Makapuku Forum

Makapuku Forum

The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 60
ILIPOISHIA:
Vijana wadogo tu kama mimi, wengine hata nawazidi lakini wanaendesha magari ya kifahari barabarani, kwa nini na mimi nisionje kidogo hata kama ni mbaya? Wakati akiendelea kunipa nasaha zake, Mkuu alinipa ishara kwamba nimfuate, harakaharaka nikainuka na kumuacha baba yake Rahma akiendelea kuongea.
SASA ENDELEA...

Alinishika mkono na kusogea pembeni na mimi, mawasiliano kati yetu kidogo yalikuwa magumu kwa sababu alikuwa akiongea maneno ya Kiswahili machache, tena yaliyopindapinda lakini muda mwingi alikuwa akizungumza lugha ambayo siielewi.
Katika yale machache niliyomuelewa, alionesha kufurahishwa na ujasiri wangu, na kuniambia kwamba japokuwa ndiyo kwanza nilikuwa nimejiunga, nilikuwa na kasi nzuri ya kujifunza. Kama alivyoniambia baba yake Rahma, kweli Mkuu aliniuliza ni zawadi gani akinipa nitafurahi?
Sikupepesa macho wala kumung’unya maneno, nikamwambia kwamba nataka dawa za kunifanya niwe tajiri. Alicheka sana, mapengo yake yakawa yanaonekana, ni hapo ndipo nikagundua kwamba kumbe naye huwa anacheka na kufurahi, ingawa sikuelewa nini hasa kilichomfurahisha.
Aliniambia kitu nilichokichagua ni kikubwa sana kuliko uwezo wangu, akaniambia atanipa dawa lakini haitakuwa ya kupata utajiri mkubwa kwa sababu utajiri una masharti magumu na nikipata pesa nikiwa bado mdogo, naweza kufa siku si zangu.
Tulirudi pale katikati alipokuwa ameweka vifaa vyake, akatoa kimkoba chake cha ngozi na kutoa kichupa kilichokuwa na dawa, akatoa na wembe kisha akaniambia nimfuate. Tulitoka pale na kupotelea vichakani kwenye giza, nikiwa namfuata nyumanyuma.
Tulitokezea kwenye eneo ambalo lina uwazi, akanielekeza kwa ishara kwamba nivue shati kisha nikae chini na kukunja miguu, kweli nilifanya hivyo, akanishika kichwani na kuanza kuzungumza maneno nisiyoyaelewa, akayaongea kwa muda mrefu kisha akachukua ule wembe na kuanza kunichanja chale kuanzia kwenye utosi kurudi mgongoni.
Aliponipaka ile dawa, nilisikia maumivu makali sana lakini nikajikaza kisabuni, alipomaliza, aliniambia nitulie hivyohivyo, akapotelea vichakani. Muda mfupi baadaye, aliibuka kutoka vichakani akiwa amembeba nyoka mkubwa, nikashtuka sana na kutaka kusimama nitimue mbio lakini akanionesha ishara kwamba nitulie.
Huku nikitetemeka kuliko kawaida, alimsogeza yule nyoka mkubwa kwenye zile chale, akawa anamlambisha damu zangu huku akiendelea kuzungumza maneno nisiyoyaelewa. Alipomaliza, aliamuachia, yule nyoka akatambaa kwa kasi na kupotelea vichakani.
Mshangao niliokuwa nao, ulikuwa hauelezeki. Akanipa ishara kwamba nisimame, nikafanya hivyo na kuvaa shati langu kisha tukarudi kule walipokuwa wenzetu, akaniambia kwamba baada ya siku saba dawa itaanza kufanya kazi lakini natakiwa kuwa naenda kutoa sadaka kwa yule nyoka mara kwa mara.
Baba alikuwa akifuatilia kila kilichokuwa kikiendelea na Mkuu alipomaliza tu kuzungumza na mimi, harakaharaka baba alinifuata. Ile furaha yote niliyokuwa nayo ndani ya moyo wangu ilitibuka kwani baba alipofika tu, alianza kunifokea kwa sauti ya chinichini na kuniambia kwamba nilichokifanya ni upumbavu wa hali ya juu na yeye hatahusika na chochote kitakachonipata nitakapokosea masharti.
“Masharti gani tena baba?” nilimuuliza kwa mshangao kwa sababu Mkuu hakuwa amenipa masharti yoyote, akaniambia kwamba siyo kwamba yeye hatamani utajiri lakini masharti yake yalivyo magumu, ndiyo maana wengi walikuwa wanaona ni bora waendelee kuishi kimaskini tu.
“Kama hajakwambia basi mimi nakwambia, kuna masharti magumu sana tena usipokuwa makini unaweza kusababisha hata sisi wazazi wako na ndugu zako wa tumbo moja wakawa kwenye hatari kubwa sana, kwa nini hukuuliza kabla?” baba aliendelea kuniwakia kwa sauti ya chini huku mara kwa mara akigeuka na kumtazama Mkuu. Nadhani alikuwa hataki asikie chochote.
Maelezo aliyonipa baba yaliniogopesha sana, japokuwa hakuwa amenifafanulia, ilivyoonesha kulikuwa na masharti magumu kwa sababu hata mimi siku nyingi nilikuwa najiuliza, kwamba kwa nini unakuta mganga anasaidia watu kupata utajiri kwa njia za kishirikina wakati yeye anaishi kwenye kijumba cha nyasi?
Nilikuwa pia najiuliza kwa nini wachawi wengi wanakuwa na maisha ya dhiki sana? Nilitamani kuyajua hayo masharti kwa sababu kama ni maji, yalishamwagika. Baba aliniambia hawezi kuniambia, kama nataka nirudi kwa Mkuu kwenda kumuuliza.
Ile furaha yote niliyokuwa nayo moyoni iliyeyuka, kurudi kwa Mkuu kumuuliza nikashindwa kwani muda nao ulikuwa umeenda sana. Nikiwa bado nimetulilia nikitafakari, yule msichana, Isrina alinifuata, hata sijui alitokea wapi, nilishtukia tu yupo pembeni yangu.
“Hongera,” alisema huku akinipa mkono, tabasamu pana likiwa limechanua kwenye uso wake, nilimpa mkono lakini sikuwa nimechangamka.
“Mbona siku hizi huna taimu na mimi? Kuna jambo nimekuudhi?” aliniuliza, nikatingishwa kichwa kukataa lakini ukweli ni kwamba nilikuwa na kinyongo kikali sana dhidi yake.
“Basi nitakutafuta tuzungumze, nakuomba ukubali,” alisema huku akiinuka, nikatingisha kichwa kwa sababu nilikuwa nataka aondoke haraka.
Mpaka muda wa kutawanyika unafika, bado nilikuwa sielewi nini itakuwa hatma yangu na nifanye nini kwa wakati huo. Tulirudi nyumbani kama kawaida ambapo nilijipa muda wa kutafakari mambo yote yaliyotokea kwa siku hiyo maana kiukweli kwenye ulimwengu wa giza, dunia inakwenda kasi sana kuliko unavyoweza kudhani. Kutokana na uchovu niliokuwa nao, nilipitiwa na usingizi mzito, nikiwa na maswali mengi ndani ya kichwa changu ambayo yote hayakuwa na majibu.
Kesho yake nilichelewa sana kuamka kwa sababu ya uchovu, nilipoamka, majira kama ya saa nne hivi, nilimfuata baba yake Rahma nikitaka ufafanuzi zaidi. Tulizungumza mambo mengi lakini kubwa aliniambia utajiri wa kishirikina, huwa unahitaji makafara ya damu mara kwa mara.
Akaniambia kwamba bahati mbaya ni kwamba, sina uwezo wa kuchagua nani atolewe kafara muda wa kufanya hivyo unapofika bali nitakuwa nachaguliwa, kwa hiyo natakiwa kuwa makini sana.
Maelezo hayo yalinitisha sana, nikawa najaribu kuunganisha matukio, ni kweli watu wenye utajiri wa kishirikina, huwa wanasumbuliwa sana na kashfa ya kuwatoa kafara watoto wao, wazazi wao au watu wao wa karibu.
Nilijaribu kujitazama kwa upande wangu, nikawafikiria wazazi wangu na ndugu zangu tuliozaliwa nao tumbo moja, nikawa najiuliza kama siku nitatakiwa kumtoa yeyote kafara nitaweza kweli? Ulikuwa ni mtihani mgumu sana kwangu.
Ila aliniambia jambo ambalo kidogo lilinipa faraja, akaniambia kwamba makafara yanakuwa ni lazima pale utajiri unapokuwa mkubwa sana, lakini kwa mambo ya fedha ndogondogo hakuna ulazima wa kufanya kafara lolote.
Maelezo hayo yalinifurahisha sana ndani ya moyo wangu, nikawa nasubiri kwa hamu hizo siku saba ziishe nikapewe maelekezo ya nini cha kufanya. Nilichojiapiza ni kwamba sitataka utajiri mkubwa, fedha ndogondogo tu za kutesea mitaani zilikuwa zinanitosha sana, hasa ukizingatia kwamba sikuwa na majukumu ya moja kwa moja.
Wakati nikiendelea kusubiri hizo siku saba, niliona huo ndiyo muda muafaka wa kuanza kushughulikia suala la Rahma. Kama nilivyoeleza, kuna ukuta mkubwa ulikuwa umejengeka kati yetu, na kama nisingefanya jambo, huenda huo ndiyo ungekuwa mwisho wetu, jambo ambalo lilikuwa likituumiza sana sote wawili, hasa Rahma.
Alikuwa hanielewi kwa nini nimebadilika ghafla, nimekuwa na mambo mengi ya ajabuajabu, sioneshi kumhitaji tena kama siku za mwanzo na wala sijali hisia zake. Ukweli ni kwamba nilikuwa namlinda na ndiyo maana ilikuwa lazima nifanye hivyo na njia pekee, ilikuwa ni kumshawishi naye ajiunge nasi, kazi ambayo isingekuwa nyepesi lakini nilishajipanga kumkabili.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
 
The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na hatia)- 61
ILIPOISHIA:
Alikuwa hanielewi kwa nini nimebadilika ghafla, nimekuwa na mambo mengi ya ajabuajabu, sioneshi kumhitaji tena kama siku za mwanzo na wala sijali hisia zake. Ukweli ni kwamba nilikuwa namlinda na ndiyo maana ilikuwa lazima nifanye hivyo na njia pekee, ilikuwa ni kumshawishi naye ajiunge nasi, kazi ambayo isingekuwa nyepesi lakini nilishajipanga kumkabili.
SASA ENDELEA...

“Rahma!” nilimuita msichana huyo baada ya kukutana naye koridoni, mimi nikitoka bafuni kuoga na yeye akitoka chumbani kwake. Tofauti na siku zote ambazo alikuwa akinichangamkia sana anaponiona, wakati mwingine hata akinifuata chumbani kwangu, siku hiyo Rahma alikuwa tofauti kabisa, alipooza na alionesha kutotaka kuzungumza chochote na mimi.
“Rahma si nakuita jamani,” nilisema baada ya kumuona amenipa mgongo, akitembea haraka kuelekea sebuleni. Licha ya kutamka maneno hayo, bado hakutaka kusimama, ikabidi nitumia nguvu kumshika mkono na kumgeuza.
“Samahani nina mazungumzo na wewe, naomba unisikilize tafadhali,” nilimwambia kwa upole, akanitazama usoni, macho yake na yangu yakagongana, nikashtuka kumuona akilia.
“Unalia nini Rahma?” nilimuuliza lakini hakunijibu kitu zaidi ya kuendelea kunitazama kwa huzuni. Ilibidi nianze kumbembeleza lakini kwa kuwa tulikuwa tumesimama koridoni, niliona haiwezi kuwa picha nzuri kwani mtu yeyote angetuona tukibembelezana hapo angeweza kutufikiria vibaya.
“Naomba tutoke tukanywe japo soda pale dukani, nina mazungumzo ya muhimu sana na wewe,” nilimwambia Rahma, akatingisha kichwa bila kunijibu chochote kisha akarudi chumbani kwake.
Ilibidi na mimi nirudi chumbani kwangu, nikachukua nauli iliyokuwa imebaki siku nilipoenda Mlandizi na kuitia mfukoni, nikajiweka vizuri na kutoka nje. Nilizugazuga pale nje, nilipoona hakuna anayenifuatilia, nilifungua geti kubwa na kutoka nje. Ile kutoka tu, madereva Bajaj na bodaboda waliokuwa wanapaki pale nje, waliacha kila walichokuwa wanakifanya na kuanza kunitazama.
Kibaya ni kwamba upande ule waliokuwa wakipaki, kwa mbele kidogo ndiyo kulikuwa na duka ambalo nilipanga tukae pale na Rahma kwa sababu kulikuwa na viti upande wa nyuma, kwa hiyo ilikuwa ni lazima niwapite palepale walipopaki.
Nimewahi kusikia matukio kadhaa ya madereva hao wa Bajaj na bodaboda kushirikiana kufanya uhalifu, hasa pale inapoonekana mmoja wao ameonewa, nikajua lazima watakuwa wamenipania kwa jinsi nilivyomsulubu mwenzao. Hata hivyo, kwa sababu nilikuwa na nguvu za giza, tena za kutosha kabisa, sikuogopa chochote, ndiyo kwanza nikawa napiga mluzi huku nikielekea kule walikokuwa.
Cha ajabu, nilishangaa kuona kila mmoja akikimbilia kwenye chombo chake na kukiwasha, wakaanza kuondoka mmoja baada ya mwingine wakikimbia kwa kasi, sekunde chache baadaye eneo lote likawa tupu.
Hakukuwa na mashaka kwamba walikuwa wakinikimbia mimi, kwa sababu hata kama wanawahi abiria, wasingeweza kuondoka wote kwa mkupuo, tena kwa kasi kubwa wengine wakinusurika kugongana wao kwa wao.
Sikuelewa nini kimetokea mpaka wawe wananiogopa kiasi hicho lakini sikuwajali maana na mimi nilikuwa na majanga yangu mengi kichwani. Nilienda mpaka pale dukani, nikamsalimia muuza duka ambaye aliponiona tu, alishtuka sana, akaitikia kwa woga.
“Naomba Fanta,” nilisema huku nikimeza mate kwani mara ya mwisho kunywa soda, ilikuwa ni siku ile tuliposafiri kuja jijini Dar es Salaam.”
“Hatuuzi soda hapa!” alisema yule muuzaji, kauli ambayo nilishindwa kuielewa ina maana gani. Juu ya meza kulikuwa na chupa tupu za soda kuonesha kwambamuda si mrefu kuna watu walikuwa wakinywa soda, na mara kadhaa nilipita pale na kuona watu wakipata vinywaji, kwa nini aniambie kwamba hawauzi soda?
Nikiwa bado nimeduwaa, nikishindwa nimuulizeje, mara Rahma aliwasili, kumbe hatukuwa tumeachana umbali mrefu, akamsalimia yule muuzaji. Alimuita kwa jina lake na ilionesha wanafahamiana.
“Kumbe anaitwa Vero,” nilijisemea moyoni, alikuwa mwanamke ambaye kwa kumkadiria alionesha kuwa bado mdogo lakini mwenye uso uliokomaa na kupoteza nuru kama walivyo wanawake wengi wa vijijini kama kule kwetu Chunya.
“Huyu ni kaka yangu, unamjua? Anaitwa Togo,” Rahma alisema huku akinishika begani, nikamuona yule mwanamke akijaribu kuvaa tabasamu la uongo usoni.
“Tuletee soda, Togo unakunywa nini?” alisema Rahma, yule mwanamke akawa anababaika, kama anayeshindwa ajibu nini maana mimi aliniambia hawauzi soda. Rahma alinishika mkono huku akionesha kabisa kwamba anailazimisha furaha, tukaenda mpaka kwenye viti na kukaa, tukawa tunatazamana huku tukisubiri yule mwanamke aje atuhutubie.
“Unataka kuniambia nini?” alisema Rahma huku akikwepesha macho yake pembeni.
“Rahma! Najua unanifikiria vibaya sana kwa sasa, najua unaona kama nakufanyia makusudi kwa sababu sikupendi lakini ukweli ni kwamba ni matatizo makubwa sana na badala ya kunichukia, unatakiwa unionee huruma mwenzio,” nilianza kumbembeleza Rahma.
Kama nilivyosema awali, sikuw anajua mambo ya mapenzi kwa hiyo hata kubembeleza kwangu, nilikuwa naungaunga tu ilimradi Rahma anielewe. Niliendelea kushuka mistari kwa kuzunguka, nikamwambia kuna jambo zito ambalo halijui nataka kumweleza.
Maneno yangu yalimbadilisha kabisa Rahma, akawa ananitazama kwa shauku huku ile huzuni aliyokuwa nayo, ikiyeyuka ghafla. Ili kumuweka sawa, ilibidi nibadilishe mada kwanza, nikamuuliza vipi yule muuzaji mbona haleti hizo soda?
“Una kiu? Ngoja nimfuate,” alisema huku akiinuka lakini alipofika pale dukani, yule mhudumu alikataa katakata kutoka, akampa Rahma funguo ya friji na kutaka ajihudumie mwenyewe. Rahma aliichukua, akaniuliza nakunywa soda gani, akatoambili pamoja na yake, akaja mpaka pale tulipokuwa tumekaa, akazifungua zote na kurudisha funguo kwa mwenyewe.
“Kwa nini amekataa kuja kutuhudumia mwenyewe?”
“Hata mimi nashangaa! Achana naye tuendelee na yetu,” alisema Rahma, nikapiga funda moja kisha nikaendelea kuzungumza. Lengo langu lilikuwa ni kumpasulia ukweli kwamba baba yake alikuwa mwanachama wa jamii ya siri, vilevile baba yangu na mimi pia wameniingiza bila ridhaa yangu.
Niliona hiyo ndiyo gia nzuri ya kumuingia kwa sababu kama ningesema mimi mwenyewe ndiye niliyetaka kujiunga, angenishangaa sana na pengine nisingeweza kumshawishi. Nilianza kwa kumdadisi kwa kina kuhusu baba yake, nikitafuta sehemu ya kuanzia.
“Mbona unaniuliza kama una kitu unataka kuniambia? Tatizo langu wala halimhusu baba, ni mimi na wewe.”
“Ni stori ndefu Rahma ila naomba unielewe nitakachokwambia,” nilisema, nikashusha pumzi ndefu na kuamua liwalo na liwe. Nilitaka kwenda moja kwa moja, kwamba baba yake na baba yangu walikuwa wachawi. Cha ajabu, kila nilipotaka kusema hivyo, mdomo ulikuwa mzito, nikawa naumauma maneno, hali iliyosababisha anikazie macho.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
 
The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na hatia)- 62
ILIPOISHIA:
“Ni stori ndefu Rahma ila naomba unielewe nitakachokwambia,” nilisema, nikashusha pumzi ndefu na kuamua liwalo na liwe. Nilitaka kwenda moja kwa moja, kwamba baba yake na baba yangu walikuwa wachawi. Cha ajabu, kila nilipotaka kusema hivyo, mdomo ulikuwa mzito, nikawa naumauma maneno, hali iliyosababisha anikazie macho.
SASA ENDELEA...

“Mbona sikuelewi Togo?”
“Ni kuhusu wazazi wetu.”
“Wamefanya nini?”
“Wanajihusisha na...” kabla sijamalizia nilichotaka kukisema, jambo la ajabu lilitokea. Yule muuzaji wa lile duka, alifungua mlango na kutoka huku akikimbia, cha ajabu, hakuwa amevaa nguo hata moja.
“Vipi kwani mbonaumeshtuka?”
“Umemuona?”
“Nani? Vero? Nini cha ajabu kwani?” Rahma alinishangaa sana, na mimi nikawa namshangaa. Yaani mtu atoke dukani akiwa mtupu, halafu aanze kukimbia mitaani, siyo jambo la kushangaza hilo?”
“Itakuwa labda kuna anaenda kuomba chenji, tuendelee na mazungumzo yetu,” Rahma alizidi kunishangaza. Sikuelewa kwamba alikichukuliaje kitendo kile kiasi cha kutokipa uzito hata kidogo, hata baadhi ya wateja waliokuwa wamekaa upande wa pili, nao wakipata vinywaji, hawakuonesha kushtuka kabisa.
“Ndiyo atoke bila nguo?”
“Togo, umeanza kuchanganyikiwa nini?”
“Rahma, ina maana huoni kama hajavaa nguo yule? Kwa hiyo kumbe ndiyo maana alikuwa anajificha dukani?”
“Nani hajavaa nguo? Una matatizo gani Togo? Usije kunitia aibu hapa, hebu maliza twende,” alisema Rahma huku akimalizia soda yake. Nadhani alihisi huenda nikatokewa na maruweruwe kama yale yaliyokuwa yakinitokea.
“Basi Rahma, tuendelee na mazungumzo yetu,” nilijaribu kumsihi lakini alishaonesha kama ameingiwa na hofu ndani ya moyo wake, hakutaka kukaa tena eneo lile, ikabidi nimalizie soda yangu na kusimama.
Sikuwa nimemlipa yule muuzaji, lakini Rahma aliniambia kwamba nisijali yeye atampa hata baadaye. Nilijisikia vibaya sana ndani ya moyo wangu kwa jinsi Rahma alivyonipuuza ila sikutaka kumuonesha.
Kwa jinsi alivyonichukulia, hata kama ningemweleza kile kilichofanya nikakutana naye pale, huenda pia angenipuuza kwa hiyo nilichokifanya, niliamua kunyamaza na dukuduku langu moyoni.
“Hujamalizia ulichotaka kuniambia,” alisema Rahma wakati tukitembea kurudi ndani, nikamwambia asiwe na wasiwasi nitamueleza siku nyingine.
“Kwani siku hizi umeshapata mwanamke mwingine anayekuzuzua?”
“Hapana Rahma, na ndiyo maana nilitaka kuzungumza na wewe, lakini basi tuyaache.”
“Sikuelewi Togo na kama unaona ulichokifanya kwangu ni sawa, wala mimi sina cha kusema ila kumbuka chozi langu haliwezi kwenda bure,” alisema Rahma, nikajaribu kumbembeleza lakini ilikuwa sawa na kazi bure.
Mpaka tunaingia ndani, Rahma alikuwa akiendelea kulalamika tu, akaniambia anashukuru kwa yote niliyomfanyia na kumuumiza moyo wake. Nilishindwa cha kusema, ikabidi ninyamaze tu, bado wale madereva bodaboda na Bajaj pale nje hawakuwa wamerejea.
Tuliingia ndani lakini Rahma hakutaka kabisa kujishughulisha na mimi, alienda moja kwa moja sebuleni, mimi nikaenda chumbani huku nikiwa nimekosa kabisa furaha. Nilijilaza kitandani, nikaanza kutafakari tukio la yule muuzaji wa lile duka.
Nilichokihisi kwa harakaharaka, huenda alikuwa akitumia nguvu za kishirikina kwenye biashara yake maana nimewahi kusikia kwamba kuna wafanyabiashara ambao ukiingia kwenye duka lake au sehemu anayofanyia biashara, hata kama umevaa nguo, anakuona kila kitu lakini wapo wengine ambao inakuwa kinyume chake, kwamba muuzaji anakaa kwenye biashara akiwa hana nguo hata moja ingawakwa macho ya kawaida anaonekana amevaa nguo.
Lengo la kufanya hivyo inakuwa ni kuvutia wateja na kiukweli hata kwenye lile duka la pale nje, lilikuwa kubwa lenye kila kitu unachokihitaji na kiukweli alikuwa akifanya sana biashara kwa sababu kwa muda mfupi tu tuliokaa pale, wateja walikuwa hawakauki.
“Ulitaka kumwambia nini Rahma,” sauti ya baba ilinizindua kutoka kwenye lindi la mawazo. Alikuwa amesimama pembeni ya kitanda changu, hata sikukumbuka ameingia saa ngapi, nilichoshtuka ni kumuona akiwa ndani.
“Mimi?” niliongea kwa kubabaika huku nikiinuka pale kitandani.
“Kwani nazungumza na nani?” baba aliniuliza akionesha kuwa na jazba, nikawa nababaika. Kwa jinsi ilivyoonesha, alikuwa anajua kwamba nilitaka kumweleza Rahma ukweli, jambo ambalo walinionya sana kwamba sitakiwi kutoa siri za jamii yetu kwa mtu yeyote asiyehusika.
“Tulikuwa tunapiga stori za kawaida tu.”
“Stori za kawaida ndiyo muende dukani?” baba alinihoji huku akinitazama kwa macho ya ukali, sikuwa na cha kujibu na kwa jinsi baba alivyo, nilitegemea kabisa kwamba pale lazima angenizibua makofi, nikawa nimekaa ‘attention’.
“Kuna maagizo yako kutoka kwa Mkuu, usiku itabidi tukupeleke sehemu, umeyaanza mwenyewe lazima uyamalize,” baba alisema huku akigeuka na kuanza kuondoka, nikabaki na mshangao mkubwa, nikiwa sijui alichokimaanisha. Akiwa anamalizikia kutoka, aligeuka na kunitazama kwa macho makali.
“Ole wako ufumbue domo lako!” Nilishusha pumzi ndefu, mambo yalianza kuwa mengi na kunielemea kwa sababu kabla moja halijaisha, lingine lilikuwa likiibuka. Kwa jinsi nilivyozungumza na baba yake Rahma, nilitambua kwamba hizo salamu kutoka kwa Mkuu lazima zitakuwa zinahusu masharti ya uamuzi nilioufanya.
Niliona kama muda unaenda taratibu sana, sikutoka chumbani, hata chakula nililetewa kulekule na Rahma ingawa safari hii alionesha kuwa na chuki za waziwazi kwangu maana hakutaka hata kunisemesha wala kunitazama usoni.
Hatimaye jioni iliwadia, baba na baba yake Rahma, wakiwa tayari wameshajiandaa, walinifuata chumbani na kuniambia muda wa safari umewadia, wakanitaka nijiandae, baba Rahma akanipa koti kubwa jeusi.
“Kwani tunaenda wapi?”
“Jiandae bwana, maswali mengi ya nini?” alisema baba kama kawaida yake, nikajiandaa na muda mfupi baadaye, safari ilianza. Kwa jinsi nilivyokuwa nimevaa, haikuwa rahisi kwa mtu yeyote kunitambua, lile koti lilinibadilisha kabisa. Tulitoka na kuelekea moja kwa moja kwenye stendi ya mabasi ya Makumbusho, tukapanda kwenye ‘coaster’ moja ambayo mbele ilikuwa imeandikwa kwamba inaenda Bagamoyo. Sikuwa nimewahi kufika Bagamoyo zaidi ya kusoma tu darasani kuhusu mji huo wa kihistoria.
Basi tulienda mpaka tulipofika sehemu moja iitwayo Mlingotini, tukateremka kwenye gari na kuvuka barabara, tukaanza kutembea kwa miguu. Tulienda umbali mrefu sana maana mpaka inafika saa tano za usiku, bado tulikuwa tukitembea.
Hatimaye tuliwasili kwenye eneo lililokuwa na nyumba kama tatu hivi, moja ikiwa imeezekwa kwa bati na zile nyingine kwa makuti, baba akabisha hodi ambapo sauti ya mwanamke ilisikika ikitukaribisha.
Muda mfupi baadaye, mwanamke mmoja mzee alitoka, ilionesha alikuwa akifahamiana vizuri na baba na baba yake Rahma kwani aliwakaribisha kwa uchangamfu, tukaingia ndani na kukaa kwenye jamvi lililokuwa pale sebuleni.
“Ndiyo huyu?” aliuliza yule mwanamke, baba akamjibu kwamba ndiyo mimi, sikuelewa kwamba ndiyo mimi nimefanyaje na kwa nini ameniuliza, ikabidi niwe mpole.
“Mchumba hujambo? Ukifanikiwa na mimi nataka uninunulie gari,” alisema yule mwanamke huku akitabasamu, mapengo yake yakaonekana. Sikuelewa kwa nini amesema vile, nikazidi kuwa gizani. Alinishika mkono na kuwapa ishara akina baba kwamba wamsubiri, tukatoka nje na kwenda kwenye kibanda cha makuti.
Wakati tunatoka, nilimsikia baba akimwambia baba Rahma kwamba kuwana mtoto kama mimi ni hasara, wakacheka. Sikuelewa kwa nini baba amesema vile lakini sikujisikia vibaya maana mimi na baba kukwaruzana ni jambo la kawaida kabisa, ingawa mimi ndiyo nilikuwa mwanaye kipenzi.
“Nimepata salamu zako kwamba umechagua kuwa tajiri, ombi lako limekubaliwa lakini kuna masharti inatakiwa kabla siku zako saba hazijaisha, uwe umeshaanza kuyafuata, vinginevyo utakufa,” alisema yule mwanamke, macho yakanitoka pima.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
 
SEVEN DAYS IN HELL (Siku Saba Kuzimu)- 56
ILIPOISHIA:
Harakaharaka nikafungua mlango nikiwa ni kama siamini nilichokisikia, nikamkuta Shenaiza akihangaika kujigeuza, jambo ambalo hakuwa amelifanya kwa kipndi kirefu tangu akiwa kule hospitalini.
“Shenaiza! Shenaiza,” nilisema huku nikipiga magoti pembeni ya kitanda chake. Bado hakuwa amefumbua macho yake.
SASA ENDELEA...

Hata hivyo, japokuwa hakuwa amefumbua macho, niliona akiyapepesa kama anayetaka kuyafumbua, nikainua mikono juu kama ishara ya kumshukuru Mungu. Kumbukumbu za yote yaliyotokea kuanzia siku ya kwanza msichana huyo aliponipigia simu mpaka muda huo zilipita kwa kasi ndani ya kichwa changu.
Kila kitu kilikuwa kikitokea kwa kasi kubwa ambayo ungeweza kudhani ni ndoto ya kusisimua na muda si mrefu nitazinduka. Kwa kuwa Junaitha aliniambia nikamsubiri chumbani kwake, sikukaa muda mrefu ndani ya chumba hicho cha Shenaiza kwa sababu nilijua hawezi kufurahi akinikuta nikifanya tofauti na maagizo aliyonipa, nikambusu Shenaiza kwenye paji la uso kisha nikatoka na kuelekea chumbani kwa Junaitha.
Maisha aliyokuwa akiishi mwanamke huyu yalikuwa na tofauti kubwa kati ya nje na ndani. Wakati kwa nje ungeweza kudhani Junaitha ni mwanamke ‘mayai’ anayependa sterehe na anasa, ndani ya nafsi yake alikuwa mtu mwingine kabisa. Nikaingia ndani ya chumba chake kilichojaa vitu vingi vya kisasa, tena vyote vya thamani kubwa na kwenda kukaa kwenye sofa dogo lililokuwa pembeni ya kitanda.
Japokuwa kimwili nilikuwa hapo lakini kiakili nilikuwa mbali sana. Nilianza kujiuliza kwamba yale yote yaliyokuwa yananitokea, yalikuwa na maana gani hasa? Nilifikia hatua hiyo baada ya kuona ni kama naishi kwenye ‘script’ fulani ambayo tayari maisha yangu yameshapangwa kwamba ni lazima nipitie hatua moja hadi nyingine kuelekea nisikokujua.
Hata mtu mwingine yeyote angeweza kufikiria hivyo kwa sababu kabla ya mfululizo wa mambo yote hayo, nilikuwa nikiishi maisha ya kawaida kabisa, nikifanya kazi kwa bidii nikiwa na ndoto nyingi maishani. Nilikuwa nikiishi kama kijana wa kisasa anavyotakiwa kuishi lakini kila kitu kilibadilika baada ya kukutana na Shenaiza.
Yaani ni kama nilikuwa nimelala na asubuhi kulipopambazuka kila kitu maishani mwangu kilikuwa kimebadilika. Nilimfikiria Raya na jinsi tulivyokuwa tukiishi naye kabla mambo hayajaanza kwenda mrama, nikamfikiria Shamila nilivyokutana naye nikiwa hospitalini na jinsi alivyotokea kunipenda na yote yaliyotokea mpaka muda huo ambao sasa nilikuwa kwenye himaya ya Junaitha, mwanamke ambaye hata sijui nimuelezee vipi.
Nilizinduka kutoka kwenye lindi la mawazo baada ya kusikia mlango ukifunguliwa, Junaitha akaingia huku akionesha kuchoka sana, nikamuona akiufunga mlango kwa funguo kisha akanisogelea pale nilipokuwa nimekaa.
“Nimechoka sana mume wangu,” alisema na kunibusu mdomoni, nikabaki nimeduwaa. Niliduwaa kwanza kwa kitendo chake cha kuniita ‘mume wangu’ kwa sababu kiumri alikuwa sawa na mama yangu mdogo au shangazi yangu lakini pia alinibusu mdomoni, miongoni mwa mambo ambayo yalikuwa yakiufanya mwili wake uwe kama umepigwa na shoti ya umeme.
“Yaani wewe pamoja na yote haya tuliyoyafanya pamoja bado tu hunizoei?” alisema baada ya kugundua kwamba nilikuwa nimepigwa na butwaa, nikajichekesha na kuvunga. Kiukweli baada ya kuuona upande wa pili wa Junaitha, nilikuwa hata sielewi mwanamke huyo ni mtu wa aina gani.
Kuna wakati hata nilikuwa nahisi kwamba hata kitendo cha mimi kujikuta nikifanya mapenzi na mwanamke huyo kilikuwa cha hatari sana kwa sababu kumbe alikuwa na uwezo mkubwa mno wa nguvu zisizoonekana kwa macho.
Kumbukumbu za tukio lililotokea muda mfupi uliopita la kumkamata yule mwanamke kichawi na kufanikiwa kumleta mle ndani, huku pia tukifanikiwa kulikimbia joka kubwa la kutisha katika ule ulimwengu wa giza, ziliufanya moyo wangu uwe na hofu kubwa mno.
“Leo umenifurahisha sana kwa sababu tumefanya kazi mbili kubwa ambazo zinatumia nguvu kubwa lakini katika zote, wewe ndiyo umekuwa kama steringi, si unaona wenzako hakuna aliyezinduka hata mmoja wakati hakuna kazi yoyote ya maana waliyoifanya?” alisema Junaitha huku akifungua vifungo vya blauzi yake na kuanza kuivua.
Wala hakuwa na wasiwasi wowote au hakuhisi aibu yoyote licha ya mimi kuwepo pale, akaivua na kuitupia kwenye kapu la nguo chafu, akabaki kifua wazi.
“Mbona unaniangalia hivyo wakati mimi nakusemesha mambo ya maana,” alisema huku akiachia tabasamu baada ya kugundua kuwa akili na mwili wangu havikuwa kwenye ushirikiano mzuri.
“Unajua mimi nina dharau sana kwa wanaume lakini sijui kwa sababu gani wewe nimetokea kukuamini na kukupenda ndani ya muda mfupi namna hii,” alisema huku akianza kuvua za chini, akatoa zote akiwa hana hata chembe ya wasiwasi, eti mimi ndiyo nikawa na kazi ya kukwepesha macho yangu kwa aibu mpaka alipochukua upande wa khanga na kujifunga.
“Hizi nguo ukishaenda nazo kule kwenye ulimwengu mwingine hutakiwi kuzivaa tena mpaka zifuliwe kwa maji yenye udi, mdalasini na karafuu, hebu acha ushamba wako,” alisema huku akinipiga kimasihara begani, akanishika mkono na kunisimamisha, akaanza kufungua vifungo vya shati langu.
“Si unaona unaelekea kupona, hebu sogea hapa ujiangalie,” alisema huku akilitazama vizuri jeraha langu la kifuani, nikasogea kwenye kioo na kujitazama. Ni kweli nilikuwa nimeanza kupona haraka kuliko hata nilivyotegemea.
Jeraha ambalo nilikaa kwa muda mrefu hospitalini lakini likawa bado hata haliponi, leo ndani ya saa chache tu lilikuwa likielekea kupona! Ilikuwa ni zaidi ya maajabu kwangu.
“Na pale mguuni alipokujeruhi yule mshenzi panaendeleaje?” alisema, nikataka nipandishe suruali juu ili nimuoneshe lakini badala yake, alinipa taulo na kuniambia nivue tu suruali kwa sababu kuna dawa nyingine alikuwa anataka tuitumie ili kutoa nuksi zote tulizotoka nazo kule kwenye ulimwengu wa giza.
Kwa jinsi Junaitha alivyokuwa anajua kunibembeleza kama mtoto mdogo, nilijikuta nikiishiwa na ile hofu iliyokuwa ndani ya moyo wangu, nikawa nafanya kila kitu alichonigiza. Muda mfupi baadaye, nilibaki na taulo tu, na yeye alibaki na upande wa khanga.
Akatembea kimikogo huku mwili wake uliojengeka vizuri kikekike ukitingishika kwa namna ya kuvutia sana, akaenda kufungua droo iliyokuwa pembeni ya kitanda, akatoa vichupa viwili vilivyokuwa na vitu kama mafuta, akanisogelea.
“Hii dawa inabidi ukaogee na hii ntakupaka tena kwenye kidonda chako, sawa baba’angu,” alisema huku akiwa amenisogelea sana, tukajikuta tumekumbatiana tena, tukagusanisha ndimi zetu.
“Nataka suala la yote tunayofanya mimi na wewe liwe siri yetu, umenielewa mume wangu,” alirudia tena kutamka neno lile, safari hii kwa sauti iliyokuwa inasikika kwa mbali kama mtu anayejilazimisha kuzungumza, nikaitikia kwa kutingisha kichwa, akanishika mkono na kunipeleka kwenye bafu la ndani ambapo alinielekeza namna ya kuogea ile dawa.
Cha ajabu, japokuwa yale mafuta hayakuwa na rangi, nilipoyajaribu kunawia mikono tu kama alivyonielekeza mwenyewe, nilishangaa mwili wangu ukitoa uchafu mwingi mweusi kama maji yaliyochanganywa na mkaa, nikawa nashangaa kwa hofu.
“Ule ulimwengu mwingine una mambo mengi machafu sana, usipojisafisha kwa hii dawa vizuri mwili mzima, unaweza kujikuta unabadilika na kuwa kiumbe wa ajabu sana,” alisema na kunifanya nishtuke sana.
“Oga fastafasta nakusubiri,” alisema huku akitoka na kuniacha bafuni, nikafanya kama alivyoniambia ambapo nilijipaka ile dawa mwili mzima na kusogea kwenye bomba la mvua, nikafungulia maji ambayo uchafu mwingi ulikuwa ukitiririka kutoka mwilini mwangu. Nilikaa kwenye maji kwa zaidi ya dakika tatu ndiyo uchafu wote ukaisha, nikashangaa ule uchovu wote niliokuwa nao umeyeyuka kama barafu juani.
Nikajifuta kwa taulo na kutoka mpaka chumbani ambako nilimkuta Junaitha naye ameshaenda kuoga, nadhani alitumia bafu la chumba kingine maana vyumba vingi ndani ya nyumba hiyo vilikuwa ‘self contained’, akanipokea kwa mabusu motomoto na kunitaka nijilaze kidogo pale kitandani kwake ‘tupunguze uchovu’.
Hata sijui nini kilitokea lakini muda mfupi baadaye, wote tulikuwa kama tulivyoletwa duniani, tukaianza safari tamu kwenye ulimwengu wa huba, ambayo lazima niwe mkweli, iliukonga mno moyo wangu, nikajikuta nimepitiliza na kuuchapa usingizi mzito.
“Jamal! Jamal! Amka, kuna tatizo,” sauti ya Junaitha ndiyo iliyonizindua kutoka kwenye usingizi fofofo, nikakurupuka nikiwana shauku kubwa ta kutaka kujua kumetokea nini tena.
Je, nini kitafuatia? Usikose
 
SEVEN DAYS IN HELL (Siku Saba Kuzimu)- 58
ILIPOISHIA:
“Yule kule aliyekuwa ananguruma kama mnyama ni nani?” Firyaal aliuliza swali, nikawaona wenzake wote wakitingisha vichwa, kuunga mkono swali hilo.
“Ni stori ndefu kidogo, ngoja nitawaeleza lakini njooni kwanza huku niwape dawa,” alisema.
SASA ENDELEA...

Wote wakamfuata mpaka kule kwenye kile chumba walichokuwa wamelala, akawaamuru wote wakae kwenye mkao wa kutengeneza duara, akatoka na kuelekea chumbani kwake, aliporudi muda mfupi baadaye, alikuwa na kichupa kidogo kilichokuwa na mafuta yaliyokuwa yananukia vizuri sana, akaanza kumpaka mafuta yale kichwani na usoni mmoja baada ya mwingine.
“Itabidi mkae dakika ishirini kisha mkaoge, baada ya hapo tutakamilisha kazi ya kumzindua Shenaiza, tumeelewana?”
“Mi nasikia njaa inaniuma sana.”
“Hatutakiwi kula chchote mpaka tukamilishe kwanza kazi hii, ukishakula tu utasababisha nguvu kubwa ambazo zinatakiwa kutumika kichwani mwako, zielekezwe tumboni kwa ajili ya mmeng’enyo wa chakula, jambo linaloweza kusababisha tukakwama, tumeshakula mbuzi mzima, hatuwezi kushindwa kumalizia mkia,” alisema Junaitha akimjibu Firyaal.
Wote walionesha kuelewa walichoambiwa na kwa sababu shauku ya kila mmoja ilikuwa ni kumuona Shenaiza akisimama tena, walikubaliana naye. Ilibidi mimi niwaache wakiendelea kusubiri hizo dakika ishirini ziishe, nikaenda kwenye chumba changu ambacho tangu niingie ndani ya nyumba hiyo nilikitumia kwa muda mfupi sana.
Kwa jinsi nilivyokuwa nikijisikia uchovu, nilipoingia tu, nilienda kujibwaga kitandani, nikawa najisikia jinsi mwili ulivyokuwa ukivuta kwa uchovu. Nilitulia nikitafakari mambo mengi ndani ya kichwa changu. Sikujua mwisho wa yote yale ungekuwa nini, nilishachoka kutangatanga, nilitamani haya mambo yafike mwisho ili nirudie maisha yangu ya kawaida kama zamani.
“Vipi umelala?”
“Hapana, nimejipumzisha tu,” alisema Junaitha huku akifungua mlango na kuingia ndani ya kile chumba. Nilijihisi kukosa amani kwa sababu nilijua kwa vyovyote, lazima akina Raya watamuona Junaitha akitoka chumbani kwangu na kuwafanya waanze kutuhisi vibaya.
Ni kweli alikuwa amenilambisha asali ambayo sikuwa tayari kuiacha lakini suala la tofauti ya umri kati yetu, lilinifanya niwe na aibu sana kuwa naye. Nilitaka kila kitu kati yetu kiendelee kuwa siri kwa sababu niliamini umebaki muda mfupi kabla ya kukamilisha mambo yote yaliyokuwa yametuelemea kisha kila mtu akaendelee na maisha yake.
Niliamini nitakuwa huru zaidi nikiwa kwangu ambapo kichwani nilishapanga kwamba mambo yakitulia tu, naenda kutafuta chumba sehemu nyingine na kuhama kabisa eneo lile.
“Najua umebaki na maswali mengi kuhusu kile ulichokiona kule ndani lakini halikuwa lengo langu kukuficha ndiyo maana nimekuja ili tuzungumze.”
“Ok sawa Junaitha lakini sidhani kama huu ni muda muafaka wa sisi kuzungumza, watatushtukia.”
“Usijali, nimewapa dawa maalum ya usingizi, hakuna atakayeamka sasa hivi, inabidi walale ili tupate nafasi nzuri ya kukamilisha hiki tulichokianza,” alisema Junaitha huku akinisogelea pale kitandani nilipokuwa nimelala, akanibusu kwenye paji la uso wangu na kunifanya nisisimke kiasi. Sikusisimka sana kama kawaida yangu kwa sababu ya uchovu na maswali mengi yaliyokuwa yakitembea ndani ya kichwa changu.
“Niulize chochote unachotaka kujua,” alisema huku naye akijilaza pembeni yangu, akawa anatazama juu kama mimi nilivyokuwa nimelala.
“Ndani ya kile chumba kuna nini?”
“Kuna vitu vingi vinavyohusu mambo ya kichawi.”
“Kwani wewe ni mchawi?” nilimuuliza swali ambalo lilimfanya ashushe pumzi ndefu, akajigeuza na kuwa ananitazama.
“Sisi sote ni wachawi ingawa tunatofautiana kiwango cha uchawi.
“Sikuelewi, una maanisha nini?”
“Sikupenda kukwambia hili lakini ngoja tu nikwambie, mimi hapa ninapoishi, ndipo alipokuwa anaishi marehemu baba yangu na mama yangu. Ndani ya familia yetu, sisi tulizaliwa watoto wawili tu, mimi na dada yangu aitwaye Munaitha, ambaye ndiyo mama mzazi wa Shamila, rafiki yako,” alisema.
“Hata hivyo, kwa kipindi kirefu kumbe baba yetu alikuwa akijihusisha na mambo ya kichawi bila sisi kujua, mpaka alipokuja kufariki ndiyo tukaja kuambiwa ukweli na marehemu mama yetu ambaye naye alifariki muda mfupi baadaye na kutuacha mimi na dada yangu tu.
“Kwa kuwa mambo ya kichawi lazima apatikane mtu wa kurithi mikoba, mimi ndiyo nilichaguliwa kurithi lakini kwa kipindi hicho, nilikuwa pia tayari nimeshafika mbali kwenye masomo ya utambuzi.”
“Masomo ya utambuzi? Ndiyo yapi?”
“Ni kama uchawi tu lakini wenyewe unafundishwa darasani, unatumika sana kwenye nchi za Magharibi. Utambuzi unakuwa ni kwa lengo la kujifunza kuhusu mwili wako na nguvu tunazozalisha, ziwe ni nzuri au mbaya na huu una nguvu kuliko hata uchawi wenyewe unaoujua.
“Kwa hiyo nikawa na nguvu mara mbili, uchawi wa darasani na uchawi mweusi ambao ndiyo huu wa kutumia matunguli, mafuvu na madawa ya kienyeji. Kile chumba ndiyo ilikuwa ofisi ya baba yangu, tangu aanze kuitumia, hakuna mtu mwingine yeyote aliyewahi kuingia zaidi ya mimi na sasa hivi wewe, wengine huwa wanaingia wakiwa mateka kama tulivyomfanya yule mshenzi.
“Kuna siri nyingi sana ndani ya kile chumba, kimsingi ni kama ikulu inayojitegemea,” alisema Junaitha, akawa ni kama amezidi kunichanganya. Nilianza kutafakari kwa kina kuhusu hicho alichoniambia kuwa ni uchawi wa darasani na uchawi mweusi. Nilitaka kujua mambo mengi kwa wakati mmoja kwa sababu kuna siku nakumbuka alituambia kuwa hata ukitaka kuingia benki na kuchukua fedha kisha ukatoka bila kuonwa, inawezekana.
“Najua una shauku ya kutaka kujua vitu vingi lakini usiwe na wasiwasi, kila kitu utakijua vizuri kabisa ilimradi umeshatua kwenye himaya yangu, kinachotakiwa hapa ni kushirkiana kwanza kulimaliza suala la Shenaiza,” alisema, na mimi nikashusha pumzi ndefu na kumgeukia.
“Muda unazidi kusonga mbele Junaitha na hakuna kinachoeleweka, nahitaji kurudi kwenye maisha yangu ya kawaida kama zamani,” nilimwambia, akaniambia nisiwe na wasiwasi mbona kila kitu kimeshakaribia mwisho!
Aliniambia kwamba tukishamaliza kazi ya kumzindua Shenaiza ambayo ingefanyika muda mfupi baadaye, tutaandaa mpango maalum wa kumkamatisha baba yake Shenaiza kwenye mikono ya dola ili kukomesha biashara hatari aliyokuwa anaifanya.
“Usione kama unapoteza muda, nakuhakikishia baada ya kufanikisha hili suala la kumkamata baba yake Shenaiza, utakuwa maarufu sana wewe, dunia nzima itakujua na kukuheshimu na huo ndiyo utakuwa muda mzuri wa wewe kuishi maisha unayotaka kwa sababu kichwa chako kinazalisha nguvu kubwa sana ambayo ina uwezo hata wa kuhamisha milima,” aliniambia.
Maneno yake yalinipa nguvu sana, akaniambia kwamba aliwalaza usingizi mzito kwa makusudi wale wengine ili tukamalizie kazi ya kumzindua Shenaiza lakini akanipa taarifa ambazo zilinishtua mno. Aliniambia baba yake Shenaiza amejizatiti vilivyo kwa nguvu za nje na ndani na ili tufanikishe azma yetu, ilikuwa ni lazima mtu mmoja kati yetu afe.
“Afe?”
“Ndiyo, lazima afe mtu kwenye kafara.”
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
 
The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 63
ILIPOISHIA:
“Nimepata salamu zako kwamba umechagua kuwa tajiri, ombi lako limekubaliwa lakini kuna masharti inatakiwa kabla siku zako saba hazijaisha, uwe umeshaanza kuyafuata, vinginevyo utakufa,” alisema yule mwanamke, macho yakanitoka pima.
SASA ENDELEA...

Nilijiweka vizuri pale chini nikiwa na shauku kubwa ya kutaka kusikia ataniambia nini, akanitazama machoni kisha akashusha pumzi ndefu na kunisogelea.
“Kwa nini umeamua kupita njia hii?” aliniuliza kwa sauti ya upole, nikashindwa kuelewa alikuwa anamaanisha nini.
“Unalingana na kijana wangu ambaye mwezi wa kumi na mbili angekuwa anatimiza miaka 21, makosa yangu yamesababisha niishi maisha ya kujuta kila siku, sitaki mtu mwingine apite njia kama niliyowahi kupita mimi na kusababisha nimpoteze mwanangu kipenzi,” alisema lakini wala maneno yake hayakuniingia akilini.
“Umeshawishiwa na mtu yeyote au ni maamuzi yako mwenyewe?”
“Nimeamua mwenyewe, wala hakuna aliyenishawishi.”
Kwa jinsi majibu yangu yalivyokuwa, yule mwanamke alishindwa kuendelea kunihoji maana nilishafikia uamuzi ndani ya moyo wangu na hakukuwa na jinsi yoyote ambayo ningebadilisha uamuzi huo.
“Unatakiwa kuwa makini sana na aina ya maisha utakayokuwa unaishi, hutakiwi kunywa pombe wala kuvuta sigara, hutakiwi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamke yeyote mpaka utakapooa, hutakiwi kulala kitandani, utakuwa unalala chini na hutakiwi kula nyama nyekundu, mengine ni ya vitendo zaidi, nisubiri,” alisema mwanamke huyo na kutoka.
Nilibaki nayatafakari yale masharti aliyonipa, sikuona jambo lolote la kunizuia kwa sababu kama ishu ya ulevi, sikuwa nakunywa pombe wala kuvuta sigara, achilia mbali bangi ingawa katika makuzi ya ujana, kuna wakati nimewahi kujaribu na kuishia kudhalilika.
Suala la uhusiano wa kimapenzi, nilichokuwa nimekiamua kutoka ndani ya moyo wangu, ni kwamba kama Rahma akikubaliana na mimi, nitamuoa awe mke wangu wa ndoa maana alikuwa na kila kitu nilichokuwa nakihitaji, achilia mbali tofauti yetu ya umri. Suala la kutolala kitandani, nalo pia halikuwa tatizo kwangu kwa sbaabu maisha yetu ya kule kijijini, tulishazoea kulala kwenye vitanda vya kamba au kulala chini kwenye mkeka kwa hiyo hilo pia halikuwa tatizo kwangu.
Suala la kula nyama nalo sikuona kama ni shida kwa sababu maisha ya kule kijijini kwetu, nyama tulikuwa tunakula siku za sikukuu au mara chache tunapoenda kuwinda, mboga yetu kubwa ilikuwa ni samaki.
Kimsingi masharti hayo aliyonipa, yalinifanya ile hofu yote niliyokuwa nayo kuhusu kumiliki utajiri, iyeyuke kama theluji iyeyukavyo juani, hamu ya kutamani kuwa na utajiri mkubwa, ikazidi kunijaa.
Moyoni nilijiambia kama masharti yenyewe ndiyo hayo, kwa nini wachawi wanaogopa kuwa matajiri? Wanachokiogopa ni nini hasa? Akilini nilianza kuvuta picha ya jinsi nitakavyokuwa ‘tajiri mtoto’, nikiendesha magari ya kifahari na kuishi kwenye majumba ya gharama kubwa.
Hata ule ushauri alionipa Mkuu pamoja na baba yake Rahma, kwamba kama nataka mambo yasiwe magumu kwangu, nisitamani kuwa na utajiri mkubwa, bali fedha za kawaida tu za kuniwezesha kuishi bila shida, niliutupilia mbali, tabasamu pana likachanua kwenye uso wangu.
Dakika kadhaa baadaye, yule mwanamke alirejea, nikashtuka kumuona akiwa na kisicho cha kawaida. Shingoni alikuwa amebeba nyoka mdogo aliyejiviringisha huku kichwa chake akiwa amekielekezea mbele, akamshika na kumshusha chini, akajiviringisha na kuinua kidogo kichwa chake.
Nilishtuka sana, kama nilivyowahi kueleza, pamoja na ujanja wangu wote, hakuna kitu nilichokuwa naogopa kama nyoka.
“Unashtuka nini? Huyu itabidi umzoee tu,” alisema yule mwanamke, nikawa nimekaa kwa tahadhari kubwa, nikimtazama kwamba akinisogelea tu nikimbie kuelekea nje. Cha ajabu, nilipomchunguza vizuri yule nyoka, alikuwa na madoadoa sawasawa na ya yule nyoka ambaye Mkuu alinichanja na kumlambisha damu yangu.
“Itabidi umtunze na kumheshimu kwa moyo wako wote, huyu ndiye atakayeamua hatima ya utajiri unaoutaka, kadiri anavyozidi kuwa mkubwa ndivyo unayoyataka yatakavyokuwa yanatimia,” alisema mwanamke huyo, bado nikawa najiuliza maswali mengi yasiyo na majibu.
“Unamshangaa kwani ndiyo mara yako ya kwanza kumuona? Hebu vua shati huko,” alisema mwanamke yule, ni hapo ndipo nilipoamini kwamba ni kweli nyoka yule ndiyo yuleyule aliyelambishwa damu yangu na Mkuu.
Nilivua shati, yule mwanamke anachukua wembe na kusogelea, akanichanja kwenye mbavu upande wa kushoto, damu zikaanza kunitoka kwa sababu alivyonichanja alikandamiza mkono, akamchukua yule nyoka ambaye sasa alikuwa akitoa ulimi wake na kuchezesha.
Akamsogeza mpaka pale kwenye jeraha langu, hofu niliyokuwa nayo ilikuwa haielezeki. Simulizi kuhusu nyoka nilizowahi kuzisikia, achilia mbali matukio niliyowahi kushuhudia jinsi watu na mifugo inavyopoteza maisha baada ya kung’atwa na nyoka, vilinifanya niwe mwoga sana kwa viumbe hawa.
Alipomsogeza tu kwenye jeraha, alijikunjua na kunigusa kwa ulimi wake, akaanza kuilamba ile damu kwa kasi kubwa. Muda mfupi tu baadaye, jeraha lilibaki kuwa alama tu, damu zote alizilamba nyoka yule na wala nyingine hazikuendelea kunitoka.
“Utamzoea tu wala usijali, si umeamua mwenyewe?” alisema yule mwanamke huku akitingisha kichupa chenye dawa ya majimaji, akanipaka pale kwenye jeraha kisha akamchukua yule nyoka, safari hii alimuingiza kwenye mfuko uliotengenezwa kwa kipande cha gunia, akatoka na kuniacha nikiwaza sana.
Nimewahi kusikia simulizi za watu waliokuwa wakifuga nyoka wakubwa ndani ya nyumba zao kwa ajili ya imani za kishirikina, sikutaka kuamini kwamba na mimi ndiyo naelekea kwenye maisha hayo, nikaanza kuelewa hatari iliyokuwa mbele yangu.
Hata hivyo, bado shauku ya kuwa tajiri haikuniisha, nilijipa moyo kwamba kama wapo watu ambao wanaweza, kwa nini mimi nishindwe? Muda mfupi baadaye, yule mwanamke alirejea na kuendelea kunielekeza mambo mbalimbali, yaani alivyokuwa akiongea na mimi ni kama tayari nimeshakuwa tajiri maana alikuwa akinipa masharti ya namna ya kutumia fedha.
Aliniambia hata niwe na fedha nyingi kiasi gani, sitakiwi kutoa kumpa mtu yeyote fedha siku za Jumatatu, Jumanne na Jumapili, akaniambia hata kama kuna mtu amepatwa na dharura kubwa na kiwango kidogo tu cha fedha kinaweza kumsaidia, sitakiwi kabisa kutoa hata shilingi kumi kwenye siku hizo alizonitajia.
Akaniambia pia kwamba katika siku hizo nilizokuwa na uwezo wa kutoa fedha, muda wa kutoa fedha kumpa mtu yeyote au kufanya kitu chochotye kinachohusiana na fedha, ni saa kumi na mbili jioni, kabla jua halijazama. Maelezo hayo yalinishangaza sana, nikawa najiuliza maswali mengi kichwani yaliyokosa majibu.
Baadaye, aliniambia kwamba natakiwa kurudi tena nyumbani kwake hapo baada ya siku sita kwa ajili ya kwenda kukamilisha baadhi ya mambo. Alinipa mkono na kunitakia maisha mema ya utajiri, mimi bado macho yangu yakawa kwenye ule mfuko aliomuweka yule nyoka mdogo.
Baadaye baba na baba yake Rahma walikuja kunichukua, wakamshukuru mwanamke huyo, tukatoka na safari ya kurejea nyumbani ikaanza. Tayari ilishagonga saa nane za usiku, tukawa tunatembea kwa miguu kuelekea kwenye barabara kubwa ya lami.
Kutoka nyumbani kwa mwanamke huyo mpaka kwenye barabara ya lami, kulikuwa na umbali mrefu sana na kibaya zaidi, ni kwamba tulikuwa tunapita kwenye pori kubwa ambalo kwa usiku ule lilikuwa likitisha sana.
Tukiwa tunaendelea kuchanja mbuga, baba akiwa mbele na baba yake Rahma akiwa nyuma, mara tulianza kusikia sauti za ajabu kutoka ndani ya pori lile, huku kukiwa na purukushani kubwa, mapigo ya moyo wangu yalilipuka na kuanza kunienda mbio kuliko kawaida.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
 
SEVEN DAYS IN HELL (SIKU SABA KUZIMU)- 59
ILIPOISHIA:
Maneno yake yalinipa nguvu sana, akaniambia kwamba aliwalaza usingizi mzito kwa makusudi wale wengine ili tukamalizie kazi ya kumzindua Shenaiza lakini akanipa taarifa ambazo zilinishtua mno. Aliniambia baba yake Shenaiza amejizatiti vilivyo kwa nguvu za nje na ndani na ili tufanikishe azma yetu, ilikuwa ni lazima mtu mmoja kati yetu afe.
“Afe?”
“Ndiyo, lazima afe mtu kwenye kafara.”
SASA ENDELEA...

“Sasa mambo ya makafara yanaingiaje tena hapa? Kama ni hivyo basi mimi najitoa.”
“Ukijitoa maana yake wewe ndiyo utakufa. Wasiwasi wa nini na wewe ni mwanaume? Hebu acha woga, nitakufundisha cha kufanya wala usiwe na wasiwasi,” alisema Junaitha lakini kiukweli alikuwa amenichanganya mno.
Mmoja kati yetu lazima afe? Nani sasa! Kama siyo mimi ni nani? Raya? Haiwezekani. Shenaiza? Hapana. Shamila? Noo! Au Firyaal? Nilijiuliza maswali mengi ambayo yote hayakuwa na majibu. Nilichokifanya ilikuwa ni kujaribu kupambana na hofu ambayo sasa ilikuwa inanitafuna ndani kwa ndani.
Hakuna kitu ambacho binadamu hawezi kukizoea kama kifo! Miaka yote watu wanakufa lakini kwa nini kila mtu anapokufa kunakuwa na msiba mzito kwa watu wanaomzunguka? Ni dhahiri kwamba kifo hakizoeleki.
“Mbona kama umepoteza umakini Jamal? Kwani wewe unaelewa nini kuhusu kifo?” aliniuliza Junaitha, swali ambalo lilinizindua kutoka kwenye lindi la mawazo.
“Kifo? Kifo si ni kufa?”
“Ndiyo ni kufa, unaelewa nini kuhusu kufa?”
“Mtu anakufa na huo ndiyo unakuwa mwisho wa maisha yake,” nilimjibu Junaitha, nikiwa nimemkodolea macho.
“Huna haja ya kuogopa kuhusu kifo kwa sababu kinachotokea inakuwa ni kuhama tu kutoka kwenye ulimwengu mmoja kwenda kwenye ulimwengu mwingine, ni kama hivi tu sisi tunavyofanya lakini tofauti yake ukifa unakuwa huwezi kurudia kwenye mwili wako lakini hakuna tofauti sana.”
“Sijakuelewa.”
“Utanielewa tu wala usiwe na haraka, sitaki kabisa kusikia ukiogopa kuhusu kifo, umenielewa?”
“Nitaachaje kuogopa Junaitha?”
“Sasa unaogopa nini? Mbona huogopi tunavyohama kutoka ulimwengu mmoja kwenda mwingine?” alisema Junaitha lakini bado alichokuwa anakisema hakikuingia kabisa akilini mwangu.
“Hebu tuachane na haya mambo kwanza, tuna kazi kubwa mbele yetu,” alisema, akanibusu mdomoni, nikashusha pumzi ndefu na kuinuka pale tulipokuwa tumelala, naye akainuka, tukatoka na kuelekea kwenye chumba alichokuwa amelala Shenaiza.
“Hebu niambie ukweli, hujawahi kufanya mapenzi na huyu msichana kweli?” Junaitha aliniuliza, akimaanisha Shenaiza, nikamjibu kwa kutingisha tu kichwa.
“Hebu nitazame usoni,” alisema Junaitha lakini sikutaka kumtazama kwa sababu ambazo nazijua mwenyewe.
“Kwa nini tusimalize kazi kwanza halafu hayo mengine yatafuata baadaye?” nilisema huku nikionesha kutofurahishwa na swali lake, ilivoonesha naye hakutaka kuniudhi kwani alibadilisha mada haraka.
“Simama kwa kule,” aliniambia, akinioneshea upande uliokuwa na miguu ya Shenaiza, nikafanya kama alivyoniambia. Yeye alisimama upande wa kichwani kwa msichana huyo, akapiga magoti na kunitaka na mimi nifanye hivyohivyo.
“Katika vidole vyako kumi vya mikono, nataka kila kimoja kiguse kidole cha Shenaiza na ushikilie hivyohivyo, usiachie,” aliniambia, nikafanya kama alivyoniambia. Kweli nilishika vidole vyote vya Shenaiza, nikawa namtazama Junaitha kusubiri maelekezo zaidi.
“Fumba macho,” alisema Junaitha na kusisitiza kwamba nisimuachie vidole wala nisifumbue macho, nikamsikia akianza kuongea maneno ambayo hata sijui ni ya lugha gani au yalikuwa yakimaanisha nini, akaendelea kuyarudiarudia na kadiri alivyokuwa anazidi kuongea ndivyo sauti yake ilivyoanza kuwa ya kutisha, ikawa inasikika kama ile aliyoitoa kule kwenye ulimwengu mwingine ambayo ama kwa hakika ilikuwa ikitisha.
Nilianza kuhisi vitu kama upepo mkali ukivuma mle ndani, sikuelewa umetokea wapi, ukabadilisha na kuanza kuwa kama kimbunga kikali, vitu vikawa vinapeperushwa huku na kule. Upepo ulizidi kuwa mkali, Junaitha naye aliendelea kuyarudiarudia maneno yake kwa ukali, mara ikaanza kusikika miungurumo ya ajabu mle ndani, ikafuatiwa na radi kubwa iliyopiga kwa nguvu kubwa mno, nilijikuta nikipoteza mwelekeo, nikarushwa mpaka ukutani, nikajibamiza na kudondoka chini.
Ninachoshukuru ni kwamba sikufumbua macho kama Junaitha alivyoniambia, nikajikuta nimepoteza fahamu, nikawa sielewi kinachoendelea.
“Wewe ni nani?”
“Na wewe ni nani?” nilijikuta nikirejewa na fahamu lakini nusunusu, jitu kubwa ambalo sikuweza kuona mwisho wake, lilikuwa limesimama mbele yangu, likiniuliza kwa sauti nzito. Cha ajabu, eti wala sikuogopa chochote na badala ya kujibu, na mimi nikaliuliza swali.
“Kwa nini mnaingilia mambo yasiyowahusu? Mnamjua huyu binti? Kwa nini mnataka kumsaidia?”
“Na nyie kwa nini mnamtesa? Si ameshawaambia hataki kushirikiana nanyi?”
“Wewe ndiyo unamsemea? Kwa nini asiseme mwenyewe?”
“Nasema mwenyewe sasa, sitaki kushirikiana na nyie, Jamal nisaidie baba?” sauti ambayo niliitambua vyema kwamba ni ya Shenaiza ilisikika lakini nilipogeuka huku na kule, sikumuona zaidi ya lile jitu.
“Unasemaje wewe?”
“Nimesema sitaki kushirikiana na nyie, niacheni na maisha yangu,” sauti ya Shenaiza ilisikika tena, ghafla ikasikika tena radi kali ambayo safari hii niliona kama imepiga jirani kabisa na pale nilipokuwa.
Fahamu zikanirudia vizuri, nikajikuta nimelala sakafuni, huku Shenaiza akipiga kelele kwa nguvu pale kitandani, Junaitha akikazana kumtuliza.
“Njoo unisaidie Jamal, inuka njoo,” alisema Junaitha, nikainuka pale sakafuni kwa kujikongoja, nikasogea pale nilipokuwa nimesimama awali, Junaitha akaniambia nimshikilie Shenaiza ambaye alikuwa akirusha miguu na kutapatapa.
“Tulia Shenaiza, kila kitu kitakuwa sawa,” alisema Junaitha, msichana huyo ambaye muda wote alikuwa amefumba macho, alifumbua na ghafla akawa ni kama amezinduka, macho yake yakatua kwangu.
“Jamal!”
“Shenaiza.”
“Hapa ni wapi na nimefikaje?”
“Ooh! Ahsante kazi imekamilika,” alisema Junaitha huku akimuachia Shenaiza, akawa anajifuta jasho jingi lililokuwa linamtoka.
“Na huyu ni nani?”
“Tulia Shenaiza, kwanza pole kwa yote yaliyokutokea, pumzika kwanza utajua kila kitu,” nilimwambia, akawa bado ni kama ana mawenge, akawa ananitazama mimi, anamtazama Junaitha, anakitazama kile chumba, anajitazama yeye mwenyewe katika namna ya kushangaa sana.
“Inabidi nikamuogeshee maji ya maiti, amka binti,” alisema Junaitha na kumshika mkono Shenaiza ambaye bado alikuwa ameduwaa. Kiukweli hata mimi nilikuwa na maswali mengi sana lakini ilibidi nijikaze ili Shenaiza atulie. Nilishangaa kwamba iweje ndani ya muda mfupi tu namna hiyo, kutokee mambo ya kutisha kiasi kile mle ndani halafu watu waliopo nje wasijue chochote?
Nini kimefanyika mpaka Shenaiza ambaye kwa siku kadhaa alikuwa amepoteza kabisa fahamu, leo arudiwe na fahamu zake kama hakuna kilichotokea? Wanaosema uchawi haupo, nawapa pole. Uchawi upo na una nguvu kwelikweli.
“Njoo kwanza Jamal,” alisema Shenaiza baada ya kuwa ameshasimama kwa msaada wa Junaitha, mwili wake ukiwa hauna nguvu kabisa. Nilimsogelea, akanikumbatia kwa nguvu na kunibusu mdomoni, tukio ambalo Junaitha alilishuhudia ‘laivu’.
“Nakupenda sana, naamini wewe ndiyo umeyapigania maisha yangu mpaka muda huu,” alisema, nikamuona Junaitha akimshika mkono bila kusema kitu na kuanza kumvuta kuelekea bafuni.
Mate ya Shenaiza yalikuwa machungu kuliko klorokwin, nikawa najikaza tu huku nikijitahidi kuachia tabasamu kwenye uso wangu. Junaitha alimkokota mpaka bafuni na kufunga mlango kwa ndani, nikabaki nimesimama pale koridoni.
Ghafla nikaanza kusikia sauti ya Firyaal akilia kama mtu anayekabwa na kitu, nikakurupuka mpaka kwenye kile chumba walichokuwa wamelala wote, nikafunga breki za ghafla mlangoni, nikiwa siamini kile nilichokuwa nakiona.
Je, nini kitaendelea? Usikose next issue.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom