Makapuku Forum

Makapuku Forum

Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 38
ILIPOISHIA:
“Mara ya mwisho mlizungumza naye lini?”
“Kiukweli tangu aondoke hatujawahi kuzungumza naye, wanasema hospitalini hawaruhusu kutumia simu,” alijibu mwanaume huyo, nikashusha pumzi ndefu.
SASA ENDELEA...

Majibu ya watu hao wawili tu yalitosha kunifanya nielewe kilichokuwa kinaendelea lakini ili kupata ushahidi mkubwa zaidi, niliendelea kuwapigia simu wengine. Wachache hawakuwa wakipatikana hewani lakini karibu watu 16 wote walikuwa wakipatikana na majibu yao hayakuwa yakitofautiana.
Wapo waliosema kwamba ndugu zao walichukuliwa kwenda kusoma nje ya nchi kwa msaada wa shirika hilo, wengine wakasema walipelekwa kwa matibabu lakini asilimia kubwa walisema kwamba ndugu zao walichukuliwa kwa ahadi ya kwenda kutafutiwa kazi nchi za Uarabuni, India, Marekani na nchi za Ulaya.
“Kwani binti yako ana elimu kiasi gani mpaka uamini kwamba anaenda kutafutiwa kazi nzuri huko anakokwenda?”
“Kiukweli wala hajasoma, aliishia darasa la saba tu lakini tukaambiwa kule kuna watu wanatafutwa kwa ajili ya kwenda kufanya kazi za ndani, na mshahara wake ni mkubwa kuliko hata mameneja wengi wa Tanzania, ndiyo maana tukamruhusu kwa shingo upande.
“Isitoshe kabla ya kuondoka, viongozi wa shirika hilo walitupa shilingi milioni moja kama shukrani tu na hapo ni nje ya mshahara wa binti yetu,” mzee mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Akilimali, aliniambia wakati akizungumza nami kwenye simu.
“Uko bize sana na simu mpenzi wangu, kitaalamu simu huwa inatoa mionzi ambayo siyo mizuri kwa mtu kama wewe kwani inaweza kukuongezea matatizo mpenzi, au wewe hulioni hilo?” alisema Shamila baada ya kuingia wodini, ikiwa imepita takribani nusu saa tangu nilipomtaka yeye na Raya watoke na kunipisha.
Nilishindwa hata nimjibu nini, akanisogelea na kunibusu kwenye paji la uso wangu, akakiweka kitanda vizuri kisha akakaa pembeni yangu.
“Eti, unalijua shirika linaloitwa Black Heart?” nilimuuliza Shamila, akanitazama kwa macho ya mshangao kama anayejiuliza ‘umelijuaje?’.
“Jamal!” aliniita huku sauti yake ikionesha kuwa na hofu kubwa.
“Kumbe hicho ndicho ulichokuwa ukikihangaikia muda wote?”
“Ndiyo, kwani kuna tatizo?”
“Ni hatari mpenzi wangu, nakupenda sana na sitaki kuona ukipatwa na jambo lolote baya.”
“Kivipi? Mbona sikuelewi Shamila?” nilimuuliza, akashusha pumzi ndefu na kunitazama usoni.
“Kuna siku uliniuliza kuhusu yule mgonjwa anayeitwa Shenaiza, nikakueleza kwa kifupi kwamba baba yake siyo mtu mzuri hata kidogo.”
“Ndiyo nakumbuka, sasa kwani kuna uhusiano gani na hiki nilichokuuliza?” nilimtega Shamila kwani ilionesha kuna mambo mengi anayajua lakini anaogopa kuniambia.
“Usinifanye mimi mjinga Jamal, najua kila kitu kuhusu unachokifanya tangu mwanzo, najua kwamba unachimba kutaka kujua baba yake Shenaiza anashughulika na nini lakini nakuomba sana, achana na hicho unachokifanya.
“Watu wengi wameshapotea kwa sababu ya kumfuatilia huyo mzee! Jamal, mwenzio nakupenda na sitaki kuona ukipotea ndiyo maana nakwambia achana na hayo mambo.”
“Hapana, ni lazima niikamilishe hii kazi Shamila, nimerudi duniani kwa ajili ya kazi hii, sitaogopa chochote wala sitarudi nyuma,” nilimwambia kwa msisitizo, akanitazama tena machoni na kushusha pumzi ndefu kwa mara nyingine, akatazama huku na kule kuhakikisha hakuna mtu anayetusikiliza.
“Mhusika mkuu wa hiyo Black Heart ni baba yake Shenaiza.”
“Ni shirika la nini?”
“Kwa nje linajitambulisha kama shirika la kusaidia watu wenye matatizo mbalimbali, kuwasafirisha wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi, kuwalipia gharama za masomo watoto na vijana kutoka kwenye familia maskini pamoja na kuwatafutia kazi nzuri wananchi nje ya nchi.”
“Umesema kwa nje, vipi kwa ndani?”
“Jamal, unajua mpaka nafikia hatua ya kuufungua mdomo wangu kukwambia masuala haya ninayahatarisha maisha yangu kwa kiasi kikubwa kwa sababu ikija kufahamika kwamba mimi ndiyo niliyekwambia nitauawa mwenzako,” alisema Shamila kwa hofu kubwa. Sikuelewa hasa hofu yake ilikuwa ikisababishwa na nini. Nikamtoa wasiwasi kwamba nitamlinda, akaniambia kuwa sina uwezo wa kumlinda kwa sababu hata mimi mwenyewe nilikuwa nahitaji kulindwa ndiyo maana nilishindwa kujitetea siku nilipovamiwa na kutaka kuuawa.
Ni kweli alizungumza pointi lakini nilijivisha roho ya kiume, nikaendelea kumtoa wasiwasi na kujitutumua kwamba siku hiyo walinibahatisha tu, akakubali kunieleza kwa upana.
Aliniambia kwamba licha ya shirika hilo kujinadi kwa sura hiyo ya nje, likijifanya linasaidia jamii ya watu maskini, ukweli ni kwamba lilikuwa likifanya biashara haramu ya viungo vya binadamu. Akaendelea kuniambia kwamba shirika lilikuwa na mtandao mpana, likiwagusa viongozi kadhaa wa ngazi za juu serikalini pamoja na watu wengine wenye taaluma mbalimbali, wakiwemo madaktari.
Aliniambia kwamba watu wote waliokuwa wakisafirishwa kwenda nje ya nchi na shirika hilo, walikuwa wakienda kutolewa viungo vyao muhimu, kama moyo, mapafu, figo na vingine vingi, vikitolewa na kupandikizwa kwa watu waliokuwa wakivihitaji.
Akaniambia kwamba kwenye nchi zilizoendelea, kuna watu wengi wanaojiweza kifedha lakini wanakuwa na matatizo mbalimbali ya kiafya kiasi kwamba fedha zao haziwasaidii kupona kwa kutumia madawa mbalimbali ya hospitalini. Ni hao ndiyo waliokuwa wateja wakubwa wa viungo hivyo vya binadamu.
Akanifafanulia kwamba; kwa mfano kama kuna tajiri ana matatizo ya figo au ini na ameshatumia madawa yote bila kupata nafuu, njia nyepesi ya kumrudishia afya bora ilikuwa ni kupandikizwa viungo vingine kutoka kwa mtu asiye na matatizo.
Akasema kwa kuwa uhitaji ni mkubwa siku hizi kutokana na mtindo wa maisha, hasa kwa nchi zilizoendelea, njia nyepesi iliyokuwa inatumiwa na baba yake Shenaiza na wenzake, ilikuwa ni kuwasafirisha watu kutoka nchi za kimaskini na kwenda kuwauza kwa bei ghali kwa ajili ya kutolewa viungo vyote muhimu ambavyo huwekewa watu wanaojiweza kiuchumi.
Maelezo yake yalinishangaza na kunishtua sana, akanihakikishia kwamba tangu shirika hilo lianze kufanya kazi miaka kadhaa iliyopita, hakukuwa na hata mtu mmoja ambaye aliondoka na kurejea nyumbani salama, wengi walikuwa wakirejeshwa wakiwa maiti na wengine hawakuwa wakirejeshwa kabisa.
Ndugu zao wanapowaulizia, hutulizwa kwa kupewa fedha na kuambiwa wapo salama na ipo siku watarejea nchini.
“Ina maana serikali kupitia kwa vyombo vya usalama hawajui kuhusu hiki kinachoendelea?”
“Watu wanajua sana, lakini nimeshakwambia huu ni mradi wa vigogo wakubwa serikalini, hakuna anayeweza kufumbua mdomo wake na ukijaribu tu, basi ujue kifo kinakuita.”
Japokuwa mle wodini mlikuwa na kipupwe, nilijikuta nikitokwa na kijasho chembamba, mapigo ya moyo wangu yakinienda mbio kuliko kawaida. Ni hapo ndipo nilipoelewa kwa nini Shamila alikuwa akinikataza kujihusisha na mambo yale.
Akaendelea kuniambia kwamba Shenaiza alikuwa akifahamu kinachofanywa na baba yake na kwa sababu ilifika hatua akawa amechoshwa na ukatili huo, alimtishia baba yake kuwa atatoa siri, jambo lililosababisha ateswe sana, ikawa mtu yeyote akionekana kuwa karibu naye, baba yake anahisi anaweza kupewa siri hiyo hivyo anauawa haraka kabla hajafumbua mdomo wake.
“Kumbe ndiyo maana na mimi wananiwinda kutaka kuniua?” nilijikuta nikisema kwa sauti kubwa.
Je, nini kitafuatia?
 
Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 39
ILIPOISHIA:
Akaendelea kuniambia kwamba Shenaiza alikuwa akifahamu kinachofanywa na baba yake na kwa sababu ilifika hatua akawa amechoshwa na ukatili huo, alimtishia baba yake kuwa atatoa siri, jambo lililosababisha ateswe sana, ikawa mtu yeyote akionekana kuwa karibu naye, baba yake anahisi anaweza kupewa siri hiyo hivyo anauawa haraka kabla hajafumbua mdomo wake.
“Kumbe ndiyo maana na mimi wananiwinda kutaka kuniua?” nilijikuta nikisema kwa sauti kubwa.
SASA ENDELEA...

“Na bado wataendelea kukuwinda mpaka watakapoyakatisha maisha yako, unapaswa kuwa makini sana mpenzi wangu,” alisema Shamila lakini alichokisema ni kama hakikuingia akilini mwangu.
Akili yangu ilianza kunienda mbio kuliko kawaida, nikawa naunganisha matukio, kuanzia siku Shenaiza aliponipigia simu na kuniambia kwamba ana tatizo kubwa na anahitaji nimsaidie, baada ya awali kuwa amekosea namba.
“Lazima nikazungumze na Shenaiza, atakuwa anajua mambo mengi zaidi,” nilisema huku nikijaribu kuinuka, Shamila akanizuia na kuniuliza kama ninakumbuka kilichotokea muda mfupi uliopita kwenye maegesho ya magari.
Japokuwa nilikuwa na shauku ya kwenda kuonana na Shenaiza, maneno hayo ya Shamila yalinivunja nguvu kabisa. Nilikumbuka jinsi wale wanaume wenye asili kama ya Shenaiza walivyokuwa wakiniwinda kwa udi na uvumba.
“Kama usingepata akili ya kuingia kwenye wa ile teksi unafikiri nini kingetokea?” alisema Shamila huku akinibusu kwenye paji langu la uso.
Kitu ambacho ningependa kukieleza hapa, ndani ya muda mfupi tu tangu nifahamiane na Shamila na kujikuta nikianguka naye dhambini, dada huyo mrembo alionesha kuchanganyikiwa kabisa na penzi langu.
Kila mara alikuwa anapenda kunibusubusu, mara anishike hapa, mara anisafishe kucha, mara anidekeze basi ilimradi roho yake ifurahi! Moyoni nilikuwa najisikia raha sana kwa sababu siyo siri, sikuwa mzoefu wa mambo hayo ya kikubwa.
Unajua kwa nini wanaume wengine huwa wanafikia hatua ya kutelekeza familia zao? Unakuta katika maisha yako, hujawahi kukutana na mwanamke anayejua kukupetipeti kama ilivyokuwa kwa Shamila. Sasa ukishaangukia kwenye mikono yake, na wewe ni mgeni wa mambo hayo, lazima utelekeze mke na watoto na kuhamia kwake.
“Kwani Shamila wewe ni mtu wa wapi?”
“Mbona unaniuliza swali ambalo haliendani kabisa na mada tunayozungumza?” aliniuliza Shamila huku akinitazama kwa yale macho yake ambayo muda wote yapo kama yana usingizi!
Nikachekacheka pale na kupotezea mada, akaendelea kunisisitiza kwamba huo haukuwa muda muafaka wa mimi kutoka na kwenda kwenye wodi aliyokuwa amelazwa Shenaiza, wala kuzungukazunguka kwa sababu ya usalama wangu.
“Lakini Shamila, kuna kazi ambayo ni lazima niikamilishe haraka iwezekanavyo, au wewe unaridhishwa na kinachofanywa na huyu mzee pamoja na kundi lake?”
“Siyo kwamba naridhishwa mpenzi wangu, Wazungu wanasema ‘dont hurt what you cant kill’ (usiwinde kitu ambacho hutaweza kukiua), hata ukifuatilia na kuujua ukweli, utafanya nini?”
Shamila alikuwa amenizidi kwa hoja, ikabidi nitulie tu wodini huku nikiendelea kutafakari nini cha kufanya kwa sababu ile hoja ya kwamba niache kufuatilia suala lile kwa sababu sikuwa na cha kufanya, sikuliona kama ni sahihi kwangu.
Baadaye, nilijifanya kama nimepitiwa na usingizi, lengo lilikuwa ni kumpumbaza Shamila, kweli aliponiona nimelala alikuja nakunifunika vizuri kisha akatoka na kwenda kuendelea na shughuli zake.
Nilisubiri kwa dakika kadhaa, nilipoona kumetulia kabisa, niliamka na kuvaa viatu, nikatazama huku na kule, niliporidhika kwamba Shamila hakuwepo, nilinyata hadi kwenye chumba cha manesi, nikachukua koti la kidaktari lililokuwa limetundikwa ukutani, nikalivaa na kusogea kwenye kioo kilichokuwa pembeni, nikajirekebisha vizuri.
Kama ungenitazama haraka, ungeweza kudhani na mimi ni muuguzi hospitalini hapo, niliamini hiyo ndiyo itakuwa njia nyepesi ya kwenda kuonana na Shenaiza kule wodini kwake bila kushtukiwa na mtu yeyote.
Harakaharaka nilitoka huku nikiwa makini jeraha langu la kifuani lisije kufumuka tena, nikaingia kwenye lifti na kushuka hadi ghorofa ya chini, nikashuka na kuanza kutembea harakaharaka kuelekea kule kwenye wodi ya wagonjwa wa akili, wanawake alikokuwa amelazwa Shenaiza.
Nilifanikiwa kufika kwenye wodi ya wagonjwa wa akili, kama ilivyokuwa kawaida ya wodi hiyo, nilipokelewa na vurugu na kelele za kila aina kutoka kwa wagonjwa, nikawa nawapita mmoja baada ya mwingine mpaka nilipofika kwenye kitanda cha Shenaiza.
Tofauti na nilivyotegemea kumkuta Shenaiza akiwa amekaa kitandani kwake akilalamika, nilishangaa kumkuta akiwa amelala tuli, akionesha kabisa kwamba hakuwa kwenye hali ya kawaida.
Nilisimama kwa sekunde kadhaa na kuanza kumtazama, kwa zile saa chache tu nilizokaa mbali naye, alikuwa amebadilika kabisa. Ngozi ya mwili wake, iliyokuwa na weupe wa kung’aa, ilikuwa imebadilika na kuwa na rangi kama ya kijivu hivi, macho yalikuwa yamefumbwa nusu na nusu yapo wazi, mdomo pia haukuwa umefumbwa, nikajikuta nikishindwa kujizuia kutokwa na machozi.
“Shenaiza! Shenaiza!” nilimuita lakini hakuitika, nilijaribu kumtingisha lakini hakutingishika, nikabaki nikihaha huku na kule, nikiwa sijui cha kufanya. Nilipotazama pembeni ya kitanda chake, kulikuwa na kichupa kidogo juu ya droo ya kitanda chake, kilichokuwa na maandishi yaliyosomeka Benzodiazepam.
Harakaharaka nilikichukua kichupa kile na kukiweka kwenye mfuko wa koti, nikatazama huku na kule kujaribu kuangalia kamakuna mtyu aliyekuwa akinitazama. Katika hali ambayo sikuitegemea, miongoni mwa wale wagonjwa wengi wa akili waliokuwa ndan ya wodi hiyo, kuna mmoja alikuwa ametulia, muda wote akinikodolea macho.
Kwa kumtazama tu, hakuonesha kwamba ni mwendawazimu kama wale wenzake kwa sababu macho yangu na yake yalipogongana tu, harakaharaka alikwepesha macho pembeni na kuvunga kama hakuwa akinitazama. Kitendo hicho tu kilitosha kunifanya niamini kwamba hakuwa mgonjwa kama wale wengine.
Niliendelea kumkazia macho, akawa ananitazama kwa wiziwizi, nikamsogelea pale kwenye kitanda alichokuwa amelala juu yake, nikashtuka kumuona akiwa na simu kubwa ya kisasa ambayo harakaharaka aliificha kwenye shuka.
“Wewe ni nani?” nilimuuliza kwa sauti ya chinichini, akanigeukia, tukatazamana.
“Kwani unataka nini?” naye aliniuliza kwa sauti iliyoonesha dhahiri kwamba ni mwanamke mjeuri sana na alikuwepo pale kwa kazi maalum.
“Naomba kuzungumza na wewe, unamfahamu Shenaiza?” nilimuuliza lakini badala ya kunijibu, alinitazama kuanzia juu mpaka chini kisha akageukia pembeni. Kengele ya hatari ililia ndani ya kichwa changu, harakaharaka nikageuka na kuanza kutembea kuelekea kwenye mlango wa kutokea.
“Unahatarisha maisha yako, achana na mambo yasiyokuhusu,” alisema yule msichana, nikageuka na kumtazama, naye akawa ananitazama. Sikuelewa kwa sababu gani amezungumza maneno yale, nikaendelea kutembea harakaharaka na kutoka.
“Mungu wangu, mbona sielewi kinachoendelea?” nilisema huku nikiendelea kutembea kwa haraka, nikaenda mpaka kwenye lifti na kupanda, nikabonyeza namba ya ghorofa ilipokuwa wodi ya ‘private’ niliyokuwa nimelazwa, lifti ikaanza kupanda.
“Unatoka wapi?” Shamila aliniuliza nilipofungua mlango tu, kumbe alikuwa amerejea muda mrefu na akawa anahangaika kunitafuta.
“Nilitoka mara moja,” nilijitetea huku nikijisikia aibu ndani ya moyo wangu.
“Kwa nini hujihurumii mpenzi wangu? Mimi sitakwambia tena kuhusu suala la kuzingatia usalama wako,” alisema huku akinisaidia kuvua lile koti la kidaktari huku akiendelea kunitazama kwa macho ya mshangao.
“Samahani, eti hii ni dawa gani?” nilisema huku nikitoa kile kichupa nilichokichukua kwenye kitanda cha Shenaiza. Akakishika na kukitazama.
“Umekipata wapi?”
“Nimekikuta kwenye kitanda cha Shenaiza, na anaonekana kama hana fahamu, rangi ya ngozi yake imebadilika na kuwa ya kijivu,” nilimwambia, akashusha pumzi ndefu na kunitazama usoni.
 
Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 40
ILIPOISHIA:
“Nimekikuta kwenye kitanda cha Shenaiza, na anaonekana kama hana fahamu, rangi ya ngozi yake imebadilika na kuwa ya kijivu,” nilimwambia, akashusha pumzi ndefu na kunitazama usoni.
SASA ENDELEA...

“Benzodiazepam,” Shamila alisema kwa sauti ya juu, akitamka maneno yaliyokuwa yameandikwa kwenye kile kichupa nilichokikuta pembeni ya kitanda cha Shenaiza.
“Kwani ni dawa gani?”
“Mungu wangu! Wameamua kummalizia kabisa mdada wa watu. Hii ni dawa ya usingizi ambayo hairuhusiwi kutumika bila uangalizi wa kutosha wa daktari. Mtu anapotumia dozi kubwa, husababisha muda wote awe analala tu na kama hali hii ikiendelea kwa muda, husababisha mgonjwa kupoteza kumbukumbu na kuwa kama mtu aliyechanganyikiwa.”
“Haa! Na siyo kwamba dawa hii hutumika kuwatibu wagonjwa wa akili?”
“Hapana Jamal, hii hutumika tu kuwatuliza watu wenye msongo mkali wa mawazo au stress kiasi kwamba wanakosa usingizi. Wakitumia dawa hii chini ya uangalizi wa daktari, huwasaidia kupata usingizi na kuwapunguzia msongo mkali au ‘stress’, lakini narudia tena, ni lazima itumiwe chini ya uangalizi mkali wa daktari.”
“Sasa kwa nini wanampa Shenaiza?”
“Jibu ni moja tu, wanataka watu wote waamini kwamba kweli amechanganyikiwa. Kama kwa siku chache tu alizokaa hapa hospitalini kichupa kimeshaisha, maana yake ni kwamba anapewa dozi kubwa sana ambayo ndani ya muda mfupi tu, itamfanya apoteze kumbukumbu na kuwa mwendawazimu.”
“Shamilaa! Cant we help her?” (Shamilaa! Hatuwezi kumsaidia?)
“Its none of our business Jamal.” (Hilo halituhusu Jamal)
“Kwa nini unasema hivyo?”
“Nikukumbushe tu kwamba mambo yote hayo yanafanywa kwa maagizo ya baba yake mzazi. Unataka kusema wewe una uchungu na Shenaiza kuliko baba yake?” alisema Shamila na kunifanya nikose cha kujibu, nikajiinamia huku nikijisikia uchungu mkali sana ndani ya moyo wangu.
Ni hapo ndipo nilipoanza kuelewa kwa nini Shenaiza alikuwa akihitaji sana msaada kutoka kwangu. Ni hapo pia ndipo nilipoelewa kwa nini alikuwa anashindwa kunieleza moja kwa moja ni msaada gani aliokuwa anauhitaji na alikuwa akisumbuliwa na tatizo gani. Nilishusha pumzi ndefu na kukaa vizuri pale kitandani.
“Utakapojaribu kutoka tena wodini na kwenda unakokujua mwenyewe, kitakachokupata mimi sitahusika maana naona hunielewi,” alisema Shamila huku akionesha kukasirishwa na kitendo changu cha kutoka wodini bila ruhusa yake, wakati nikijua kwamba nilikuwa nikisakwa na watu wenye nia ovu.
“Nisamehe Shamila, lakini muda mwingine nakuwa sina namna zaidi ya kuvunja sheria zako,” nilisema kwa upole, akanisogelea, tukawa tunatazama, nikambusu kwenye paji lake la uso.
“Kwa nini unaonekana kuguswa sana na matatizo ya Shenaiza?” Shamila aliniuliza huku akikaa vizuri, nikashusha tena pumzi ndefu nikitafakari nianzie wapi kumueleza. Kwa jinsi hali ilivyokuwa, kumsaidia Shenaiza peke yangu lilionekana kuwa suala gumu, ilikuwa ni lazima nimueleze Shenaiza ukweli ili kwa pamoja tujue namna ya kumsaidia.
Ilibidi nianze kumsimulia Shamila kila kitu kuhusu mimi na Shenaiza. Nilimueleza kilichotokea kuanzia siku ya kwanza msichana huyo alipopiga simu yangu na baadaye kuniambia kwamba alikuwa amekosea namba. Nilimueleza alivyoendelea kunisumbua akidai kwamba hata kama amekosea namba, anaamini mimi naweza kumsaidia kumtoa kwenye matatizo makubwa yaliyokuwa yanamkabili.
“Nilimueleza Shamila jinsi nilivyoendelea kuwasiliana na msichana huyo, jinsi tulivyoenda kukutana na kumkuta akiwa na hali mbaya hospitalini baada ya kuvamiwa na kujeruhiwa vibaya. Sikumficha kitu, niliendelea kumueleza jinsi alivyonishawishi nimtoroshe hospitali na yote yaliyotokea baada ya hapo.
Shamila alikuwa kimya kabisa akinisikiliza, kadiri nilivyokuwa naendelea kumsimulia kuhusu sakata hilo la Shenaiza, taratibu nilianza kumuona na yeye akiguswa, nilimfafanulia kila kitu isipokuwa kilichotokea baada ya mimi kushambuliwa na kunusurika kufa, na kujikuta nikizinduka nikiwa kwenye ulimwengu mwingine.
Nilimficha kuhusu kipengele hicho kwa sababu maalum kwani nilijua hata nimueleze kwa lugha gani, hawezi kunielewa, sanasana atahisi labda na mimi nimeanza kuchanganyikiwa.
Nashukuru Mungu kwamba maelezo yangu kuhusu Shenaiza yalimuingia sana moyoni mwake, naye akaguswa kama nilivyokuwa nimeguswa mimi lakini kabla ya yote akanitahadharisha.
“Mara kwa mara nimemsikia Raya akilalamika kwamba wewe una uhusiano wa kimapenzi na Shenaiza,” alisema Shamila, kauli ambayo ilinishtua sana. Nikajua kwamba kumbe hata kabla sijaanzisha uhusiano naye wa siri, Shamila alikuwa akinifuatilia kwa karibu sana na tayari alikuwa anajua mambo yangu kadhaa.
Akaendelea: “Sasa isije kuwa mi nakusaidia kumuokoa Shamila kumbe nakurahisishia mpango wako wa kumuokoa mpenzi wako, nikija kujua kwamba ni kweli mna uhusiano naye wa kimapenzi nitafanya jambo hilo ambalo hutakuja kulisahau maishani mwako.”
“Siyo hivyo Shamila, wala sina uhusiano naye wa kimapenzi, ni kama nilivyokueleza na hakuna chochote zaidi ya hayo niliyokwambia.
“Ndiyo nimeshakwambia hivyo, kwa jinsi ninavyokupenda sitaki kuona mtu mwingine akikusogelea, hata huyo Raya naandaa mpango wa kumtoa kwenye maisha yako, nataka nibaki peke yangu, wewe ndiyo mume wangu mtarajiwa,” alisema Shamila na kunibusu na lipsi zake laini, mkondo wa raha za kipekee ukapita kwa kasi kwenye mishipa yangu ya damu, nikajikuta nikisisimka mno hasa nilipokumbuka asali aliyonilambisha.
“Nakuhakikishia, suala kama hilo haliwezi kutokea,” nilisema kwa kumnong’oneza sikioni, akaruka kidogo kwa msisimko na kunibusu tena, akaniambia kwamba ananipenda sana na anaamini mimi ndiyo baba mtarajiwa wa wanaye.
“Kwa hiyo utanisaidia kuhusu suala la Shenaiza,” nilimchombeza, akanihakikishia kwamba yupo tayari kunisaidia kwa chochote ambacho nakihitaji, hata kama kitayagharimu maisha yake.
Nilifurahishwa mno na majibu yake kwani kiukweli, naomba Mungu anisamehe! Hilo ndiyo lilikuwa lengo langu kubwa la kuanzisha naye uhusiano wa kimapenzi, nilitaka nimtumie kukamilisha baadhi ya mambo yangu!
Siyo jambo zuri hata kidogo kucheza na hisia za mtu anayekupenda, nawashauri watu wenye tabia hii waache mara moja kwa sababu mapenzi huwa hayajaribiwi, kama ambavyo ilitokea kwangu na Shamila, Raya na Shenaiza. Nitafafanua kwa kina baadaye jinsi ujanja wangu wa kucheza na hisia za wote watatu kwa wakati mmoja zilivyonigharimu.
Tulichokubaliana na Shamila ilikuwa ni kufanya kila kinachowezekana kwanza kumjua daktari aliyekuwa akisimamia matibabu yake, na ikiwezekana kumbadilishia dawa bila mwenyewe kujua, kwamba badala ya kuendelea kumpa sumu Shenaiza, ampe dawa zitakazomsaidia mwili wake kurudiwa na nguvu zake upya na akipata nafuu tu, tufanye utaratibu wa kumtorosha.
Tulijadiliana pia kwa kina juu ya nini cha kufanya baada ya kugundua mchezo haramu uliokuwa ukifanywa na baba yake Shenaiza kwa kutumia Shirika la Black Heart, wa kuwasafirisha watu na kwenda kuwauza kisha kuwaua na kuwatoa viungo muhimu miilini mwao, kwa kivuli cha kujifanya wanaenda kuwasomesha, kuwapatia matibabu au kuwatafutia kazi.
Kutokana na upana wa mtandao wa baba yake Shenaiza, Shamila alinishauri kwamba kwa sababu tayari nilikuwa nimeshapata pa kuanzia, niendelee kukusanya taarifa kimyakimya kisha nikishapata nafuu na kuruhusiwa kutoka hospitalini, ndiyo tukae tena na kuamua nini cha kufanya kuhakikisha tunamuangusha baba yake Shenaiza na kuokoa maisha ya watu wengi waliokuwa wakienda kutolewa kafara bila wenyewe kujua chochote.
“Lakini sitakiwi kuendelea kukaa hapa hospitalini zaidi, wanaweza kuja hata huku na kunichukua kiulaini, wakaenda kuniua au kunifanya chochote wanachotaka ili kuniziba mdomo,” nilimwambia Shamila, akaniondoa wasiwasi kwamba naye analijua hilo lakini hatutakiwi kufanya mambo kwa kukurupuka. Akanihakikishia kwamba kila kitu kitaenda vizuri, nimuachie yeye.
Wakati tukiendelea kuzungumza, Raya alifungua mlango na kuingia akiwa na kikapu cha chakula, mazungumzo yakakatika ghafla, Shamila akajifanya yuko bize kwenye meza ya dawa, akipangapanga vitu.
“Habari za saizi nesi,” Raya alimsalimia Shamila kwa unyenyekevu, jambo ambalo hakuwahi kulifanya kabla. Shamila naye akajibu kwa uchangamfu, nikabaki njia panda. Sikujua walizungumza nini muda ule mpaka wakamaliza tofauti zao. Raya akaja mpaka pale kitandani na kunibusu mdomoni, Shamila akageuka na kulishuhudia tukio hilo.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
 
Anko obe kasema hujaona kule na tumosa ...

Story leo weka chache mama d miko ya 25

Na mm ndo story ya kwanza hapa make nakumbuka na ya mwanafunzi mchawi kitambo ilinishinda


...nawaangalia tu, niko bia ya tatu, na bado wanapiga taarabu, wakiweka kisanola nitakuja kuwaambia kinachoendelea. kwa sasa nipo na mzigo wa anko umekuja na rafiki yake wanakula kuku tu hapa wa kienyeji , kitu cha foil
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom