Makapuku Forum

Makapuku Forum

Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na hatia) - 5
ILIPOISHIA:
MWANAUME mzee mwenye macho mekundu sana na midomo myeusi, akiwa amejifunga shuka refu lenye rangi nyekundu na nyeusi, kichwani akiwa amejifunga kitambaa cheusi, shingoni akiwa na hirizi kadhaa na shanga, alisimama na kunyoosha juu mkia wa mnyama ambaye sikuwa namjua, watu wote wakashangilia kwa nguvu.
SASA ENDELEA...

“Sina mengi ya kuzungumza, naomba ushirikiano wenu tuwakomeshe wachawi wa kijiji hiki,” alisema mwanaume huyo kwa Kiswahili kibovu, watu wakashangilia tena kwa nguvu kisha Mwene akaendelea na maelezo, akisisitiza kwamba kazi lazima ianze siku hiyohiyo usiku.
Baada ya maelezo marefu yaliyojaa vitisho kwa watu waliokuwa wakitajwa kuhusika na uchawi, mkutano uliahirishwa, watu wakatawanyika huku kiongozi huyo wa kijiji akiwataka watu wote kutoa ushirikiano kwa mganga Mabwanji atakapoenda kuwatembelea kwenye nyumba zao.
Hofu niliyokuwa nayo ilikuwa kubwa mno, kwa jinsi watu walivyokuwa wanatuchukia pale kijijini nilijua lazima moto utawaka. Baadhi ya wazee waliokuwa wanaheshimika pale kijijini, walianza maandalizi ya kumsaidia mganga huyo kwa kila alichokuwa anakihitaji, dawa zikaandaliwa na hatimaye muda uliokuwa ukisubiriwa na wengi ukawadia.
Saa tatu juu ya alama usiku, kazi ya kuzunguka kwenye nyumba za watu waliokuwa wakishukiwa kuwa wachawi ilianza, kutokana na jinsi nilivyokuwa na shauku kubwa ya kutaka kuona kazi hiyo inavyofanyika, nilichomoka nyumbani kimyakimya na kwenda kushuhudia licha ya kwamba baba alitutaka wote tukae ndani kwa sababu siku hiyo ilikuwa mbaya kwa familia yetu.
Mtu wa kwanza kufuatwa alikuwa ni mwanamke mjane ambaye tulizoea kumuita mama Chinga, Mmakonde kutoka Kusini ambaye alikuwa akifanya kazi ya kupika pombe za kienyeji.
Kwa kipindi kirefu nilikuwa nikisikiasikia kwamba eti mwanamke huyo alikuwa akitumia viungo vya binadamu kupikia pombe zake ndiyo maana alikuwa na wateja wengi sana hapo kijijini. Tangu nikiwa mdogo niliaminishwa kwamba eti ule ambao huwa tunaona kama ni mwiko mkubwa anaoutumia kukorogea mapipa yake ya pombe, ulikuwa ni mkono wa binadamu.
Watu hao walipofika, huku ngoma ikipigwa na pembe za wanyama zikipulizwa, kila mtu akiwa ameshika tochi za kienyeji ambazo hutengenezwa kwa kuviringisha matambara mbele ya kipande cha mti kisha kuchovya kwenye mafuta ya taa, nyumba yake ilizungukwa kisha mganga akaanza kazi yake.
Akawa anafanya uchawi wake pale, mara afukue kwenye kona ya nyumba na kutoa hirizi kubwa, mara afukue pembeni ya mlango na kutoa fuvu la mnyama wa ajabu, yaani ilikuwa ni patashika nguo kuchanika.
Mwanamke huyo na yeye akatolewa na kukalishwa chini, mbele ya nyumba yake, akapakwa unga mweupe kichwani na kuanza kunyolewa nywele huku ngoma zikiendelea kupigwa, mganga akawa anaimba nyimbo za ajabu na kumtolea vitisho vingi mwanamke huyo kwamba akirudia tena kujihusisha na uchawi lazima atakufa.
Baada ya zoezi hilo lililochukua karibu saa zima, watu wote waliondoka na kumuacha mwanamke huyo akilia kwa uchungu, huku akiendelea kusisitiza kwamba yeye siyo mchawi wala haujui uchawi. Safari ya kuelekea kwenye nyumba nyingine ikaanza, na mimi nikawa nawafuata kwa nyuma.
Cha ajabu, niliwaona wakielekea nyumbani kwetu, mapigo ya moyo yakawa yananienda mbio kuliko kawaida, sikujua mwisho wake utakuwaje. Walipofika, walifanya kama walivyofanya kwa yule mwanamke, wakaizunguka nyumba yetu huku wakiimulika na tochi za kienyeji, ngoma ikawa inapigwa huku mganga akiimba nyimbo ambazo hakuna aliyekuwa anazielewa.
Akawa anazunguka huku na kule kama anayetafuta kitu fulani pale nje kwetu, ghafla nikaona mlango ukifunguliwa, baba akatoka kwa kasi na kuwapita watu wote, akasogea mpaka pale yule mganga alipokuwa amesimama, wakawa wanatazamana.
“Ni nani aliyekupa mamlaka ya kuingia kwenye miji ya watu na kutapeli ukijifanya unawatoa watu uchawi?”
“Wewe ni nani wa kunihoji maswali hayo? Wewe ni mchawi na wanakijiji wenzako wamekuchoka hapa kijijini. Hii safari ya ujio wangu ni kwa ajili yako, lazima nikunyooshe.”
“Wewe bado ni mwepesi sana kwangu, huna ubavu wa kushindana na mimi. Isitoshe mimi siyo mlozi kama wewe, mimi ni mtaalamu, tena gwiji,” alisema baba kwa sauti ambayo niliisikia vizuri kisha baada ya hapo akageuka na kurudi ndani, nikamuona yule mganga akivuta na kutoa pumzi ndefundefu kama anayejiandaa kufanya tukio moja kubwa sana.
Alipoingia ndani na kufunga mlango, huku nje yule mganga aliendelea kuzunguka huku na kule, wasaidizi wake wakawa wanampigia manyanga na kumuimbia nyimbo ambazo walizielewa wenyewe.
“Inatakiwa tumkamate kwa nguvu na kumtoa nje, anaonyesha ni jeuri sana,” alisema mganga huyo kwa Kiswahili kibovu, watu wote wakawa wanatingisha vichwa kuonyesha kukubaliana na alichokuwa anakisema.
Nilijikuta nikitetemeka sana pale nilipokuwa nimejibanza, nikajua arobaini za baba zilikuwa zimewadia. Japokuwa bado sikuwa na majibu kamili kichwani mwangu kama baba ni mganga au mchawi, bado sikukubaliana na kitendo alichokuwa anataka kufanyiwa kwa sababu ulikuwa ni udhalilishaji wa hali ya juu.
Wakati kundi la wanaume wakijiandaa kuingia ndani kwa nguvu na kuvunja mlango, nilimuona baba akitoka kwa kujiamini, kifua akiwa amekitanguliza mbele na kusimama tena mbele ya mganga, wale watu wote wakamzunguka kisharishari.
“Mnataka kutumia nguvu kunikamata? Hivi mna akili timamu nyie? Haya mwenye ubavu anyooshe mkono wake na kunigusa,” alisema baba kwa hasira. Nilibaki namshangaa baba kwani sikujua amepata wapi ujasiri wa kiasi kile. Kauli hiyo iliwashtua hata wale watu waliokuwa wanataka kumkamata, nikaona wote wakirudi nyuma lakini mganga aliendelea kusisitiza kwamba ni lazima wamkamate kwa nguvu.
Watu wote walipojaribu kufanya hivyo, tulishtuka kuona kimbunga kikubwa ambacho hata sikujua kimetokea wapi, kikianza kuvuma kwa nguvu pale baba alipokuwa amesimama, vumbi jingi na takataka za kila aina zikawa zinarushwa huku na kule, kufumba na kufumbua, baba hakuwepo tena eneo hilo.
Wale watu wote, akiwemo na mganga mwenyewe, walibaki wamepigwa na butwaa, kila mmoja akawa anajifuta vumbi. Sikuwahi kushuhudia kimbunga kikubwa kikitokea, tena usiku kama ule, nikabaki na maswali mengi yaliyokosa majibu.
“Ametukimbia! Ametukimbia!” alisema yule mganga kwa sauti ya juu, huku na yeye akionyesha dhahiri kuwa na taharuki kubwa ndani ya moyo wake.
“Siwezi kuwakimbia kwa sababu hakuna wa kunitisha hata mmoja kati yenu,” ilisikika sauti ya baba kisha nikashangaa kumuona akitokea gizani na kurudi tena pale alipokuwa amesimama awali, nikaona watu wote wakianza kurudi nyuma kwa hofu kubwa kwa sababu walishajua baba anaweza kufanya chochote muda wowote.
“Nataka hili liwe funzo kwako na kwa watu wengine wenye akili kama zako,” alisema baba kwa kujiamini huku akiendelea kumsogelea yule mganga, akafanya ishara kama ananyonga kitu kwa nguvu, kufumba na kufumbua mganga yule alidondoka chini na kuanza kutapatapa kama anataka kukata roho.
Kuona hivyo, watu wote waliokuwa wameandamana na mganga huyo, walitimua mbio, kila mmoja kuelekea njia yake na muda mfupi baadaye, wote walikuwa wametokomea gizani, ikabidi nitoke pale nilipokuwa nimejibanza huku na mimi nikiwa na hofu kubwa ndani ya moyo wangu.
“Hebu beba huko miguuni tuutoe huu mzoga hapa,” alisema baba, akimaanisha tumtoe yule mganga.
Huku nikitetemeka nilisogea mpaka pale yule mganga alipokuwa amelala, akiendelea kukoroma kwa nguvu, mimi nikamshika miguuni na baba akamshika kichwani, tukaanza kumkokota kumtoa nje ya eneo letu, tukaenda kumbwaga pembeni kabisa kwenye vichaka kisha tukarudi ndani. Ile tunaingia ndani tu, tukasikia mlango ukigongwa kwa nguvu.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
 
Tena si kidogo, nilijitahidi kuweka bati juu ya vigae lakini wapi bhana watu wanajumlisha moja na mbili wanapata tatu watashindwa kutofautisha ngao ya kidonge na ngao ya maji

Ha hahahahaha
Ila nyie kibokoo

Hivi wewe ndo ulimshauri binamu wako mpendwa wa aunt yako azame ndani na hii??
43c3d5584ddce8dbaabc1eda1f426142.jpg


yako ninayo
 
Seven Days In Hell (Siku Saba Kuzimu)- 6
ILIPOISHIA:
Mara simu yake ilianza kuita mfululizo, akaishika na kutazama namba ya mpigaji lakini katika hali ambayo sikuielewa, aliiachia simu hiyo, ikadondoka chini na kufunguka betri ikaangukia kivyake, mfuniko kivyake na simu nayo kivyake. Akaanza kuangua kilio kwa uchungu huku akiniomba nimsaidie, nilibaki nimepigwa na butwaa.
SASA ENDELEA…

“Nikusaidie nini Shenaiza?” nilimuuliza huku nikiiokota ile simu na kuiunganisha upya.
“Nakuomba usiniache, fanya kila kinachowezekana unitoroshe hapa hospitalini usiku huuhuu, watakuja kunimalizia,” alisema msichana huyo na kuzidi kunichanganya.
“Watakuja kukumalizia? Akina nani? Na Kwa nini tutoroke wakati hali yako bado siyo nzuri?”
“Naomba ufanye nilichokuomba mengine utaenda kuyajua mbele ya safari,” alisema msichana huyo huku akiendelea kulia.
Nikiwa bado nimeduwaa, nikiwa sijui cha kufanya, nilishtuka kumuona akichomoa sindano ya dripu aliyokuwa amechomwa mkononi mwake na kusababisha damu zianze kumtoka mkononi, akajikongoja huku akionesha kuwa na maumivu makali, akanitaka nimpe bega langu ili apate balansi ya kutembea.
Sikuwa na cha kufanya zaidi ya kukubaliana na matakwa yake, japokuwa nilikuwa najua kwamba ninachokifanya ni hatari sana lakini sikuwa na namna zaidi ya kumsaidia msichana huyo ingawa mpaka muda huo sikuwa najua nini kinachomsumbua.
Huku damu zikimvuja na kudondokea sakafuni, nilimsaidia kutembea, tukatoka mpaka nje ya wodi hiyo huku mara kwa mara nikigeuka nyuma kutazama kama hakuna mtu aliyekuwa akitufuatilia.
Kwa bahati nzuri, kwa kuwa muda ulikuwa umeenda sana, madaktari wengi walishaondoka sambamba na manesi ambapo waliosalia walikuwa ni wale wenye ‘shift’ ya usiku ambao nao hawakuwa wengi.
“Heeei! Mnakwenda wapi usiku wote huu,” mwanaume wa makamo ambaye bila hata kuuliza tulijua ni mlinzi wa hospitali hiyo kutokana na kuvalia sare huku mkononi akiwa na kirungu, alituuliza huku akifunga geti la kutokea nje.
Ilibidi nimdanganye kwamba nilimleta mgonjwa wangu kutibiwa majeraha aliyoyapata kwenye ajali lakini hatukumkuta daktari kwa kuwa alishaondoka, nikamdanganya kwamba tunaenda kujaribu kwenye hospitali nyingine lakini hakutaka kuelewa. Akasema hawezi kuturuhusu kutoka mpaka tupate kibali kutoka kwa daktari aliyekuwa zamu usiku huo.
Shenaiza ni kama alijua kilichokuwa ndani ya akili yangu kwani alianza kuugulia kama anayesikia maumivu makali, nikatumia kigezo hicho kuendelea kumshawishi yule mlinzi aturuhusu na alipozidi kukomaa, nilichomoa noti moja ya shilingi elfu kumi na kumshikisha, nikamuona akiachia tabasamu na kututaka kuwa makini.
Akafungua geti ambapo breki ya kwanza ilikuwa ni kwenye kituo cha teksi kilichokuwa nje ya hospitali hiyo, tukaingia kwenye teksi moja na kuondoka huku nikimuelekeza dereva kutupeleka nyumbani kwangu, Mikocheni.
Kwa kuwa ulikuwa ni usiku na hakukuwa na foleni, haikutuchukua muda mrefu tukawa tayari tumeshawasili Mikocheni, nilipotaka kumlipa dereva teksi fedha zake tulizokubaliana, Shenaiza ambaye muda wote alikuwa amejilaza huku kichwa chake akiwa amekiweka kwenye mapaja yangu, aliniambia nisilipe.
“Nina fedha za akiba kwenye pochi yangu ndogo, hebu fungua,” aliniambia, kweli nikafungua pochi yake ndogo aliyokuwa ameiweka kwenye mfuko wa gauni refu alilokuwa amelivaa. Nilipoifungua, nilishangaa kukuta kuna noti kadhaa za dola miamia za Kimarekani na noti mbili za shilingi elfu kumi, zote mpya.
Nikatoa na kumpa dereva na kutaka kurudisha pochi mahali pale lakini aliniambia kwamba nikae nayo mimi, nikakubali na kuiweka kwenye mfuko wa suruali niliyokuwa nimeivaa.
Wakati wa kushuka, kama ilivyokuwa wakati wa kupanda, ilibidi yule dereva teksi anisaidie kumtoa Shenaiza ambaye bado alikuwa akiugulia maumivu makali, akapitisha mkono wake kwenye bega langu na nikawa namsaidia kutembea kuelekea ndani kwangu.
Nilifungua mlango na kumkaribisha ndani, japokuwa alikuwa kwenye maumivu makali, nilimuona akiachia tabasamu hafifu kisha akanisifia: ”Mh! Jamani wewe msafi hadi raha, inatakiwa umpate mwanamke msafi kama wewe ndiyo awe mke wako ndiyo mtaendana,” alisema huku akikodolea macho huku na kule ndani ya sebule yangu.
Japokuwa sikuwa nimeoa lakini hakuna kitu nilichokuwa nakipenda kama kuiweka nyumba yangu katika hali ya usafi, kuanzia sebuleni mpaka chumbani huku nikinunua vitu vingi vya kisasa.
Nilimsaidia Shenaiza kukaa pale sebuleni kwenye sofa kisha nikamvua viatu alivyokuwa amevaa pamoja na koti alilovaa juu ya gauni lake na mtandio aliokuwa amejizibia lile jeraha la kichwani.
“Shenaiza mwenzio naogopa kulala na wewe ukiwa kwenye hali hiyo, ukizidiwa usiku itakuwaje? Kwa nini tusiende hospitali nyingine? Hapa siyo mbali na Hospitali ya Kairuki,” nilimwambia lakini alikataa katakata na kuniambia kwamba hospitalini haikuwa sehemu salama kwake kwa wakati huo.
“Basi kuna rafiki yangu anaishi hapo mtaa wa pili ni daktari lakini bado hajaajiriwa, anafanya ‘field’ hapo Kairuki, unaonaje nikamuite aje kutusaidia?”
“Hapana usijali, nitakuwa sawa kwa sababu kama ni damu nimeshaongezewa ya kutosha, ondoa hofu,” alisema huku akiinua mkono wake taratibu na kunigusa kwenye shavu langu la upande wa kushoto, akawa ananivutia pale alipokuwa amekaa.
Kwa tahadhari kubwa nikiogopa nisije nikamtonesha majeraha yake, niliulanisha mwili wangu, akanivutia mpaka nilipomsogelea kabisa, akanibusu kwenye shavu langu na kuninong’oneza.
“Ahsante sana kwa msaada wako, ni Mungu pekee ndiye atakayekulipa, upo tofauti sana,” nilitabasamu na kumtazama, macho yetu yakagongana, naye akaachia tabasamu hafifu.
Kwa kuwa sikuwa nimekula chochote, ilibidi nimuage kwamba naenda kubahatisha kama nitapa chipsi kwenye banda lililokuwa mtaa wa pili kutoka pale nilipokuwa naishi. Nilitoka huku Shenaiza akinisisitiza niwahi kurudi pia nifunge mlango kwa nje ikiwa ni pamoja na kuzima taa zote. Sikujua kwa sababu gani bado alikuwa na hofu kubwa kiasi hicho. Nilifanya kama alivyoniambia na kutoka, nikafunga mlango kisha nikafunga na geti la chuma kwa nje na kuondoka kuelekea mtaa wa pili.
Kwa bahati nzuri nilikuta bado hawajafunga, nikaagiza chipsi sahani mbili na vipande vya kuku kwani nilitaka nikambembeleze Shenaiza naye ale japo kidogo. Dakika kadhaa baadaye chakula changu kilikuwa tayari, nikalipa na kuanza kuondoka huku nikijitahidi kutembea haraka kwani nilipoteza muda mwingi pale kusubiria chakula.
Katika hali ambayo sikuitegemea, nilipotokeza kwenye uchochoro wa kuelekea kwangu, kwa mbali niliwaona wanaume kama watatu hivi wakiwa wamesimama mlangoni kwangu, mmoja akiwa anagonga mlango kwa nguvu.
“Mungu wangu, akina nani tena hao usiku wote huu?” nilijiuliza huku nikirudi nyuma na kujibanza pale uchochoroni, nikawaona wale wanaume wakiendelea kugonga mlango kwa nguvu. Ugongaji wao ulionesha dhahiri kwamba hawakuwa wamekuja kwa heri, nikawa natetemeka nikiwa sijui nitafanya nini.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
 
Graves of the Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 7
ILIPOISHIA:
WALE wageni waliaga na kuondoka, baba akatuita tena ndani na kuanza kuhesabu fedha zilizopatikana. Zilikuwa ni shilingi milioni mbili na laki tatu, akasema zingetosha kabisa kwa safari yetu. Tukakubaliana kwamba tumalizie maandalizi na asubuhi ya siku ya pili tuianze safari ya kuelekea jijini Dar es Salaam.
SASA ENDELEA...

KWELI usiku huo hakuna hata aliyepata lepe la usingizi, ‘kimuhemuhe’ cha safari kilitufanya tukae macho mpaka jogoo la kwanza lilipokuwa linawika. Baba alituagiza kwamba tubebe vile vitu vya muhimu tu kwa sababu maisha ya kijijini yalikuwa tofauti sana na maisha ya mjini.
Akatuambia vitu vingine tuviache palepale na vitakuwa salama kwa sababu kuna walinzi anawaacha kwa ajili ya kutulindia mji wetu. Aliposema walinzi sikumuelewa kwa haraka anamaanisha nini, akili nyingine zikanituma kuamini kwamba labda watakuwa ni mgambo lakini nilijiuliza anaweza kuwaacha mgambo ndiyo walinde nyumba yetu wakati hawakuwa wakielewana? Sikupata majibu.
Saa kumi na nusu za usiku, tulitoka na kuanza kutembea kuelekea stendi, kila mmoja akiwa na mzigo wake. Tukaenda mpaka stendi ambapo tulipanda gari la kwanza kabisa ambalo lilikuwa likielekea Mbeya mjini, lakini cha ajabu, wakati wote tumeshapanda kwenye gari, baba yeye alibaki chini.
Tukawa tunasubiri na yeye apande lakini hakufanya hivyo, sanasana tukamuona akiwa anazungumza na mama, kupitia dirisha la gari lile tulilokuwa tumepanda, nadhani alikuwa akimpa maelekezo muhimu sana kwa sababu muda wote mama alikuwa akitingisha kichwa kuashiria kuelewa kile alichokuwa akiambiwa.
Baada ya kumaliza kuzungumza na mama, baba alikuja moja kwa moja pale nilipokuwa nimekaa mimi, akanipa mkono na kuniambia kwamba tutangulie yeye atafuata, akaniambia ananiamini mimi zaidi kwa hiyo lazima niwe makini kuwalinda ndugu zangu.
Nilijisikia fahari sana kwa jinsi baba alivyokuwa akinipa kipaumbele kwenye mambo ya msingi japokuwa nilikuwa na kaka zangu na mimi ndiyo nilikuwa mdogo. Baada ya dakika chache, dereva aliingia ndani ya gari, akawasha na safari ya kutoka Makongorosi kuelekea Mbeya mjini ikaanza.
Safari haikuwa nyepesi, kwa sababu sehemu kubwa ya njia ya kutokea Chunya kuelekea Mbeya mjini, ni milima na mabonde makubwa, ikiambatana na miteremko ambayo kama dereva hayupo makini hamuwezi kufika salama. Ukizingatia na lile giza la alfajiri ile, kila mmoja alikuwa akiomba moyoni tufike salama. Baada ya safari ndefu, hatimaye tuliwasili Mbalizi, gari likashusha baadhi ya abiria na kuingia Barabara Kuu ya Mbeya-Tunduma ambayo ni ya lami, likaendelea na safari ya kuelekea Mbeya Mjini.
Nikiri kwamba hiyo ndiyo ilikuwa mara yangu ya kwanza kufika mjini na kila kitu kwangu kilikuwa kigeni. Sikuwahi kuona barabara ya lami, sikuwahi kuona magari mengi ya kila aina wala sikuwahi kuona nyumba nzuri na za kisasa, nyingine zikiwa na maghorofa.
Ilikuwa ni safari ambayo iliufurahisha mno moyo wangu, nikawa nachekacheka tu mwenyewe. Hali ilikuwa hivyohivyo kwa ndugu zangu wengine ambao nao walikuwa na ushamba ulioonekana waziwazi kwenye sura zao. Safari yetu ilienda kuishia kwenye Stendi Kuu ya Mabasi ya Mbeya au maarufu kama Mbeya Terminal.
Cha ajabu, wakati gari likikata kona kuelekea sehemu ya kushushia abiria, nilimuona baba akiwa chini, akilitazama gari tulilokuwa tumepanda. Nikabaki na maswali mengi yasiyokuwa na majibu, kwamba alifikaje kabla yetu? Kumbukumbu zangu zilinionyesha kwamba kule Chunya, stendi kulikuwa na gari moja tu ambalo ndiyo hilo ambalo sisi tulipanda.
Na safari nzima, hatukupitwa na gari lingine lolote, wala chombo kingine cha usafiri, si bodaboda wala Bajaj, sasa baba alifikaje pale kabla yetu? Yalikuwa ni maswali ambayo sikuwa na majibu yake. Lakini cha ajabu, nilipomgeukia mama wala hakuonyesha kushtushwa na uwepo wa baba eneo lile, nikamuona akimpungia mkono kama anayemwambia ‘tuko hapa’.
Gari liliposimama, baba ndiye aliyekuwa akitupokea mizigo, ndugu zangu wote walionekana kuchukulia uwepo wa baba eneo lile kama kitu cha kawaida, kwa kifupi hakuna aliyekuwa na akili ya udadisi kama niliyokuwa nayo mimi, nadhani ndiyo maana baba alikuwa akinipenda zaidi yao.
Alitupokea mizigo na kutusaidia kushuka, tukasimama pembeni ya gari, mimi nikawa namtazama nikiwa sina majibu ya maswali yangu kabisa. Mimi na ndugu zangu wote tulikuwa tumechafuka miili yetu kwa sababu ya kusafiri kwenye barabara ya vumbi kutoka Chunya lakini baba yeye alikuwa msafi kabisa.
“Tunasafiri na basi lile pale,” alisema baba kwa sauti ambayo wote tuliisikia vizuri, akatuonyesha kwenye basi kubwa lililokuwa limeinama upande wa mbele kama ndege ya kijeshi, wote tukawa tunalitazama basi lile kwani muundo wake ulikuwa wa aina yake na sidhani kama kuna yeyote kati yetu ambaye aliwahi kuliona basi kama hilo kwa macho.
Basi tulibeba vifurushi vyetu na kuanza kumfuata baba ambaye alitupeleka mpaka kwenye lile basi, yeye akawa wa kwanza kuingia, akawa anatusaidia kupanda ngazi mmoja baada ya mwingine. Wa mwisho alikuwa mama ambaye alikuwa na mzigo mkubwa, baada ya kuingia, baba alianza kusoma namba za siti zilizokuwa zimeandikwa upande wa juu wa basi hilo kubwa, mpaka alipozipata.
Kila mtu alikuwa na siti yake, akawa anatuelekeza sehemu za kukaa, akampa mama tiketi zetu wote kisha nikamuona akizungumza naye mambo fulani, akaingiza mkono mfukoni na kutoa noti kadhaa za shilingi elfu kumikumi, mama akamshukuru, kisha akamuinamia sikioni na kumuongelesha mambo ambayo hakuna aliyesikia.
Wakati akimnong’oneza mama, macho ya baba yalikuwa kwangu, nilipoona ananiangalia, ikabidi nikwepeshe macho yangu kwani tulifundishwa kwamba siyo heshima kuwatazama baba na mama wanapokuwa na mazungumzo yao ya siri.
Baada ya hapo, alikuja pale nilipokuwa nimekaa, akaniinamia na kurudia kuniambia maneno yaleyale aliyoniambia wakati tukiondoka kule Chunya. Aliniambia kwamba ukimtoa mama, mimi ndiye niliyepaswa kuwa mkuu wa msafara na lazima nihakikishe tunafika salama salmini tuendako, akanipigapiga mgongoni kisha akanipa mkono.
Alifanya hivyohivyo kwa ndugu zangu wengine pia, akawapa mkono mmoja baada ya mwingine kisha akarudi kwangu na kuniambia kwamba tutangulie yeye anafuata.
“Lakini baba... sisi wote ni wageni huko tunakoenda, kwa nini usikae na sisi kwenye hili basi? Tukipotea je?” nilimuuliza, swali lililomfanya anitazame usoni kwa makini, nikakwepesha macho yangu kwa sababu baba alikuwa na hali fulani ambayo akikukazia macho lazima utazame pembeni.
“Kwani kutoka Chunya kuja hapa nani alikuwa wa kwanza kufika?” aliniuliza, swali lililonifanya nipate nafasi ya kutoa dukuduku nililokuwa nalo moyoni.
“Tena nilitaka kukuuliza, kwani ulikuja na usafiri gani na kwa nini wewe hujachafuka kama sisi?”
‘Wewe ni mwanaume, lazima ujifunze kuwa na akiba ya maneno, siyo kila unachokiona ukizungumze au uulize, sijakuzaa kuja kuwa msindikizaji maishani mwako,” alisema kwa sauti ya chini ambayo ni mimi tu niliyeisikia lakini iliyokuwa imebeba ujumbe mzito sana ndani yake, nikashusha pumzi na kukaa vizuri kwenye siti yangu.
Tayari dereva alishaanza kupiga ‘resi’ nyingi na kupiga honi, kuonyesha kwamba muda mfupi baadaye safari ingeanza. Baba akatembea harakaharaka kuelekea kwenye mlango wa kushukia, akateremka mpaka chini na kusimama upande ule tuliokuwa tumekaa, gari likaanza kuondoka ambapo alitupungua mikono, na sisi tukafanya hivyo.
Safari ikaanza, hiyo ilikuwa ni karibu saa kumi na mbili na nusu, basi likaanza kuchanja mbuga kuelekea Dar es Salaam.
Baada ya kusafiri umbali mfupi, tukiwa tumefika eneo maarufu liitwalo Mlima Nyoka, lililokuwa kilometa chache kutoka Uyole mjini, tulishangaa kuanza kuona gari likiyumbayumba. Nilikuwa nikisikia sifa za eneo hilo mara kwa mara kwamba magari mengi, hasa ya abiria yalikuwa yakipata ajali na kuua abiria wengi, mapigo ya moyo yakawa yananienda mbio kuliko kawaida.
Kulikuwa na mteremko mkali wenye kona za hatari, na baada ya kuvuka daraja kulikuwa na mlima mkali pia, jambo ambalo lilimaanisha kama dereva akishindwa kulimudu gari, ajali yake ingekuwa si ya mchezo. Dereva alizidi kuyumba huku gari likiongeza kasi, hali iliyofanya abiria waanze kupiga kelele kwa nguvu, wengi wakilitaja jina la Mungu.
Gari lilizidi kuongeza kasi, likawa linashuka kwenye mteremko huo kwa kasi kubwa huku likiendelea kuyumba huku na kule, kelele ndani ya basi zikazidi kuongezeka.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
 
The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 8
ILIPOISHIA:
Dereva alizidi kuyumba huku gari likiongeza kasi, hali iliyofanya abiria waanze kupiga kelele kwa nguvu, wengi wakilitaja jina la Mungu.
Gari lilizidi kuongeza kasi, likawa linashuka kwenye mteremko huo kwa kasi kubwa huku likiendelea kuyumba huku na kule, kelele ndani ya basi zikazidi kuongezeka.
SASA ENDELEA...

Katika hali ambayo hata sielewi ilikuwaje, nilijikuta nikipata nguvu na kusimama, nikawa natazama nje kwa kupitia kioo cha dereva. Cha ajabu na cha kushtua, nilimuona baba akiwa anapigana na mtu ambaye sikumtambua ni nani, pembeni ya barabara.
Kwa macho yangu, nikamshuhudia baba akimpiga yule mtu kwa nguvu, akamdondosha chini na kuanza kumbamiza kwenye lami, damu nyingi zikatapakaa eneo lote.
Kufumba na kufumbua, nilishtukia baba akiwa ameshika usukani wa lile basi tulilokuwa tukisafiria, sikuwahi kumuona baba hata siku moja akiendesha gari lakini eti siku hiyo ndiyo alikuwa ameshika usukani. Sikukumbuka ameingiaje ndani ya basi, tena likiwa katika mwendo mkali kiasi kile.
Kila kitu kilifanyika kwa kasi kama ya radi, akamtoa dereva na kumsukumia pembeni, akaanza kubadilisha gia huku akiwa ameung’ang’ania usukani, katika hali ambayo hakuna aliyeitegemea, gari liliacha kuyumbayumba ingawa halikupunguza mwendo, likawa linazidi kukimbia kwa kasi kubwa, likishuka kwenye mteremko mkali maarufu kama Mlima Nyoka.
Abiria wote walitulia, hata wale waliokuwa wakipiga kelele, walikaa kimya, wakawa wanaendelea kumuomba Mungu ndani ya mioyo yao, hakuna aliyeona mabadiliko yaliyofanyika upande wa dereva zaidi ya mimi nadhani na watu wachache waliokuwa wamekaa mbele.
Nilimshuhudia baba akiendelea kupangua gia kwa kasi, gari likaanza kupunguza mwendo na mita chache mbele, alifunga breki, gari likaserereka na hatimaye likasimama kandokando ya barabara, watu wote waliokuwa ndani ya basi walianza kushangilia na kumpongeza dereva huku wakikimbilia kwenye mlango wa kutokea nje.
Harakaharaka na mimi nilielekea kule mbele lakini lengo langu kubwa ilikuwa ni kwenda kumuuliza baba nini kilichotokea maana sikuwa naelewa chochote.
Cha ajabu, nilipofika pale kwenye siti ya dereva, nilimuona yule dereva ambaye ndiye aliyetoka na sisi Mbeya mjini akiwa ameegamiza kichwa kwenye usukani, akiwa ni kama amepitiwa na usingizi.
Nilibaki nashangaa kwa sababu kitendo cha kuinuka kutoka pale kwenye siti niliyokuwa nimekaa mpaka pale kwa dereva, sikuwa nimetumia hata dakika moja kamili, zilikuwa ni sekunde tu lakini eti baba hakuwepo tena na aliyekuwa amekaa pale kwenye usukani alikuwa ni dereva.
Niligeuka huku na kule kutazama kama nitamuona baba lakini sikumuona, abiria walikuwa wakiendelea kugombea kutoka na muda mfupi baadaye, wote walikuwa wameshateremka, kila mmoja akawa anamshukuru Mungu wake. Yaani kama ingetokea ajali, kwa jinsi mteremko ulivyokuwa mkali, sidhani kama kuna mtu angetoka salama ndani ya basi lile.
Ilibidi nimguse begani yule dereva ambaye bado alikuwa amelala na kuegamia usukani ili nimuulize nini kilichotokea. Cha ajabu, nilipomgusa, alishtuka sana, akawa ni kama aliyezinduka kutoka kwenye usingizi mzito, akawa anageuka huku na kule. Hakukuwa na mtu mwingine yeyote ndani ya gari, isipokuwa mimi na yeye tu.
“Nini kimetokea? Hatujapata ajali? Mungu wangu,” alisema yule dereva huku akianza kujikagua mwili wake. Nilishangazwa sana na hali ile, yaani kumbe na yeye hakuwa anaelewa kilichotokea kwa hiyo kama zisingefanyika jitihada zile, ni kweli tungepata ajali mbaya sana.
“Kwani wewe unakumbuka nini?” nilimuuliza.
“Wakati tunauanza huu mteremko wa Mlima Nyoka, nilianza kuhisi kizunguzungu, nikajaribu kupunguza mwendo ili nisimame lakini cha ajabu, badala ya kukanyaga breki nilikanyaga mafuta, gari likaongeza mwendo na kizunguzungu kikazidi, sikumbuki tena kilichotokea,” alisema yule dereva huku akiendelea kugeuka huku na kule.
“Tushuke,” nilimwambia, harakaharaka akafungua mlango na kushuka, na mimi nikashuka. Wale abiria waliokuwa chini, walimzunguka dereva na kuanza kumpongeza kwa kazi kubwa aliyoifanya. Ilibidi awe anaitikia tu lakini kiukweli hakuwa anajua nini kimefanyika na imekuwaje mpaka basi limesimama.
Akiwa anaendelea kupongezwa, tabasamu la uongo likiwa limechanua kwenye uso wake, alishtuka baada ya kuanza kuona damu zikimtoka puani, abiria wote nao wakashtuka. Mara ya kwanza alipojifuta, zilikuwa ni damu kidogo lakini mara ya pili, zilikuwa nyingi, tena zikiwa na weusi fulani hivi, kila mmoja akapatwa na hofu kubwa ndani ya moyo wake.
Kwa bahati nzuri, miongoni mwa wale abiria alikuwepo daktari ambaye ilibidi amshike mkono na kumsogeza pembeni, akawataka abiria wengine wasogee pembeni ili apate hewa, akamlaza chini na kuanza kumpa huduma ya kwanza.
Nikiwa bado sielewi nini cha kufanya, nilimuona baba akiwa ng’ambo ya pili ya barabara, akanionesha ishara kwamba nimfuate. Nikaangalia kushoto na kulia, nilipoona hakuna gari, nilivuka barabara na kusogea kule baba alipokuwa amesimama.
“Huku nyuma, mama na ndugu zangu wengine walishangaa kwa nini navuka barabara, mama akaanza kuniita. Nilishangaa kwa nini ananiita mimi tu wakati pembeni yangu alikuwepo baba, nikakosa majibu.
“Vipi, umeona kilichotokea?” baba aliniuliza huku akinitazama usoni, nikawa namtazama huku nikiwa na maswali mengi yasiyo na majibu.
“Baba wewe si tulikuacha stendi? Umefikaje hapa? Halafu uliingiaje kwenye gari na kuzuia ajali isitokee? Yule uliyekuwa unapigana na...” nilijikuta maswali mfululizo yakinitoka. Alichokifanya baba, ilikuwa ni kuniziba mdomo kwa kutumia kiganja cha mkono wake, ambao bado ulikuwa na damudamu.
“Nimeshakwambia, ukiwa mwanaume maana yake unatakiwa kuwa na kifua, siyo kila unachokiona unatakiwa kukisema, umenielewa?” alinihoji baba huku akinitazama, nikatingisha kichwa.
Akaniambia kwamba safari yetu ilikuwa imeandamwa na mabalaa makubwa na mtu pekee ambaye angeweza kushirikiana naye kuhakikisha tunafika salama, ni mimi. Akaingiza mkono mfukoni na kutoa kikaratasi ambacho kilifungwa unga fulani mweusi, akaumimina kidogo mkononi na kuniambia natakiwa kwenda kumpulizia yule dereva usoni.
Akaniambia baada ya hapo, mambo yote yangekuwa sawa na akaniambia natakiwa kukaa siti ya nyuma ya dereva, nikiona jambo lolote haliendi sawa, nivue viatu kisha nivivae upya kwa kuvigeuza, yaani cha kushoto nivae kulia na cha kulia kushoto kisha nishike sehemu zangu za siri.
“Umenielewa?”
“Ndiyo baba.”
“Mimi natangulia kusafisha njia,” alisema kisha akaniambia nivuke barabara, nikafanya hivyo. Kwa bahati mbaya, wakati navuka barabara, safari hii sikutazama kushoto wala kulia, nikavuka tu kama ng’ombe. Nikiwa nimefika katikati ya barabara, nilisikia mama akipiga kelele kwa nguvu pamoja na watu wengine, wote wakinionesha ishara kwamba nikimbie.
Sikuelewa kwa nini wananiambia vile, ghafla niligeuka kutazama upande wangu wa kushoto, lori kubwa la mafuta, lilikuwa limeshanisogelea huku likiwa kwenye mwendo wa kasi kubwa, taa zote za mbele zikiwa zimewashwa.
“Mungu wangu!” nilisema kwani nilijua hakuna kinachoweza kuniokoa kutoka kwenye mdomo wa mauti, ilikuwa ni lazima linisagesage palepale kama chapati.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom