Wazazi wa Florian Wirtz kupokea Euro Milioni 8.6 kwa kumwakilisha Kijana wao!
Katika tukio la kipekee na lisilo la kawaida kwenye soka la kimataifa, Wazazi wa Nyota wa Ujerumani Florian Wirtz wanatarajiwa kupokea Euro milioni 8.6 (takriban Tsh bilioni 25) kufuatia uhamisho wa mwana wao kwenda klabu ya Liverpool FC.
Kwa mujibu wa gazeti maarufu la Bild la nchini Ujerumani, wazazi hao walifanya kazi ya uwakala kwa niaba ya Mtoto wao katika dili hilo kubwa.
“Wazazi wa Florian Wirtz wataingiza Euro milioni 8.6 kutokana na uhamisho wake kwenda Liverpool, kwa kuwa ndio waliomwakilisha kama mawakala wake,” limeripoti Bild.
Ni jambo adimu sana kuona Wachezaji wa kiwango cha juu Duniani wakiwa na Wazazi wao kama Mawakala, hasa kwenye makubaliano ya fedha kubwa kama haya.
Wirtz alikuwa Mchezaji wa Bayer Leverkusen, na uhamisho wake kwenda Liverpool umevutia hisia nyingi kwa sababu ya staili yake ya kiuchezaji, uwezo wa kufunga na kutoa pasi za mwisho akiwa bado na umri mdogo.
Hatua ya Wazazi wake kuchukua jukumu la uwakala inafungua mjadala mpya kuhusu nafasi ya familia katika uamuzi wa taaluma za Wachezaji, hasa katika soka ya kisasa yenye nguvu ya kibiashara. Kwa familia ya Wirtz, hili si tu ni mafanikio ya Mwana wao, bali pia ni ushindi wa Wazazi kama Wawakilishi wa ndoto za Watoto wao.