Leo Magufuli hayupo madarakani, Wapinzani hawapo bungeni, Job Ndugai sio Spika tena na Prof. Asaad sio CAG tena

Bujibuji Simba Nyamaume

JF-Expert Member
Feb 4, 2009
74,870
155,834
Nature imetenda haki.

Hii ni hotuba ya Kambi ya Upinzani bungeni ambayo Job Ndugai na Magufuli hawakutaka kabisa isomwe ili wananchi wajue mauvundo, dhuluma na mauchafu wanayofanyiwa.

HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KATIKA WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO, MHESHIMIWA HALIMA JAMES MDEE (MB), KUHUSU BAJETI YA WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO KWA MWAKA WA FEDHA 2019/20
Inatolewa chini ya Kanuni ya 99(9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge,
Toleo la Januari, 2016
_______________

A. UTANGULIZI:
1. Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika Wizara ya Fedha na Mipango, Mheshimiwa Halima James Mdee, naomba kuwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kuhusu bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka wa Fedha 2019/20

2. Mheshimiwa Spika,ni bahati mbaya sana kwamba huu ni mwaka wa tatu mfululizo, nawasilisha maoni ya Kambi ya Upinzani Waziri wangu Kivuli akiwa hayupo Bungeni kutokana na kuzuiliwa kuhudhuria vikao vya Bunge. Jambo hili linaonekana kufanywa kimkakati ili kupunguza nguvu ya upinzani Bungeni katika kuisimamia na kuiwajibisha Serikali kupitia Wizara hii ambayo imeshindwa kusimamia uchumi wa nchi yetu na kulifanya Taifa liendelee kuogelea katika lindi la umasikini katika miaka yote ya utawala wa CCM.

3. Mheshimiwa Spika, kama mkakati ndio huo, wa kudhoofisha upinzani bungeni kwa kuwafukuza wabunge wa upinzani, napenda kulithibitishia Bunge lako kwamba mkakati huo umeshindwakabala hata haujaanza kutelezwa. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni iko imara zaidi leo kuliko jana; ndio maana kila wakati tunapowasilisha maoni yetu hapa Serikali yote inahaha kuzuia maoni ya Kambi yasitolewe kwa hofu tu ya kutojiamini na pia uwezo mdogo wa kujibu hoja za msingi tunazoziibua.

4. Mheshimiwa Spika, Wizara ya Fedha na Mipango ndiyo msimamizi mkuu wa Uchumi wa nchi, na majukumu yake mahsusi ni pamoja na kusimamia ukusanyaji wa mapato ya ndani na ya nje; kusimamia matumizi ya Serikali, kusimamia utendaji wa Taasisi na Mashirika ya Umma, kusimamia manunuzi ya Serikali na Taasisi na Mashirika ya Umma, kusimamia Deni la Taifa na dhamana za Serikali, kutafuta suluhisho na kusimamia mfumo wa kodi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na kupambana na Fedha haramu. Aidha, jukumu linguine ni kusimamia na kutekeleza Mpango wa Kupunguza Umasikini nchini kupitia Programu ya MKUKUTA II.

5. Mheshimiwa Spika, Wizara ya Fedha na mafungu yote yaliyo chini yake ndio moyo wa Serikali na hivyo ni lazima kuitazama Wizara hii kwa jicho kali na kutilia mashaka kila jambo ambalo inalifanya ili kuhakikisha kuwa moyo huu hausimami ukisimama maana yake ni kifo cha uchumi; na uchumi ukifa ni kifo cha Taifa. Kwa sababu Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni itatimiza wajibu wake wa kikatiba na kikanuni kuisimamia ipasavyo Wizara ili fedha za umma, ziweze kutumiwa kimaadili kwa manufaa ya umma wenyewe; lakini zaidi sana mipango ya uchumi iweze kutekelezwa kwa ufanisi ili kuleta ustawi na maendeleo kwa wote.

6. Mheshimiwa Spika, kwa kuwa hoja zitakazoibuliwa katika hotuba hii zinalenga kutoa mawazo mbadala kuhusu namna ya kuboresha ili kama taifa tuweze kuondoka katika hali duni na kwenda kwenye hali ya neema zaidi, ni rai ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuwa Waziri mwenye dhamana na Wizara hii, atajibu hoja hizo kwa utulivu bila ushabiki wa kisiasa ili kwa pamoja tulijenge taifa letu.

B. WIZARA YA FEDHA KUJIPENDELEA KATIKA MGAWO WA KEKI YA TAIFA

7. Mheshimiwa Spika, kulingana na kanuni na utaratibu tuliojiwekea, Wizara ya Fedha ina jukumu la kugawa fedha kwa wizara nyingine zote kwa uwiano ulio sawa kwa kuzingatia ukomo wa bajeti uliopangwa kwa mwaka wa fedha husika. Kwa msingi huo, ukomowa bajeti uliopangwa kwa mwaka wa fedha 2019/20 ni asilimiai 1.9

8. Mheshimiwa Spika, kinyume cha utaratibu huo, Wizara ya Fedha imevunja rekodi kwa kukiuka masharti ya ukomo wa bajeti uliowekwa, na kujipendelea kwa kujitengea fedha zaidi ya ukomo huo kwa mwaka wa fedha 2019/2020. Ushahidi wa kujipendelea unatokana na ukweli kwamba; katika mwaka wa fedha 2018/19, fungu 21- Hazina; lilitengewa shilingi bilioni 531 kwa ajili ya matumizi ya kawaida; lakini katika mwaka 2019/2020 wamejitengea shilingi trilioni moja (1) na bilioni 302 sawa na ongezeko la asilimia 245 ambazo ni sawa na shilingi bilioni 771. Kwa upande wa fedha za maendeleo mwaka 2018/19 fungu 21 lilitengewa shilingi bilioni 12.6 lakini mwaka 2019/2020 limetengewa shilingi bilioni 806 ikiwa ni ongezeko la shilingi bilioni 793.4 sawa na asilimia 6,700 nje ya ukomo wa asilimia 1.9. Halikadhalika fungu 50 - Wizara ya Fedha bajeti yake imeongezeka kwazaidi ya asilimia 15 tofauti na ukomo uliowekwa wa asilimia 1.9.

9. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inaitaka Serikali kupitia Waziri wa Fedha kulieleza Bunge hili; uthubutu wa kukiuka masharti ya ukomo wa bajeti unatokana na ubeberu wa wizara hii dhidi ya wizara nyingine au ni kwa ajili ya maslahi ya watu binafsi ndani ya wizara. Tunauliza swali hili kwa kuwa ni jambo la ajabu sana kurundika fedha nyingi namna hiyo kwenye wizara ambayo haizalishi wala haiajiri sehemu kubwa ya watanzania ambao kimsingi ndio wazalishaji wakubwa wanaochangia maendeleo ya uchumi wetu. Serikali hii inayojinasibu kuwa ni Serikali ya wanyonge – wanyonge ambao ni wakulima, wavuvi na wafufaji na wafanya biashara ndogondogo; imekataa kuongeza bajeti kwa wizara zinazowagusa moja kwa moja wanyonge hao na kujipendelea yenyewe kwa kujitengea zaidi ya ukomo uliowekwa.

C. WIZARA YA FEDHA KUSHINDWA KUSIMAMIA SERA YA FEDHA

10. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa ‘Instrument’ ya Mgawanyo wa kazi za Wizara mbalimbali, Wizara ya fedha pamoja na mambo mengine, ina mamlaka na wajibu wa kusimamia sera ya fedha kikamilifu. Hata hivyo, wizara hii imeonyesha udhaifu mkubwa sana wa kutotekeleza madaraka yake ya kisheria kutimiza wajibu huo.

11. Mheshimiwa Spika, suala la vitambulisho vya wajasiriamali lilitakiwa, kwa mujibu wa sheria, kuratibiwa na kutekelezwa kwa asilimia 100 na Wizara ya Fedha. Kinyume na uhalisia huo, Taifa limebaki kwenye mshango mkubwa kuona suala hilo likishughulikiwa na vyombo vingine ambavyo havina mamlaka ya kisheria kuhusu masuala ya fedha.

12. Mheshimiwa Spika, jambo hili limeleta mkanganyiko mkubwa na mgongano wa majukumu miongoni mwa Wizara ya Fedha na Ofisi ya Rais - TAMISEMI. Mpaka sasa Wizara ya Fedha haijatoa tamko au mwongozo wowote wa namna ya kuendesha zoezi hilo. Matokeo yake kila Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa anajitengenezea mwongozo wake. Ni Tanzania pekee ambapo Serikali haina mfumo mmoja makini wa utendaji; isipokuwa kila mtu anafanya analojisikia na kwa namna atakavyo ilhali Serikali ni moja. Huku ni kuwachanganya wananchi!!!!

13. Mheshimiwa Spika, pamoja na vitambulisho vya wajasiriamali kutofuata utaratibu, zoezi hilo limekwenda kunyanganya vyanzo vya mapato vya halmashauri na kuziacha zikiwa mufilisi. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa maelezo, ni kwa nini Ofisi ya Rais TAMISEMI inaingilia majukumu ya Wizara ya Fedha? Au ni kwa sababu Wizara ya Fedha ni dhaifu na imeshindwa kutunga na kusimamia utekelezaji wa Sera ya Fedha? Na kama jibu ni ndiyo; kwanini Wizara hiyo isifutwe na badala yake majukumu yake yatekelezwe na kitengo kitakachoanzishwa ndani ya Ofisi ya Rais- TAMISEMI kwa ajili hiyo?

D. KIBURI CHA WIZARA YA FEDHA KUKIUKA SHERIA YA BAJETI

14. Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa Sheria ya Bajeti ya mwaka 2015 kifungu cha 31, 34(2)(3) na (4); 41(1); 43 na fasili zake zote ni kwamba; Serikali haitakuwa na mamlaka ya kubadili kwa namna yoyote ile bajeti iliyopitishwa na Bunge, bila kuleta mabadiliko hayo Bungeni kwa ajili ya kupata idhini ya Bunge.

15. Mheshimiwa Spika,kinyume na utaratibu huo wa kisheria; Wizara ya Fedha imekuwa ikifanya mabadiliko kwenye bajeti iliyopitishwa na Bunge kimyakimya, bila kuomba ridhaa ya Bunge, jambo ambalo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inalitafsiri kuwa ni dharau kwa Bunge – Bunge ambalo,kwa mujibu wa ibara ya 63(2) ya Katiba ndio chombo kikuu katika Jamhuri ya Muungano chenye madaraka ya kuisimamia Serikali katika utendaji wake wa kazi.

16. Mheshimiwa Spika, mpaka kufikia mwezi machi 2019, Wizara ya Fedha ilikuwa imeshatoa mgawanyo wa fedha za matumizi ya kawaida kwa wizara na idara zinazojitegemea, mikoa na halmashauri, kiasi cha shilingi bilioni 355.815 zaidi ya bajeti iliyokuwa imepitishwa na Bunge ya shilingi trilioni 20.468 na kufanya jumla ya fedha iliyotolewa kuwa shilingi trilioni 20.824.

17. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa malezo kiburi hiki cha Wizara ya Fedha kukiuka sheria ya bajeti kwa makusudi kimetoka wapi? Na ni lini tabia hii itakoma? Kitendo cha Wizara hii kuweka sheria pembeni na kufanya itakavyo kuhusu masuala ya fedha; na kitendo hiki kikaachwa hivi hivi bila kukomeshwa kitafungua mianya ya ubadhirifu na wizi wa fedha za umma, na matokeo yake ni nchi kuendelea kuogelea kwenye lindi la umasikini licha ya rasilimali nyingi tulizo nazo.

18. Mheshimiwa Spika, imefika mahali inabidi Bunge lichukue hatua dhidi ya dharau za namna hii. Kwa sababu hiyo; Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inashauri na kupendekeza kwaba, Bunge hili litoe karipio na onyo kali kwa Wizara ya Fedha kwa vitendo vya ukiukaji wa sheria ya bajeti na sheria ya fedha; lakini mbaya zaidi kwa kulidharau bunge kwa kufanya mabadiliko ya bajeti iliyopitishwa na bunge bila kuomba ridhaa ya bunge.

E. UDHAIFU WA KITENGO CHA KUDHIBITI FEDHA HARAMU

19. Mheshimiwa Spika, wizara ya fedha ina kitengo cha kudhibiti fedha haramu. Hata hivyo, jukumu hilo kwa sasa linaonekana likifanywa na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP) jambo ambaolo linadhihirisha uzoefu wa wizara ya fedha kukwepa na kuyakimbia majukumu yake kama ilivyokimbia jukumu la kuratibu vitambulisho vya wajasiriamali.

20. Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya udhaifu wa kitengo cha kudhibiti fedha haramu, kumekuwa na malalamiko mengi sana kwa wafanyabiashara kubambikiwa kesi za utakatishaji fedha na uhujumu uchumi; kwa kuwa jukumu hilo linafanywa na watu wasiojua sheria za fedha. Kwa sababu hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa maelezo mbele ya Bunge hili; kwamba mamlaka ya DPP kuingilia shughuli za ‘Financial Inteligence Unit’ ameyatoa kwenye sheria ipi ya fedha?Kambi Rasmi ya Upinzani inauliza swali hili kwa kuwa inaeleweka kwamba kazi ya DPP ni kumkamata na kumpeleka mahakamani mtuhumiwa aliyebainika na Kitengo hicho kuhusu masuala ya utakatishaji fedha na uhujumu uchumi, na sio kazi ya DPP kuwabaini watu hao kwa kuwa hana taaluma ya mifumo ya fedha.

F. MSEREREKO WA KUPAA WA DENI LA TAIFA

21. Mheshimiwa Spika, miongoni mwa majukumu msingi ya Wizara ya fedha ni pamoja na jukumu la kusimamia deni la Taifa. Wizara imeonyesha udhaifu mkubwa katika kusimamia Deni la Taifa, kwa kuwa Deni hili limeendelea kuwa kubwa kila mwaka jambo ambalo limekuwa na athari kubwa katika bajeti ya Serikali na hivyo kuathiri uchumi wetu na maisha ya wananchi kwa jumla.

22. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2017/18; ni kwamba hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2018, deni la Serikali lilikuwa limefikia Shilingi trilioni 50.926. Kati ya fedha hizo, shilingi trilioni 14.732 zilikuwa ni deni la ndani na shilingi trilioni 36.194 zilikuwa ni deni la nje.

23. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa ripoti hiyo, deni la Serikali limeongezeka kwa shilingi trilioni 4.845 sawa na asilimia 10.5 ikilinganishwa na deni la Shilingi trilioni 46.081 lililoripotiwa tarehe 30 Juni, 2017.

24. Mheshimiwa Spika,Deni linaendelela kukua kila mwaka kutokana na:-
i. kuwepo kwa nakisi ya mapato ya serikali dhidi ya matumizi.Na jambo hili tumelipigia kelele miaka mingi; Serikali imekuwa ikiweka makisio makubwa ya makusanyo ya mapato na matokeo yake hushindwa kukusanya mapato hayo. Aidha, imekuwa ikipanga matumizi makubwa kuliko mapato inayokusanya Kwa mfano; katika mwaka wa fedha 2016/17 Serikali ilipanga kukusanya kiasi cha shilingi trilioni 29.54 lakini iliweza kukusanya mapato kutoka vyanzo vyote yaliyofikia shilingi trilioni 20.7 sawa na asilimia 70.1 ya lengo. Hii ina maana kwamba, asilimia takriban 30 iliyobaki (sawa na shilingi trilioni 8.83) ilikuwa ni nakisi ya bajeti husika na kwa maana hiyo kiasi hicho inabidi kikopwe ili kukidhi matumizi ya bajeti husika. Aidha, katika mwaka wa fedha 2017/18 Serikali ilipanga kukusanya jumla ya shilingi trilioni 31.71 lakini iliweza kukusanya kiasi cha shilingi trilioni 21.89 sawa na asilimia 69 ya lengo. Hii ina maana kwamba, asilimia 31 iliyobaki (sawa na shilingi trilioni 9.82) inabidi kikopwe ili kukidhi matumizi ya bajeti husika.
ii. Aidha, deni limeendelea kukua kila mwaka kutokana na ubadilishwaji wa hati fungani,
iii. ukopaji kwa ajili ya shughuli za maendele na
iv. hasara katika kubadilisha fedha za kigeni ikisababishwa na kushuka kwa thamani ya shilingi dhidi ya fedha nyingine za kigeni ambazo ni imara.
Jedwali Na. 1 linaonyesha mwenendo wa ukuaji wa deni kwa miaka mitatu iliyopita:-
Jedwali Na. 1. Mwenendo wa Ukuaji wa Deni la Serikali kwa miaka mitatu iliyopita
2015/16 2016/17 2017/18
Shilingi bilioni
Jumla ya Deni 41,039 46,081 50,927
Deni la Nje 29,846 32,746 36,194
Deni la Ndani 11,193 13,335 14,732.45
Chanzo: CAG 2017/18 (uk. 138)

25. Mheshimiwa Spika, ukiangalia mwenendo huo wa ukuaji wa deni utaona kwamba Serikali hii ya awamu ya tano inayojigamba kwamba haikopi nje, na kwamba inatumia fedha zake za ndani kuendesha miradi yake ya maendeleo, ilipoingia madarakani ilikuta deni la taifa likiwa shilingi trilioni 41.039 ikaongeza deni hilo kwa shilingi trilioni 5 hadi kufikia shilingi trilioni 46.081 kwa mwaka wake wa kwanza tu madarakani. Aidha, katika mwaka wake wa pili madarakani, Serikali hii imeliongeza deni kwa takribani shilingi trilioni 5 nyingine hadi kufikia shilingi trilioni 50.927.

26. Mheshimiwa Spika, deni la shilingi trilioni 50 .9 ambayo ni karibu sawa na trilioni 51 ni asilimia 40.6 ya Pato la Taifa ambalo kwa sasa ni shilingi trilioni 125.6 . Kiwango hiki cha deni ni kikubwa mno na kina mwelekeo wa kuiweka nchi rehani kwa kuwa kinakaribia kufikia nusu ya pato letu.

27. Mheshimwiwa Spika, Sababu za kuongezeka kwa Deni la Serikali kwa kiasi kikubwa kunasababishwa na mikopo halisi (mikopo halisi hapa inajumuisha mapokezi ya fedha za mikopo, ulipaji wa mtaji, malipo ya riba za dhamana za Serikali za muda mfupi na misamaha ya madeni).

28. Mheshimiwa Spika, Kwa miaka mitatu iliyopita, sababu hii imekuwa ikichangia ukuaji wa deni kwa zaidi ya asilimia 70, ambapo mwaka 2016/17 ilikuwa juu zaidi na kufikia asilimia 88 . Uchambuzi wa Ofisi ya Ukaguzi ulibainisha kuwa, kushuka kwa thamani ya sarafu/fedha ya Tanzania kumechangia ongezeko la deni la taifa kwa asilimia 20 kwa mwaka 2017/18 (hili ni ongezeko kubwa ikilinganishwa na asilimia 9 ya mwaka 2016/17).

29. Mheshimiwa Spika,kwa mujibu wa CAG, kushuka kwa thamani ya sarafu ya Tanzania kunaathiri vibaya ongezeko la deni, hivyo wito unatolewa kwa watunga sera kubuni mikakati itakayopunguza athari hizo.

30. Mheshimiwa Spika, kuhusu malimbikizo ya riba, CAG alibaini kwamba Malimbikizo hayo yanatokana na nchi tano (Iraq, India, Romania, Angola na Iran) za kundi lisilo la wanachama wa Paris, ambazo hazijatoa misamaha ya madeni kwa Tanzania kulingana na makubaliano.

F1. Deni la Ndani

31. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani imeona ni muhimu kuzungumzia deni la ndani kwa kuwa kitendo cha Serikali kukopa ndani kinawaathiri sana wananchi hasa wajasiriamali kushindwa kupata mikopo kwenye mabenki na taasisi za fedha za ndani. Kwa mujibu wa Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya mwaka 2017/18; hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2018 deni la ndani lilifikia shilingi trilioni 14.732. Hili ni ongezeko la shilingi trilioni 1.396 sawa na asilimia 10 kutoka shilingi trilioni 13.335 kwa kipindi kama hicho mwaka 2017.

32. Mheshimiwa Spika, deni hilo linatokana na Serikali kukopa fedha katika soko la ndani kwa ajili ya kusaidia bajeti na kwa ajili ya kulipia dhamana za Serikali zilizoiva kwa kipindi cha mwaka 2017/18. CAG anasema kwamba; Ijapokuwa deni la ndani haliathiriwi na kushuka kwa thamani ya shilingi lakini linakuwa; na linaathiri ukopeshaji kwa sekta binafsi, na ni mzigo kwa serikali kwa siku zijazo.

33. Mheshimiwa Spika, Uchambuzi wa CAG unaonesha kuwa, jumla ya Shilingi trilioni 5.704 zilizokopwa kwenye mabenki na taasisi za fedha za ndani hazikuweza kulipa deni na riba za mwaka husika zilizofikia shilingi trilioni 6.152 Hivyo, serikali ilitumia Shilingi billion 448.75 toka vyanzo vingine vya mapato ili kuhudumia deni la ndani. Kwa sababu hiyo CAG anasema deni la ndani halikuchangia miradi ya maendeleo. Kiwango cha kuhudumia deni la ndani kilifikia asilimia 108 ya fedha zilizopatikana toka mikopo ya ndani.

34. Mheshimiwa Spika, kutokana na mwenendo huo wa Serikali kukopa ndani kwa kiwango kikubwa na kushindwa kulipa fedha hizo, Kambi Rasmi ya Upinzani ina mtazamo kwamba jambo hilo lisipotafutiwa ufumbuzi wa mapema, kuna hatari ya uchumi wetu kuendelea kuporomoka na kusababisha hali ngumu zaidi ya maisha kuliko ilivyo sasa. Kwa sababu hiyo, ni rai ya Kambi Rasmi ya Upinzani kwamba; Waziri wa Fedha na timu yake ambao ndio watunga sera za fedha kuvaa viatu vyao sawasawa maana inaonekana vinawapwaya.

35. Mheshimiwa Spika, ni aibu kwetu sisi wabunge kuimba wimbo uleule kila mwaka wa bajeti kuhusu madeni ya Serikali, lakini ni aibu zaidi kwa Serikali kubanana na wananchi kwenye mabenki na taasisi za fedha za ndani, kukopa fedha ajili ya kulipa madeni yake ya ndani!!

F2. Deni la Nje
36. Mheshimiwa Spika,ni Serikali hii hii ya awamu ya tano iliyoingia madarakani kwa tambo kwamba haina haja na fedha za wahisani na kwamba ina uwezo wa kujiendesha na kugharamia miradi ya maendeleo kwa kutumia fedha za ndani. Imefikia hatua Serikali inawaita watu wanaoikosoa na kuielekeza mambo mazuri ya kufanya, kuwani vibaraka wanaotumika na mabeberu – ikimaanisha mataifa ya nje.

37. Mheshimiwa Spika, hayo mabeberu ambayo Serikali imeamua kuyaita hivyo, yanaidai Serikali hii jumla ya shilingi trilioni 36.194. Kwa mujibu wa CAG, deni hilo ni sawa na asilimia 71 ya deni lote la Serikali. Deni hili liliongezeka kwa shilingi trilioni 3.448 ambazo ni sawa na ongezeko la asilimia 10.5 kutoka shilingi trilioni 32.745 za mwaka 2016/17. Kwa mujibu wa CAG, taasisi za Kimataifa ndio wakopeshaji wakubwa zaidi wakiwa na asilimia 58 zikifuatiwa na nchi marafiki asilimia 11.

F3. Usimamizi Dhaifu wa Deni la Taifa

38. Mheshimiwa Spika, suala la kuendelea kupaa kwa deni la taifa kunasababishwa pia na usimamizi dhaifu wa deni hilo kupitia kitengo cha usimamizi wa deni la taifa. Kwa mfano, ukaguzi wa CAG ulibaini mapungufu yafuatayo katika usimamizi wa deni la taifa.
i. Upotoshwaji wa mapokezi ya mikopo kutokana na mapungufu ya Udhibiti wa Ndani katika kurekodi na kutaarifu,
ii. Kuchelewesha kulipa madeni ya Benki Kuu, Shilingi bilioni 212.7;
iii. Kutokuwapo kwa uwiano wa taarifa za mfumo wa malipo (Epicor) na mfumo wa kutunza taarifa za deni la taifa (Common Wealth Secretariat-Debt Record Management System – (CSDRMS));
iv. Kushindwa kutambua madeni yatokanayo na malimbikizo ya michango ya pensheni;

39. Mheshimiwa Spika, licha ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuonyesha madhaifu ya kitengo cha usimamizi wa deni la Taifa kwa miaka mingi, na licha ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kutoa rai kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kufanya ukaguzi maalum (Special Audit) katika kitengo cha deni la Taifa (Fungu 22) ili tuweze kujua mikopo tunayoichukua kila mwaka inatumika kufanyia nini, na kama miradi iliyotekelezwa kutokana na mikopo hiyo ni ya kipaumbele au la kwa mujibu wa mpango wa Taifa wa Maendeleo; na licha ya kuitaka Serikali kutenganisha deni halisi la Taifa na matumizi mengineyo yanayohusu Mfuko Mkuu wa Hazina ili kuziba mianya ya ubadhirifu au matumizi mabaya ya fedha za umma kwa kisingizio cha Deni la Taifa; na licha ya kuionya Serikali kuacha kukopa mikopo mikubwa yenye masharti ya kibiashara, ambayo hatimaye inaliingiza taifa kwenye mzigo wa madeni; na licha ya kuitaka Serikali kuleta pendekezo la mkopo Bungeni kabla haijakopa pamoja na orodha ya miradi itakayotekelezwa kwa kutumia mkopo huo ili Bunge liidhinishe; Serikali hii ya awamu ya tano imepuuza mapendekezo yote hayo na badala yake imeendelea kukopa mikopo yenye mashari ya kibaishara – jambo ambalo limeongeza kiwango cha deni kwa hali ya juu sana. Athari za jambo hili ni kwamba fedha nyingi karibia nusu ya Pato la Taifa, zitatumika kulipa madeni na kuwaacha wananchi wakiwa hawana huduma muhimu za jamii na pia kuacha miradi mingi ya maendeleo bila kutekelezwa.

40. Mheshimiwa Spika,CAG anasema; kwa kuwa mapendekezo ya kurekebisha mfumo wa usimamizi wa deni la taifa ni ya muda mrefu; na kuwa kuwa Serikali haikutekeleza mapendekezo hayo licha ya kukumbushwa kila wakati; hii inaashiria kuwa, serikali imekuwa na umakini hafifu katika utekelezaji wa mapendekezo ya Ukaguzi. Na kwa sababu hiyo; Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaipa changamoto Serikali hii ya awamu ya tano, na kuitaka kulieleza Bunge hili; inatoa wapi mamlaka ya kimaadili (moral authority) ya kusema inapiga vita rushwa na ufisadi; na kwamba inataka kujenga uchumi wa kati kupitia mapinduzi ya viwanda, ikiwa imeshindwa kudhibiti madeni na upotevu wa fedha za umma kwa uzembe na udhaifu mkubwa wa Wizara ya Fedha ambayo kwa kila kigezo, imeshindwa kutumia mamlaka yake ya kisheria kusimamia na kutekeleza sera ya fedha.

G. MAMLAKA YA MAPATO TANZANIA HAINA UWEZO WA KUKUSANYA MAPATO

41. Mheshimiwa Spika,kwa mujibu wa ripoti ya CAG ya mwaka 2017/18; Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilikusanya jumla ya shilingi trilioni 15.386 ikiwa ni pungufu ya shilingi trilioni 1.929 ya lengo la kukusanya shilingi trilioni 17.315. Upungufu huo ni sawa na asmilimia 11 ya lengo.

42. Mheshimiwa Spika, taarifa ya CAG inaonyesha pia kwamba; kwa ujumla, idara zote tatu za mapato zilishindwa kufikia malengo kwa mwaka wa fedha 2017/18. Taarifa hiyo inaonesha kwamba Idara ya walipa kodi wakubwa ilikusanya asilimia 41 ya makusanyo yote ambayo ndiyo sehemu kubwa kuliko idara zote; ikifuatiwa na Idara ya Forodha yenye asilimia 40 na idara ya kodi za ndani yenye asilimia 19 ambayo ndiyo ya mwisho kwa mwaka wa fedha 2017/2018, makusanyo haya hayahusishi vocha ya misamaha ya kodi kutoka Hazina.

43. Mheshimiwa Spika, Kutokana na mchanganuo huo, ni dhahiri kuwa mchango wa makusanyo kutoka Idara ya Mapato ya Ndani umekuwa nyuma ikilinganishwa na idara nyingine. Aidha, taarifa hiyo inaonesha kuwa mwelekeo wa makusanyo ya mapato kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita kwa wastani, ulikuwa chini ya makadirio yaliyoidhinishwa,isipokuwa kwa mwaka wa fedha 2015/16 wakati wa Serikali ya awamu ya nne ndipo makusanyo halisi yalikuwa juu ya makadirio kwa asilimia 0.13.

44. Mheshimiwa Spika, Taarifa ya CAG inaeleza kuwa ufanisi katika ukusanyaji mapato kwa mwaka wa fedha 2017/18 haukuwa mzuri kwani uwiano wa kodi dhidi ya pato la ndani la taifa ulipungua (kodi kwa pato la taifa) mpaka kufikia asilimia 12.8 ikilinganishwa na asilimia 13.2 kwa mwaka 2016/17. Kwa sababu hiyo, Mamlaka ilishindwa kutimiza lengo na mkakati wa kufikia uwiano wa asilimia 19.9 wa kodi dhidi ya pato la ndani la taifa, lengo ambalo Mamlaka ilijiwekea kulifikia katika mwaka 2018.

45. Mheshimiwa Spika, hakuna fedheha na aibu mbaya kama kujiwekea lengo na kushindwa kulifikia. Kitendo hicho kikitokea, kinadhihirisha uwezo mdogo wa kufikiri, kupanga na kutekeleza. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haioni mantiki ya Serikali hii kutafuta umaarufu uchwara (cheap popularity) kwa wananchi kwa kuwaaminisha kuwa ina uwezo mkubwa wa kukusanya mapato wakatitofauti kati ya tambo hizo na uhalisia wenyewe ni sawa na tofauti ya umbali kati ya Mbingu na Ardhi.

46. Mheshimiwa Spika, uwezo mdogo wa TRA kukusanya kodi unafahamika pia kimataifa. Ripoti ya CAG inasema kwamba; Mchanganuo linganifu wa ufanisi wa kodi kwa nchi za Afrika Mashariki unaonesha kwamba, Tanzania ilishika nafasi ya mwisho katika ukusanyaji mapato kwa mwaka wa fedha 2017/18. Kambi Rasmi ya Upinzani inaionya Serikali kuacha kujitapa kuwa ina uwezo mkubwa wa kukusanya mapato wakati tafiti zimeonyesha kuwa ina uwezo mdogo na badala yake ijielekeze kutekeleza mapendekezo ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni tuliyoyatoa siku nyingi.

47. Mheshimiwa Spika, mapendekezo hayo ni pamoja na kuongeza wigo wa vyanzo vya kodi, kudhibiti mianya ya upotevu wa kodi na kuwapa motisha walipa kodi, ili kuongezaulipaji kodi kwa hiari.

H. UDHAIFU WA WIZARA YA FEDHA KATIKA KUGAWA FEDHA

48. Mheshimiwa Spika, Kwa muda mrefu sasa Serikali kupitia Wizara ya Fedha imekuwa ama ikichelewa kupeleka fedha kwenye wizara na idara mbalimbali za Serikali au kutoa fedha pungufu na katika mazingira mengine kutokutoa fedha kabisa kama ambayo zimeidhinishwa na Bunge. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imekuwa ikiitaka Serikali kuandaa makisio yake ya mwaka, yanayoshabihiana na makusanyo ya mapato!!Kwa kufanya hivyo, inatarajiwa kwamba shughuli zilizopangwa zitatekelezwa kama zilivyopangwa.

49. Mheshimiwa Spika, Hali hii inaondoa umuhimu wa Bunge kukaa kwa gharama kubwa kupitisha bajeti ya Serikali ambayo haitekelezwi ipasavyo. Tofauti na awamu za utawala wa CCM zilizotangulia, Serikali hii ya awamu ya tano ambayo imekuwa ikijigamba kwamba imefanikiwa kukusanya mapato Kwa kiwango cha hali ya juu kuzidi makisio iliyoyaweka kila mwezi, lakini ukweli ni kuwa imekuwa na hali mbaya zaidi katika utekelezaji wa bajeti na hasa bajeti ya maendeleo kuliko awamu zilizopita.

50. Mheshimiwa Spika, katika kuonesha ukweli huo, zifuatazo ni baadhi ya wizara na fedha za maendeleo zilizotolewa hadi Mwezi Machi, 2019 kulinganisha na fedha zilizokuwa zimeidhinishwa na Bunge hili tukufu:

i. Wizara ya Maliasili na Utalii

51. Mheshimiwa Spika, fedha ya maendeleo iliyotengwa kwa ajili ya Wizara ya Maliasili na Utalii ilikuwa kwa mwaka wa fedha 2018/19 ni shilingi bilioni 29.978. Hata hivyo, fedha iliyotolewa hadi kufikia mwezi Februari, 2019 ilikuwa shilingi bilioni 10.551 sawa na asilmia 35 ya bajeti ya maendeleo. Hii ina maana kwamba asilimia 65 ya fedha za maendeleo katika wizara hii hazikutolewa.

ii. Wizara ya Ardhi

52. Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha 2018/2019 Wizara ya ilitengewa jumla ya shilingi bilioni 30.537 ikiwa ni fedha za maendeleo; lakini hadi kufikia Februari, 2019 fedha iliyokuwa imetolewa ni shilingi bilioni 16.858 sawa na asilimia 55 ya bajeti ya maendeleo. Kwa maana hiyo, asilimia 45 ya bajeti hiyo haikutekelezwa.

a) Tume ya Ardhi

53. Mheshimiwa Spika,kwa mwaka 2018/19 Tume ya Ardhi ilitengewa shilingi bilioni 5 kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo; lakini hadi kufikia Januari, 2019 hakuna hata senti moja iliyokuwa imetolewa na hazina. Pamoja na Serikali kujigamba kwamba; tengeo la 2018/19 liliongezeka kwa asilimia 234 ikilinganishwa la lile la shilingi bilioni 2.115 la mwaka 2017/18; lakini kama fedha hazikutolewa kabisa ongezeko hilo lina maana gani?

iii. Wizara ya Mifugo na Uvuvi

54. Mheshimiwa Spika, fedha za miradi ya maendeleo zilizotolewa katika Sekta ya mifugo hadikufikia Aprili, 2019 ni shilingi bilioni 2.173 sawa na asilimia 43. Aidha, fedha za maendeleo zilizotolewa katika idara ya uvuvi kwa kipindi hicho zilikuwa bilioni 4.012 sawa na asilimia 56.3 ya bajeti iliyopangwa. Hivyo, kwa wastani, utekelezaji wa bajeti ya maendeleo kwa sekta zote mbili, ulikuwa chini ya asilimia 50.

iv. Wizara ya Maji

55. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2018/19 Wizara ya Maji ilitengewa shilingi bilioni 673.214 kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo; lakini hadi kufikia mwezi februari, 2019, ni shilingi bilioni 100.068 sawa na asilimia 14.5 tu ndizo zilizokuwa zimetolewa na hazina.

56. Mheshimiwa Spika,hii ina maana kwamba asilimia takriba asilimia 85 ya bajeti ya miradi ya maji hakikutekelezwa. Na pia takwimu zinaonesha kuwa fedha za maendeleo zinazotolewa katika wizara hii zimekuwa na mserereko wa kupungua kila mwaka. Huu ni ushahidi tosha kwamba, maji sio kipaumbele kwa Serikali yah ii ya CCM.

v. Wizara ya Elimu

57. Mheshimiwa Spika, kati ya miradi ya maendeleo 41 yenye thamani ya shilingi 929,969,402,000/= miradi 24 yenye thamani ya shilingi 100,894,000,000/- haikupatiwa hata senti moja kwa ajili ya utekelezaji wa miradi katika mwaka wa fedha 2018/19.
vi. Wizara ya Kilimo

58. Mheshimiwa Spika,Wizara ya Kilimo – fungu 43 ilitengewa shilingi bilioni 98.119 ikiwa ni fedha za kugharamia miradi ya maendeleo; lakini fedha zilizotolewa hadi kufikia Machi, 2019, zilikuwa shilingi bilioni 41.222 sawa na asilimia 42 ya bajeti ya maendeleo iliyotengwa.

59. Mheshimiwa Spika, bajeti ya Wizara inayoajiri takriban asilimia 75 ya watanzania; haikutekelezwa kwa asilimia 58. Kwa hiyo, hizi tambo za Serikali kwamba inawajali wanyonge wakati haipeleki fedha kwenye sekta zinazotoa ajira kwa wanyonge hao; ni chukizo hata kwa Mwenyezi Mungu; maana huo ni uongo na ni unafiki.

vii. Wizara ya Viwanda na Biashara

60. Mheshimiwa Spika,katika mwaka 2018/19, Wizara ya Viwanda na Biashara ilitengewa shilingi bilioni 90.5 ikiwa ni fedha za maendeleo. Hata hivyo fedha zilizopokelewa kutoka hazina hadi kufikia Machi, 2019 ni shilingi bilioni 6.477 sawa na asilimia 6.5 tu ya bajeti ya maendeleo.
Aidha, Idara ya Biashara na Uwekezaji Fungu 60 ilikuwa imetengewa shilingi bilioni 7 kwa ajili ya maendeleo; lakini hadi Machi, 2019 hakuna hata shilingi moja iliyokuwa imepokelewa. Hii ina maana kwamba bajeti ya maendeleo katika idara hii haikutekelezwa kabisa.

61. Mheshimiwa Spika,ni bahati mbaya sana kwamba Serikali hii ya awamu ya tano inatekeleza uchumi wa viwanda kwa kupeleka asilimia 6 ya fedha za maendeleo kwenye Wizara ya Viwanda; na pia bila aibu haipeleki chochote kwenye Idara ya biashara na uwekezaji.

62. Mheshimiwa Spika, ipo methali isemayo, akutukanaye hakuchagulii tusi; kitendo cha Serikali hii kutotekeleza bajeti ya maendeleo katika Wizara ya Viwanda na Biashara na wakati huohuo ikijivika mabango kuwa kuwa inajenga uchumi wa viwanda ni matusi kwa watanzania kwamba wao ni wajinga hawaelewi nini maana ya uchumi wa viwanda ndio maana Serikali haiogopi kuendelea kuwandanganya watanzania.

viii. Wizara ya Madini

63. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2018/2019 Wizara iliidhinishiwa jumla ya shilingi Bilioni 19.620 kw ajili ya miradi ya maendeleo. Hata hivyo, fedha iliyopokelewa kutoka hazina hadi kufikia February, 2019 ilikuwa ni shilingi shilingi milioni 100 tu, sawa na asilimia 0.5% ya bajeti yote ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo. Kwa uwekezaji duni namna hiyo; tutaendelea kulalamika kuwa tunaibiwa madini lakini tatizo sio wizi bali ni uwekezaji usio na tija. Huwezi kuvuna usikopanda!!!

64. Mheshimiwa Spika,kwa kifupi, ukitafuta wastani utakuta kwamba bajeti ya maendeleo imetekelezwa chini ya asilimia 50 jambo ambalo ni kikwazo katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Kwa vyovyote vile utekelezaji huu duni unatokana na mipango duni inayoandaliwa na wizara ya fedha kuanzia kwenye kupanga makisio ya bajeti, ukusanyaji wa mapato na ugawanyaji wa fedha kwa kuzingatia vipaumbele vya taifa katika bajeti ya mwaka wa fedha husika.

65. Mheshimiwa Spika, Wizara ya Fedha haiwezi kukwepa lawama kwa uzembe na udhaifu huo. Kwa mantiki hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inamtaka Waziri wa Fedha alieleza Bunge hili kuna nini kinamkwamisha katika kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi? Je, ni ukosefu wa rasilimaliwatu wenye ujuzi wa masuala ya mipango; Je ni Seriali imefilisika; au ni mashinikizo kutoka juu; au viatu vya mtangulizi wake vinampwaya.

I. UWIANO HASI KATI YA MAUZO YA NJE NA MAUNUNUZI YA BIDHAA NA HUDUMA KUTOKA NJE YA NCHI

66. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya kila mwezi ya mapitio ya Uchumi, inayotolewa na Benki Kuu ya Tanzania toleo la April, 2019 ni kwamba; kwa kipindi kinachoishia Machi, 2019 Tanzania ilikuwa na nakisi katika biashara ya nje ya dola za Kimarekani milioni 654.8 Kwa kipindi cha hiki cha 2019 nakisi ya akaunti ya mauzo nje ya nchi inaonesha dolla za kimarekani milioni 2,526.8 kulinganisha na dolla za Kimarekani milioni 2,049.3 kwa kipindi cha Machi, 2018. Hii inatokana na kuagiza nje zaidi kuliko tunavyouza bidhaa na huduma nje.

67. Mheshimiwa Spika, taarifa hiyo inaonesha kuwa; kwa kipindi kinachoishia Machi, 2019, mauzo nje ya nchi yaliongezeka kuwa dolla ya kimarekani milioni 8,544.5 kwa kulinganisha na dolla za Kimarekani milioni 8,488.2 kipindi kama hicho mwaka 2018. Ongezeko hilo lilitokana na mauzo ya bidhaa zisizo asilia zilizokuwa kwa asilimia 78 ya bidhaa zilizouzwa nje na asilimia 40.7 ya mauzo yote nje ya nchi. Mauzo haya yalikuwa ni dhahabu ambayo ni takriban nusu ya bidhaa zisizo za asili kwenye mauzo nje ya nchi.

68. Mheshimiwa Spika,kwa upande wa manunuzi nje ya nchi, kwa huduma na bidhaa takwimu zinaonesha kuwa hadi Mwezi Machi, 2019 tulitumia bidhaa na huduma zenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 10,550.4 kulinganisha na Dola za Kimarekani milioni 9,916.1 kwa kipindi kilichoishia Machi, 2018. Ongezeko hilo, likichangiwa kwa kiwango kikubwa uagizaji wa mafuta kwa kasi. Aidha uagizaji wa bidhaa za vyakula ulishukakutokana na mavuno mazuri kwa kipindi cha msimu wa 2017/18.

69. Mheshimiwa Spika, Wizara ya fedha ndiye mpangaji mkubwa wa uchumi wetu, mvurugano wa kushindwa kuuza nje bidhaa asilia ambazo ni bidhaa za kilimo kama Kahawa, Korosho, Pamba n.k ni kutokana na ukweli kwamba Serikali iliingilia kwa makusudi/ ilihujumu mfumo wa ndani wa ununuzi wa mazao hayo na hivyo kupelekea kukatisha tama wazalishaji wakubwa wa mazao hayo. Hivyo kupelekea kushuka sana kwa mauzo yetu bidhaa za asilia nje ya nchi. Aidha, kwa kuwa Wizara ya fedha imeshindwa kurekebisha mfumo mzima wa uzalishaji hasa kwa kutumia gesi asilia na hivyo kuendelea kutoa mwanya kwa nchi kuendelea kujikita katika matumizi makubwa ya mafuta na hivyo kuendelea kutoa fedha zetu kidogo za kigeni kwenda nje.

70. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitakaSerikali kutoa maelezo mbele ya Bunge hili, kuhusu hatua iliyofikia ya uzalishaji wa gesi asilia huko mtwara – gesi ambayo kwa kiasi kikubwa ingepunguza manunuzi ya mafuta kutoka nje jambo ambalo limesababisha kuwe na uwiano hasi kati ya mauzo yetu na maununuzi yetu nje ya nchi.

J. UDHAIFU WA OFISI YA MSAJILI WA HAZINA KATIKA KUSIMAMIA MASHIRIKA YA UMMA

71. Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa Sheria ya Mashirika ya Umma kama ilivyofanyiwa markebisho mwaka 2010 ni kwamba; Msajili wa Hazina ndiye Msimamizi Mkuu wa Mashirika yote ya Umma. Kwa mujibu wa Sheria hiyo, majukumu ya msingi ya ofisi ya Msajili wa Hazina ni kudhibiti uendeshaji wa mashirika ya Umma kwa kutoa miongozo ya namna ya kutekeleza kazi zake; kukusanya mapato yasiyo ya kodi kutoka katika mashirika na taasisi ambazo serikali imewekeza kupitia gawio na michango; kusimamia uwekezaji wa serikali katika mitaji ya mashirika au taasisi za umma na kampunia binafsi; kutoa ushauri kwa serikali juu ya njia bora za kuendeleza uwekezaji wake katika mashirika ya umma na kampuni binafsi; kuchambua na kuidhinisha nyaraka mbalimbali zinazohusu uendeshaji wa taasisi na mashirika ya umma kwa lengo la kubaini tija na ufanisi wa mashirika hayo; na kufanya uhakiki wa kimenejimenti kwa lengo la kubaini namna ambavyo utekelezaji wa nyaraka na miongozo mbalimbali ya serikali unavyofanyika.

72. Mheshimiwa Spika, majukumu hayo kwa ofisi ya Msajili ni makubwa sana na ili kuyatekeleza kwa ukamilifu wake inatakiwa kuwa na rasilimali watu ya kutosha na yenye weledi wa kutosha sambamba na uwepo wa teknolojia ya kisasa kwenye mifumo ya computer. Hivyo basi Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali iwaeleze watanzania ni kwa kiwango gani ofisi ya Msajili wa Hazina imeimarika katika utendaji kazi wake?

73. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani imehoji hivyo kutokana na ukweli kwamba mashirika mengi na taasisi za umma zimekuwa zikikabiliwa na madeni makubwa kiasi kwamba yanashindwa kujiendesha na madeni hayo ni madeni ya Serikali kama ilivyo kwa mifuko ya hifadhi za jamii. Kwa kipindi cha ukaguzi cha mwaka wa fedha 2015/16 serikali ilikuwa inadaiwa madeni ya shilingi trilioni 1.60 yaliyozidi muda wake wa kulipwa kutoka katika taasisi tofauti kumi na tisa (19). Madeni haya yanatokana na mikopo ya moja kwa moja, dhamana, na michango ambayo haikuwasilishwa kulingana na matakwa ya sheria. Hapa ofisi ya Msajili wa hazina inazungumza vipi kuhusu madeni hayo na ambayo hadi sasa hayajawahi kulipwa kwa ukamilifu wake?

74. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inashawishika kusema kuwa kutokana na udhaifu mkubwa wa ukosefu wa rasilimali watu na fedha vimepelekea mashirika yanayokaribia kufilisika kuunganishwa na mashirika yaliyo na unafuu katika utendaji, jambo ambalo linaleta usumbufu na ukata mkubwa kwa mashirika hayo mapya. Mfano ni uunganishwaji wa Benki ya Wanawake, Twiga na Benki ya Posta. Hii maana yake ni kuwa madeni yote ya benki hizo mbili yanabebwa na benki ya posta na mwisho mzigo wa madeni unapunguza uwezo wa kiutendaji wa Benki ya Posta.

75. Mheshimiwa Spika, Uunganishwaji wa Self Microfinance na UTT Microfinance ambayo ilikuwa inadaiwa na inafilisika na hivyo kuhamisha mzigo kwa Self Microfinance. Hapa maana yake upembuzi yakinifu kuhusu utendaji wa taasisi hizo mbili haukufanyika au kulikuwa na kulindana kwa kifisadi katika mchakato mzima wa kuunganisha taasisi hizo.

76. Mheshimiwa Spika,Udhaifu wa Ofisi ya Msajili wa hazina umeelezwa pia na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kama ifuatavyo:
i. Benki ya Azania kutokuwa chini ya usimamizi wa Msajili wa Hazina,
ii. Msajili wa Hazina hajaweza kuonyesha uhalali wa kisheria katika umiliki wa PRIDE;
iii. Kukosekana kwa mkataba na dhamana kwa mkopo wa Shilingi bilioni 44.29 uliotolewa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF);
iv. Benki ya Wanawake Tanzania (TWB) kutofikia kiwango cha chini cha mtaji;
v. Kuporomoka kwa wa ufanisi kibiashara kwa Shirika la Posta Tanzania (TPC);
vi. tatizo la uendelevu wa Benki ya Twiga, kuchelewa kutekeleza mpango mkakati kuhusiana na ujenzi wa nyumba za walimu;
vii. Wizara ya Nishati kutokulipa deni la pango la Shilingi bilioni 1.117 kwa Kampuni ya Umeme Tanzania (TANESCO);
viii. Pamoja na upunjifu katika ulipaji wa kodi ya pango uliofanya na Mlima ni City Holding Limited kwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

77. Mheshimiwa Spika, mapungufu haya mbali ya kukosekana kwa rasilimali watu ya kutosha na yenye weledi vile vile ni rasilimali fedha.; mathalani kwa mwaka wa fedha 2018/19 fedha zilizoidhinishwa kwa ofisi hiyo ni shilingi bilioni 56.242; lakini hadi mwezi Machi 2019 fedha zilizotolewa ni shilingi bilioni 11.761 sawa na asilimia 20.9 tu ya fedha zote zilizopangwa.

78. Mheshimiwa Spika,kwa kiwango hicho cha utoaji fedha maana yake ni kiashiria pia cha jinsi Ofisi hiyo inavyotekeleza majukumu yake kwa kusuasua na hivyo matokeo yake ni ya kusuasua pia kwa mashirika inayoyasimamia. Hii ndio maana tunaambiwa TTCL imetoa gawio kwa serikali lakini kesho yake shirika hilo linaiomba Serikali fedha za mtaji wa kiuendeshaji.

K. SERIKALI INA LENGO LA KUDHULUMU MAFAO YA WASTAAFU
79. Mheshimiwa Spika, mafao ya wastaafu katika nchi hii yameendelea kuzua migogoro mbalimbali na manung’uniko katika jamii. Kuna makundi mengi yenye malalamiko, kuanzia Wanajeshi, waliokuwa wafanyakazi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na wastaafu waliokuwa watumishi wa Umma ambao wamebaguliwa na Sheria ya Mafao kwa Watumishi wa Umma, ya mwaka 1999 (The Public Service Retirement Benefits Act, Cap. 371, R.E. 2002).

80. Mheshimiwa Spika, Sheria hii, pamoja na kufuta Sheria ya Pensheni ya mwaka 1954 (The Pensions Ordinance of 1954, Cap. 371 of the Laws of Tanzania), bado ilibakiza matumizi ya Sheria hiyo kwa watumishi wa umma waliokuwa wakipokea mafao yao kwa Sheria na kanuni za Sheria iliyofutwa. Hali hii inajidhihirisha kwenye kifungu cha 73 na 84 cha Sheria ya mwaka 1999.

81. Mheshimiwa Spika,tarehe 24/02/2016 wawakilishi wa wafanyakazi wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki walimwandikia barua Mheshimiwa John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakimtaka aingilie kati dhuluma waliofanyiwa na Serikali ya CCM kwa kutokulipwa stahiki zao kikamilifu baada ya Jumuiya kuvunjika na kila nchi kupewa mgawo wake kwa malipo ya wafanyakazi wa Jumuiya wanaotoka katika nchi zao!

82. Mheshimiwa Spika,Kambi Rasmi ya Upinzani ni sauti ya wasio na sauti, ikiwa ni miaka 42 toka Jumuiya hiyo ivunjike inalileta tena suala hili mbele ya Bunge lako tukufu ili Serikali itoe ufafanuzi wa madai ya watanzania hawa wanaodai kwamba bado hawajalipwa kikamilifu stahiki zao zilizotokana na ajira zao kwa kuzingatia kumbukumbu,taratibu na Sheria za ajira zao ambazo zilihitimishwa kwa nguvu ya Mkataba wa East African Community Mediation Agreement 1984 ulioidhinishwa na kutiwa saini na Mamlaka (The Authority ) ambao ni marais wa Afrika Mashariki wakati huo. Pamoja na Mkataba huo kulitayarishwa pia Acturial Report ya 1986 iliyotoa ufafanuzi wa malipo hayo.

83. Mheshimiwa Spika,Viashiria vya wizi na dhuluma dhidi ya watanzania hawa vilianza mwaka 1987 pale Mkataba wa The East African Community Mediation Agreement 1984 (Ulioidhinishwa na kusainiwa na Marais wa nchi wanachama, akiwemo hayati Julius Kambarage Nyerere) ulipoletwa kwenye Bunge ili upate uthibitisho kama sheria rasmi ya nchi. Katika hali ya kushangaza Serikali ilinyofoa baadhi ya vipengele muhimu vya Mkataba mama (Ibara za 1,2,6,13,16,17 na 18) kabla ya kuupeleka Bungeni kwa uthibitisho. Tendo hili la Serikali lilikuwa ni kinyume kabisa na mwongozo wa Ibara ya 95 ya Mkataba wa Jumuiya ya Africa Mashariki (The Treaty for East African Co-operation) .

84. Mheshimiwa Spika, Kitendo hiki cha dhuluma kilichofanywa na Serikali ya CCM kilipunguza nguvu na thamani ya mafao ya watanzania hawa na hususani kifungu cha 1(n) ambacho kiliweka bayana kwa kutoa maagizo na mwongozo uliotakiwa kufuatwa katika ukokotoaji na ulipaji wa mafao. Hatua hii ya Serikali kwa kiwango kikubwa imekuwa ikiathiri wazee wetu hawa kwani Mahakama zetu zimekuwa zikitoa uamuzi wake kwa kutumia Mkataba wa ndani uliochakachuliwa !

85. Mheshimiwa Spika, Swala la wazee hawa (Watanzania zaidi ya 28,831) halitofautiani sana migogoro ya mirathi , hasa pale baba mkubwa anapoteuliwa kusimamia mirathi ya marehemu ndugu yake ambae aliacha mali na watoto wadogo.

86. Mheshimiwa Spika, Mwaka 2005 iliundwa Kamati ya muafaka baada ya Serikali kuomba suala limalizwe nje ya Mahakama. Kwa ridhaa ya Mahakama Kuu, Kamati husika iliundwa na watu 10 toka Serikali Kuu ikiongozwa na Bwana, Ramadhani Khija (ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Muafaka na baadae alikuwa Katibu Mkuu Hazina. Na watu 10 wakiwakilisha upande wa wastaafu wakiongozwa na Ndugu Alfred Kinyondo kama Mwenyekiti wa Wastaaafu.

87. Mheshimiwa Spika, Baada ya majadiliano ya miezi mitatu Muafaka ulifikiwa na kupelekwa kwa Waziri wa Fedha, wakati huo Bwana Basil Mramba. Makubaliano yakiwa Serikali itawalipa jumla ya shilingi billion 450 kwa wastaafu 28,831

88. Mheshimiwa Spika, Makubaliano haya yalithibitishwa na kauli ya aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Benjamin Mkapa katika kilele cha sherehe za wafanyakazi za Mei Mosi tarehe 1/05/2005 Songea, alitamka rasmi kwamba Serikali yake imeridhai kulipa Tshs. 419 bilioni ikiwa ni malipo ya wastaafu wa Jumuiya hiyo na mashirika yake japo kwa awamu na alimuagiza Waziri wa Fedha wakati huo ndugu Basil Mramba kutekeleza maamuzi hayo kwa haraka,

89. Mheshimiwa Spika, Katika hali ile ile ya dhuluma kama ilivyotokea katika uchakachuaji wa Mkataba kama nilivyoainisha hapo juu, Serikali hiyo hiyo iliyoingia makubaliano katika Kamati ya mwafaka, ikaandaa Deed of Settlement yenye kuonyesha kwamba kiasi cha shilingi bilioni 117 zitalipwa kwa wastaafu 31,831, kutoa shinikizo kwa wastaafu kupitia wakili wa ndugu Lukwaro wasaini. Mkataba ulisainiwa Kwa shinikizo (21/09/2005) Mahakama ikatoa hukumu siku hiyo hiyo! Siku ya pili 22/09/2005 Serikali ikachapisha majina ya wastaafu 28,831 na kuagiza wakachukue malipo yao kuanzia tarehe hiyo hiyo 22/09/2005!!

90. Mheshimiwa Spika, Swali la kujiuliza hapa ni kwa miujiza gani Serikali iliweza kukokotoa ndani ya siku moja stahiki za watumishi wote 28,831 ambao wako kada tofauti na waliohudumu kwa muda , mishahara na vyeo tofauti ndani ya nusu siku/siku moja?

91. Serikali ikijua kwamba inafanya hila ilifanya siri sana katika ‘kukokotoa mahesabu’ bila hata kuwashirikisha wawakilishi wa wastaafu, ni pale tu Mstaafu alipofika kuchukua hundi yake na kuona payment voucher, ndipo alipoweza tambua kuwa alicholipwa hakiendani na stahihi yake!

92. Mheshimiwa Spika, Dhuluma kama hii hatuwezi kuacha iendelee kutafuna Taifa letu kudhulumu wazee waliolitumikia Taifa na Jumuiya ni laana kubwa, laana ambayo haturuhusiwi kuiacha kama Taifa! Hivi kwa nini hatujiulizi kwa nini hawa wazee wetu kwa miaka yote wamekuwa wakisisitiza kwamba wamedhulumiwa?? Kwa nini nafsi yao hairudi nyuma licha ya vitisho mbalimbali wanavyokabiliana navyo?? Kwa nini ni wastaafu hawa tu kati ya wengi ambao hawachoki kuililia Serikali yao (baba yao Mlezi) iwape urithi halali walioachiwa na baba yao (Jumuiya) wakati anafariki??

93. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani imelazimika kurejea upya maelezo hayo ambayo tayari ilikwishayawasilishwa ndani ya Bunge hili, kutokana na ukweli kuwa Ofisi ya Msajili wa Hazina katika Mpango Mkakati wake kwa mwaka wa fedha 2019/20 inataka kufanya uhakiki wa wastaafu wa Ex TRC na TTCL ili waweze kulipwa mafao yao.

94. Mheshimiwa Spika, kwa nyaraka na vielezo na hadi hatua za majadiliano zilizokuwa tayari zimefikiwa wakati huo baina ya Serikali na wawakilishi wa wastaafu hao, kuanza upya uhakiki si ni kupoteza muda ili hata wazee waliokuwa bado hadi wapoteze uhai wao kutokana na ugumu wa maisha?

L. HITIMISHO
95. Mheshimiwa Spika, napenda kumalizia hotuba yangu kwa kusema kwamba; mdororo wa uchumi wetu kama taifa, hali ya maisha kwa wananchi kuendelea kuwa ngumu; kuongezeka kwa umaskini na madhila mengine yanayotokana na kupungua kwa ukwasi, yanatokana pasi na shaka yoyote, na udhaifu mkubwa wa Wizara ya Fedha wa kupanga mipango; kutunga na kusimamia sera na sheria za fedha.

96. Mheshimiwa Spika, nasema hivyo kwa kuwa wizara ya fedha ndio inayoandaa mpango wa maendeleo wa taifa na ndiyo inakusanya na kugawa fedha kwa ajili ya kuutekeleza mpango huo. Kushindwa kukusanya fedha za kutekeleza mpango iliyouandaa yenyewe ni dalili ya ‘over-ambition’ya kutaka kufanya mambo makubwa wakati uwezo haupo. Hali ya namna hiyo ni hatari kwa kuwa inapoteza imani ya wananchi kwa Serikali.

97. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inamtaka Waziri wa Fedha na Mipango aache kumdanganya Rais kuwa kuwa makusanyo ya mapato ni makubwa kwa kuwa Taarifa ya CAG imeonyesha ukweli wote jinsi ambavyo TRA imeshindwa kukusanya mapato kufikia malengo iliyojiwekea.

98. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inatoa agalizo kali kuhusu deni la taifa; deni kwa sasa linakaribia nusu ya Pato la Taifa. Kwa hiyo, Serikali iwe makini; isije ikakopa kupita kiasi na kukiacha kizazi kijacho kikiwa hakina rasilimali yoyote isipokuwa mzigo wa madeni.

99. Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa keki ya taifa ni yetu sote. Kila wizara inatakiwa ipate haki yake ili iweze kutimiza majukumu yake kwa ufanisi. Wizara ya Fedha iache kujipendelea katika mgawo wa fedha. Izingatie ukomo wa bajeti uliowekwa.

100. Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuwasilisha.

David Ernest Silinde (Mb)
KNY. WAZIRI KIVULI NA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI, KATIKA WIZARA YA
FEDHA NA MIPANGO
3 Juni, 2019
 
Mdee mwenyewe alishanunuliwa Kwa hivyo hivyo vipande vya fedha! Vilivyoongezeka kwenye bajeti!
Wanafiki wote, wachumia tumbo! Mikononi na midomoni wananuka pilau nyama, huku wakiongea na sisi wanajidai kulia njaa pamoja nasi!

Samiah Rais wangu. Nitakuita mtukufu endapo utafyekelea mbali mihela ya wabunge, walipwe kama walimu!
 
Nature imetenda haki.

Hii ni hotuba ya Kambi ya Upinzani bungeni
HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KATIKA WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO, MHESHIMIWA HALIMA JAMES MDEE (MB),

2. Mheshimiwa Spika,ni bahati mbaya sana kwamba huu ni mwaka wa tatu mfululizo, nawasilisha maoni ya Kambi ya Upinzani Waziri wangu Kivuli akiwa hayupo Bungeni kutokana na kuzuiliwa kuhudhuria vikao vya Bunge. Jambo hili linaonekana kufanywa kimkakati ili kupunguza nguvu ya upinzani Bungeni katika kuisimamia na kuiwajibisha Serikali
100. Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuwasilisha.

David Ernest Silinde (Mb)
KNY. WAZIRI KIVULI NA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI, KATIKA WIZARA YA
FEDHA NA MIPANGO
3 Juni, 2019

Mkuu @bujibuji Simba Nyamaume, kwanza asante kutukumbusha hii. Maadam shujaa huyu aliyezuiliwaga Bunge lile bado yupo na bahati nzuri sana, Bunge hili hajazuiliwa, mbona sasa hatuzioni tena cheche zake hizi?!.

Kuhusu hao kutokuwepo, huu ni mwaka wa mabadiliko...

P
 
Somo hapa upinzani bungeni Ni muhimu Kama hewa kwa kiumbe hai, Leo wapo peke yao wanapingana wao kwa wao mpaka wanamtimua ndugai, ninachoamini upinzani wa maana ungekuwepo bungeni Ndungai angekuwa spika maana alilolisema lingesemwa na Heche.

Hata nyumbani mkiwa hata wawili tu na mkeo lazima mkeo awe mpinzani hii Ni nature.
 
Back
Top Bottom