BAK
JF-Expert Member
- Feb 11, 2007
- 124,769
- 288,284
Dk. Mwakyembe: Nitapambana na Rostam
• Amtaka asiwe bubu kujadili hoja anapokuwa bungeni
na Moses Ng'wati na Richard Kilumbo, Mbeya
Tanzania Daima~Sauti ya Watu
MBUNGE wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe (CCM), amesema atapambana kwa hoja na Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz nje na ndani ya Bunge hadi kieleweke.• Amtaka asiwe bubu kujadili hoja anapokuwa bungeni
na Moses Ng'wati na Richard Kilumbo, Mbeya
Tanzania Daima~Sauti ya Watu
Dk. Mwakyembe, alitoa kauli hiyo jana katika mkutano mkubwa wa hadhara, ulioandaliwa na wananchi na kufanyika katika viwanja vya Siasa mjini hapa, kwa lengo la kulaani kauli zinazotolewa dhidi yake kupitia vyombo vya habari vinavyomilikiwa na Rostam.
Alisema mbinu anayoitumia sasa Rostam pia wa CCM, ya kumchafua kupitia vyombo vyake vya habari, inatokana na ububu alionao anapokuwa bungeni. Dk. Mwakyembe alisema licha ya Rostam kuamua kuanzisha Bunge lake kupitia vyombo vya habari anavyovimiliki, hawezi kukaa kimpya, huku akiona watu wachache wakitumia uwezo wao kifedha alizodai wamezipata kwa njia ya ufisadi wakitaka kuiendesha nchi kama wanavyotaka.
Aliendelea kusema kuwa Watanzania wanatambua wazi kuwa fedha katika akaunti ya madeni ya nje (EPA), zaidi ya sh bilioni 40, zilichotwa na Kampuni ya Kagoda, aliyodai inamilikiwa na Rostam kwa maslahi na faida ya watu wachache.
Mbunge huyo machachari, alisema hawezi kuvunjika moyo kutokana na mbinu chafu zinazofanywa na kundi la watu wachache aliodai kuwa ni mafisadi, za kutaka kuvuruga kazi nzuri ya Kamati Teule ya Bunge aliyoiongoza kuchunguza mkataba wa zabuni ya Kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond, iliyosababisha aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, kujiuzulu.
Mawaziri wengine waliojiuzulu kutokana na kashfa hiyo ni pamoja na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi na Dk. Ibrahim Msabaha ambaye alikuwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Kama alivyotoa ufafanuzi katika mkutano wake na vyombo vya habari wiki mbili zilizopita, Dk. Mwakyembe alisema hakuna suala la ugongano wa maslahi kwa kutotangaza maslahi aliyonayo kwenye Kampuni ya kuzalisha umeme wa upepo ya Power Pool East Africa Ltd.
"Shutuma zinazotolewa na Rostam Aziz kupitia vyombo vyake vya habari zinashangaza, maana hakuna mgongano wa maslahi na sijavunja kanuni za Bunge, kwani kampuni inayosemwa kwamba nina hisa nayo ni ya wazalendo wa Kitanzania wapatao 50 wa ndani na nje ya nchi, hapa hakuna mgongano wa maslahi na kama kuna wanaobisha, warejeshe hoja hiyo bungeni ili tufumue yaliyojificha," alisema Dk. Mwakyembe.
Alisema malumbano yanayotokea sasa ni matokeo ya baadhi ya watu waliotemwa bungeni baada ya ripoti ya kamati yake, ambao hawakuridhika na kazi hiyo, hivyo kujaribu kulipiza kisasi kupitia vyombo vyao vya habari.
"Unajua wakati tunawasilisha ripoti yetu, kuna mambo hatukuyasema kwa sababu kuna watu walioamua kusema basi yaishe, wakaachia ngazi, hivyo hatukutoa mambo yote, sasa kama wanaona hawakutendewa haki, turudi bungeni tukatoe yale tuliyoamua kuyaacha," alisema Dk. Mwakyembe.
Mkutano huo uliohudhuriwa na maelfu ya wananchi wa Kyela, wakiwamo viongozi wa vyama vya upinzani, ulitawaliwa na mabango ya kumlaumu Rostam na watu waliodai kuwa ni mafisadi, huku wakiapa kufa na mbunge wao (Dk. Mwakyembe) waliodai kuwa anaonewa na mafisadi.
Baadhi ya mabango ambayo yalibebwa na baadhi ya wanachama wa upinzani, yalimtaka Mbunge huo kujitoa CCM na kujiunga na vyama vingine vya upinzani ili kuungana na wabunge wa kambi hiyo katika kukabiliana na vita dhidi ya ufisadi.
Awali, mkutano huo ulipangwa kuanza kwa maandamano, lakini yalikataliwa na polisi kwa sababu za kiusalama.
Hii ni mara ya pili kumshutumu hadharani Rostam kwamba anatumia vyombo vyake vya habari kupotosha umma na kumchafua kisiasa.
Hatua ya Mwakyembe kujibu tuhuma hizo, inakuja baada ya magazeti mawili ya kila siku (Si Tanzania Daima) kuchapisha habari zinazomhusisha yeye na umiliki wa hisa 1,000,000 zenye thamani ya sh bilioni 1.5 katika Kampuni ya Power Pool East Africa Ltd.
Mbali ya habari hizo kuandikwa katika magazeti hayo mawili, moja la binafsi na jingine la serikali, nyaraka kadhaa zinazomhusisha Mwakyembe na kampuni hiyo, zimesambazwa katika mtandao wa intaneti.
Mbali ya Mwakyembe, taarifa hizo zinamtaja Mbunge wa Lupa, Victor Mwambalaswa ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya TANESCO, kuwa miongoni mwa wanahisa wa kampuni hiyo binafsi ambayo wakati fulani Dk. Mwakyembe alipata kuwa mtendaji mkuu wake.
Taarifa hizo zinajaribu kujenga hoja zinazojaribu kumuondolea Mwakyembe uhalali wa kuendelea kudai kupambana na ufisadi ndani na nje ya Bunge, ilhali yeye mwenyewe akionekana kuwa na ukwasi mkubwa unaotiliwa shaka.
Taarifa hizo zinaonyesha kuwa, Mwakyembe licha ya kuwa na hisa nyingi katika kampuni hiyo, ameisaidia katika mambo mbalimbali ambayo hata hivyo hayakufafanuliwa, wakati akiwa katika wadhifa wa mtendaji mkuu.
Taarifa ambazo Tanzania Daima imezikusanya kutoka miongoni mwa wabunge kadhaa zinaonyesha kwamba, lengo kuu la kusambaza nyaraka hizo ni kujaribu kumnyoshea kidole Mwakyembe na kumuondolea uhalali wa kuendelea kupigania sekta ya nishati ilhali yeye mwenyewe akijua kuwa na maslahi.