Sehemu ya 25
"Mbona mmechelewa sana inspekta pia hamkuja na muhusika! kulikoni?" Aliuliza kamishna Shebby.
"Mkuu tumefanya kila jitihada za kufanikisha kuja na mtuhumiwa lakini hatukufanikiwa kumpata baada ya kutoweka masaa machache kabla hatujafika."
"AMETOWEKA!!!?" wote watatu, Shebby, John na Kimaro walitaharuki na kuuliza pamoja.
"Ametoweka toweka vipi! wakati nilimuacha mimi mwenyewe pale misibani na hayakupita hata masaa sita?!" Aliuliza zaidi Shebby.
"Ndio hivyo mkuu tumerudi baada ya kuona muda unaenda pia tulisahau mawasiliano. Ila tuko tayari kwa amri mtayotupa ila tumewaleta hawa wake wa marehemu wanaweza kutwambia wapi alipo mtoto wao."
"Huo ni upumbavu. Sikutaka aletwe mjane yeyote hapa. Chukueni vitu vyenu kusanya vijana wako msako uanze mara moja hadi apatikane huyo kijana." Alitoa amri Kamishna Shebby na kumuamuru Kimaro aendeeshe gari yao ambapo safari hii walipanda watatu sambamba na mkuu wa kituo Mkuyuni. Jumla ya gari mbili zilitoka kituoni kuelekea Mkuyuni stendi. Jumla ya vijana wenye bunduki zaidi ya kumi na tano walikuwa tayari kwa kazi. Kituo kilibaki na askari wachache sana wakiongozwa na mama mmoja aliyekuwa na cheo cha inspekta.
Wahuni na watu wote Mkuyuni walipigwa na bumbuwazi mara baada ya kuuona msafara ule uktia nanga kama meli ya kivita stendi kuu.
"Oya wana Kimenuka anga hizi tujikataeni.." aliongea muhuni mmoja aliyekuwa anacheza kamari na wenzake pale stendi mara baada ya kuona polisi. Kwa ushupavu askari walitawanyika na msako mkubwa ukaanza huku wahuni wengine wakikimbia ovyo kwa kuhofia huenda walikuja kukamatwa wao. Kamishna Shebby na Kimaro walichukua bastola zao ziliyokuwa wanaacha garini.
Moja kwa moja wakiwa na Ocs John waliongoza njia mpaka pale msibani sambamba na askari watatu wenye bunduki.
Watu wote pale msibani walizidi kustaajabu. Muda mfupi uliopita walikamatwa wake wa marehemu na ujio wa askari mara ya pili ulizidi kuzua sintofahamu kwa kila mtu aliyekuwa pale. Jicho la Shebby lilitua kwenye kikundi fulani cha watu waliomzunguka babu mwenye baraghashia aliyekuwa anaongoza mazungumzo ya tukio lililojitokeza.
"Babu, naomba usiwe na wasiwasi tutajie wapi alipoenda yule mtoto wa huyu marehemu." Alisaili Kamishna Shebby mara baada ya kufika na kumfata yule babu aliyestuka kuwaona askari kwa mara nyengine.
"Baba nani yule mtoto mjukuu wa Mnyungunyungu?"
"Ndio huyo huyo."
"Ukweli baba alituaga anakwenda msalani kule nyuma, nasi kila mmoja alipitiwa kuulizia kama alisharudi hadi tunakuja kustuka baada ya kuja polisi hapa na kumuulizia ndipo tulipokumbuka na kugundua hayupo mara baada ya kumtafuta bila mafanikio. Msalani hatujamuoa hata tukazunguka maeneo yote haya baba hadi tukawaulizia majirani kote hatujamuona baba mpaka muda huu hakuna yeyote kati yetu anayeelewa wapi alipo hata sisi tunashangaa kapoteaje kimaajabu kiasi hiki." Mzee alisema kwa sauti ya mtetemo wa hofu huku akimshangaa kamishna Shebby asielewe ni mtu wa aina gani. Hakutegemea awali hata kidogo kumuona akiwa katika hali ile na kumpa maswali kichwani asijue ni nani.
"Sawa mzee usiwe na hofu pia wazee wengine wote na vijana mliopo hapa nataka mjue kuwa mimi ni Kamishna Shaaban Mwinchande kutoka idara ya ulinzi wa ndani au polisi na nipo hapa kwa sababu maalum za kimsingi na kiusalama pia. Kwa hiyo ondoeni shaka, kushoto kwangu huyu ni Sajent Kimaro na kulia huyu ni mkuu wenu wa kituo cha polisi hapa Mkuyuni. Hivyo tunaomba ushirikiano wenu wa dhati hatuna ubaya wowote na huyu mtoto wa marehemu tunayemtafuta lakini tunafanya hivi kwa usalama wake na wa kijiji pia kwani tayari kuna hatari mbele yake. Tunawaomba vijana wote tujumuike pamoja kumtafuta."
Alimaliza kuongea Kamishna Shebby huku kila mmoja aliyesikia maneno yale akistaajabu na kukubali kuungana na wale maaskari tayari kuanza kumtafuta kona zote za Mkuyuni yule mtoto wa mganga.
* * * * *
Wakati huohuo upande wa pili ndani ya gereza alilofungwa Hussein kulionekana ugeni ukiwasili geti kuu. Baada ya ukaguzi uliruhusiwa kuingia ndani kabisa na kwenda kuegesha eneo maalum kulipokuwa na ofisi ya mkuu wa gereza sambamba na nyumba nzuri ya kisasa ya kuishi. Ulikuwa ni msafara wa gari mbili huku moja akionekana dereva peke yake na ile nyengine kulikuwa na watu watatu. Dereva sambamba na mtu mmoja aliyekuwa na mwili mkubwa ambaye alionesha wazi ni mlinzi wa karibu wa mzee mmoja aliyekaa nyuma akiendelea kusoma gazeti. Gari ziliposimama ndipo alishuka mzee yule ambaye heshima yake katika jeshi la polisi ilikuwa kubwa licha ya kuwa hakuwa askari tena. Hakuwa mwengine bali ni Mkuu wa jeshi la polisi mstaafu IGP Mzee Mwinchande ambaye pia ndiye alikuwa baba wa mkuu wa mteule wa gereza lile kamishna Shaaban. Safari ya mzee Mwinchande ilikuwa ya kustukiza tu. Hakukuwa na usumbufu wowote pale getini kutokana na heshima yake ambayo bado ilikuwepo licha ya kwamba alishastaafu kwa zaidi ya miaka kumi nyuma.
"Karibu mzee, shikamoo" alisalimia askari mmoja wa makamo aliyeonesha wazi kumfahamu vizuri mzee Mwinchande mara baada ya kumpa heshima ya stahiki na kumkaribisha ofisini.
"Ahsante sana bwana Khasim... vipi kwema hapa?" alisaili mzee Mwinchande pindi alipokuwa anaingia ndani.
"Vipi yuko wapi kijana wangu?" Aliuliza mzee Mwinchande huku akitazama huku na kule.
"Aaa..Mkuu ametoka kidogo ila nadhani muda si mwingi atarejea karibu sana mzee."
"Ok, Asante vipi kwani alipata dharula? maana mara nyingi anapokuwa anatoka nje ya hapa huwa ananitumia ujumbe kama si kunipigia."
"Hapana mzee wangu, nadhani hakutoka kiofisi itakuwa maswala yake binafsi lakini pia mi si msemaji wake nipo hapa kumuwakilisha tu pindi anapokuwa na dharula ama anapotoka."
"Sawa baba, lakini kumbuka simuulizii kikazi ila namuulizia kifamilia kama baba yake napaswa kujua alipo. Pia kumbuka unayeongea naye na kumtajia sheria ni nani! hahahaaaa usiogope kijana wangu hebu acha masikhara tuongee kidogo." Alitia mkwara kidogo mzee Mwinchande na kucheka kwa masikhara. Kwa sheria na kanuni za kijeshi, askari yeyote anapostaafu hasa yule aliyewahi kutunukiwa wadhifa au cheo jeshini basi cheo chake hakistaafu na kitaendelea kuishi mpaka atapokufa anapaswa kupewa heshima stahiki na askari yeyote ambaye hajakifikia kile cheo kama ilivyokuwa kwa mzee Mwinchande na yule mkuu wa gereza msaidizi. Baada ya kutia utani mzee Mwinchande aliuvaa utulivu na kuendelea kusema.
"Hebu nambie ukweli kijana maana wiki hii nimemfanyia suprise mkuu wenu sasa kutomkuta kwake imekuwa suprise tena kwangu. Sasa wewe ndiye msaidizi wake ina maana hajakuaga wala kukwambia wapi anaenda?"
"Mh! Kiukweli ameniaga tu kwa kunambia anatoka mara moja lakini hajanambia wapi anakwenda."
"Basi sawa mwanangu ngoja nimpigie simu sasa hivi anambie alipo nijue nimsubiri ama niondoke maana muda ushaenda sasa." Alitoa simu yake ya mkononi na kumpigia mwanaye. Simu iliita lakini haikupokelewa hadi ikakatika. Alirudia kupiga mara ya pili ndipo ikapokelewa.
mzee Mwinchande - "Hallow! vipi mwanangu uko wapi?"
Kamishna Shaaban - "Niko ofisini baba."
mzee Mwinchande - "Ha! baba mbona nami niko ofisini kwako! au umehamishwa ofisi..!"
Kamishna Shaaban (huku akikohoa) - "Aaah! Samahani sana mzee wangu sikutegemea kama ungekuwa hapo muda huu wala sikuwa na maana ya kukudanganya. Nitaporudi nitakueleza kimapana baba ila kwa sasa nipo kwenye mission ya dharula Morogoro. Samahani sana baba hii nimefanya siri tu."
mzee Mwinchande (huku akishusha pumzi - "Ooooph! but hebu nidokeze kidogo mission gani tena eeh!.....hallow......hallooow Shabani halloow."
Simu ilikatika na mzee Mwinchande kubaki na taharuki asijue kinachoendelea huko alipo mwanae.
****
|MKUYUNI|
Wakiwa wamegawana maeneo wengine wakipasua pori kwa pori huku wengine wakiweka vizuizi vya magari mabarabarani, mbali na waliokuwa wanakatiza mitaani kwenye vijiji vyote, asakri wakisaidiwa na wanakijiji waliendelea na sakasaka ya mtoto wa marehemu. Huku wakiongozwa na Kamishna Shebby mwenyewe sambamba na Ocs wa Mkuyuni bila kumsahau Sajent Kimaro.
Hadi muda huo walishatembea umbali mrefu bila kuwa na dalili zozote za kuonekana yule kijana mtoto wa marehemu mganga aliyejiua. Ndipo Kamishna Shebby aliposimamisha kikosi alichokuwa nacho baada ya kuwasiliana na vikosi vyote vilivyokuwa kwenye msako ule. Akili zake zilizunguka haraka haraka kufikiria kwanini zoezi limekuwa gumu maradufu. Aligundua wanazidi kutokomea nyikani na kuanza kuhofia kupoteza muelekeo kabisa.
"Ocs wambie vijana turudi nyuma tukaanze upya pale msibani." Alitoa amri kamishna Shebby na safari ya kurudi ilianza mpaka pale msibani kwa mara ya pili. Ocs John alikuwa hoi kwa mwendo lakini alijikaza. Hakuzoea kuhangaika kama askari kuruti.
Kazi ilikuwa ngumu na ya kuchosha kwa kumtafuta mtu wasiyejua hata muelekeo aliotoka nao. Lakini hawakuwa na jinsi zaidi ya kutii amri za Kamishna ambaye hakuonesha kuchoka wala kukata tamaa.
"Sasa hapa utulivu wa akili unahitajika katika msako wetu." Kamishna Shebby alisema baada ya kufika pale msibani huku akikitazama choo cha makuti kilichokuwa kaskazini mwa nyumba ile.
"Kile si ndicho choo alichoelekea mara ya mwisho?" Aliuliza na kujibiwa na inspekta aliyeongoza kikosi awali walipokuja wenyewe kumkamata kijana mpotevu.
"Ndio afande. Ila tulishatafuta kote huko." Alijibu yule inspekta lakini Shebby alisogea pale chooni na kuangalia kwa makini sana mazingira yale. Macho yake yalitazama juu ambako kulionekana matawi makubwa yaliyoshona majani yaliyokuwa usawa wa kile choo kilichokuwepo jirani na mti mmoja mkubwa.
Wakati huo akiendelea kuangaza huko na huko na kuzunguka kile choo kwa nje akielekea usawa ule wa ule mti ndipo simu yake alipoisikia inaita lakini hakuwa na haraka kuipokea. Lakini ilipoita mara ya pili ndipo alipoipokea baada ya kujua aliyekuwa anapiga ni baba yake mzee Mwinchande.
Lakini kipindi alipokuwa anaongea na babaye huku macho yake yakiangaza huku na huko hususani juu ya matawi ya ule mti ndipo mara moyo wake ulilipuka na macho kumtoka. Hakuamini kile alichokuwa anakiona juu kabisa ya ule mti uliokuwa na matawi mengi makubwa sambamba na majani yalishonana vizuri.
Alijikuta anakata simu aliyokuwa anazungumza na babaake na kuwaita wenzake haraka waje washuhudie kile alichokuwa anashuhudia. Wote walipofika na kutazama kule juu walistaajabu na kutaharuki sana kwa kile kilichoonekana. Mwili wa yule kijana ulikuwa ukining'inia mtini huku shingoni mwake kupitia juu ya kichwa kukionekana kamba iliyofungwa tawini.
"Haa!! Ina maana naye kaamua kujinyonga!!?" Alitahayuri Ocs John wote wakabaki wamekodoa macho mtini.
.......