MARK LAWRENSON, NGAZI YA MAFANIKIO NDANI YA LIVERPOOL MIAKA YA 1980's
Wapenzi wa soka wa kizazi cha sasa wakiambiwa jina βMark Lawrensonβ huenda wengine wasielewe uzito wa jina hilo, lakini kwa mashabiki wa Liverpool wa miaka ya 1980, jina hilo linawakumbusha beki madhubuti aliyekuwa nguzo ya ulinzi wa klabu hiyo katika enzi ya dhahabu.
Mark Lawrenson, mzaliwa wa Preston, England, alijiunga na Liverpool mwaka 1981 akitokea Brighton & Hove Albion kwa ada ya karibu paundi 900,000. Ingawa bei hiyo ilionekana kubwa kwa wakati huo, iligeuka kuwa uwekezaji wa dhahabu kwa Liverpool. Lawrenson alikuja kujenga safu ya ulinzi iliyojaa maarifa, utulivu na ukakamavu, hasa kwa kushirikiana kwa karibu na Alan Hansen mmoja wa ushirikiano bora wa ulinzi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya soka la Uingereza.
Miaka ya Dhahabu ya Liverpool
Kuanzia msimu wa 1981β82, Liverpool chini ya kocha Bob Paisley, na baadaye Joe Fagan na Kenny Dalglish, ilitawala soka la ndani na la kimataifa. Katika kipindi cha Lawrenson ndani ya kikosi cha kwanza, klabu ilinyakua mataji matano ya ligi kuu (First Division), ikiwemo ile ya 1981β82, 1982β83, 1983β84, 1985β86 na 1987β88. Alikuwa chachu ya mafanikio hayo kwa kuzuia mashambulizi na kuchangia kuanzisha mashambulizi kutoka nyuma.
Katika msimu wa 1983β84, Lawrenson alikuwa sehemu ya kikosi kilichotwaa Kombe la Mabingwa Ulaya (European Cup) baada ya ushindi wa mikwaju ya penalti dhidi ya AS Roma, mechi iliyopigwa katika jiji la Roma. Huu ulikuwa ushindi wa kihistoria, si tu kwa klabu, bali pia kwa wachezaji kama Lawrenson ambao walidhihirisha ukomavu wa kiakili na kiuchezaji.
Mtindo wa Uchezaji na Haiba Uwanjani
Mark Lawrenson alikuwa aina ya beki ambaye hakuhitaji kutumia nguvu kubwa sana kuonyesha ubora wake. Aliwasoma washambuliaji kabla hawajafanya maamuzi, alijua wakati sahihi wa kukaba na wakati wa kurudi nyuma. Hakuwa mbabe, lakini alikuwa na akili ya kuzima hatari kabla mapema, Kwa lugha rahisi, alikuwa "specialist wa ulinzi".
Mara nyingi alihamishwa kutoka beki wa kati hadi kushoto pale ilipohitajika, jambo lililoonyesha wigo wa uwezo wake. Uwezo wake wa kupiga pasi fupi zenye maana, pamoja na uelewa wa mbinu za uchezaji, ulimfanya kuwa mchezaji mpendwa kwa makocha na wapenzi wa Anfield.
Majeruhi Yaliomaliza Safari Yake
Kwa bahati mbaya, miaka yake ya mwisho katika soka yaligubikwa na majeraha ya mara kwa mara, hasa ya goti. Mwaka 1988, akiwa bado na miaka 31, alilazimika kutundika daluga. Kwa mashabiki wa Liverpool, ilikuwa huzuni kubwa kuona beki wao tegemeo akilazimika kutundika daluga huku akili ikiwa bado inahitaji kusukuma kabumbu lakini mwili unakataa.