Makapuku Forum

Makapuku Forum

tumblr_m8i9y2qXYn1rbf36no1_500.gif
Cha arumeru..
 
Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 24
ILIPOISHIA:
Treni ilizidi kushika kasi, ikafika kipindi nikawa nahisi kwamba haikanyagi kwenye reli bali inapaa angani kwa jinsi ilivyokuwa ikienda kasi. Ghafla, nilipogeuka huku na kule, nilishtuka kugundua kwamba nilikuwa nimebaki peke yangu kwenye treni hilo, sikukumbuka kama kuna sehemu lilisimama, nikawa najiuliza wale abiria wengine wameenda wapi?
SASA ENDELEA...

Kuna wakati nilihisi pengine huenda nilikuwa kwenye ndoto lakini bado sikuwa na uwezo wa kuthibitisha kwamba ile ilikuwa ni ndoto, maisha halisi au kitu gani, kila kitu kilikuwa gizani. Treni lilizidi kushika kasi, moshi mwingi ukiwa unazidi kuingia ndani na kufanya hata ule mwanga hafifu niliokuwa nauona awali nao umezwe na moshi huo mweusi.
Ghafla, nilihisi kama naguswa na mtu pembeni yangu, nikajikuta nikiruka kwa hofu kubwa, nilipogeuka na kumtazama aliyenigusa, alionesha ni mwanamke kwa jinsi alivyokuwa amevaa lakini uso wake alikuwa ameuinamisha chini.
“Jamal! Jamal, ni wewe?” alisema yule mtu kwa sauti ya chini lakini ambayo ilisikika vizuri licha ya kelele ya vyuma vya treni lile, muungurumo mkubwa na upepo uliokuwa unavuma.
Badala ya kuitikia, niligeuka na kumtazama kwa hofu kubwa mno, yeye wala hakugeuka kunitazama zaidi ya kuendelea kujiinamia vilevile, akisubiri majibu kutoka kwangu. Licha ya zile kelele na yeye mwenyewe kuzungumza kwa sauti ya chini, bado niliweza kuitambua vyema sauti hiyo, haikuwa ngeni kabisa masikioni mwangu.
“Mbona hunijibu!” aliuliza tena lakini tofauti na mwanzo, sauti yake ilisikika kwa nguvu ikiambatana na mwangwi ambao uliyaumiza masikio yangu.
“Wewe ni nani?” nilimuuliza lakini nikashangaa sauti haitoki, nikakumbuka sheria za huko ambapo haraka nilifumba mdomo na kuzungumzia moyoni, sauti kubwa ikasikika lakini badala ya kunijibu, nikamuona akiinua uso wake taratibu na kunigeukia.
“Mungu wangu!” nilijisemea kwa hofu kubwa. Kwa msaada wa mwanga hafifu uliokuwepo ndani ya treni hiyo, niliweza kumtambua kwamba yule mtu alikuwa ni Shenaiza lakini tofauti na yule ninayemfahamu, maeneo yake ya kwenye macho yalionesha kutokuwa na macho ya kawaida kama binadamu wengine, yalikuwa meusi tii ambayo hata sijui niyafananishe na nini.
“Ni mimi Shenaiza, au umenisahau? Nataka kukufuata huko uliko, nimechoka maisha ya duniani, nichukue Jamal!” alisema na kuanza kugugumia kwa kilio kilichoonesha kwamba yupo kwenye maumivu makali mno.
Nilishindwa kuelewa kilichokuwa kinaendelea, muda mfupi uliopita nilikuwa nikizungumza naye katika kile mwenyewe alichoeleza kwamba yupo ndotoni na ameniona mimi kama mzimu, lakini muda huo tulikuwa tukizungumza kwa kawaida, akiniambia kwamba anahitaji nimchukue!
Kwanza nilishangaa, nimchukue kumpeleka wapi? Na hapo tulipokuwepo ni wapi? Na yeye alitokea wapi kwa sababu wakati mimi napanda kwenye treni hilo la ajabu, hakuwepo, aliingiaje? Nilijiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu.
“Mbona unanishangaa hivyo Jamal?” aliniuliza huku mkono wake mmoja akinishika shingoni, nikashangazwa na jambo jingine kwamba mwili wake ulikuwa wa baridi kuliko kawaida. Nilitamani kupiga kelele kwa hofu niliyokuwa nayo, nilihisi kama nimekutana na kiumbe wa ajabu mwenye sura ya kibinadamu na sasa alikuwa anataka kuyakatisha maisha yangu.
“Usiniogope Jamal! Hata mimi mwanzo nilikuwa nakuogopa lakini hushangai sikuogopi tena?”
“Kwani hapa ni wapi Shenaiza na wewe umefikaje huku?”
“Mh! Hata mimi sielewi hapa ni wapi lakini nafikiri tunaelekea sehemu nzuuuri ambayo ndiyo itakuwa makazi yetu ya milele, si unajua duniani tunapita tu?”
“Sijakuelewa, kwa hiyo hapa siyo duniani?”
“Siyo duniani Jamal, duniani si kule tulikokuwa tunaishi siku zote? Kwani unaona hapa kunafanana na kule?”
“Sasa kama siyo duniani ni wapi na wewe imekuwaje uje huku?”
“Sijui hapa ni wapi, mimi nimekuja huku kwa sababu nimechoka kuishi, yaani kila siku wananichoma dawa za usingizi, nikiamka tu wananichoma tena, leo nimeamua kujiovadozi kwa makusudi ili nife?”
“Niniii? Shenaiza, unazungumzia nini mbona sikuelewi?”
“Nimeamua kukufuata Jamal, kwa kuwa wewe ulikufa na mimi nikiwa ndiyo chanzo, nimeamua na mimi nife tu.”
“Lakini mimi sijafa Shenaiza, mimi niko hai.”
“Ungekuwa hai ndiyo ungekuwa huku? Acha kujidanganya Jamal!”
“Hapana sijafa! Mimi sijafa! Niko haiii,” nilisema kwa sauti kubwa iliyofuatiwa na kilio.
***
Hali ilikuwa ya patashika nguo kuchanika ndani ya makazi ya siri ndani ya jumba la kifahari la baba yake Shenaiza, lililokuwa Kurasini. Hakuna ambaye alielewa nini kimetokea kwa sababu kama ilivyo kawaida, Shenaiza alizinduka kutoka usingizini baada ya dawa alizokuwa amedungwa awali kuisha nguvu.
Tofauti na awamu zote, safari hii alipozinduka usingizini, alijikokota na kuinuka kutoka kitandani kwake, akasogelea mpaka kwenye kabati lililokuwa ndani ya chumba hicho. Mfanyakazi maalum aliyepewa jukumu la kuhakikisha anapata huduma zote muhimu, alishtuka kumuona akiwa amefungua kabati, ikabidi amuwahi na kumlaza kitandani.
“Nasikia njaa sana, kaniletee chakula,” alisema Shenaiza, harakahara yule mhudumu akatoka kwenda kumletea chakula kwani tayari kilishaandaliwa kwa ajili yake. Alipotoka tu, Shenaiza alisimama na kurudi tena pale kabatini.
Muda mfupi baadaye, alichukua kichupa kidogo pamoja na bomba la sindano, harakaharaka akarudi pale kitandani kwake na kujilaza, akavificha vile vitu chini ya mto. Mhudumu alipoingia akiwa na sinia lililokuwa limejaa vyakula vya kila aina, Shenaiza alitulia kimya kama hajui kinachoendelea.
Yule mhudumu alimuandalia chakula ambapo tofauti na alivyotegemea kwamba atakula kwa sababu alikuwa na njaa kama mwenyewe alivyodai, Shenaiza alishikashika tu kisha akamwambia atoe.
“Mbona sasa hujala?”
“Hamu ya kula imeniisha ghafla, weka nitakula baadaye.”
“Lakini dada, mimi nilikuwa na ushauri mmoja juu yako. Unajua baba anakupenda sana ila anase...”
“Shiii! Ishia hapohapo, we toa vyakula vyako kisha uondoke, sitaki kusikia kitu chochote kwa sasa, niache,” alisema Shenaiza kwa sauti iliyoonesha kutokuwa na masihara hata kidogo.
Yule mhudumu alikusanya vyombo vyake na kutoka nje, akawaacha walinzi wakiwa mlangoni hapo kumlinda Shenaiza kama walivyoelekezwa na baba yake.
Baada ya mhudumu huyo kutoka, harakaharaka Shenaiza alichukua kile kichupa kilichokuwa na maandishi yaliyosomeka Diazepam, akakitingisha na kuchukua bomba la sindano, akavuta dawa nyingi kiasi cha kulifanya bomba lote lijae, akachukua mtandio wake na kujifunga mkononi kwa nguvu, akatafuta mshipa mkubwa wa damu.
Akajichoma na kuanza kuisikumia ile dawa ndani ya mshipa wake wa damu. Hakuweza kuimaliza yote, aliposukuma kiasi cha nusu ya bomba kuingia mwilini mwake, usingizi mzito ulimpitia, akalala huku bomba hilo likiwa bado linaning’inia mkononi.
Yule mhudumu aliporudi kwa mara ya pili kuja kumalizia vyombo vichache vilivyosalia, alishtuka kupita kiasi baada ya kuona damu nyingi ikiwa inatoka kwenye mkono wa Shenaiza na kulowanisha shuka lake huku mwenyewe akitapatapa kama anayetaka kukata roho, mapovu yakimtoka kwa wingi mdomoni na puani.
Harakaharaka, huku akilia, aliwaita walinzi ambao nao walimuita daktari wa familia hiyo, muda mfupi baadaye wote wakawa wamejaa ndani ya chumba hicho wakijaribu kuokoa maisha ya msichana huyo lakini ilionesha kwamba tayari walikuwa wamechelewa.
Je, nini kitafuatia?
 
Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 25
ILIPOISHIA:
Harakaharaka, huku akilia, aliwaita walinzi ambao nao walimuita daktari wa familia hiyo, muda mfupi baadaye wote wakawa wamejaa ndani ya chumba hicho wakijaribu kuokoa maisha ya msichana huyo lakini ilionesha kwamba tayari walikuwa wamechelewa.
SASA ENDELEA...

Shenaiza alikuwa akitapatapa, akirusharusha mikono na miguu, mapovu mengi yaliyochanganyikana na damu yakimtoka mdomoni na puani, harakaharaka Shenaiza alitolewa kwenye chumba alichokuwa amefungiwa na kulazwa juu ya kitanda cha magurudumu, akakimbizwa kwa kasi mpaka nje na kupakizwa kwenye gari.
Muda mfupi baadaye, gari lililombeba lilikuwa tayari lipo barabarani, likikimbia kwa kasi kubwa, taa zote za mbele zikiwa zimewashwa huku yule daktari akiwa bize kuhakikisha anaokoa maisha ya Shenaiza.
Japokuwa baba wa msichana huyo mrembo hakuwepo nchini kwa muda huo, tayari taarifa zilimfikia huko alikokuwa juu ya kilichomtokea binti yake.
Naye akajikuta akichanganyikiwa mno kwani Shenaiza alikuwa mtu muhimu sana kwake. Bila yeye, mambo yake mengi yangekwama, jambo ambalo hakuwa tayari kuona linatokea. Muda hohuo aliwapigia simu wasaidizi wake na kuwaambia ni lazima wafanye kila kinachowezekana kuhakikisha anapona.
Baada ya kufikishwa hospitalini, harakaharaka Shenaiza alilazwa juu ya kitanda chenye magurudumu, akakimbizwa kupelekwa kwenye wodi ya wagonjwa mahututi, madaktari kadhaa, wakisaidiana na yule daktari wa familia, walianza kuhaha kuhakikisha wanaokoa maisha ya msichana huyo.
***
“Lakini mimi sijafa Shenaiza, mimi niko hai.”
“Ungekuwa hai ndiyo ungekuwa huku? Acha kujidanganya Jamal!”
“Hapana sijafa! Mimi sijafa! Niko haiii,” nilisema kwa sauti kubwa iliyofuatiwa na kilio.
“Sasa unalia nini Jamal? Kwani kufa ni jambo la ajabu? Mbona mimi mwenyewe nimeamua kuyakatisha maisha yangu?”
“Hapana, mimi bado nina ndoto zangu nyingi sana sijazitimiza maishani. Isitoshe umri wangu bado mdogo, familia yangu haijafaidi matunda yangu hata kidogo, bado sijaoa wala sina mtoto hata mmoja, itakuwaje nife?”
“Kwani wote wanaokufa wanapenda wenyewe kufa? Usikufuru Jamal, inabidi umshukuru Mungu kwa kila kitu, naamini hakuna kilichoharibika, si utakuwa hapa na mimi?”
“Hapana Shenaiza, hapanaaa!” nilizidi kupingana naye, akazidi kuning’ang’aniza kwamba eti nilikuwa tayari nimekufa na hilo halikuwa tatizo kubwa kwa sababu hata yeye aliamua mwenyewe kufa.
Bado akili yangu ilikuwa na maswali mengi yaliyokosa majibu. Unajua mtihani ambao Mungu ametupa sisi wanadamu, ni kushindwa kuelewa kinachotokea baada ya mtu kufa. Kama angekuwepo mtu hata mmoja, ambaye angekuwa na uwezo wa kuelezea kwa ufasaha kinachotokea baada ya mtu kufa, pengine angewasaidia sana binadamu kupunguza hofu ya kifo inayowatesa.
Kwangu mimi hali ni tofauti, hata sielewi nitumie maneno gani kuelezea kilichotokea lakini naamini kwamba ukiendelea kunifuatilia msomaji wangu, utaelewa ni nini hasa kilichotokea na pengine kitakusaidia na wewe kuweza kuyaelewa maisha na kifo katika upeo mpana zaidi, pengine kuliko ulivyokuwa unafikiria mwanzo.
Bado mjadala mkubwa kati yangu na Shenaiza, ulikuwa ni juu ya suala la kifo. Msichana huyo alikuwa akisisitiza kwamba mimi na yeye tumekufa na ndiyo maana tulikuwa kule lakini mimi nikawa naendelea kumbishia kwamba sijafa kwa sababu bado nilikuwa na akili zangu timamu.
Nilikuwa naelewa vizuri kila kilichokuwa kinaendelea, jambo ambalo bado hakuna ushahidi wa kutosha kwamba wafu huwa wanaelewa kinachoendelea. Nitakuja kulifafanua hili zaidi hapo baadaye.
Basi ile safari ambayo hata sijui mwisho wake ulikuwa ni wapi, iliendelea, treni lilizidi kuchanja mbuga, moshi ukazidi kuongezeka mle ndani sambamba na kelele za vyuma kugongana. Hata hivyo, bado niliweza kumsikia vizuri Shenaiza kwa kila alichokuwa anakizungumza.
Bado nilikuwa na hamu ya kutaka kujua ni nini kilichotokea mpaka na yeye aseme amekufa kwa sababu mpaka muda huo, bado nilikuwa gizani. Nilifumba macho na kujaribu kuvuta picha kwa nguvu, nikashtuka kuliko kawaida kujikuta nimetokezea kwenye wodi nyingine tofauti na ile ambayo mwili wangu ulikuwepo.
Nilipotazama vizuri ndani ya wodi hiyo, kama ilivyokuwa mwanzo kule kwenye ile wodi niliyokuwa nimelazwa, madaktari wengi walikuwa wakihangaika kuokoa maisha ya mtu aliyekuwa amelala juu ya kitanda, akionesha kabisa kwamba alikuwa kwenye hatua za mwisho za uhai wake.
Nilipomtazama vizuri mtu huyo, hakuwa mwingine bali Shenaiza ambaye sekunde chache zilizopita nilikuwa nimekaa naye kwenye siti moja ya treni la ajabu. Ni hapo ndipo nilipoelewa kile alichokuwa anakisema Shenaiza kwamba ameamua kuyakatisha maisha yake.
Madaktari walikuwa wakihangaika mno, Shenaiza akaunganishwa kwenye mashine ya kumsaidia kupumua huku dripu nyingi zikitiririka kwa kasi kuingia kwenye mishipa yake ya damu.
Kibaya zaidi, kadiri muda ulivyokuwa unazidi kusonga mbele ndivyo mashine maalum ya kusoma mapigo ya moyo aliyokuwa ameunganishiwa msichana huyo na kuunganishwa kwenye kompyuta, ilivyokuwa ikionesha kwamba mapigo yake ya moyo yalikuwa yakishuka kwa kasi kubwa, jambo ambalo lilimaanisha kwamba muda mfupi baadaye, mapigo ya moyo yatasimama kabisa na kukata roho.
“Hapana! Hapana... Shenaiza noooo!” nilipiga kelele kwa sauti kubwa, nikajikuta muda huohuo nimehama kutoka kule hospitalini mpaka ndani ya treni, nikageuka kumtazama Shenaiza, nikamuona akiwa amejikunyata na kujiinamia, kama anayesubiri jambo fulani litokee.
Sijui nilipata wapi nguvu lakini nilijikuta nikimshika Shenaiza na kuanza kumtingisha kwa nguvu, akashtuka kwa nguvu na kunitolea macho akionesha kukasirishwa na kitendo changu cha kumshtua.
Wakati ananitazama, alianza kupiga chafya mfululizo, akili yangu ilihama tena na kurudi wodini, nikapigwa na butwaa baada ya kumuona mgonjwa akipiga chafya mfululizo huku damu ikimtoka puani na mdomoni kwa mabongemabonge!
“She is back into her consciousness! Ooh thanks God! She was almost dead!” (Amerejewa na fahamu zake! Ooh ahsante Mungu, alishafikia hatua ya kufa) nilimsikia daktari mmoja akipaza sauti mle wodini, nikaona nyuso za wote waliokuwemo ndani ya wodi hiyo ya wagonjwa mahututi zikianza kuonesha matumaini makubwa, tofauti kabisa na mwanzo.
Harakaharaka Shenaiza alizungukwa pale kitandani, kazi ya kunusuru maisha yake ikazidi kupamba moto. Nikiwa naendelea kushangaashangaa, nilishtuka nikiguswa begani, akili zangu zikarudi tena kule kwenye treni.
“Kwa nini umeniokoa? Ungeniacha nife,” alisema Shenaiza huku akilia, nikatanua mikono yangu kama ishara ya kumkumbatia, akajilaza kifuani kwangu na kunikumbatia kwa nguvu huku akiendelea kulia.
Nikiwa katika hali ileile, nilishtuka muda mfupi baadaye na kujikuta nikiwa nimejikumbatia mwenyewe. Shenaiza hakuwepo tena, nikageuka huku na kule, hakukuwa na mtu mwingine yeyote kwenye lile treni, nilibaki peke yangu huku mwanga wa ile taa iliyokuwa ndani ya behewa nililokaa ukizidi kufifia, muda mfupi baadaye giza nene likatanda kila mahali.
“Jamal! Jamal! Jamal!” nilishtuka baada ya kuisikia tena ile sauti nzito ya kutetemeka, iliyoniita kwa mara ya kwanza kabisa, ikiniita tena, ikafuatiwa na vicheko vya kutisha vya watu wengi, nikawa nageuka huku na kule lakini sikuona chochote zaidi ya giza nene, hofu kubwa ikatanda moyoni mwangu.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom