Husna anatuleteaaa kitu...
"Twaha, nenda nyumbani. Usihuzunike sana kuhusu mimi. Nitaishi tu kwa kuwa uhai wangu na wa baba vilikuwa vitu viwili tofauti. Hakuna kilichobadilika zaidi ya uwepo wake baba yangu. Nenda usimtie mashaka shangazi yako." Aliongea kwa huzuni sana. Moyo uliniuma nikitamani kuwa nae. Umri wake ulikuwa mdogo kama mimi. Nilijiuliza kwanini hakujitokeza jirani hata mmoja wa kuwa naye? Lakini mwishowe nakumbuka German alitabasamu na kuingia ndani akinisihi niondoke nimuache. Hakika siku ile nilibaki nimeganda nikiwa mwingi wa maumivu kana kwamba mimi ndiye nilifiwa. Daaaah! Masikini German...leo na yeye ameelekea kule alipotangulia baba yake miaka 12 nyuma.
Niliondoka kwa upweke moyo uliniuma lakini sikuwa na jinsi. Siku hiyo nilimkuta shangazi ananisubiri nje akiwa amekasirika kupita maelezo. Nilipofika kabla sijasema lolote alinivaa na kuanza kuniadhibu. Alinichapa sana na kunifokea kwa tabia ya kuchelewa kurudi. Nililia huku nikimsihi shangazi anisikilize kwanza. Lakini hakuniacha mpaka alipotosheka moyoni kuniadhibu ndipo aliniweka kitako na kuniuliza.
"Haya! kwanini umechelewa na kunitia roho juu hata ukarudi usiku?"
Ndipo nilipomwambia kilichotokea hata nikachelewa. Shangazi alionesha sikitiko na kunionya siku nyengine niwe narudi kutoa taarifa inapotokea hali kama hiyo. Nilimuitika, usiku ukapita.
Siku ya pili baada ya kumaliza kazi nilichemsha magimbi na kumuomba shangazi ruhusa ya kwenda kula na rafiki yangu German. Shangazi aliniruhusu na hapo niliyatwaa magimbi sufuriani na kwenda kwa kina German.
"German......! Germaaaan..! Germaaaaaan Machineeee!!" Niliita lakini nyumba ilibaki kimya. Nilizunguka na kuchungulia chumbani kwake kupitia matundu ya ukutani. Ndani hakukuwa na dalili ya uwepo wa mtu. Wasiwasi ulinishika na kufungua mlango wa mianzi uliosindikwa nje. Niliingia ndani na kuendelea kuita na kumtafuta bila mafanikio. Lakini nikiwa napepesa macho huku na kule chumbani kwake ndipo nilipoiona picha yenye michoro minne iliyonistua sana na kubaki nimeikodolea kwa mshangao. Kulikuwa na michoro ya bendera mbili, moja ya Ujerumani na nyengine ya Tanzania huku katikati kukiwa na mchoro wa mkono wa mtu ulioshika kalamu na chini yake kulichorwa jeneza. Ilikuwa picha ngeni machoni mwangu. Nilikumbuka mara ya mwisho kuingia chumbani mwa German sikuiona michoro kama hiyo. Nilisimama nikijaribu kuisoma na kuifasiri bila majibu. Nilipoisogelea zaidi ndipo niligundua kila mchoro ulio ndani ya ile picha ulipewa namba sita chini yake. Kati ya zile namba sita kuna mbili ziliwekewa alama ya tiki na mbili hazikuwekewa. Mchoro wa bendera ya Tanzania ulipewa namba sita yenye tiki pamoja na ule wa mkono wenye kalamu. Lakini mchoro wa bendera ya Ujerumani ilipewa namba sita bila alama nyengine yoyote sambamba na ule wa jeneza. Duwazo lilinivaa nikabaki nimeduwaa na sufuria la magimbi mkononi kabla sijazinduliwa na sauti ya German.
"Twaha! karibu."
Nilistuka baada ya kujisahau kwa muda na kugeuka nyuma sauti ilipotokea. Nilimuona German akiwa amelowa jasho. Nilikumbuka kuwa itakuwa ametoka kusimama juani kama kawaida yake. Lakini nilijiuliza mbona sikumuona pale kwenye kichuguu anaposimamaga? Lakini shauku ya michoro ya picha ya ajabu ukutani ilifuta maswali mengine yote kichwani mwangu.
"Asante German, samahani kwa kuingia bila ruhusa nilipatwa wasiwasi baada ya kukwita kwa muda mrefu."
"Usijali Twaha, karibu mkekani." Alinionesha uchangamfu kana kwamba siye aliyefiwa. Nilikaa na kuiweka sufuria ya magimbi mkekani huku nikiendelea kuitazama ile picha.
"Hayo ni maono ya mwisho ya mkono wa baba kabla hajafariki." Aliongea German kwa sauti ya chini huku naye akiitazama ile picha.
"Sijakuelewa una maana gani German." Nilimuuliza huku nikimtazama. Uso wake aliuelekezea pale ukutani na macho yake yakaganda kwenye ile picha.
"Twaha, baba yangu alikuwa na kipawa kikubwa cha maono mkononi mwake. Na kwa kuwa mkono haukupewa fursa ya sauti, basi aliyasema kwa michoro. Na hiko ndicho kipawa chake hakika japo hakuwahi kuchora vitu vya wakati wake. Siku zote alichora vitu vya wakati uliopita ama unaokuja. Ingawa mwenyewe aliwahi kunambia hakuwahi kufikiria kichwani kitu chochote alichowahi kuchora wala hakuwahi kukiota. Lakini huwezi amini Twaha kupitia michoro ya baba ndani yake kuna maisha yangu. Mimi sina kipawa mkononi mwangu wala siwezi kuchora nikiwa macho. Daah! Twaha sijui hata nikueleze vipi ili unielewe kwa haraka lakini naamini siku moja utanielewa vizuri hata nisiponyanyua mdomo kukuelewesha." Alinena huku machozi yakilenga macho yake yaliyoganda pasipo kupepesa. Alinyamaza German na kunigeukia kisha akachanua tabasamu usoni mwake.
"Twaha, wewe ni rafiki yangu wa kweli. Najua nimekuchanganya kwa kukwambia kuwa baba yangu hakuwahi kuchora vitu vya wakati wake bali alichora vitu vya wakati uliopita na ule ujao. Lakini hapohapo nimekwambia kuwa ndani ya michoro ya baba yangu kuna maisha yangu. Unaweza kujiuliza kivipi? Lakini usiwe na shaka Twaha nitakufafanulia vyema maana yake hususani kupitia huu mchoro." Aliongea German huku akisimama na kuniashiria nami nisimame na kumfata. Tuliingia kwenye chumba cha pili ambacho kilikuwa cha marehemu baba yake. Nilishangaa kuona rangi rangi zimemwagika chini sambamba na vijiti. Pembeni kulikuwa na godoro dogo chakavu sambamba na karatasi kubwa nyeupe.
"Twaha hapa ndipo nilipomkuta baba amelala usingizi wa mwisho baada ya kumaliza kuuchora ule mchoro uliokushangaza. Kumbuka Twaha, alikuwepo baba kabla yangu na pia ameondoka kabla yangu. Hiyo ndiyo maana ya maisha yangu kuishi ndani ya michoro ya baba. Kila alichokichora kilinihusu ingawa alianza kuchora kabla ya kuzaliwa kwangu lakini mchoro wake wa mwisho umehitimisha maisha yangu yote yaliyosalia. Lakini nasikitika baba yangu hakujua maana ya mchoro wake wa mwisho kwa kuwa alimaliza kuuchora usiku na alifariki usiku ule ule pasipo kunionesha. Twaha, hii ni elimu inayohitaji utulivu wa imani na fikra pana. Ukweli baba yangu alipokuwa anachora alichora bila kujua nini akichoracho. Lakini mkono wake ulifanya kitu ambacho binafsi niliweza kukielewa na kumpa fasiri ambayo ilimshangaza siku zote ingawa awali hakuniamini hadi pale nilipomfasiria picha ya Johannes Kepler ambayo aliichora kabla ya kuzaliwa kwangu." Aliongea German Machine na kuzidi nistaajabisha kwa maneno yake. Wakati huo alikuwa amechutama na kufungua sanduku kubwa la chuma lililokuwa pembeni mwa kile chumba.
"Hili ni sanduku la baba yangu alilopewa na wajerumani miaka 12 kabla ya kuzaliwa kwangu. Kipindi hiko baba yangu alikuwa anaishi jijini Dar es salaam. Hakuwa mlemavu wa wala hakuwa fukara kama sasa ingawa pia hakuwa tajiri. Shika hili daftari usome kumbukumbu za baba miaka yote 12 hadi nakuja kuzaliwa. Ukimaliza itakuwa rahisi kukuelewesha maana ya ule mchoro na utanielewa vyema." Alinambia German na kunikabidhi daftari lililojaa vumbi la sandukuni. Nililifuta na kurudi pamoja chumbani kwa German na kukaa tena pale mkekani.
"Sasa Twaha, mimi naelekea mtoni kuoga."
"Haa! German, kuna magimbi haya ungekula kwanza?"
"Hapana, jotomwili lishapungua sasa yafaa kuoga na kuviweka huru vinyweleo ili nitaporudi kula magimbi yatapokewa vizuri mwilini. ha ha ha Asnate Twaha kwa kunionesha upendo."
"Basi twende wote mtoni German."
"Hapana Twaha. Huu ni wasaa mzuri wako kuweza kusoma kwa utulivu hilo daftari. Naamini nitaporudi kuoga utakuwa ushamaliza. Hapo tutakula magimbi kisha nitakufafanulia hiyo picha naamini kiu yako itaisha." Alisema German na kunifanya nitabasamu. Nilijituliza mkekani na sasa nikawa tayari kufungua kurasa moja baada ya nyengine kusoma daftari lile ambalo nje liliandikwa MIAKA 12 YA MATESO. Nilishusha pumzi na kutuliza akili kichwa kusoma kilichomo. Hakika nilisisimka na kila kilichoandikwa katika kila kurasa. Daah! Hakika ilikuwa miaka kumi na mbili ya Mateso yaliyobeba matukio ya kushangaza ndani ya maisha ya babaake German Machine.
.....