Makapuku Forum

Makapuku Forum

WANAWAKE NI WAUAJI?

SEHEMU YA 02


Nilirejea sebuleni baada ya kujiridhisha kwa nguo nilizovaa siku hiyo na kabla sijatoka nilipiga tena simu ya Mamu lakini jibu lilikuwa lile lile kwamba namba ninayopiga ipo bize.
Sikuwa na jinsi ilibidi nitoke na kuchukua bodaboda kuelekea kwa kina Mariam nikiwa na nia na madhumuni ya kwenda kuomba msamaha ili mapenzi yetu yaendelee kwani nilimpenda sana na nilijua kama nisingeenda muda huo basi ingebidi nisubiri hadi wiki ijayo kwani nisingepata nafasi kutokana na kuwa kazini muda mwingi. Baada ya mwendo wa dakika kumi tulifika maeneo ya kina Mam na kumlipa ujira wake yule dogo aliyenileta nami moja kwa moja nikaanza kuongoza njia ya kwa kina Mamu huku nikiwazia jinsi ya kuanza.
“Karibu baba.” Sauti ya mama mkwe mtarajiwa ilinikarimu nilipomkuta akiwa nje amekaa kwenye kolido ya nyumba yao akiwa anasukwa na mwanaye mwengine wa kike.
“Asante mama shikamoo”
“Marahaba baba za huko”
“Safi tu mama sijui ninyi”
“Sisi kama unavyotuona baba tunamshukuru Mungu. Enhee mbona hivyo baba kwema!”
“ehe!hee..! Kwema tu mama.” Nilijibalaguza kwa kujichekesha baada ya kuhisi huenda mama Mamu kashastukia mchezo ila ananitega. Lakini kabla sijakaa sawa nilishangazwa na swali ambalo nilijikuta nashindwa kulielewa na kuuliza tena.
“Unasemaje mama!!?”
“Nimekuuliza mwenzio yuko wapi? maana alituaga anakuja huko kwako muda mlefu tu aliondoka hapa sasa umenishangaza nawewe umekuja muda huu ukiwa peke yako! ndio maana nimekuuliza awali kwema?”
Nilijikuta nashusha pumzi kwanza mara baada ya kusikia na kubaini kuwa Mamu hajafika kwao tangia muda ule alipoondoka kwangu.
“Vipi baba mbona huongei..! unatutisha wenzako” Sauti ya mshangao ya mama mkwe ilinitoa kwenye dimbwi la mawazo ya ghafla nilipokuwa nafikiria alipoenda Mamu muda wote ule hajafika kwao.
Niliogopa kimtindo ila nilificha machoni. Niliwaza kama kitampata kitu kibaya huko basi namimi nitahusika kwa kiasi kikubwa pia nilivyoelewa kuwa Mamu atakuwa kachanganyikiwa sana na anaweza kujifanyia hata kitu kibaya mwenyewe kutokana na kujua kiasi gani ananipenda na mara nyingi hakutaka nimuudhi kabisa.
“Hah, ni hivi mama kweli Mamu alikuja lakini hakukaa sana akadai kuwa kuna vitu amesahau na alinambia nimsubiri sasa nimekaa na nilipoona anachelewa sana ndipo nikaamua kuja huku kwa lengo la kumfata yeye. Ndio maana ulivyoniuliza yuko wapi nimeshangaa ina maana hujamuona huku kurudi?”
“Hee!! We babaa eeh ina maana awe karudi halafu mi nikudanganye! Mwanangu si mzururaji hebu usitufiche baba nambie umemuacha wapi mwenzio au nini kimetokea huko kwenu..?” Uso wa mama mkwe ulinawiri mseto wa mashaka na hasira hata kumsimamisha mwanae aache kumsuka.
“Hakuna chochote mama, usiwe na wasiwasi.” nilijaribu kumtuliza.
“sasa mbona hueleweki eleweki simu unayo kwanini hukumpigia kujua alipo hadi unakuja kumuulizia?”
“Okeeey, samahani mama nimekumbuka alinambia kabla ya kuja huku kuna sehemu kwa shogaake angepitia kule mwenge. Tena ngoja nimfate huko kabisa nahisi hajatoka”
Ilinibidi kudanganya na kuongea maneno ya matumaini hasa mara baada ya kumuona yule mama akizidi kubadilika.
Kiukweli nilitambua kitambo kuwa Mariam anapendwa sana na mamaye na ukizingatia yule mama alikuwa na watoto wawili tu. Wote wa kike, babayao alishafariki muda mlefu sana hivyo hata jinsi alivyowalea wanae kwa taabu na maadili walikuwa si watu wa kutokatoka ovyo wala kuzurura. Na ndio sababu kitendo cha kusikia mwanae hayupo kwangu kilianza kumchanganya kidogo nami nikatumia akili ya ziada kumtuliza na kumkwepa kwa kujidai naenda Mwenge kwa huyo shoga yake Mamu.
“Baba naomba utavyorejea uje na mwanangu tafadhali, kwanza kisheria na kidini bado hujakabidhiwa. Asilale huko! oohooo”
Aliongea yule mama kipindi nikiondoka kuelekea kituo cha daladala nikiwa na mawazo mara mbili na niliyokuja nayo.

* * * * *

Safari yangu ilinipeleka mpaka pande za fukwe za coco na lengo halikuwa kuogelea wala kufanya mazoezi bali ni kupunguza angalau robo ya mawazo yaliyoandamana kichwani. Niliichukia siku ile kwa kulaumu ni heri tusingekutana tu na Mamu kwani mipango yote ya kufurahi pamoja wikiendi iliyeyuka ghafla kama machozi ya samaki kwenye maji. Niliwazia nitamwambia nini yule mama endapo Mariam asingeonekana siku hiyo kabisa. Niliwaza pia ina maana Mamu anaweza akajifanyia tukio hata la kunywa sumu kwa kajiugomvi kale tuu! Na kama akifanya hivyo nini kitanikuta baadae..! si ndio itakuwa basi tena! Niliwaza mambo mengi sana na kuchukua tena simu kupiga namba ya Mamu lakini bado jibu likawa lilelile ndipo nilipogundua sasa Mamu atakuwa kani-'reject'.
Nilijisonya na kumtumia ujumbe nikimsihi na kumuomba popote alipo basi arudi nyumbani haraka wanamtafuta. Japo nilituma zaidi ya meseji tano lakini hakuna hata moja iliyojibiwa. Nikiwa bado nimekaa juu ya jiwe moja nimening’iniza miguu huku nikiirusharusha na kuangalia watu mbalimbali wakifurahia maisha ufukweni, ndipo nilipoangaza macho huku na kule moyo wangu ulilipuka ghafla nilipomuona binti mmoja akiwa kavaa kipensi chepesi kifupi kilichom-bana barabara huku akiacha sehemu kubwa za mwili wake nje ambapo kifuani alijisitiri na kisidilia kidogo cha kamba.
Macho hayakuamini nikionacho huku mapigo ya moyo yakiongeza mwendo wa msukumo wa damu. Kilichonistua zaidi si uzuri wake wala umbo lake ama mavazi, la hasha! bali nilipouona uso wake ambao niliujua vizuri mno. Nilishindwa stahimili kumtazama binti akiwa kashikwa kiuno na baunsa mmoja ambae kushoto kwake alishika pira kubwa la kuogelea. Hakuwa mwengine yule binti bali kipenzi changu Mariam akiwa na yule njemba wakielekea majini huku wakionesha nyuso za furaha.
Nilijikuta mwili ukinitetema kwa hasira na midomo kunichezacheza huku macho yakiwa hayaamini kile kilichokuwa kinaonekana.
"!!Shiit!!!...?!" Nilihamaki na kuruka pale juu ya jiwe na kukanyaga maji licha ya kuwa nilivaa viatu simpo na suruali ya jeans lakini sikujali wala kufikiria hilo zaidi nilitembea haraka kama mwanajeshi macho yamenitoka nikielekea kule alipokuwa kipenzi changu Mamu na yule baunsa kabla hawajafika kwenye kina cha kuogelea.
“Mamu hapa unafanya nini na huyu boya ni nani yako?” Nililianzisha punde nilipofika kwa kuwaputisha mikono waliyoshikana.
“Boya? Hii we kaka vipi.. Eti baby unamjua huyu!!?” Alijibu kwa taharuki Mariam huku akinishangaa na kujisogeza jirani zaidi kwa yule njemba aliyekuwa ananitazama kwa hasira. Moyo ulinichoma na kujikuta naongea huku midomo ikinicheza cheza kwa kutoamini kama yule ndie Mamu ninayemjua mimi au kivuli chake.
“Mamu !!? hivi umepatwa na nini lakini..!”
“Hivi baby unamuelewa huyu..” Aliongea Mamu kumuuliza yule baunsa kwa kauli iliyonichoma zaidi ya msumali wa moto uliopigiliwa katikati ya kidonda na kubaki natazamana na yule mwamba aliyevimbiana kishari. Alikuwa mtu wa miraba minne aliyestahili kuitwa jitu. Umbo lake komavu lililovimbiana misuli lilitosha kumuogopesha mpenda amani yeyote kama mimi. Jitu jeusi kipara lenye sura iliyobeba alama zote za uvunjifu amani lilinikazia macho na kunikoromea.
“Oyaa wee bwege, usitupotezee muda katika starehe zetu hebu jikatae haraka kabla sijakufanya kitu mbaya sasa hivi, tena usinihamshie wazimu oooohoooo POTEA!” Lilifoka lile baunsa na kunisukumia majini. Haa! nami sikukubali japo sikuwa baunsa wala kuwahi kucheza mchezo wa ngumi, nilijikaza kiume na kumsukuma pia huku nikirusha maneno ya ndaro.
“Oyaa usinitishe wewe hizo nyama tu hata kwenye sambusa zipo. Sikuogopi wala nini! kwan......”
Nilipayuka nikisahau kuwa mdomo huponza kichwa. Ndipo hamadi! Kabla sijamaliza kauli nilistukia napigwa ngumi kali ya meno iliyonipeleka moja kwa moja chini na niliponyanyuka ili nikabiliane naye alinibamiza na lile pira usoni hadi nikaona cheche za moto mbele yangu na nafsi yangu kutamani watu waje kutugombezea haraka kabla uhai haujaniponyoka. Lakini ubaya wa watu wa jiji la Dar ndio kwanza walikusanyika na kuzunguka eneo lile wakitufanya sinema pasipo kuniokoa. Hata kipenzi changu Mamu hakujali wala kusema chochote.
’PWAATCHAAA’
Maji yalichapachika zaidi ingawa yalikuwa ya ugoko lakini kwa nilivyodondoshwa mara ya tatu ilitosha kulowana mwili mzima huku mengine yakiniingia puani na mdomoni kana kwamba nilitupwa kwenye kina kilefu. Kilichonisikitisha zaidi ulinzi eneo la fukwe naweza kusema kama haukuwepo kabisa kwa raia zaidi askari wachache walikuwepo eneo la nyuma za fukwe wakilinda magari yaliyoegeshwa. Nilipiga hesabu za haraka na kuona kama nitazembea zaidi naweza kukata moto mikononi mwa njemba yule aliyenichachamalia kuutafuta ujiko mbele ya Mamu na umati ule.
Nilinyanyuka kwa mbwembwe huku nikijifanya nami namtafuta nimpachike zangu ndipo 'paaap' kwa kwa kasi ya kope niliinama sambamba na kutoa ukelele wa hatari na kumrushia maji sambamba na michanga usoni yule baunsa na alipozubaa tu sekunde zilezile nilipenya kwenye ukuta wa watu na kukimbia eneo lile kwa kasi ya mshale nikiwaacha wakizomea na wengine wakivunjika mbavu kwa vicheko.
Daaah!! katika siku nilizowahi kujisikia vibaya na kupatwa aibu kubwa ambayo sitoweza kusahau na hii pia ni mojawapo. Niliumia sana hususani pale nilipoisikia sauti ya Mamu ikiambaa juu ya sauti zile zilizokuwa zikinizomea pale ufukweni. Sikumbuki kwa kasi niliyotoka nayo kama lile jitu lilinifukuzia ama laa, lakini ninachokumbuka vizuri ni pale nikiwa ndani ya daladala mara baada ya kustuliwa na sauti ya dada mmoja.
“Wee kaka vipi! Simama vizuri unaniloweshaa…!!” Sauti hii ilinifanya nijibane zaidi mlangoni aliposimama konda huku abiria wengi wakinishangaa kwa mwonekano wangu. Nilikuwa zaidi ya kituko nilivyolowa chapachapa mchana ule wa jua kali. Ilinibidi nishuke tu kituo cha mbele kwa aibu. Taratibu mguu mosi mguu pili, nilihesabu hatua macho chini kama mwali wa kimakonde huku njia nzima kila niliyepishana nae akinishangaa si mkubwa wala mtoto.
Kwa mwendo wa sawajiko nilifika 'getto' na kuchojoa zile nguo za masahibu na kuvaa taulo. Ndipo niliduwaa zaidi nilipojitazama kwenye kioo cha 'dressing table' na kubaini kuwa nilikuwa na uvimbe kwenye paji la uso, jicho moja lilivilia damu pia mdomo wangu wa chini ulipasuka na kulikuwa na damu zimegandia sehemu ya kidevu. Nilisonya na kumlaani Mariam kwa uchungu mara machozi yalibisha hodi usoni mwangu na kilio kuniponyoka. Maumivu yaliyokufa ganzi awali sasa yalifufuka upya mwilini mwangu. Nilijikaza na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniokoa kwenye mikono ya jitu lile lililokosa huruma. Nilijikagua vizuri kinywa kilichosheheni uzito wa maumivu na kubaini kumbe hata jino moja la mbele liling'oka na fizi kuvimbiana. Nilidata zaidi kwa uchungu punde taswira iliporudisha tukio lile machoni mwangu na muda uleule niliamuaa kuifuta kabisa namba ya Mamu kwa amri ya nafsi yangu iliyotibuka na kutotamani kuonana nae tena..! Niliiendea ile suruali niliyoivua muda mfupi pale chini lakini nilipotazama mifukoni kutafuta simu nayo sikuiona hata pochi yangu ya fedha pia haikuwepo.
"Dooh! nimepoteza kila kitu shaabash!" Nilisema mwenyewe nilipobaini kuwa lazima nilividondosha kwenye hekaheka ile hasa nilipokumbuka kuwa hata kwenye daladala nauli sikulipa wala konda hakunidai punde niliposhuka kule njiani. Nilishusha pumzi na kumshukuru tena Mungu na kuwazia hata nitaponunua simu sitokuja kuirejesha namba yangu wala sitomtafuta tena Mariamu kivyovyote. Niliwasha jiko la mchina na kuchemsha maji kisha nilielekea moja kwa moja bafuni kwa zoezi la kujikanda na kujisafisha kabla ya kwenda famasi kununua dawa za kutuliza maumivu.

....to be continued. .....
Baba D asante jamaan ila nimecheka sana kafumania mchumba ake na kupigwa kapigwa mtu umeshaona mchumba ako ana baunsa unakufa na tai shingoni utajua mbele kwa mbele ila mam mtu mbaya sana huyu jamaa kapigwa jamaan kama nimemuona ila pole yake sana kwa kipigo cha baunsa
 
Baba D asante jamaan ila nimecheka sana kafumania mchumba ake na kupigwa kapigwa mtu umeshaona mchumba ako ana baunsa unakufa na tai shingoni utajua mbele kwa mbele ila mam mtu mbaya sana huyu jamaa kapigwa jamaan kama nimemuona ila pole yake sana kwa kipigo cha baunsa
Na wewe umequote...walahii mama angu mwanamke siendeleiii
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom