Makapuku Forum

Makapuku Forum

Sehemu ya 26


Alijikuta anakata simu aliyokuwa anazungumza na babaake na kuwaita wenzake haraka waje washuhudie kile alichokuwa anashuhudia. Wote walipofika na kutazama kule juu walistaajabu na kutaharuki sana kwa kile kilichoonekana. Mwili wa yule kijana ulikuwa ukining'inia mtini huku shingoni mwake kupitia juu ya kichwa kukionekana kamba iliyofungwa tawini.
"Haa!! Ina maana naye kaamua kujinyonga!!?" Alitahayuri Ocs John wote wakabaki wamekodoa macho mtini.
Hali ile ilimtisha kila mtu na kuwachanganya vichwa askari wote. Kwa upande wa kamishna Shebby alibaki na bumbuwazi na kuzidi kuamini kuwa hawa watu hawajiui bali yupo muuaji tena hayupo mbali kabisa na wao na huyo anayewaua atakuwa kwenye mtandao wa mr. X tu si vinginevyo. Aliamini hivyo nafsini na kuwaza jambo.
"Itakuwa siku ile niliyoropoka chumbani jina la Mr X alipokuwa anaugua mzee Mnyungunyungu huwenda ikawa ndio chanzo cha matatizo kwenye hii familia na kusababisha hivi vifo. Mh! ina maana kama kweli basi mmoja wa wale wazee atakuwa anahusika tu. Lakiniiii.....hivi huyu Mr. X ni mtu wa aina gani mwenye mbinu kiasi hiki hadi kugundua mitego yetu yote na kutuwahi kabla hatujafanikisha walau kupata njia ya kuanzia. Daah!! siku ya kumgundua huyu mtu sitothubutu kumfikisha kwenye sheria ya nchi. Nitamuhukumu mwenyewe haiwezekani aaaaagh!!" Maneno yalimtoka nafsini na kujiapiza Kamishna ndani ya moyo wake. Askari walipiga picha ule mwili kabla ya kuanza harakati za kuushusha kule mtini. Vijana waliokuwa pande nyengine wakiendelea na msako, walipigiwa simu na kutakiwa kusitisha zoezi hilo na kuja kujumuika na wenzao. Umati mkubwa wa watu ulijazana maeneo yale na kila mtu kutoamini kile akisikicho ama akionacho eneo lile. Baada ya ule mwili kushushwa amri ilitoka kwa kamishna ubebwe kupelekwa hospital kwaajili ya uchunguzi zaidi wa kidaktari. Katika tafiti na maswali yalikuwa kichwani mwake kamishna Shebby alizidi kuhisi lazima kati ya wale wazee mmoja wapo akawa kwenye mtandao wa mr. X na ndie aliyevujisha siri za yeye kutaka kumjua mr. X na ndio sababu za vifo vya wale watu ambao aliamini wangemsaidia kwa namna moja kuijua njia ya kumjua mr.X.
Ndipo hapo Kamishna Shebby alipowaita pembeni kina Kimaro na kujadili nao.
"Eti mmepata picha gani kuhusu haya matukio hususani hili la sasa ni kweli yule mtu amejinyonga mwenyewe au nini kimefanyika?"
"Daah! kiukweli mkuu hii inachanganya sana, nikisema hajajinyonga mwenyewe sasa nani kampandisha kule juu!! dah! kama nae kajinyonga ni kwasababu zipi? yaani bado mimi sijapata picha" Aliongea ocs John huku akiwa katika hali ya sintofahamu.
"Vipi Kimaro unasemaje?" aliuliza tena Shebby.
"Mkuu, mi naona kama huyu mtu hajajinyonga kwa ridhaa yake na nimeanza kutia shaka huenda hata babaake naye hakujichinja kwa ridhaa yake na vifo vyao wote vimesababishwa na mtu mmoja ambaye nahisi atakuwa na mbinu kubwa sana za kijeshi na yupo karibu mno na hii familia." Maneno ya Kimaro yaliungwa mkono moja kwa moja na Kamishna Shebby.
"Sawa kabisa, sasa hapa kuna mchezo wa akili nyingi sana unaendelea na usikute muuaji anatuangalia tunavyopagawa na pengine tuko jirani naye muda mwingi baada ya tukio. Sikia Kimaro nina mashaka na wale wazee watano huenda mmoja wapo akawa ni mtu wa karibu na mr. X na ndie aliyevujisha habari kwa mr. X kwamba kuna watu wanamfatilia kutaka kumjua. Sasa mr. X ameamua kuwaua wote walio na fununu walau kidogo kuhusu yeye na hii inanihakikishia kuwa MR. X yuko hai."
"Duh! mkuu sasa hapa tufanyeje."
"Inabidi sasa hivi ocs tuongozane na vijana tuwakamate wazee hawa wote twende nao tukawabane tuweze kumjua anayevujisha siri kwa mr. X kabla hatujachelewa kwani kwenye hii familia watu pekee waliokuwa na siri za mr. X wote washakufa na aliyebaki ndio kichaa hana kumbukumbu zozote hawezi kusaidia kitu naamini sasa hata huyo mzee anaweza kutoroka na habari zake kubaki kizani milele." Baada ya Kamishna Shebby kuongea yale wote walikubaliana na kumuunga mkono. Ocs alichukua radio call na kuongea na inspector wake kumpa maelekezo kamili.

*****

Baada ya mwanae kukata simu na kubaki na taharuki asijue kulikoni mzee Mwinchande alimuangalia yule mkuu msaidizi wa gereza kwa mshangao.
"Vipi baba kulikoni? anasemaje mkuu."
"Kijana kumbe kuna mission za kijeshi zinaendelea huko tena mbali nawe unajifanya hujui?" Kwa mshangao mzee Mwinchande aliuliza na kujikuta anafichua kile alichozungumza na mwanaye ambaye alimuomba asimwambie mtu zaidi atakuja kumuelezea mwenyewe.
"Mission zinaendelea? mbona sifahamu mzee wangu kuhusu hiko usemacho?"
"Ufahamu vipi na uko ofisi moja na mwanangu tofauti vyumba tu? ina maana hujui kama Kamishna wako yupo Morogoro muda huu kwenye kazi maalum tena inaonekana nyeti sana kwa jinsi alivyokuwa anaongea hadi akanikatia simu!!" aliongezea mzee Mwinchande na kumfanya yule mkuu msaidizi abaki ameduwaa mithili ya mtu aliyebaini kitu fulani.
"Anhaaaaaaa" Alihamanika na kufikiri jambo. Kutokana mzee Mwinchande kuwa na uzoefu wa miaka mingi wa kipolisi aligundua baada ya kuutazama uso wa yule msaidizi wa Shebby na kum'bana maswali pale pale.
"Hivi kuna mabadiliko gani alikuwa nayo Kamishna wako hivi karibuni au mna tatizo gani baina yenu hadi aanze kuondoka pasi na kukuaga mtu wa jirani kama wewe?"
"Mh! kiukweli mzee wangu hatuna tatizo lolote mimi na mkuu wangu ilaaa..." aliongea na kusita kidogo baada ya kuhisi si vyema kuongea habari za mkuu wake na kuijadili tabia yake pasi na lidhaa ya mkuu wake mwenyewe.
"sasa mwanangu unataka kunificha habari za mwanangu mwenyewe?"
"hapana mzee"
"Basi kama sivyo unasita nini. Hebu niambie ukweli umeona mabadiliko gani kuhusu mwanangu siku za karibuni hadi aondoke na kuwa na mission pasi na kukutaarifu mission gani." Alikazia mzee Mwinchande na kumfanya yule msaidizi kueleza kila kitu alichokuwa anakijua na kuhisi ndicho kilichom'badilisha Kamishna wake mpaka kuwa na 'mission' za siri.
"Kiukweli mzee wangu huenda hili ninalohisi likawandio ama sio sina uhakika ila tokea mkuu alipoanza kuwa karibu na mfungwa mmoja humu gerezani alikuwa na mambo ya ajabu ajabu ya kuandika kwenye kuta ovyo ovyo kuwa wanawake ni wauaji mara kwenye miti anachunachuna na kuandika hayo maneno halikadhalika na tabia yake ya kuropoka kwa sauti kubwa muda mwengine hayo hayo maneno na gereza zima lilimtambua yule bwana nusu chizi lakini ajabu mkuu akafanya jitihada anazozijua yeye hadi akafanikisha kuzungumza nae na inaonekana hadithi ya huyo bwana ilimgusa sana mkuu na hapo ndipo akaanza kuwa bussy sana na kutoka nje ya gereza mara kwa mara so, nahisi huenda kuna upelelezi amaeamua kuufanya binafisi juu ya kesi ya yule bwana ambayo ilisemekana ameonewa kwa mujibu wake mwenyewe."
"Oooohoooo! Duh! sasa mwananguuu ina maana anataka kumsaidia huyo mtu."
"Nahisi mzee, lakini sijui kilichomshawishi maana kesi yenyewe ni ya zaidi ya miaka ishirini na saba."
"Hee!! hivi Shebby mwanangu akili zake zimeingiwa nini hadi ashawishike kufanya upelelezi wa kesi ya miaka kibao namna hiyo? hee!!"
Alitahayuri na kukunja uso mzee Mwinchande kisha akatoa tena simu yake na kuanza kubinya binya namba.

****

Upande wa pili kamata kamata iliendelea. Shebby na Kimaro waliongoza kuwaelekeza askari wazee wa kuwatia nguvuni.
Watu wengi walizidi kuhamaki na kushangaa tukio lililokuwa linaendelea kufanywa na wale askari licha ya kuwa walikuwa kwenye huzuni na msiba mzito. Kitendo kile cha kamata kamata kilizidisha kilio kwa familia nyengine hususani watoto na wake wa wale wazee waliotiwa nguvuni.
"Halooo babu yule mwenzako mwenye baraghashia yuko wapi?" Aliuliza Kimaro pindi alipomfata mzee ambaye tayari alishadhibitiwa na vijana wa polisi.
"Haa! jamani mjukuu wangu kwani tumekosea nini mbona mwatuumiza kiasi hiki?" alihoji yule mzee.
"babu jibu swali usiulize swali lasivyo utafanya nitumie nguvu kukuuliza tena." Aliongea kwa ukali Kimaro. Wazi alishachanganyikiwa na matukio yaliyokuwa yanajitokeza pale. Dakika zilezile kamishna Shebby akiwa na askari mwengine walifika pale.
"Vipi Kimaro inaonekana bado mzee mmoja." aliuliza Shebby baada ya kuona idadi ya wazee waliokusudia wakamatwe haikukamilika.
"Kweli mkuu na ndio nilikuwa namuuliza huyu alipo mwenzake kabla vijana hawajaondoka naye." Alijibu Kimaro lakini dakika zile zile walisikia ukelele mmoja kutokea upande wa kaskazini kulipokuwa na nyasi nyingi na miti mikubwa michache. Walitaharuki wote na kutega masikio vizuri kabla hawajachukua hatua mara alikuja mtoto mmoja akilia na kuhema sana.
"Vipi wewe?" Aliuliza Shebby na kumshika yule mtoto ambaye macho yalimtoka akishindwa kuzungumza zaidi ya kuonesha kidole kutokea upande aliotokea. Kichwa chote kilitapakaa majani.
"Huyu ni mjukuu wa mzee Ally jamani..?" Aliongea yule babu huku akionesha kuchanganyikiwa zaidi.
"Mzee Ally ndio yupi?"
"Yule mwenye baraghashia mnayemuulizia!" Alipojibu hivyo yule babu papo hapo Kamishna Shebby alichomoa pisto yake na kuwataka askari wote waelekee haraka kule iliposikika sauti ya ukelele.
"Babuu.. babuu yupo kuleee tulikuwa tunakimbia na jitu moja halina usoo aaaah! babuu..." Alijikaza na kusema jambo yule mtoto aliyeachwa na askari mmoja sambamba na yule babu.
Kundi la polisi wakiongozwa na Kamishna Shebby walikata pori haraka haraka huku wakiruka visiki. Shebby alikuwa kinara kwa mbio kuliko wenzake na kuwahi sehemu ambapo walimkuta yule mzee akiwa amelala chini akifurukuta mwenyewe. Damu zilimtapakaa huku nyengine zikimvuja mdomoni na puani. Kifuani mwake kulionekana ameshikilia mpini wa kisu kilichozama chote eneo la kifua upande ule wa moyo. Haraka Shebby alipiga magoti na kumpakatia yule babu huku akihema, macho yamemtoka na jasho kumvuja. Taharuki iliwavaa na wenzake walipofika huku wengine wakikagua maeneo ya jirani kuona kama kuna mtu mwengine.
"Nambie babu.. nambie tafadhali najua unajua nani Mr. X! Nitajie mzee wangu jitahidi nitajie hata cheo alichokuwa nachoooo. Najua nawe umetengenezewa kifo uonekane umejiua lakini ukweli unajua babu yangu nambieee" Huku machozi yakimlenga Shebby alimsemesha yule mzee aliyekuwa bado hajafa akiwa amempakata kichwa. Hali ilikuwa mbaya kwake yule mzee lakini alijikaza na kujilazimisha kuongea kwa shida huku mdomo wake ukirusha mafunda ya damu yaliyokuwa yanamrukia Shebby bila kujali.
"Huu.. missss..ta.X ni... nii..aaaghhhrrr...niii....." Alihangaika kusema mzee yule na kabla hajamalizia kutamka juu ya huyo mr. X mara kichwa chake kilifumuliwa vibaya huku ubongo ukitawanyika sambamba na damu. Ilikuwa ni risasi ya kichwa iliyommaliza mzee yule ikitua bila kutoa mlio wowote mbele ya macho ya Kamishna Shebby, Ocs John na Sajent Kimaro.
"Ooooooh! hatariiiiiii kuna mdunguaajiiiiiiiiii!." huku akijichopa pembeni kwa sambasoti alitoa ukelele Shebby baada ya kugundua wapo katikati ya mtego wa mdunguaji hatari.

......
 
UF...
0a49fc051e60110ec8368dada83bc996.jpg
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom