Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetengua hukumu ya kesi ya uchochezi dhidi ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na wenzake na kuamuru warejeshewe kiasi cha TSh. Mil. 350 walicholipa kama faini.
Uamuzi huo umetolewa leo na Jaji Irvin Mgeta ambapo Mbowe na wenzake walihukumiwa Mahakama ya Kisutu March 10, 2020 kulipa faini ya shilingi milioni 350 za Tanzania ambazo ni sawa na dola elfu kumi na tatu.
Mbowe na wenzake walihukumiwa baada ya kutiwa hatiani kwenye makosa 12 ikiwemo la kufanya maandamano, Washtakiwa wengine kwenye kesi hiyo walikuwa ni Esther Matiko, Mchungaji Peter Msigwa, Salum Mwalimu, John Mnyika, Halima Mdee, John Heche, Ester Bulaya na Dk Vicent Mashinji.
Hukumu hiyo iliyochukua takribani saa 4, kuanzia saa 7 mchana hadi saa 11 jioni, ilitolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba baada ya kusikiliza ushahidi wa Mashahidi 23 baina ya utetezi na Serikali.