Mafisadi wamwandama Spika Sitta hadi NEC
Na Mary Edward Nipashe
18th August 2009
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Samuel Sitta.
Mvutano mkali uliibuka jana ndani ya mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi Taifa (NEC) baada ya kundi linalotuhumiwa kwa ufisadi kushawishi wajumbe wa mkutano huo kumpigia kura ya kutokuwa na imani na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Samuel Sitta.
Kundi hilo linadai Spika amekuwa kikwazo kwao na ndiye anayeshawishi baadhi ya wabunge ndani ya Bunge kuendeleza kuliumiza kundi hilo.
Kundi hilo linalalamikia taarifa ya hivi karibuni iliyotolewa bungeni na Sitta kuwa kundi hilo linalotuhumiwa kwa ufisadi linataka kumuua hali ambayo ilimlazimu kuomba ulinzi wa ziada kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Kundi hilo linatuhumiwa kuwashawishi wa wajumbe kwa nguvu zote na kutumia fedha nyingi ili kuungwa mkono kufanikisha kumngoa Spika.
Unajua tangu jana mvutano uliopo ni suala la kundi hili la watu wanaotuhumiwa kwa ufisadi kushinikiza Spika aondelewe kwenye nafasi yake... limekuwa likifanya kampeni kubwa na kushawishi wajumbe kwa fedha nyingi...lakini hali inavyoonekana limeshindwa kwa sababu wajumbe wanaoliunga mkono ni wachache hata kama zingepigwa kura kwa vyovyote vile lisingeshinda, kilisema chanzo chetu cha habari.
Chanzo hicho kiliongeza kuwa mvutano huo uliibuka kwenye kikao cha Kamati Kuu kilichoketi kwa muda wa siku mbili kuanzia Jumamosi na Jumapili ambapo kundi hilo lilitaka hoja hiyo ya kumngoa Spika iwe sehemu ya ajenda katika mkutano wa NEC.
Hata hivyo, baada ya mvutano mrefu bila kupatiwa majibu, suala hilo liliibuliwa tena kwenye mkutano huo ambapo kundi hilo limekuwa likishikilia msimamo wake wa kungolewa kwa Sitta.
Taarifa hizo zinaeleza kuwa ushawishi wa kundi hilo umekuwa hauna nguvu kwa vile wajumbe wengi walikuwa upande wa Spika na kusababisha nia yake kutotekelezwa.
Rais Kikwete alitarajiwa kulitolea uamuzi suala hilo baadaye katika kikao kilichokuwa kinaendelea jana usiku.
Kuhusu kungolewa kwa Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, chanzo hicho kimedai kuwa halikuwa kwenye ajenda lakini tetesi zilidai kuwa huenda likaibuka kwenye ajenda ya mengineyo.
Huyo mzee sijui ana nini, maana wajumbe wengi walishapeleka mapendekezo kwa Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete la kumwondoa, lakini hadi sasa hakuna kinachoendelea, kilisema.
Wakati huo huo, Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Said Bwanamdogo, amechaguliwa kuwa Mjumbe wa NEC kupitia Jumuiya ya Wazazi.
CHANZO: NIPASHE
Nimefatilia magazeti mengi nadhani "Tanzania Daima" kama Spika alivyoelezea kuwa wanamwandama, bado hawamtendei haki.