na Watanzania kwa TARURA ni makubwa sana tunaomba msituangushe mkafungue Barabara za mijini na vijijini."
Ummy alisema Rais Samia Suluhu Hassan amedhamiria kutatua changamoto za barabara mijini na vijijini kupitia ongezeko la bajeti.
“Mmeniambia kupitia mpango huu wenu wa miaka mitano mtaongeza Kilomita 73,242 za Barabara kiwango cha changarawe, hii itakuwa ni hatua kubwa na mmesema mnahitaji Tsh.Trilioni 3.6, niwatoe hofu tu kama Rais Samia ameweza kutenga Tsh. Bilioni 966.43 mwaka huu sidhani kama atashindwa kutoa hiyo fedha kwa kipindi cha miaka mitano”———Ummy