Bunge lisilaumiwe kuhusu tozo - Lusinde
-
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (MNEC) na Mbunge wa Mvumi mkoani Dodoma, Livingstone Lusinde amefunguka kuhusu makato ya miamala katika simu za mikononi ambapo amedai Bunge wao walipitisha sheria na kiwango kilipagwa na Waziri wa Fedha na Mipango,(Dk. Mwigulu Nchemba) hivyo Bunge lisilaumiwe.
Amesema mjadala kwa sasa uwe tozo ni kubwa hivyo waziri apunguze sio lilaumiwe bunge kwa kupitisha sheria hiyo kwani hata mwanzo makato yalikuwepo na watu walikuwa wanalipa.
Pia amedai Wabunge wanakatwa kodi ambazo zinaenda kwenye shughuli za maendeleo hivyo jamii ipuuze maneno kwamba wao hawakatwi kodi.
Hatua hiyo, imekuja mara baada ya hivi karibuni Mbunge wa Ukonga, Jerry Silaa akiwa katika mkutano wa hadhara uliowashirikisha Wananchi wa Mzinga Ukonga Jijini Dar es Salaam kudai wabunge waanze kulipa kodi kupitia mishahara yao ili wapate uwezo wa kuwaambia Wananchi na wao walipe kodi.
Pia hivi karibuni Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mstaafu, Ludovick Utouh alisema wabunge hao wanatakiwa kukatwa kodi katika mishahara yao.
Akizungumza leo Agosti 3, na Waandishi wa Habari, Lusinde amesema bunge wametunga sheria na wala sio kiwango kwani hilo ni jukumu la Waziri wa Fedha na Mipango.
“Sisi tumetunga sheria sio kiwango, mbona hata mwanzo makato yalikuwa kwenye simu, kiwango anapanga Waziri na wanatengeneza kanuni ninauhakika makato yatapungua ndugu zangu tujifundishe kulipa kodi nani wa kutupa hela za bure?Mjadala uwe hapo tozo ni kubwa hivyo Waziri apunguze sio lilaumiwe Bunge,” amesema Lusinde.
Kuhusiana na mishahara yao kukatwa kodi, Lusinde amesema wao wanakatwa kodi ambazo zinaenda kwenye shughuli za kimaendeleo hivyo jamii iondokane na maneno kwamba wao hawakatwi kodi.