Makapuku Forum

Makapuku Forum

Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 31
ILIPOISHIA:
Alionesha kama kuna jambo muhimu anataka kuniambia kuhusu Shenaiza na baba yake ingawa sikujua ni jambo gani.
“Ha..pa...na! Hapana!” nilijibu kwa kubabaika huku nikiwa makini kutaka kusikia ataniambia nini.
SASA ENDELEA...

“Kuwa makini, baba yake siyo mtu mzuri,” alisema nesi huyo ambaye baadaye nilikuja kugundua kwamba anaitwa Shamila.
“Unamaanisha nini?” nilimuuliza kwa sauti ya chini, akanisogelea zaidi na kukaa pembeni ya kitanda changu.
“Kuwa tu makini, nakupenda na sitaki jambo lolote baya likutokee,” alisema huku akinitazama kwa macho yake mazuri, macho yetu yakagongana. Tulitazamana kwa sekunde kadhaa, akakwepesha macho yake huku aibu za kikekike zikiwa zimetawala uso wake.
“Ahsante kwa kunisaidia kunifunga upya jeraha langu,” nilimwambia tena, nikamuona akitabasamu kisha akanishika mkono wangu.
“Usijali, hiyo ni kazi yangu ila inabidi uijali afya yako. Hata kama angekuwa ni mgonjwa mwingine, ningemsaidia kama nilivyokusaidia wewe.”
“Ahsante pia kwa fulana uliyonipa, ni nzuri na inanukia vizuri,” nilimwambia kwa sauti ya chini, akatabasamu tena na kuniambia:
“Nilijinunulia hiyo fulana kama zawadi siku ya Valentine Day.”
“Kwa nini ujinunulie mwenyewe zawadi katika siku muhimu kama hiyo? Kwani shemeji hakukupa zawadi?”
“Shemeji? Shemeji gani? Niliamua kujionesha upendo mwenyewe.
“Unataka kusema msichana mrembo kama wewe unaweza kuwa huna mtu?”
“Huwezi kuamini, sina mtu yeyote karibia mwaka unaelekea kuisha sasa. Niliyekuwa naye aliniumiza sana moyo wangu na kunifanya niyachukie mapenzi,” alisema Shamila kwa sauti ya upole, nikawa namtazama usoni alivyokuwa anaongea.
“Mbona unaniangalia sana usoni? Mi nasikia aibu bwana,” alisema huku akiniachia mkono wake na kusimama, aibu zikiendelea kutawala uso wake.
“You are so beautiful Shamila!” (Wewe ni mrembo sana Shamila) nilimwambia, akacheka sana na kurudi tena kukaa pale pembeni ya kitanda changu, akaniambia zimepita siku nyingi hajasikia kauli kama hiyo kutoka kwenye kinywa cha mwanaume mzuri kama mimi, wote tukacheka na kugongesheana mikono.
Kuna jambo kubwa lilikuwa limebadilika maishani mwangu, kwa kipindi kirefu sikuwa na mazoea ya kukaa karibu na wasichana wala kupiga nao stori.
Mtu pekee niliyekuwa nimezoeana naye alikuwa ni Raya ambaye hata hivyo mara kwa mara nilikuwa nikimkwepa lakini cha ajabu, katika siku za karibuni, nilijikuta nikivutiwa na wasichana wawili, Shenaiza na sasa Shamila, achilia mbali Raya ambaye tayari tulishaanza naye uhusiano wa kimapenzi.
Hata ujasiri wa kuzungumza pia ulikuwa umeongezeka. Nikaendelea kupiga stori za hapa na pale na Shamila, nikawa namchangamsha kwa sababu nilijua kuna jambo nilikuwa nimemkera lakini pia nilitaka kumuingia ili nipate habari kumhusu Shenaiza na baba yake kwani ilionesha kwamba nesi huyo anawajua vizuri.
“Hujaniambia ubaya wa baba yake Shenaiza, kwani amefanya nini?”
“Tuachane na hayo, usije ukaenda kumwambia binti yake bure, inaonesha unampenda sana. Hivi nikuulize, kwani wewe una wapenzi wangapi?”
“Nijibu kwanza swali langu na mimi nitakujibu la kwako. Ubaya wa baba yake Shenaiza ni upi?” nilimkomalia Shamila, akashusha pumzi ndefu na kugeuka huku na kule kama anayehakikisha kwamba hakuna mtu aliyekuwa akitusikiliza.
“Anafanya biashara za hatari sana, siyo mtu mzuri hata kidogo.”
“Biashara za hatari ndiyo biashara gani? Anauza madawa ya kulevya?”
“Si bora hata angekuwa anauza madawa ya kulevya! We elewa kwamba anafanya biashara za hatari sana, kama huamini endelea kumchunguza taratibu.”
“Nitamchunguza vipi wakati hata simfahamu?”
“Humfahamu?” aliniuliza Shamila kwa mshangao, nikamhakikishia kwamba simfahamu kabisa. Aliniambia inawezekanaje nikawa na ukaribu na Shenaiza lakini nisimfahamu baba yake? Sikuwa na cha kumjibu lakini ukweli ni kwamba sikuwa nimewahi kumuona zaidi ya kusikia tu habari zake.
Akaniambia kuwa muda mwingi huwa hakai nchini na hata akija, huwa haonekani kwa urahisi. Nikamuuliza yeye amemfahamia wapi? Akanijibu kwamba huwa anakuja mara kwa mara hospitalini hapo kwa sababu ana marafiki wengi ambao ni madaktari.
“Kwani na yeye ni daktari?”
“Hapana.”
“Sasa iweje awe na marafiki madaktari?” nilimuuliza, akashusha pumzi ndefu na kuniambia kwamba ana urafiki nao kwa sababu huwa anashirikiana na baadhi yao wasio waaminifu kwenye hizo biashara zake.
Nilijaribu kumbana aniambie ni biashara ya namna gani anayofanya na madaktari lakini hakuwa tayari kuniambia chochote kwa maelezo kwamba anahofia maisha yake. Nilimbana sana lakini alikataa katakata kuniambia zaidi ya kunitaka niendelee kufuatilia mwenyewe nitaujua ukweli.
Kiukweli alinichanganya kichwa lakini alinipa mwanga. Ukichanganya na yale maelezo ya Shenaiza, tayari nilikuwa na sehemu ya kuanzia, nikajiapiza ndani ya moyo wangu kwamba ni lazima nitaujua ukweli na nitafanya kazi niliyotumwa, ya kumzuia kuendelea kufanya alichokuwa anakifanya japokuwa sikujua ni kitu gani.
Ni kazi ambayo nilipewa nikiwa kule kwenye ulimwengu mwingine kama masharti ya kurejea kwenye ulimwengu wa kawaida. Sikujua nitafanya nini lakini nilichojiapiza ni kwamba ilikuwa ni lazima nifanikiwe kumzuia alichokuwa anakifanya.
“Mbona kama umezama kwenye dimbwi la mawazo?” Shamila aliniuliza na kunizindua kutoka kwenye mawazo mazito, nikashusha pumzi ndefu na kumtazama usoni.
“Haya na wewe nijibu maswali yangu!” alisema Shamila huku tabasamu likianza kuchanua kwenye uso wake. Jambo ambalo sikuwa na uhakika nalo, ni juu ya uchangamfu wa Shamila. Sikujua huwa anachangamka hivyohivyo akiwa na watu wengine au ni kwangu tu.
“Nimekuuliza una wapenzi wangapi?”
“Mmoja tu, anaitwa Raya, yule niliyekuwa namkimbilia muda ule.”
“Muongo wewe, na Shenaiza?”
“Shenaiza siyo mpenzi wangu, ni rafiki yangu tu.”
“Rafiki yako ndiyo mna-kiss? Yaani hamjifichi kabisa, inaonesha ni mpenzi wako.
“Siyo mpenzi wangu, kweli tena,” nilimwambia Shamila lakini akaendelea kukataa, akaniambia hata Shenaiza mwenyewe alikuwa akiwaambia manesi kwamba mimi ndiyo mpenzi wake na tuna mipango ya kuja kufunga ndoa, kauli iliyonishangaza sana.
Shamila aliendelea kunishutumu kwamba sijatulia, naonesha nina wanawake wengine wengi na ndiyo maana nashindwa kuwathamini watu wanaonipenda kwa dhati. Sikuelewa msingi wa lawama zake ni nini kwa sababu mimi na yeye ndiyo kwanza tulikuwa tumejuana, akaendelea kuniambia kwamba kwa sababu sijatulia nitakosa vitu vizuri.
Akaonesha kususa na kutoka wodini kwa hasira, akaniacha nikiwa na maswali mengi yaliyokosa majibu, wakati anatoka mlangoni, alipishana na Raya aliyekuwa akiingia akiwa na kikapu ambacho hata bila kuuliza nilijua kwamba kina chakula. Nilipomtazama usono, macho yake yalikuwa mekundu na yamevimba kuonesha kwamba alikuwa amelia kwa muda mrefu, hata ule uchangamfu wake haukuwepo tena. Macho yake yakatua kwenye fulana niliyokuwa nimevaa, akanikazia macho.
Je, nini kitafuatia?
 
Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 32
ILIPOISHIA:
Nilipomtazama usoni, macho yake yalikuwa mekundu na yamevimba kuonesha kwamba alikuwa amelia kwa muda mrefu, hata ule uchangamfu wake haukuwepo tena. Macho yake yakatua kwenye fulana niliyokuwa nimevaa, akanikazia macho.
SASA ENDELEA...

“Umebadilisha nguo saa ngapi? Na hiyo fulana umeipata wapi mbona inanukia pafyumu ya kike?” alinihoji Raya uso akiwa ameukunja, nikashusha pumzi ndefu na kumtazama usoni, huku nikiuvaa ujasiri wa kiume.
“Yaani hiyo ndiyo salamu? Ama kweli mapenzi yamepungua, kwa hiyo hata nikifa huwezi kujali tena?” ilibidi nimgeuzie kibao Raya. Moyoni nilikuwa najua kwamba nakosea lakini ilikuwa ni lazima nifanye hivyo ili kutuliza hali ya mambo.
“Wewe ndiyo wa kunitamkia mimi maneno hayo? Nikupende vipi Jamal, kwa nini unautesa moyo wangu?” alisema Raya na kuanza kuangua kilio. Kauli yangu ni kama ilikuwa imeenda kutonesha donda ndani ya nafsi yake.
Nilijisikia vibaya lakini ikabidi niendelee ‘kumkazia’, nikamwambia wakati anaondoka kwa kususa, nilikuwa nikimfuata lakini kwa bahati mbaya nikaanguka na kusababisha jeraha langu lifumuke na kuanza kumwaga damu.
“Huoni kwamba nimefungwa plasta na bandeji upya? Kama huamini muulize yule nesi, amenisaidia sana, huenda sasa hivi ungekuja na kukuta stori nyingine,” nilimwambia Raya, kauli ambayo ilionesha kumshtua mno.
“Mungu wangu, kwani ilikuwaje?” alisema Raya huku akikaa pembeni ya kitanda changu, akawa anajifuta machozi huku akionesha kushtushwa mno na nilichomweleza, nikamwambia shati langu lilikuwa halitamaniki kwa damu na kwamba hiyo fulana nilikuwa nimesaidiwa tu na msamaria mwema.
Maskini Raya! Alianza kujihisi kuwa na hatia kubwa ndani ya moyo wake, ule moto aliokuja nao ukazimika, akaanza kunipa pole na kuniomba msamaha kama ameniudhi! Yaani japokuwa mimi ndiyo nilikuwa na makosa, yeye ndiyo alikuwa akiniomba msamaha!
Nilimkubalia na kumuomba apunguze wivu kwa sababu nampenda yeye peke yake na ukaribu wangu na Shenaiza ulikuwa ni kwa sababu maalum tu. Hakutaka tena kuendelea kulizungumzia suala hilo, akili yake yote akaielekeza kwangu kuhakikisha nakula vizuri chakula alichokuwa ameniandalia.
Nilikifurahia chakula alichokuwa ameniandalia, nikala vizuri na kumfanya na yeye afurahi, nikamshukuru kisha akatoa vyombo na kuvirudisha kwenye kikapu chake, akasafisha kila kitu pale kitandani kwangu kisha akakaa tena pembeni yangu, mkono wake mmoja ukiwa kwenye mwili wangu, mara kwa mara akawa ananibusu kwa mahaba mazito.
“Niambie kama kweli unanipenda Jamal!”
“Nakupenda sana Raya na kwangu wewe si tu mpenzi, bali mke mtarajiwa, namshukuru Mungu kwa kukuleta karibu yangu,” nilimwambia, nikamuona akitabasamu.
Maneno yangu matamu yalienda kumaliza kila kitu, nikaendelea kumpamba, akawa anacheka kwa furaha utafikiri siyo yule aliyeingia macho yakiwa yamemvimba na kuwa mekundu kwa kulia. Nikawa nimefanikiwa kabisa kumsahaulisha mabaya yote.
Mpaka muda wa kuondoka unafika, Raya alikuwa na furaha kubwa ndani ya moyo wake, akaniaga kwa kunimwagia mvua ya mabusu na kuniambia kwamba anatamani angelala na mimi wodini lakini kwa kuwa sheria haziruhusu, tutaonana asubuhi ya siku inayofuatia, akaondoka zake.
“Huyo ndiyo Raya?”
“Ndiyo! Vipi kwani mbona umeniuliza hivyo?”
“Aah, nilitaka tu kumjua vizuri,” nesi Shamila aliongea huku akionesha kabisa kuwa na kinyongo ndani ya moyo wake. Kumbe muda wote wakati nikizungumza na Raya, alikuwa kwenye ofisi ya manesi akitusikiliza kila kitu kwa mbali, akajikausha kama hayupo mpaka Raya alipoondoka.
“Kumbe hanizidi kwa uzuri, tena isitoshe mimi tayari nina kazi, naishi kwangu na kuendesha maisha yangu bila tatizo lolote. Mwanaume atakayenioa atafaidi sana,” Shamila alijipigia debe, nikawa nimeshamuelewa kwa nini anasema vile, nikakosa hata cha kumjibu.
“Si naongea na wewe mbona hunijibu?”
“Sasa nitakujibu nini Shamila? Ndiyo maana nimebaki kimya,” nilimwambia kwa upole. Sikutaka kumuudhi kwa sababu naye alikuwa na umuhimu mkubwa kwenye maisha yangu, katika kipindi hicho nilichokuwa hospitalini hapo chini ya uangalizi wake.
Tuliendelea kupiga stori za hapa na pale, mara kwa mara akimtoa kasoro Raya na kujisifia, nikawa namuunga mkono kwa sababu kama nilivyosema sikutaka kumuudhi na kubwa zaidi, nilikuwa nataka kumtumia kufahamu mambo mengi zaidi kuhusu baba yake Shenaiza.
“Hivi ukiniangalia unahisi nitaruhusiwa lini kutoka?”
“Mh! Yaani wewe unafikiria kutoka? Unajiona umeshapona siyo? Unajua wewe unashangaza sana!”
“Nashangaza kivipi?”
“Hivi unajua tangu ulipoletwa hapa hospitalini na kulazwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi, ulikaa siku ngapi bila kurudiwa na fahamu zako?” Shamila aliniuliza.
“Sasa kwani kuna uhusiano gani kati ya nilichokuuliza na hayo unayoyasema?”
“Nakuona una mambo mengi sana. Ndiyo kwanza umerudiwa na fahamu zako lakini hutulii, mara uinuke kitandani, mara umkimbilie huyo Raya wako, mara uende wodini kwa Shenaiza na sasa hivi unaulizia siku ya kutoka,” alisema Shamila, nikaona ni kama alikuwa amenipania.
Nilijua nini kilichokuwa kikimsumbua ndani ya moyo wake. Ni kweli sikuwa na muda mrefu tangu nirejewe na fahamu lakini kwa kuwa mwili wangu ulikuwa na nguvu, sikuona sababu ya kuendelea kupoteza muda, hasa ukizingatia kwamba kuna kazi kubwa ilikuwa inanisubiri.
“Hata madaktari wenyewe nikiwaeleza hizo hekaheka ulizonazo, watashauri uwe unachomwa sindano za usingizi muda wote ili uendelee kupumzika, sijawahi kuona mgonjwa msumbufu kama wewe,” Shamila alizidi kunishukia.
Nisingeweza kuendelea kusubiri wodini hapo eti mpaka niruhusiwe na madaktari, kitu pekee nilichoona ni kikwazo kwangu kufanya kazi niliyotumwa, niliona ni lile jeraha la kifuani tu ambalo nilikuwa nimelitonesha.
Hayo mambo ya kupoteza fahamu hayakuniingia akilini kwa sababu kwanza siyo kweli kwamba nilipoteza fahamu na kulala tu kitandani nikiwa sielewi kinachoendelea bali kilichokuwa kimetokea ilikuwa ni kama tu kuhama kutoka ulimwengu mmoja mpaka mwingine.
Jambo ambalo kwa mtu mwenye akili alipaswa kujiuliza, hivi inawezekana vipi mtu aliyekuwa amepoteza fahamu, awe na pilikapilika nyingi muda mfupi baada ya kurejewa fahamu hizo kama mimi?
Yaani mtu umetolewa leo kwenye mashine ya kukusaidia kupumua ukiwa mahututi halafu saa chache baadaye unaweza kusimama na kutembea mwenyewe kutoka wodi moja hadi nyingine? Kulikuwa na siri kubwa iliyojificha ndani ya moyo wangu.
Kwa jinsi Shamila alivyoanza kunibadilikia kwa sababu ya wivu wake wa kimapenzi, niliona njia nyepesi ya mimi kupata kile nilichokuwa nakitaka, ni kumuingiza kwenye mtego wa mapenzi, kwamba nijifanye nampenda sana yeye kuliko Raya, nimuaminishe kwamba atakuwa mpenzi wangu ili nimtumie vizuri kupata kile nilichokuwa nakitaka.
Ilikuwa ni lazima kesho yake niende kule nilikoelekezwa na Shenaiza kukutana na mdogo wake anipe hiyo bahasha yenye maelezo yote kuhusu kilichokuwa kinafanywa na baba yake lakini hilo lingewezekana tu kama ningekula njama na Shamila, ikabidi nianze kucheza na akili yake.
“Lakini Shamila, kwa nini unaongea na mimi kwa ukali kiasi hicho? Au nimekosea kukuonesha hisia zangu kwamba nakupenda?” nilimwambia, nikamuona akishtuka kuliko kawaida, akanitazama kwa macho yake mazuri.
“Kwani umewahi kuwa na hisia za kunipenda Jamal?” alinihoji, safari hii kwa sauti ya chini na ya upole, akawa ananisogelea pale kitandani huku akinitazama kwa macho yaliyobeba hisia nzito.
“Nakuapia kama ningekutana na wewe kabla ya Raya, huenda wewe ndiyo ungekuwa mpenzi wangu na si ajabu ningeshakuwa nimekuoa, naogopa kukueleza ukweli wa moyo wangu kwa sababu mtu mwenyewe unakuwa mkali kwangu,” nilizidi kumseti kwa maneno matamu, akashindwa kujizuia na kuniinamia pale kitandani, akanibusu kwa hisia za hali ya juu na kunikumbatia bila kujali kwamba anaweza kunitonesha tena jeraha langu la kifuani.
Je, nini kitafuatia?
 
Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 33
ILIPOISHIA:
“Nakuapia kama ningekutana na wewe kabla ya Raya, huenda wewe ndiyo ungekuwa mpenzi wangu na si ajabu ningeshakuwa nimekuoa, naogopa kukueleza ukweli wa moyo wangu kwa sababu mtu mwenyewe unakuwa mkali kwangu,” nilizidi kumseti kwa maneno matamu, akashindwa kujizuia na kuniinamia pale kitandani, akanibusu kwa hisia za hali ya juu na kunikumbatia bila kujali kwamba anaweza kunitonesha tena jeraha langu la kifuani.
SASA ENDELEA...

“Hata mimi nakupenda sana Jamal lakini nilikuwa nashindwa namna ya kukufikishia ujumbe, ahsante kwa kuzielewa hisia zangu,” alisema Shamila huku akiwa amenikumbatia, akaendelea kunibusu sehemu mbalimbali za mwili wangu.
Niliona jinsi kitendo changu cha kuingiza masuala ya mapenzi kilivyomfurahisha, tukaendelea kupiga stori mbalimbali huku mara kwa mara akinikumbatia na kunibusu, na mimi nikawa nazidi kumsifia kwani miongoni mwa ‘maradhi’ ya wanawake, ni kupenda kusifiwa! Dalili za kutimia kwa nilichokuwa nakitaka zikaanza kuonekana waziwazi.
Hatukuwa nesi na mgonjwa kama ilivyokuwa awali, sasa tukawa zaidi ya hapo, nikamuona Shamila akizidi kuninyenyekea, kunipa huduma bora zaidi na muda mwingi akiwa pembeni ya kitanda changu.
Sikujihisi tena kama niko hospitali, ungeweza kusema nipo tu nyumbani. Japokuwa siku hiyo Shamila alikuwa na ‘shift’ ya kutoka saa kumi na mbili jioni, hakutaka kuondoka, akaniambia kwamba ataenda kuongea na kiongozi wao ambadilishie zamu, alale tena kazini mpaka kesho yake ndiyo arudi nyumbani.
“Nimechoka kukaa hospitali mpenzi wangu, naona kama kuna mambo ya muhimu yanazidi kuchelewa, sijui utanisaidieaje?” nilimwambia Shamila, akiwa amekaa pembeni yangu, muda wote mikono yake ikiwa mwilini mwangu.
“Kwani unataka kwenda kufanya nini Jamal, mi nakuonea huruma bado hujapona vizuri. Kuna kazi ya muhimu inatakiwa nikaifanye.”
“Kwa nini usiniagize mimi nikakufanyie?”
“Hapana, ni lazima niifanye mimi mwenyewe labda kama utanisindikiza tu.”
“Lakini bado hujapona.”
“Kwani haiwezekani nikatoka asubuhi halafu baadaye nikarudi?”
“Sasa madaktari wakipita ‘raundi’ na kukukosa wodini itakuwaje? Si unajua wewe bado unatakiwa kuwa chini ya uangalizi maalum na ndiyo maana umeletwa huku kwenye wodi ya peke yako mpenzi?” alisema Shamila.
Kimsingi hakukuwa na uwezekano wowote wa mimi kutoka kirahisi hospitalini lakini nikaona niendelee kumbembeleza Shamila. Kwa kuwa sasa nilikuwa mpenzi wake na nilishaanza kumpa ahadi kemkemu kuhusu maisha yetu ya kimapenzi yatakavyokuwa, nilifanikiwa kumteka akili.
“Basi kesho inabidi mimi asubuhi nisiondoke mapema, nitasubiri mpaka madaktari wakishapita raundi wodini tu, tutaondoka wote mpaka nje ya hospitali. Nitawaambia walinzi umeandikiwa vipimo ambavyo hapa hospitalini havipo,” alisema Shamila, nikaachia tabasamu pana.
Waliosema mapenzi yana nguvu hawakukosea. Shamila alikuwa tayari kuhatarisha kazi yake kwa sababu ya kutetea penzi! Basi tulifikia muafaka, ukaribu wa mimi na Shamila ukazidi kuongezeka utafikiri tulifahamiana miaka mingi iliyopita.
Hata yale masihara aliyokuwa ananiletea awali, nikaona yamepungua sana, muda mwingi akawa anapenda tuzungumzie kuhusu penzi letu. Unajua wanaume wengi huwa wanafanya makosa sana kushindwa kufahamu namna ya kuishi na mwanamke ambaye anaonesha hisia za kukupenda.
Tofauti na wanaume ambao akimpenda mtu huweza kumwambia moja kwa moja kwa ujasiri, wanawake huwa hawana ujasiri huo labda wachache. Kama mwanamke anakupenda, kuna baadhi ya dalili atakuwa anakuonesha akiamini ukiziona, utajiongeza mwenyewe kichwani.
Ukishaziona dalili hizo, hata kama huna malengo ya kuanzisha naye uhusiano wa kimapenzi, kuna namna ya kumuonesha kwamba umemuelewa hata kabla hajatamka chochote na kwamba unaziheshimu hisia zake.
Ikitokea anakuonesha dalili fulani lakini wewe unaendelea kujifanya kipofu, kihulka wanawake ni wepesi sana wa kujisikia vibaya, atahisi umemdharau, ataamini hajakuvutia ndiyo maana umeshindwa kuelewa hisia zake na mwisho utashangaa anaanza kujitenga mbali na wewe na kukujengea chuki.
Kwangu mimi niliamua kupiga ndege wawili kwa mpigo kwa Shamila, japokuwa kiukweli hakuwepo kwenye mawazo yangu kwa sababu tayari nilishaamua kumkabidhi moyo wangu Raya, niliamua kumuonesha kwamba nampenda sana kwa sababu mbili; kwanza sikutaka ajisikie vibaya kwamba ananionesha ishara kwamba ananipenda lakini nampuuza lakini kubwa, nilitaka anisaidie kwenye ile kazi kubwa iliyokuwa inanisubiri.
Malengo yangu yalianza kutimia haraka kuliko hata nilivyotegemea kwa sababu tayari jambo moja muhimu lilikuwa likienda kutimia; kwenda kuonana na Firyaal, mdogo wake Shenaiza ambaye angenipa bahasha yenye taarifa kuhusu baba yao na biashara hatari alizokuwa anazifanya.
Usiku huo Shamila wala hakwenda kukaa kwenye chumba cha manesi kama utaratibu ulivyo, muda wote alikuwa na mimi wodini na hata muda wa kulala ulipofika, alisogeza kitanda tupu kilichokuwa pembeni karibu kabisa na kitanda changu, akajilaza juu yake huku tukiendelea kupiga stori za hapa na pale mpaka nilipopitiwa na usingizi.
Kesho yake asubuhi, Shamila aliwahi kuamka na kuniamsha na mimi, akanisaidia kubadilisha shuka pale kwenye kitanda changu, akaniandalia mswaki na taulo na kuniambia inatakiwa nikaoge ili nipate nguvu. Akanisisitiza kwamba nihakikishe maji hayagusi kwenye jeraha langu.
Nilijikaza na kuamka, nikaenda bafuni ambako nilioga kwa mara ya kwanza tangu nirudiwe na fahamu zangu, nikajisikia mwili ukipata nguvu kubwa, nikarudi wodini ambako nilikuta Shamila akiandaa kahawa, niliporudi kitandani tukakaa pamoja na kuanza kunywa, sote tukachangamka.
Baadaye madaktari walipita kwa ajili ya kutazama maendeleo yangu, wakafurahishwa sana na jinsi nilivyokuwa nikipona haraka, wakawa wanampongeza Shamila kwamba amefanya kazi yake ipasavyo ndiyo maana nilikuwa napona haraka, wote tukafurahi.
“Bila shaka sasa unaweza kutusimulia kuzimu kulivyo maana naamini ulifika na kukutana na mtoa roho ila akaamua kukusamehe tu,” alisema yule daktari kijana aliyezoea kunitania, wote tukacheka.
Nikaandikiwa dawa nyingine za kukausha jeraha langu kisha wakaondoka na kuendelea kuwatembelea wagonjwa waliokuwa wamelazwa kwenye wodi nyingine, Shamila akanitazama, macho yetu yakagongana, nikamuona akishusha pumzi ndefu na kunisogelea huku akitabasamu.
“Sasa itabidi uwe makini sana, mtu yeyote akituuliza tunaelekea wapi utamjibu kwamba nakufanyisha mazoezi, sawa?” Shamila aliniambia kwa sauti ya mamlaka, nikatingisha kichwa kuonesha kukubaliana naye.
Tukajiandaa kisha akachukua mkoba wake, tukatoka taratibu huku tukiendelea kupiga stori za hapa na pale. Kwa kuwa Shamila alikuwa akifahamika hospitalini hapo, hatukupata usumbufu wowote, tukatoka mpaka nje kabisa ya geti bila kuulizwa chochote na mtu yeyote.
Tukaenda mpaka kwenye maegesho ya teksi, madereva wakatudaka juujuu na kuanza kutukaribisha, tukaingia kwenye teksi moja kisha Shamila akanigeukia.
“Tunaanzia nyumbani kwangu, sawa?”
“Hapana, naomba kwanza twende Kurasini halafu ndiyo tutaenda kwako, niko chini ya miguu yako nakuomba,” nilimwambia, akanitazama kwa macho yake mazuri na kutingisha kichwa kuonesha kukubaliana na nilichokisema.
“Naomba tupeleke kwenye Mtaa wa Mama Zayumba, Kurasini,” Shamila alimwambia dereva huyo. Alishakuwa anaujua mpaka mtaa kwa sababu aliniuliza na nikamuelekeza kama na mimi nilivyokuwa nimeelekezwa na Shenaiza, safari ikaanza.
Safari iliendelea na hatimaye tukawasili kwenye mtaa huo ambao ndiyo ilikuwa mara yangu ya kwanza kufika, tukafuata ramani aliyonipa Shenaiza na hatimaye tukatokezea kwenye jengo la kisasa la ghorofa tatu, likiwa na geti kubwa lililozungushiwa nyaya zinazopitisha umeme upande wa juu huku kukiwa na mlinzi mwenye silaha.
Tukasogea na teksi mpaka jirani kabisa na lile geti, yule mlinzi akamuonesha dereva ishara ya kusimama kisha akatusogelea na kutusabahi,mimi nidyo nikawa mzungumzaji mkuu.
“Nikajitambulisha kwamba ni rafiki yake Shenaiza na kuna kitu alikuwa amenituma kuja kukichukua kwa mdogo wake, Firyaal. Kwa jinsi nilivyompa maelezo, wala hakututilia mashaka, hasa alipomuona pia Shamila akiwa amevaa nguo zake za kazini, akajua tumetoka kuonana na Shenaiza hospitalini.
Nikamuona akiingia kwenye chumba cha walinzi na kushika mkonga wa simu, akawa anazungumza na upande wa pili kisha akarudi pale tulipokuwa tumepaki gari na kutuambia tusubiri hapohapo. Tulikaa kwa zaidi ya dakika tatu, tukaona mlango mdogo uliokuwa pembeni ya geti ukifunguliwa, wote tukakazia macho kutaka kuangalia ni nani aliyekuwa anatoka.
 
Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 34
ILIPOISHIA:
Safari hii maneno hayakuwa mengi, tuliendelea kupasha miili yetu, tayari kwa ngwe ya pili ya pambano letu la kirafiki. Safari hii yeye ndiye aliyekuwa akiniongoza nini cha kufanya, nami nikawanafuatisha kwa utii mkubwa, haikuchukua muda, kipyenga kikalia kuashiria kuanza kwa ngwe ya pili, huku safari hii akionesha kupania kuwa nyota wa mchezo.
SASA ENDELEA…

Mikikimikiki iliendelea, kwa mud nilisahau kama nilikuwa mgonjwa ambaye haukuwa umepita muda mrefu tangu nizinduke kutoka kwenye usingizi wa kifo, wala usingeweza kuamini kwamba ndiye mimi ambaye nilifikishwa hospitalini kila mmoja akiamini kwamba siwezi kurejewa na fahamu zangu.
“Jamal! Jamaa..aa..al!” Shamila alipiga ukelele na kunikumbatia kwa nguvu kifuani kwangu kuonesha kwamba tayari alishasalimu amri, mapigo ya moyo wake yakawa yanamuenda mbio kuliko kawaida, huku kila kiungo cha mwili wake kikiwa kimelegea kama mlenda.
Akaangukia pembeni, na mimi nikaangukia upande mwingine, huku kijasho chembamba kikinitoka. Ni hapo ndipo nilipogundua kwamba kuna majimaji yalikuwa yakinitoka pale kwenye jeraha langu, nikahisi huenda ni jasho.
Nilipopeleka mkono na kujishika kisha nikausogeza mkono machoni, nilishtuka kupita kiasi baada ya kugundua kuwa zilikuwa ni damu znanitoka pale kwenye jeraha langu.
“M ungu wangu,” nilisema huku nikiinuka harakaharaka na kusogea kwenye kioo cha dressing table ya kisasa iliyokuwa ndani ya chumba hicho cha Shamila. Bandeji yote ilikuwa imelowa kwa damu kuashiria kwamba kumbe zilikuwa zimeanza kunitoka muda mrefu uliopita.
Kumbe zile purukushani na Shamila zilikuwa zimenitonesha lakini cha ajabu, wala sikusikia maumivu yoyote mpaka muda huo. Nadhani utamu wa pambano letu la kirafiki ulifanya kazi kama sindano ya ganzi, kweli waliosema mapenzi yana nguvu ya ajabu hawakukosea.
Cha ajabu, eti tayari Shamila alikuwa akikoroma kwa uchovu, ikabidi nimtingishe kwa nguvu huku nikiliita jina lake. Alionekana kuwa mzito sana, akafumbua macho kivivu na kunitazama.
“Amka, angalia mwenzio kilichonitokea,” nilimwambia huku nikimuonesha kifua change, nikamuona jinsi alivyoshtuka, japokuwa mwili wake haukuwa na nguvu, alkijikongoja na kuamka, akawa anashangaa nini kimetokea.
Harakaharaka alichukua upande mmoja wa khanga na kujifunga akainuka na kunisogelea, akionesha kuwa na hofu kubwa ndani ya moyo wake.
“Pole Jamal, ooh! Mimi ndiyo nimekusababishia,” alisema na kunibusu, harakaharaka akatoka huku akikimbia, macho yangu yakawa yanamsindikiza kwa nyuma, japokuwa nilikuwa kwenye hali mbaya, nilijikuta nikitabasamu kwani kilichotokea ilikuwa sawa na nzi kufia kwenye kidonda, umbile lake likaacha mtikisiko adhimu na kunifanya nitingishe kichwa changu.
Muda mfupi baadaye, alirejea akiwa na kiboksi kidogo cha huduma ya kwanza kilichokuwa na alama ya msalaba mwekundu, akanilaza kitandani na kuanza kunihudumia. Cha ajabu zaidi, safari hii wala sikuhisi kabisa maumivu, nikawa muda wote namtazama Shamila usoni.
Waliosema mapenzi hayajaribiwi hawakukosea, japokuwa mwenyewe nilikuwa najiona kama namzuga Shamila, kwa yale ‘maujanja’ aliyonionesha, nilijikuta akianza kuugusa moyo taratibu, nikawa naendelea kumtazama wakati mwenyewe akinihudumia kwa unyenyekevu wa hali ya juu.
“Mbona unaniangalia usoni, mi nasikia aibu bwana,” alisema huku akinitazama kwa macho yake yaliyoonesha dhahiri jinsi alivyokuwa amechoka, wote tukatabasamu.
“Haya inuka nimalizie kukufunga bandeji,” alisema, ni hapo ndipo nilipogundua kwamba kumbe tayari alishamaliza kunifungua ile bandeji iliyokuwa imelowa damu na kunifunga nyingine, nikainuka kwa umakini kwani hii ilikuwa mara ya pili kujitonesha, akamalizia kunifunga, akarudia kunipa pole na kunibusu kwenye paji la uso wangu.
Akaanza kubadilisha lile shuka pale kitandani kwake ambalo nilikuwa nimelichafua, huku akiendelea kuniomba radhi kwa kunitonesha, nikawa nachekacheka tu.
“Muda umeenda sana, watakuwa wanakutafuta hospitali, inabidi nikurudishe haraka,” alisema, nikaangalia saa ya ukutani na kugundua kuwa tulikuwa tumetumia muda mrefu sana nje ya hospitali, kinyume na utaratibu kwani ikumbukwe kwamba nilikuwa nimelazwa wodini ila njama zangu na Shamila ndiyo zilizowezesha mimi kutoka.
“Naomba unisaidie kitu kimoja,” nilimwambia Shamila wakati akiandaa mazingira ya sisi kwenda kuoga, baada ya kuwa nimeshakunywa dawa za kutuliza maumivu alizonipa baada ya kumaliza kunifunga jeraha langu.
“Jambo gani mpenzi wangu wa moyo,” alisema Shamila huku akiniegamia kwa kudeka, nikamwambia naomba aniazime simu yake nihamishe baadhi ya mafaili kutoka kwenye kompyuta ili nikaendelee kuyapitia nikiwa wodini.
“Kwani ni mafaili gani? Halafu kwa nini uyakopi kwenye simu wakati nina laptop?” alisema, jambo lililonifurahisha sana kwani alikuwa amenirahisishia sana kazi, nikamzugazuga pale, akatoka na kwenda kwenye chumba cha pili, aliporudi alikuwa na laptop ndogo mkononi, akanipa huku tabasamu pana likiwa limechanua kwenye uso wake.
Nilimshukuru sana, harakaharaka nikaenda pale sebuleni, nikaiunganisha laptop na ile kompyuita ya mezani na kuanza kukopi mafaili yote yaliyokuwa kwenye ile hard disk niliyopewa na Firyaal, mdogo wake Shenaiza. Wakati mafaili yakiendelea kukopi, nilirudi chumbani kwa Shamila ambaye alikuwa amejilaza akinisubiri.
“Ahsante kwa yote uliyonifanyia Jamal, unajua mwanzo nilikuwa siamini kama kweli unanipenda, nilihisi kama mimi ndiyo nakulazimisha lakini kwa haya uliyonifanyia leo, hata sijui nikwambie nini, kwa kifupi elewa kwamba nakupenda sana na haijawahi kutokea mimi nikampenda mtu kama ilivyotokea kwako,” alisema Shamila kwa sauti yenye uwezo wa kumtoa nyoka pangoni, nikawa nachekacheka tu.
Aliinuka pale kitandani kichovu, tukaelekea bafuni ambapo aliniogesha kama mtoto mdogo huku akiwa makini maji yasiguse kidonda changu, alipomaliza, na yeye alioga kisha tukarudi chumbani ambapo harakaharaka tulivaa, tukatoka sebuleni ambapo nilienda kuchungulia pale kwenye kompyuta, nikakuta haijafika hata nusu kukopi.
“Inabidi nikukaangie mayai ule harakaharaka tuondoke,” alisema Shamila huku akimalizia kuvaa vizuri nguo zake za kazini, nikakosa cha kumjibu kwa sababu kiukweli nilihitaji muda zaidi ili nikopi yale mafaili yote.
Aliwasha jiko la gesi, akanikaangia mayai na dakika tatu tu baadaye, tayari yalikuwa tayari, akaniandalia mezani na juisi, nikaanza kula taratibu ili angalau nivutevute muda, akampigia simu dereva teksi na kumuelekeza atufuate.
Cha ajabu, wala hakuonesha kutaka kujua nilikuwa nikihangaika na nini kwenye kompyuta, akaendelea kujiandaa kwa kujipodoa kama ilivyo kawaida ya wanawake muda mfupi baadaye honi za gari zikasikika nje kuonesha kuwa tayari ile teksi aliyoiita ilishafika. Bado kompyuta haikuwa imefikisha hata asilimia ishirini na tano za kukopi, nikawa sina ujanja zaidi ya ‘ku-cancel’ palepale ilipoishia, nikiamini lazima kuna mambo mengi tu yalishaingia kwenye ile laptop.
“Wala usiwe na wasiwasi, hapa ni kama kwako, kama hujamaliza kazi zako nitakuandalia utaratibu mwingine tuje tena,” alisema Shamila, nikakualiana naye. Nikaichomoa ile laptop na kuzima kompyuta huku ile hard disc ikia ndani yake. Nilijua nafanya makosa lakini nikaamini Shamila hawezi kuiwasha hiyo kompyuta kwa sababu kwanza hakuwa akiijua password.
Harakaharaka tukatoka na kuingia ndani ya teksi, safari ya kurudi hospitalini ikaanza huku muda wote Shamila akiwa na furaha ya ajabu, akawa ananimwagia mvua ya mabusu.
Dakika kadhaa baadaye, tuliwasili hospitalini lakini mazingira ya pale yalinishtua mno, hofu kubwa ikaukumba moyo wangu tulipofika kwenye maegesho ya magari.
Je, nini kitafuatia?
 
Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 35
ILIPOISHIA:
Harakaharaka tukatoka na kuingia ndani ya teksi, safari ya kurudi hospitalini ikaanza huku muda wote Shamila akiwa na furaha ya ajabu, akawa ananimwagia mvua ya mabusu. Dakika kadhaa baadaye, tuliwasili hospitalini lakini mazingira ya pale yalinishtua mno, hofu kubwa ikaukumba moyo wangu tulipofika kwenye maegesho ya magari.
SASA ENDELEA...

Gari jeusi lililokuwa na vioo vya rangi nyeusi (tinted), Isuzu Bighorn lilikuwa limepaki kwenye maegesho hayo huku milango ya upande mmoja ikiwa wazi. Kumbukumbu zangu zilionesha kwamba hiyo haikuwa mara ya kwanza kuliona gari hilo machoni mwangu, nikawa najaribu kukumbuka ni wapi?
Shamila alimlipa dereva teksi na kutaka kushuka lakini nikamzuia, akabaki anashangaa. Niliendelea kulitazama lile gari na kwa makini, ghafla kengele ya hatari ikalia ndani ya kichwa changu baada ya kumuona mmoja kati ya watu waliokuwa ndani ya gari hilo.
Alikuwa ni kijana mmoja mwenye asili ya Bara la Asia, ambaye rangi ya ngozi yake ilikuwa ikifanana sana na ya Shenaiza pamoja na mdogo wake, kuonesha kwamba walikuwa na aina fulani ya unasaba kati yao. Nilipozidi kumtazama, nilimkumbuka kwamba mimi na yeye tulikutana kwenye matukio mawili tofauti, tena yote ya hatari yakimhusisha Shenaiza.
Tukio la kwanza lilikuwa ni siku nilipokuwa najaribu kumtorosha Shenaiza hospitalini, kipindi hicho wakati ndiyo kwanza tumeanza kufahamiana. Tukio la pili, ambalo liliyafanya mapigo ya moyo wangu yaniende kasi kuliko kawaida.
Lilikuwa ni tukio ambalo almanusra liukatishe uhai wangu baada ya kuvamiwa na watu nisiowafahamu kwenye foleni, maeneo ya Magomeni Mataa ambao walinishambulia vikali na kunijeruhi vibaya na kitu chenye ncha kali kifuani.
“Ni yeye! Ni mwenyewe...” nilijikuta nikitamka kwa nguvu, Shamila na yule dereva teksi wakabaki kunishangaa, wakiwa hawaelewi nilichokuwa namaanisha.
“Upo sawa kweli? Kama kuna tatizo si uniambie mpenzi?” alisema Shamila huku na yeye akiwa makini kutazama kule nilikokuwa naangalia, ghafla nikamuona amekazia macho pale kwenye lile gari, naye akawa ni kama ameona kitu.
Kwa bahati nzuri, ile teksi tuliyopanda ilikuwa pia na vioo vyenye tinted kwa hiyo haikuwa rahisi kwa watu waliokuwa nje kutuona. Tulitulia kwa dakika kadhaa, wote tukiwa tunawatazama wale vijana ambao walionekana kama wanajadiliana kitu huku macho yao yote yakiwa upande zilipokuwepo wodi, hasa ile niliyokuwa nimelazwa mimi.
“Unawafahamu?”
“Ndiyo, wana ukaribu na Shenaiza na ndiyo waliohusika kwenye jaribio la kutaka kuyakatisha maisha yangu.”
“Sasa hapa watakuwa wamefuata nini?”
“Kuna mawili, wanaweza kuwa wamemfuata Shenaiza au wamenifuata mimi.”
“Wakufuate wewe? Kwa kipi hasa?”
“Nimeshakwambia kuwa ni hawa ndiyo walioshiriki kwenye jaribio la kutaka kuyakatisha maisha yangu, yule mmoja namkumbuka vizuri kabisa.”
“Basi kama ni hivyo kwa nini tusiwapigie simu walinzi wa hospitali wawasiliane na polisi na kuwakamata? Mimi nina namba za mlinzi wetu wa kule getini,” alisema Shamila huku akitoa simu yake lakini nikamzuia.
Yule dereva teksi aliendelea kutulia kama haelewi chochote kinachoendelea, tukaendelea kujadiliana mle ndani ya teksi kwa muda mrefu huku nikiwa nimekosa kabisa amani.
Hakuna kitu kibaya maishani kama kuwaona wabaya wako lakini ukawa huna namna ya kulipa kisasi, nikaamua kufuata ule usemi maarufu ambao Waingereza hupenda kuutumia; ‘dont hunt what you can’t kill’ wakimaanisha usiwinde usichoweza kukiua!
Tukiwa bado tumetulia pale kwenye gari, ghafla kwa mbali tulimuona mtu aliyekuwa amevalia mavazi ya kidaktari akitoka kwenye wodi niliyokuwa nimelazwa, akatazama huku na kule kama anayetafuta kitu kisha akatembea harakaharaka mpaka pale kwenye lile gari, akawa anazungumza na wale watu waliokuwa mle ndani ya lile gari huku mara kwa mara wakigeuka kutazama kama kuna mtu aliyekuwa akiwatazama.
“Mungu wangu, nini kinachoendelea hapa? Mbona huyu aliyevaa kama daktari siyo mfanyakazi hapa hospitalini?”
“Siyo daktari? Kivipi? Na kama siyo daktari mbona amevaa nguo za kidaktari na ameingia hadi wodini?”
“Niamini ninachokwambia, madaktari wote wa hapa nawafahamu, huyu siyo mfanyakazi,” alisema Shamila kwa kujiamini, nikaiona hatari kubwa iliyokuwa mbele yangu. Kwa tafsiri nyepesi, mtu huyo alikuwa akishirikiana na wale watu waliokuwa ndani ya gari.
Kilichozidi kunishangaza, aliwezaje kuingia mpaka ndani ya wodi niliyokuwa nimelazwa bila kugunduliwa na walinzi wa hospitali hiyo? Kama angekuwa na nia ya kunidhuru ingekuwaje?” nilijikuta kijasho chembamba kikinitoka.
Waliendelea kujadiliana pale kwenye gari kisha tukamuona yule aliyejifanya daktari akivua koti lake jeupe na kuliweka kwenye siti za nyuma za gari, akaingia kwenye gari, milango ikafungwa na gari hilo ambalo muda wote lilikuwa likinguruma taratibu bila kuzimwa (silencer), likaanza kurudi nyuma likitafuta upenyo wa kutoka kwenye maegesho hayo.
Muda mfupi baadaye, liliondoka kwa kasi kubwa huku likitimua vumbi bila kujali kwamba eneo hilo lilikuwa ni hospitali na kulikuwa na wagonjwa waliokuwa wakihitaji utulivu, nikashusha pumzi ndefu na kuegamia kwenye siti niliyokuwa nimekaa, Shamila naye akafanya hivyohivyo.
“Sasa itakuwaje?”
“Sipo tayari kuendelea kulazwa kwenye hii hospitali, ni bora nikafie mbele ya safari, hapa si sehemu salama tena,” nilimjibu Shamila, akawa anatingisha kichwa kuonesha kuniunga mkono kwa kile nilichokuwa nakisema.
Tukiwa bado ndani ya teksi ile, nilishtuka sana baada ya kumuona Raya akifungua mlango na kutoka kwenye ile wodi niliyokuwa nimelazwa, mkononi akiwa amebeba kikapu kilichokuwa na chakula, akionesha kuwa na huzuni kubwa ndani ya moyo wake.
Baada ya kutoka wodini, alikaa kwenye benchi lililokuwa pale nje na kuweka kikapu chake chini, akawa anatazama huku na kule huku akionesha kuwa na wasiwasi mkubwa ndani ya moyo wake. Kwa kumtazama tu, japo nilikuwa kwa mbali, nilielewa kilichokuwa kikipita ndani ya kichwa chake, nikajikuta nikimuonea huruma sana.
Kumbe wakati nikimtazama Raya kwa huruma, Shamila naye alikuwa akinitazama usoni! Haya mambo ya mapenzi hatari sana, akashikwa na wivu mkali, akanizindua kwa kunigeuza kule nilikokuwa natazama na kunigeuzia kwake.
“Uko sawa?” aliniuliza huku hisia kali za wivu zikijionesha waziwazi kwenye uso wake.
“Nitakuwaje sawa katika mazingira kama haya? Naomba unisaidie jambo, kamuulize Raya yule daktari feki alipoingia wodini amesemaje?” nilimwambia Shamila, akaendelea kunitazama machoni huku akionesha dhahiri kwamba kuna jambo alikuwa anataka kuniambia.
Kwa shingo upande alishuka na kutuacha mimi na dereva teksi ndani ya ile teksi, aliposhuka tu, nilimwambia dereva aloki milango, tukawa tunamtazama Shamila anavyotembea kwa maringo kuelekea kule nje ya wodi alikokuwa amekaa Raya.
“Vipi kaka ndiyo unakaa hapa nini?” aliniuliza yule dereva teksi kwa lugha za vijana, akimaanisha kama mimi ndiye niliyekuwa nikitoka kimapenzi na Shamila, nikashindwa cha kumjibu kwani kwa muda huo akili yangu ilikuwa ikienda ‘resi’ sana, akaendelea:
“Duh! Si mchezo, utakuwa unafaidi sana, bonge la kifaa, ningekuwa mimi ningetangaza ndoa kabisa!”
Alikuwa na haki ya kusema hivyo kwa sababu kama nilivyoeleza awali, Shamila alikuwa mwanamke aliyejaaliwa uzuri wa kipekee mno, ukichanganya na umbile lake lililojazia kwa nyuma, hakuna mwanaume ambaye amekamilika angeweza kupishana naye bila kugeuka mara mbilimbili.
Japokuwa alikuwa amevaa nguo zake za kazini, uzuri wake haukuweza kujificha, nikajikuta kwenye wakati mgumu kwani Raya nilikuwa nampenda na alikuwa na mapenzi ya dhati kwangu, ukichanganya pia kwamba mimi ndiye niliyekuwa mwanaume wake wa kwanza maishani, nilijihisi kuwa sehemu ya maisha yake!
Niliendelea kutulia mle ndani ya teksi, Shamila akaenda mpaka pale Raya alipokuwa amekaa huku amejiinamia, alipomuona Shamila tu, harakaharaka alisimama na kumsogelea, akawa anamuuliza jambo ambalo japokuwa sikuwa nasikia, nilitambua kwamba ananiulizia mahali nilipokuwa mimi ‘mgonjwa wake’.
Tofauti kabisa na tulivyokubaliana, nilishangaa Shamila akimuonesha kwa kidole kwenye ile teksi niliyokuwemo, nikamuona Raya akiacha kila kitu palepale na kuanza kutimua mbio kuja kwenye ile teksi, Shamila akawa amesimama akimtazama. Nilijua wazi kwamba amefanya hivyo kwa sababu ya wivu.
Ghafla akiwa anakuja mbio, lile gari lilitokeza tena na kuja kwa kasi pale lilipokuwa limepaki awali, nikashtuka kugundua kuwa kumbe wale watu hawakuwa wameondoka, nikajua lazima watashtukia mahali nilipo kutokana na jinsi Raya alivyokuwa anakuja kwa kasi.
Je, nini kitafuatia?
 
Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 36
ILIPOISHIA:
Ghafla akiwa anakuja mbio, lile gari lilitokeza tena na kuja kwa kasi pale lilipokuwa limepaki awali, nikashtuka kugundua kuwa kumbe wale watu hawakuwa wameondoka, nikajua lazima watashtukia mahali nilipo kutokana na jinsi Raya alivyokuwa anakuja kwa kasi.
SASA ENDELEA...

“Naomba unisaidie kitu, huyu dada akifika hapa kuniulizia mwambie nimeshashuka kwenye gari nimeelekea upande wa wodi za wanaume, nikishuka funga huu mlango haraka,” nilimwambia dereva teksi ambaye alibaki ameduwaa, akiwa haelewi kinachoendelea.
Harakaharaka nikafungua mlango wa upande wa pili, nikashuka kwa kasi na kubingirika mpaka chini ya ile teksi, nikatulia huku mapigo ya moyo wangu yakinienda mbio kuliko kawaida. Nilimuona Raya akikimbia mpaka pale kwenye ile teksi, nikajikausha kimya.
“Kaka samahani, nimeelekezwa kuwa mgonjwa wangu yupo ndani ya hili gari, yuko wapi?” nilimsikia Raya akimuuliza yule dereva teksi huku akihema.
“Alikuwepo lakini ameshuka ameelekea kule kwenye wodi za wanaume,” yule dereva teksi alijibu kama nilivyomuelekeza. Nikasikia Raya akiguna akiwa ni kama haamini, mara nikaliona lile gari limekuja na kupaki palepale lilipokuwa limepaki mara ya kwanza, nikaiona miguu ya watu wakishuka na kusogea pale Raya alipokuwa amesimama akizungumza na dereva teksi.
Yaani kama mtu angepata wazo la kuchungulia chini ya ile teksi, basi huenda siku hiyo ndiyo ingekuwa mwisho wangu.
“Habari yako kaka,” nilimsikia mmoja kati ya wale wanaume walioshuka kwenye lile gari, Isuzu Bighorn.
“Safi!”
“Kuna mtu tunamtafuta, tunahisi yupo ndani ya hili gari lako,” alisema mwingine kwa sauti nzito, bila kusubiri kujibiwa, nikawasikia wakifungua milango ya teksi hiyo, yule dereva na Raya wakawa wanashangaa.
“Kwani nyie ni akina nani?” nilimsikia Raya akiwauliza lakini hakuna aliyemjibu, nikasikia wakibamiza milango ya teksi hiyo kwa nguvu, nadhani ni baada ya kufungua na kunikosa.
Nikawaona wakiondoka kwenye teksi hiyo bila kusema kitu, wakaelekea kwenye gari lao, wakapanda kisha nikaona gari likirudi nyuma na kuondoka tena.
“Kwani wale ni akina nani? Mbona wamekuja kisharishari namna hiyo?” nilimsikia Raya akimuuliza yule dereva teksi lakini hakuwa na majibu. Baada ya kuhakikisha wameshaondoka na gari lao, nilibingirika na kutoka uvunguni mwa gari.
Kwa bahati nzuri, pale kwenye maegesho ya magari palikuwa na lami kwa hiyo sikuchafuka sana, Raya akapigwa na butwaa kuniona nikitoka uvunguni mwa gari.
“Jamal! Ooh maskini pole mpenzi wangu, wale ni akina nani wanaokusaka kama jambazi?” alisema Raya huku akinisogelea na kunikumbatia huku akinimwagia mvua ya mabusu.
“Na muda wote huo ulikuwa umeenda wapi? Mbona nimekuja muda mrefu tu kukuletea chakula lakini haukuwepo?” Raya alizidi kunihoji, nikamwambia atulie kwanza nitamueleza kila kitu vizuri.
Yule dereva teksi akawa ananitazama kwa macho yaliyoonesha kuwa na maswali mengi yasiyo na majibu.
“Yule daktari alikuwa anasemaje kule wodini?” nilimuuliza Raya kimitego, akanijibu kwamba alikuwa akiniulizia kwa madai kwamba kuna kipimo inatakiwa nikafanyiwe nje ya hospitali, akawa anashangaa kwa nini sikuwepo wodini.
“Kwani wewe ulikuwa wapi mpaka madaktari wanakutafuta?” Raya aliniuliza tena, nikaendelea kumjibu vilevile kwamba atulie, nitamueleza kila kitu baadaye.
“Basi twende ukale nimekuletea chakula unachokipendaga,” alisema Raya, nikamjibu kwamba hospitalini hapo hapakuwa sehemu salama tena kwangu. Sikutaka kumuudhi Raya lakini pia sikutaka afahamu kwamba nilikuwa nimetoka nyumbani kwa Shamila na tayari mimi na yeye tulishaanzisha uhusiano wa kimapenzi.
“Naomba hicho chakula kaniletee kwenye gari, nichukulie na vitu vyangu mle wodini,” nilimwambia, akaondoka harakaharaka huku akigeuka huku na kule.
“Kaka kwani nini kinaendelea? Mbona sielewielewi?” alisema yule dereva teksi, naye nikamjibu tu kwa kifupi kwamba mambo yalikuwa magumu.
“Hawa jamaa mbona wamekuja kibabe sana halafu yule mmoja anaonekana kama ana mashine kwenye koti?” alisema yule dereva, nikashtuka sana kusikia kwamba kumbe mmoja kati yao alikuwa na bunduki, nikahisi maisha yangu yako hatarini zaidi.
“Au wanakudai?” yule dereva teksi alizidi kunihoji lakini bado sikumpa ushirikiano aliokuwa anautaka.
Akili yangu ilikuwa ikiwaza mambo tofauti kabisa, kwanza ilikuwa ni lazima nijue kuhusu biashara aliyokuwa akiifanya baba yake Shenaiza lakini pia ilitakiwa niwe makini kulinda maisha yangu kwani kwa ilivyoonesha, tayari walikuwa wameshtukia kwamba nawafuatilia.
Muda mfupi baadaye, Raya alirudi akiwa ameongozana na Shamila, wote wakaingia kwenye ile teksi, Raya akakaa pembeni yangu na Shamila akakaa siti ya pembeni ya dereva.
“Nimepata wazo, unajua hapa kuna wodi za ‘private’ ambazo zinalindwa, unaonaje tukikuhamishia huko maana hali imeshachafuka,” alisema Shamila, wazo ambalo kwa kiasi fulani niliona kama ni la msingi.
“Kwani huyu ni nani?” Raya aliuliza baada ya kumsikia Shamila.
“Huyu ndiyo nesi anayesimamia matibabu yangu lakini ameguswa na matatizo yangu na ndiyo maana ameamua kunisaidia kwa karibu. Shamila, kutana na Raya, mchumba wangu,” nilisema kwa kujiamini, nikamuona Shamila akitoa tabasamu la uongo.
Dereva teksi kwa kuwa alikuwa anajua mchezo unavyoenda, alijifanya yuko bize kurekebisharekebisha vitu pale kwenye ‘dashboard’ ya gari lake.
“Nimefurahi kukufahamu,” Raya alijibu kwa kifupi, Shamila akanyoosha mkono na kumpa, wakashikana kwa sekunde chache na kuachiana. Ilikuwa ni lazima nifanye vile na kusimama kama mwanaume kwani nilishaanza kumuona Raya akikosa raha.
“Unalionaje wazo alilolitoa nesi?” nilimuuliza Raya, naye akaliunga mkono.
“Basi tufanye hivyo haraka, wanaweza kurudi tena,” nilisema, wote tukashuka kwenye teksi harakaharaka na kuanza kumfuata Shamila ambaye ndiye aliyekuwa akituongoza.
“Usitembee haraka hivyo, utajiumiza tena kidonda,” alisema Raya huku akitaka kunipokea laptop niliyokuwa nimeing’ang’ania lakini nikamkatalia. Muda mfupi baadaye tayari tulikuwa kwenye lifti, tukapanda mpaka ghorofani kulikokuwa na wodi za private.
Mazxingira ya wodi hizo yalikuwa mazuri kwa sababu kwanza kulikuwa na walinzi wenye silaha koridoni, halafu milango ya wodi ilikuwa imara, kidogo nikawa na amani moyoni mwangu. Tulipoingia tu wodini, harakaharaka niliiwasha ile laptop na kuanza kuyaangalia yale mafaili machache niliyokopi kutoka kwenye ile ‘hard disk’.
“Hivyo ni vitu gani unavyoviangangalia kwenye hiyo laptop?” Raya aliniuliza wakati akiandaa chakula huku Shamila naye akiwa bize kuwekaweka vitu vyote vizuri ndani ya wodi hiyo, nikamdanganya Raya kwamba kuna kazi nilikuwa nimetumiwa kutoka kazini.
“Mh! Kutoka kazini? Nani anayeweza kukupa kazi wakati watu wote wanajua kwamba unaumwa? Isitoshe asubuhi nilipitia kule kazini na kila mtu akawa anakupa pole,” Raya alizidi kunibana, nikamwambia nitamfafanulia baadaye.
Niliendelea ‘kuperuzi’ yake mafaili, moja baada ya jingine. Kama nilivyokuwa nimeona awali, yalikuwa yamejaa taarifa za watu mbalimbali, wakubwa kwa wadogo, yakiwa na taarifa kuhusu hali zao za kiafya na viungo mbalimbali kwenye mwili, bado nikawa sielewi.
Niliendelea kuchimba kwa undani, taratibu nikaanza kugundua mambo ambayo ama kwa hakika yalinishangaza sana. Kwa jinsi ilivyoonesha, kulikuwa na mtandao mpana sana wa watu kutoka hapa nyumbani Tanzania, India, Marekani, Uingereza na nchi za kiarabu ambao ulikuwa ukihusisha hospitali kubwakubwa duniani.
Nilipoendelea kufuatilia kwenye mafaili yake, nikaanza kugundua kwamba kumbe kulikuwa na biashara ya viungo vya binadamu ilikuwa ikifanyika katika nchi mbalimbali, kwamba baba yake Shenaiza alikuwa akiwakusanya watu kutoka maeneo mbalimbali ya nchi na kuwasafirisha kwenda kwenye hospitali kubwakubwa duniani kwa ajili ya kuchangia viungo mbalimbali vya miili yao.
Kilichonishangaza sana ni kugundua kuwa wengi walikuwa wakisafirishwa kutoka Tanzania, wakiwa hawajui chochote kinachoenda kuwatokea. Mbaya zaidi, kulikuwa na watu ambao wameandikwa kwamba wanaenda kuchangia moyo, ninavyofahamu mimi binadamu anakuwa na moyo mmoja tu, kwa hiyo akichangia inakuwaje?
Nikajiuliza pia kwamba kuna baadhi ya watu ilionesha kwamba wanaenda kuchangia ubongo, sasa ukichangia ubongo na wewe nini kinakutokea? Unawezaje kubaki ukiwa hai? Kengele ya hatari ikalia ndani ya kichwa changu, nikawa nahisi pengine nipo ndotoni.
 
Anko obe kasema hujaona kule na tumosa ...

Story leo weka chache mama d miko ya 25

Na mm ndo story ya kwanza hapa make nakumbuka na ya mwanafunzi mchawi kitambo ilinishinda
Sijawaona wapi tena na tumosa jaman me naomba tu niwawekee nitakapoishia ni hapo yaan sasa hivi nitakuwa mvivu kuingia jf yenyewe nimeingia tu hapa mara moja kuwawekea story najua adha ya arosto ya story nimewaonea huruma watu na arosto najua maumivu yake
 
Sijawaona wapi tena na tumosa jaman me naomba tu niwawekee nitakapoishia ni hapo yaan sasa hivi nitakuwa mvivu kuingia jf yenyewe nimeingia tu hapa mara moja kuwawekea story najua adha ya arosto ya story nimewaonea huruma watu na arosto najua maumivu yake
Ndo umekatazwa ?? Ila nyie
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom