Kutoka Bungeni: 2006 - 2010

Kutoka Bungeni: 2006 - 2010

Kesho siku ya jumatatu ni siku waziri mkuu atatoa hotuba yake ya ofisi ya Waziri mkuuu.

Kutokana na utamaduni wa kambi ,msemaji wa upinzani ni Dr.Slaa, sasa kesho anategemewa kuja na jmbo gani?

Kwani itakumbukwa kuwa mwaka jana 2007/2008 ndipo issue za BOT ziliweza kuibuliwa kutokana na hotuba yake.

Nafuatilia kwa karibu kama nikiipata hotuba mapema leo nitaiweka hapa japo nimeweza kuiona draft ya kwanza.

Ashauriwe kuweka kitu gani ili kuboresha hotuba?

Wewe, huwezi kuiweka hotuba ya watu kabla haijasomwa! Utasababisha upuuzi kama ule wa hotuba ya bajeti ya serikali kupatikana hapa 24 hours before. Please be serious and respect proffessionalism. Hotuba inasomwa tarehe 23 Juni, leo tarehe 22 watu wanaweza tu kutoa mapendekezo yao nini kiwepo. Period. Na si kuweka hotuba hapa. JF sio draftpersons wa kambi ya upinzani au whoever! Sasa tukishaiona hapa leo, kesho itakuwa story tena?

PM
 
Wewe, huwezi kuiweka hotuba ya watu kabla haijasomwa! Utasababisha upuuzi kama ule wa hotuba ya bajeti ya serikali kupatikana hapa 24 hours before. Please be serious and respect proffessionalism. Hotuba inasomwa tarehe 23 Juni, leo tarehe 22 watu wanaweza tu kutoa mapendekezo yao nini kiwepo. Period. Na si kuweka hotuba hapa. JF sio draftpersons wa kambi ya upinzani au whoever! Sasa tukishaiona hapa leo, kesho itakuwa story tena?

PM

Nimesema nafuatilia kwa karibu na kama nitaipata in time leo, wewe huelewi ama umekurupuka tuu?

Wewe unataka kupata story tuu ama ?nimesema wale wenye mapenzi mema wapendekeze nini kiwekwe kwenye bajeti ya mwaka huu sasa uinalalama kuwa JF sio draft persons wa upinzani ...kumbe kinakuuma sana eeh.....

Hapa wapo watanzania wenye nia njema na nchi yao ndio maana wanatakiwa kusema kupitia msemaji wao ambaye anajali masilahi ya taifa.
 
Jamani tujaribu kuepuka kususa WAARABU tutawatukana wake wa viongozi wetu na watoto wao ndio waongozaji wa taifa la kesho sasa tizameni viongozi wote wa juu Zanzibar haridhiki mpaka waoe Waarabu ndio aone kaoa tukiazia shekh Ali Hassa na akina Karume na wengi tuu na watoto wao ndio tayarisho la taifa.
 
Alaa kumbe zenji ni nchi ya waarabu? na Sheik Karume je? kumbe naye mwarabu au aliteka kwa nguvu nchi ya wenyewe ndiyo sababu vifo kila leo?
Jamani tujaribu kuepuka kususa WAARABU tutawatukana wake wa viongozi wetu na watoto wao ndio waongozaji wa taifa la kesho sasa tizameni viongozi wote wa juu Zanzibar haridhiki mpaka waoe Waarabu ndio aone kaoa tukiazia shekh Ali Hassa na akina Karume na wengi tuu na watoto wao ndio tayarisho la taifa.
Hpa nakubaliana na wewe!
 
Jamani tujaribu kuepuka kususa WAARABU tutawatukana wake wa viongozi wetu na watoto wao ndio waongozaji wa taifa la kesho sasa tizameni viongozi wote wa juu Zanzibar haridhiki mpaka waoe Waarabu ndio aone kaoa tukiazia shekh Ali Hassa na akina Karume na wengi tuu na watoto wao ndio tayarisho la taifa.
Hakuna hata kiongozi mmoja wa juu aliekuwa na mke muarabu hivi kuwa mweupe ndio kuwa muarabu waliopo wote ni Wazanzibar ila mazezeta wa CCM ndio wanaoleta na kuzungumza mambo wasiyo yajua ,unajua viongozi wengi wa Serikali ya Zanzibar ni watu wa shamba shamba na kama hamuamini hata elimu yao ni ndogo sana sana ,jaribuni kutafuta profile zao muone na sidhani kama mtazipata maana hakuna na wala hawajui kitu profile ni nini.
 
Wakuu ni ndefu kidogo, lakini sima mamlaka ya kuifupisha



HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI DR.WILLIBROD PETER SLAA (MB) KUHUSU MAKADIRIO YA MATUMIZI YA FEDHA YA OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA KWA
MWAKA WA FEDHA 2008/2009:

UTANGULIZI:
1: Mheshimiwa Spika,
Napenda kuchukua nafasi hii, kwa niaba ya Kambi ya Upinzani kuwasilisha Maoni ya Kambi ya Upinzani kuhusu Hotuba ya Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Matumizi ya Fedha, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha, 2008/2009 kwa mujibu wa Kanuni za Bunge Kifungu cha 96(6) Toleo la Mwaka 2007.

2: Mheshimiwa Spika,

Kwa namna ya pekee namshukuru Mwenyezi Mungu kunifikisha Kwenye Haki na Ukweli, baada ya kuishinda tena CCM kwenye Kesi ya Uchaguzi namba 20/2005 ambapo Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ilinitangaza kama Mbunge halali wa Karatu na kutupilia mbali malalamiko yaliyowasilishwa na waliojiita wakereketwa wa CCM. Nawashukuru sana wananchi wa Karatu ambao waliendelea kuniunga mkono wakati wote wa kesi hiyo ya Uchaguzi. Nawapa pole kwa usumbufu wote waliopata kipindi chote cha kesi. Nachukua fursa hii kuwahakikishia kuwa nitawatumika kwa akili, moyo na uwezo wangu wote katika kufanya yale yote tuliyocheleweshewa kwa kipindi chote cha kesi. Nachukua fursa hii pia kuwashukuru Watanzania wote kutoka kona zote za Tanzania wenye mapenzi mema ambao kwa maelfu waliniletea salamu za pongezi baada ya Mahakama Kuu kutangaza ushindi huo tarehe 15 May, 2005. Asanteni sana Salamu zenu zilinifariji sana. Mwenyezi Mungu awarudishie mara mia kwa upendo wenu.

3: Mheshimiwa Spika,
Nitakuwa nimekosa fadhila iwapo sitatoa shukrani kwa Chama changu CHADEMA , vyama vya CUF, TLP, NCCR-Mageuzi , pamoja na Waheshimiwa Wabunge wenzangu wa Kambi ya Upinzani wakiongozwa na Mhe. Hamad Rashid Mohamed, (Mb) Mbunge wa Wawi na Kiongozi wa Upinzani Bungeni, na wengi wa Wabunge wenzangu wa Chama Tawala ambao wote kwa ujumla wao wakati wote wa Kesi walikuwa wakinitakia heri na ushindi. Ni kweli haki inaweza kucheleweshwa tu, lakini haiwezi kamwe kupotea na wala Ukweli hauwezi kufunikwa kwa mbinu na hila. Ninamshukuru sana Wakili wangu Tundu Lissu kwa kufanya kazi yake kwa umakini mkubwa.

Mhe. Spika, kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu, tumepata ushahidi wa dhahiri kwani kila tulipokuwa tukisema kuwa baadhi ya watu wa CCM huwa wanaiba kura watu wengi walikuwa hawaamini na wengine hutuzomea. Kwa uamuzi wa Mahakama Kuu katika kesi na 20/2005 hasa kwa wakereketwa husika kuingiza nyaraka za “kugushi”, na za “udanganyifu” Mahakamani ushahidi wa wazi umepatikana na mbinu moja ya wazi ya wizi wa kura nayo imebainika hadharani. Ninawashukuru sana wahusika wakereketwa waliotufungua macho kwa njia ya kesi hiyo kwani itatusaidia sana katika kupanga mikakati bora zaidi katika kuthibiti wizi wa kura katika chaguzi zijazo. Ni kweli kesi si jambo jema, lakini ‘hakuna baya lisilo na jema’, kwani bila kesi hiyo tusingeliweza kufahamu siri kubwa inayotumika katika kuiba kura.

4: Mheshimiwa Spika,
Napenda kumpongeza kwa dhati kabisa Mhe. Mizengo K.P.Pinda (Mb) Waziri Mkuu kwa kuteuliwa na Rais kuwa Waziri Mkuu na hatimaye kuthibitishwa na Bunge lako Tukufu. Ninampongeza pia Mhe. Celina O.Kombani (Mb) kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa pia Mhe.Aggrey Mwandri kwa uteuzi huo, lakini pia kwa kuandaa Bajeti yao hii ya kwanza, wakisaidiana na Makatibu wao Wakuu na Wataalam wao wote.

5: Mheshimiwa Spika,
Nitakuwa mtovu wa shukrani iwapo sitakushukuru wewe binafsi, Naibu Spika na Wenyeviti wa Bunge kwa kazi nzuri mnayofanya ya kuliongoza Bunge letu Tukufu. Ninamwomba Mwenyezi Mungu awajalie hekima na busara na kuwapatia nguvu na afya mnazohitaji katika kuliendesha vizuri Bunge letu hasa katika kipindi hiki kigumu katika historia ya nchi na Bunge letu.

6: Mheshimiwa Spika,
Hii ni bajeti ya Tatu tangu Serikali ya Awamu ya Nne iliposhika uongozi wa nchi yetu. Kambi ya Upinzani inatoa maoni yake kwa kufanya tathmini ya Malengo na Mwelekeo wa kazi za Serikali katika vipindi mbalimbali vya nyuma ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa malengo ya Serikali ya Awamu ya Nne kwa kipindi cha tangu waliposhika madaraka.

7: Mheshimiwa Spika,
Kwa vile Waziri Mkuu ni msimamizi wa Shughuli za Serikali Bungeni, na mjadala wa Waziri Mkuu unaihusu serikali yote, tunapenda Mheshimiwa Waziri Mkuu atoe majibu ya kuridhisha katika maeno yote ambayo Waziri wa Fedha hakutoa majibu ya Kuridhisha, hasa kwa vile Waziri Mkuu ndiye mwenye kauli kuhusu shughuli za Serikali Bungeni. Mheshimiwa Spika, kwa vile kupanga bajeti ni hatua moja muhimu, lakini usimamizi wa fedha hizo ni muhimu zaidi, Mchango wa Kambi ya Upinzani safari hii utajikita zaidi kwenye maeneo mengi yenye utata ili Bunge na Wananchi kwa ujumla wapate majibu ya kuridhisha.

Aidha, Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu sasa Taifa letu, ndani ya Bunge hili Tukufu, kwenye mikutano ya hadhara na kwenye vyombo vya Habari limegubikwa na Taarifa za kusikitisha kuhusu Tuhuma za uvunjifu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma namba 13 ya mwaka 1995, zinazomhusisha Mhe. Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Mhe. Benjamin William Mkapa kuhusiana au kupitia makampuni anayomiliki ya Tanpower Resources Ltd na ANBEM. Tuhuma hizo pia zimemhusisha aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini wa kipindi hicho hicho. Kambi ya Upinzani inaona si vema kujadili maswala ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, bila kupata ufafanuzi wa kina wa maswala haya muhimu kwani imani ya Watanzania wengi imeguswa na Tuhuma hizi na hivyo kuwa na mashaka na fedha nyingi zinazoidhinishwa na Bunge kama kweli zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.



Kwa niaba ya Kambi ya Upinzani na wananchi wote wanaopenda kujua ukweli, Mchango wetu unajikita katika maeneo yafuatayo:

7:1 UBADHIRIFU/RUSHWA NA UFISADI.
Mheshimiwa Spika,
Bajeti inatumika na Serikali kupanga matumizi ya fedha kidogo zilizopo katika maeneo na Sekta muhimu zinazohitaji kipaumbele katika kuleta maendeleo kwa Taifa na Wananchi wote kwa ujumla. Hivyo ni kweli kuwa Bajeti ni silaha na chombo muhimu sana katika kutoa dira ya utendaji kazi katika Taifa. Hata hivyo, Kambi ya Upinzani, ina maoni kuwa kupanga ni kitu kimoja na kutumia kilichoidhinishwa na Bunge ni kitu kingine. Tatizo kubwa zaidi ni katika nidhamu ya Matumizi na Uadilifu wa kutumia kilichoidhinishwa na Bunge kwa malengo yaliyopitishwa katika Bajeti. Ni kwa msingi huu, haiwezekani kutenganisha masuala ya Bajeti na masuala ya udhibiti wa matumizi, nidhamu ya matumizi na uadilifu wa wanaopewa majukumu ya kusimamia utekelezaji wa Bajeti husika .

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Katiba yetu, Ibara ya 63(2) Bunge ndiyo “chombo kikuu” katika Jamhuri ya Muungano na majukumu yake ya kikatiba, tukiacha ya kutunga Sheria ni “kuisimamia na kuishauri” Serikali. Kambi ya Upinzani ina maoni kuwa kwa vile viko vyombo vingi na watu wenye sifa mbalimbali wanaofanya kazi ya “kuishauri Serikali, Bunge ni chombo pekee cha “kuisimamia”. Hivyo ni lazima Bunge nalo lifanye kazi hii kwa uadilifu mkubwa Mhe. Spika, Bunge lisipotimiza vizuri wajibu wake huu, na mambo yakaharibika katika nchi, Bunge halitakuwa na maelezo yeyote kwani hakuna chombo kingine chochote kwa mujibu wa Katiba yetu chenye uwezo wa “kuisimamia Serikali”. Tunaposema Serikali ni pamoja na kusimamia Matendo na Maamuzi ya Rais, jambo ambalo watu wengi hawalielewi kwa kudhani kuwa Rais yuko juu ya Sheria ya Nchi. Kambi ya Upinzani imependa kuweka hili wazi kutokana na mawazo mbalimbali yanayojitokeza mara kwa mara katika mijadala mbalimbali kama yalivyoripotiwa na vyombo mbalimbali vya Habari. Huu ni msingi mkubwa katika nchi ya kidemokrasia na hasa inayofuata mfumo wa ‘mgawanyo wa Madaraka’ yaani Separation of Powers. Bunge basi linajukumu pekee la kuisimamia Serikali na vyombo vyake vyote bila kuingilia utendaji wao.

Mhe. Spika, jukumu la kusimamia ni pamoja na kupata Taarifa zote zinazohitajika kutekeleza jukumu la Usimamizi, kufanya maamuzi na kusimamia maamuzi hayo muhimu pale inapohitajika kama chombo cha Usimamizi.

7.1.1 UBADHIRIFU KUPITIA EPA NA RICHMOND:

Mheshimiwa Spika,
Mwaka uliopita, wakati nawasilisha Hoja ya Kambi ya Upinzani kuhusu Ofisi ya Waziri Mkuu nilitoa hoja mbalimbali kuhusu Ubadhirifu mkubwa ndani ya Benki Kuu ya Tanzania, (BOT) kama ilivyonukuliwa na Kumbukumbu za Bunge “Hansard” ya Kikao cha Tisa, Tarehe 25 June, 2007. Pamoja na kwamba hoja hiyo ilipingwa sana na baadhi ya Wabunge wenzangu. Nashukuru kuwa sasa suala la Ubadhirifu katika vyombo vyetu mbalimbali na ndani ya Serikali siyo tena suala la mjadala kwani mengi zaidi yamejitokeza. Jamii nayo sasa imezoea neno Ufisadi, na Ufisadi unajadiliwa kwa uwazi bila woga tofauti na ilivyokuwa hapo awali.
Vyombo vya Habari navyo vimefanya kazi nzuri sana kufanya uchunguzi wa kina na kuwapa habari Watanzania kuhusu hali ya ufisadi katika nchi yetu. Kambi ya Upinzani inavipongeza sana vyombo vyote vya habari kwa kazi nzuri waliyoifanya na waendelee na moyo huo huo wa kuwaelimisha Watanzania.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani imefarijika sana kwamba sasa pazia kubwa lililofunika masuala ya Ubadhirifu limeondoka na masuala haya yanajadiliwa siyo tu ndani ya Bunge lako Tukufu bali na Watanzania ambao kimsingi ndiyo wadau wakubwa na wamiliki wa mali na Rasilimali za Taifa hili.

Mheshimiwa Spika, mjadala wa ubadhirifu na Ufisadi ndani ya BOT kuhusu Kasma ya EPA ulishafika ndani ya Bunge kama chombo cha Usimamizi. Bunge kama wawakilishi wa Wananchi wamestushwa na kiwango kikubwa cha Ubadhirifu huu, tena wakati wananchi wanajifunga mikanda, wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha kutokana na gharama ya maisha ambayo imepanda sana. Maelezo kuwa gharama ya maisha imepanda kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wetu hazikubaliki kwa sababu haiwezekani hali hiyo iwe kwa wananchi wa kawaida tu, wakati kundi dogo la watu, kama ilivyoainishwa kwenye Ufisadi wa EPA linaneemeka na limeachiwa tu.

Mheshimiwa Spika,
Wananchi wengi wa Tanzania wameacha kunywa chai kwa vile Sukari sasa imekuwa bidhaa ya anasa, mikate iliyokuwa kimbilio la walala hoi hasa mijini imekuwa haishikiki tena kwa vile bei ya mkate unakimbilia shs 1,000. Nyama inazidi kuwa hadithi ya kusadikika kwa Watanzania wengi kwani bei ya kilo inakimbilia zaidi ya shs 2,500 kwa kilo katika maeneo mengi. Mchele ambao ukiacha mahindi unakuwa chakula cha Watanzania wengi unakimbilia Tshs 1,500/ kwa kilo. Mhe. Spika, lazima Bunge kama mwakilishi wa Wananchi lichukue nafasi yake kusimamia maslahi ya Watanzania na kulinda haki zao.

Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 8, na ninanukuu;
“8(1)(a) Wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na Serikali
Itapata madaraka yake yote kutoka kwa wananchi …”
“8(1)(b) lengo kuu la Serikali kwa Wananchi ni ustawi wa wananchi..
“8(1)c) Serikali itawajibika kwa Wananchi….”
“8(1)(d)Wananchi watashiriki katika shughuli za
Serikali yao kwa masharti ya Katiba…..
Mheshimiwa Spika, hali ilivyo haielekei kabisa kama Serikali inawajibika kwa Wananchi. Wananchi wamebaki kuwa watazamaji katika shughuli za Serikali tofauti na matakwa ya Katiba kwani kama Bunge hili ambalo linawawakilisha Wananchi linashindwa kushirikishwa hata kwa mambo ya msingi ni kwa namna gani Serikali itajitetea kuwa Wananchi wanashirikishwa? Maoni haya yanatokana na mambo yafuatayo:-
 Hadi sasa, Takriban miezi sita, tangu Taarifa ya Ukaguzi wa EPA kuwasilishwa kwa Mheshimiwa Rais, Taarifa hiyo imebaki kuwa Siri. Usiri huu ndio unaosababisha minong’ono mingi na mashaka kuwa Serikali haiko makini na vita dhidi ya Ufisadi. Ufisadi uliohojiwa ndani ya Bunge na ilikuwa muhimu kwa Serikali kutoa Taarifa ya kina kwa Bunge na kwa umma wa Watanzania.
 Kambi ya Upinzani imestushwa sana na Taarifa ya Mhe. Mkullo Waziri wa Fedha alizotoa Bungeni ijumaa wakati anahitimisha hoja yake kuwa “Fedha za EPA si za Serikali bali za wafanyibiashara walizolipa kwa ajili ya kununua bidhaa nje” Mhe. Spika kutokana na Taarifa hiyo ambayo dhahiri ni ya kupotosha, Kambi ya Upinzani imefanya utafiti wa kina na kugundua kuwa Fedha hizo kimsingi zinatokana na programu inayoitwa “Debt Buy Back Program”. EPA imefanyiwa kazi sana na Timu ya Lazard na baadaye ukaguzi wa PricewaterhouseCoopers (France) tarehe 25 November, 2004. Hata hivyo ukaguzi uliofanywa na Deloitte and Touche 2006 na baadaye kuthibitishwa na Ernst and Young, 2007 ulithibitisha kuwa Kampuni 22 zilifanya biashara na Makampuni yanayodhaniwa “hewa”. Hivyo wafanyibiashara hao, wala “principles “ wao nchi za nje hawakuweka fedha zozote BOT kwa lengo kutumiza masharti ya Debt Buy Back Program kama alivyotaka kueleza Waziri wa Fedha. Kwa msingi huo fedha zilizoibiwa ni za Serikali ya Tanzania.
 Kwa Taarifa tuliyonayo, Ripoti ya Ukaguzi wa EPA katika kifungu cha 3.20, 3.23, na 3.24, kinatamka wazi uwepo wa “fraudulent supporting documents submitted in to support claims” Yaani ufisadi uliotumika ni pamoja na kutumia hati za kugushi katika kutoa fedha kutoka BOT; malipo ya viwango visivyo sahihi au kutumia viwango visivyo sahihi vya kubadilisha fedha ( yaani incorrect amounts and incorrect exchange rate). Ukaguzi ulionyesha kuwa kati ya Tshs 133 Billioni malipo ya zaidi ya 90.3 Billioni yalifanyika kwa kutumia Hati za kugushi (invalid and fraudulent supporting documents), nyaraka hizi zimeonyeshwa katika kiambatanisho C ikionyesha na majina ya Makampuni husika.
 Katika kifungu cha 3.25 Ukaguzi huo ulishauri kuwa kwa malipo ya zaidi ya 42.6 Billioni uchunguzi wa kina unahitaji kufanyika. Taarifa hii haikutolewa wazi kwa Bunge wala kwa Watanzania ambao ndio wenye mali hiyo na Serikali ni mdhamini kwa niaba yao tu.
 Ufisadi unaotisha zaidi ni ule uliofanyika kupitia Kampuni ya Kagoda Agriculture Ltd iliyosajiliwa nchini chini ya Sheria ya Makampuni Sura ya 212 tarehe 29 September, 2005 na kupata Hati na 54040. Wakurugenzi waliosajiliwa wa Kagoda ni watu wawili wenye anuani za Kipawa Industrial area, Plot no 87 Temeke Dar-Es-Salaam, na P.O.Box 80154 Dar-Es-Salaam, kinyume na utaratibu wa usajili Brella ambao unahitaji wakurugenzi wa Makampuni kujisajili kwa kuonyesha anuani ya mahali anapoishi na siyo Sanduku la Posta. Isitoshe, kwenye Fomu za usajili, ambapo John Kyomuhendo amejionyesha kuwa “Promoter” hawakuonyesha kama ni wakurugenzi mahali pengine kwenye kampuni nyingine yeyote. Cha kushangaza ni kuwa Kampuni hiyo ambayo wakurugenzi wake dhahiri wanaonekana wapya kabisa katika uwanja wa biashara ndani ya wiki 8 walikuwa wamekwisha kuchotewa zaidi ya Dolla za Marekani 30.8 Millioni yaani karibu zaidi ya shs Billioni 40 kwa kinachoelezwa na ukaguzi wa EPA kuwa hati bandia ambazo dalili za wazi ni kuwa Hati hizo karibu zote zimesainiwa na watu wasiohusika na Makampuni zinazodhaniwa zimefanya biashara na Kampuni ya Kagoda (Kif.cha 3.27); baadhi ya Makampuni yaliyodhaniwa kufanya Biashara na Kagoda au hayako kabisa au yamekwisha kubadilisha majina yao (Kif.3.27), Makampuni hayo ambayo yako Marekani, Japan, Ujerumani, Italia, Ufaransa mengine hata anuani zake hazikujulikana kabisa. Katika hali hii inayoonyesha wazi kuwa kulikuwa na kugushi. Mhe. Waziri Mkullo alipokuwa akijibu alitetea kuwa fedha za EPA si za za Serikali. Kinachotisha zaidi, Mhe. Spika, hata Kampuni ya Ukaguzi ya Deloitte kwa Barua yao kwa Gavana wa Benki Kuu ya tarehe 6 September 2006 na kwa Wakurugenzi wote wa BOT ya tarehe 10 October, 2006 walipomjulisha Gavana, pamoja na wajumbe wote wa Bodi, kati yao akiwemo Katibu Mkuu wa Hazina Bwana Gray Mgonja, kuwa kuna utata kuhusu Kampuni ya Kagoda, ambayo japo ilisajiliwa 29 September,2005 tarehe 10 September 2005 ilikuwa tayari na Mkataba wa kiasi cha fedha za Japan (Japan Yen)JPY 956,110.986 na Kampuni ya Nishizawa Ltd na Mkataba mwingine wa Dola za Marekani 9,057,463.90 wa Tarehe 12 September, 2005 na Kampuni ya Textima Ltd na mikataba hii yote inatamka kuwa “Kampuni hii imesajiliwa Tanzania kwa mujibu wa Sheria” jambo ambalo dhahiri ni udanganyifu na ni uvunjifu wa Sheria.
 Isitoshe Mhe. Spika, Kampuni ya Deloitte ilionyesha katika Barua walizomwandikia Gavana na Wajumbe wa Bodi dosari zifuatazo kuwa Mikataba (Deeds of Assignments) yana maneno na mfumo unaofanana jambo linaloashiria kuna kugushi, kwani makampuni kwa kawaida yanapenda kuwa na vipengele visivyofanana. Kati ya hati zote hizo hakuna hata moja iliyowekwa kwenye “Letter Head” ya Kampuni zao, mikataba yote imesainiwa ukurasa wa mwisho tu tofauti na kawaida ya kusaini mikataba, Makampuni 12 yana muhuri (seal) unaofanana na ule wa Kampuni ya Kagoda, Mikataba ya Makampuni ya Fiat Veicoli Industriali ya Italia, Valmet (USA) Adriano Gardella S.P.A (Italy) yote haikuwa na mihuri japo Mkataba unaonyesha kuwa muhuri umewekwa, Kampuni ya Valmet yenye Mkataba wa Dolla za Marekani 2,398,439.96 umewekewa saini na mtu anayeitwa Patrick Kevin, Mhasibu (accountant) jambo ambalo si kawaida kwa mkataba wa kiwango kikubwa kiasi hicho. Mambo haya yote yalipaswa kutoa ishara kwa Benki Kuu kuwa mikataba yote imegushiwa lakini wala siyo Benki Kuu wala Wakurugenzi waliostuka na kuchukua hatua pamoja na barua hiyo ya Deloitte.


 Mheshimiwa Spika, fedha hizi zililipwa kupitia Benki zetu wenyewe yaani Benki ya Kitanzania ambayo ni CRDB Benki. Hii ni Benki ambayo ilipaswa kuonyesha uzalendo kwani pamoja na ukweli kuwa mabenki ya kigeni kama vile Kenya Commercial Bank na Barclays Bank walikataa kulipa fedha hizo baada ya kuona kuwa zina harufu ya kifisadi na hata ikafikia mahali wakafunga Account za mteja mmojawapo baada ya kutilia shaka malipo hayo na kuwaandikia BOT pamoja na kuwarudishia hundi zao ,ila Benki yetu wenyewe ya CRDB haionekani ikichukua hatua zozote zile hata pale ambapo malipo hayo yalipofanyika kwa mkupuo kwa siku moja kwenye matawi tofauti ya Benki hiyo Jijini Dar es salaam kama vile matawi ya Kijitonyama, Azikiwe,Vijana , Lumumba, na Holland.
 Badala ya Gavana au Wakurugenzi ambao walijulishwa rasmi kuchukua hatua yeyote ya kisheria, badala yake Gavana wa Benki Kuu alimjulisha bwana Samuel Sithole Mkurugenzi wa Kampuni ya Deloitte ambaye alisafiri toka Afrika Kusini kuokoa hali hiyo, kuwa Waziri wa Fedha (wa wakati huo) anafahamu malipo (Transactions) hayo na angeliweza kuwapatia wakaguzi nyaraka zote husika kuthibitisha uhalali wa malipo hayo. Wakaguzi walikutana na Waziri wa Fedha wa wakati huo wiki ya 11 September 2006 na kuelezwa kuwa Malipo hayo yanahusu “ masuala ya Usalama wa Taifa” (State Secrets) na kwamba wakaguzi hawatapewa nyaraka zozote kuthibitisha uhalali wa Malipo hayo. Tarehe 14 September, 2006 Wakaguzi wa Deloitte walipewa ‘Draft Confirmation Letters” lakini bila Nyaraka zozote (supporting documents). Ndipo wakaguzi walipomweleza Governor tarehe 14 kuwa kutokana na hali hiyo wanatoa kwa BOT “Hati ya Mashaka (qualified Opinion) ya Ukaguzi. Sababu ya msingi ni kuwa wakaguzi waliamini kuwa nyaraka zilizotumika katika malipo hayo ‘ni za kugushi’ na kuwa kulikuwepo na uwezekano mkubwa wa Ufisadi mkubwa katika Malipo hayo. Badala ya kuchukua hatua, kwa mshangao mkubwa tarehe 21 September 2006 Wakaguzi wa Deloitte walifukuzwa kazi kwa kusema ukweli kwa Barua kutoka BOT. Mhe. Spika hii ni hali ya kutisha. Ni dhahiri kabisa kuwa Uongozi wa Benki Kuu, Wakurugenzi wa Benki Kuu akiwemo Gray Mgonja Katibu Mkuu wa Wizara ya fedha, na Waziri wa Fedha wote walihusika au kuficha au kwa uzembe katika njama za kuficha au kutaka kuficha ukweli huu uliowekwa bayana na Wakaguzi wa Kampuni ya Kimataifa ya Deloitte ambayo kwa hakika walionekana wazi kufanya kazi nzuri sana. Isitoshe kitendo hicho cha kufuta mkataba wa wakaguzi wakati kazi ya ukaguzi imekamilika na wakaguzi wameonyesha dosari kubwa katika mahesabu (irregularity) ni kukiukwa kwa taratibu za Kimataifa za ukaguzi (Taz. Barua ya Deloitte ya 10 October,2006 iliyopelekwa kwa Mhe. Zakia Meghji).
 Utekelezaji wa maazimio ya Bunge kuhusu Kampuni ya Richmond iliyoingiza nchini majenereta kwa ajili ya Umeme wa dharura haujatolewa Taarifa. Kimsingi Kambi ya Upinzani inashangazwa na hali ilivyo, kwani tulitegemea Serikali itatoa Taarifa ya utekelezaji wa Maazimio ya Bunge na si majibu ya kisiasa. Maazimio kuhusu watu waliotakiwa kuchukuliwa hatua za kinidhamu hayajatekelezwa. Watu hao bado wako kazini kama desturi; mikataba iliyotakiwa kusitishwa haikusitishwa miezi kadhaa tangu maazimio hayo kupita. Kambi ya Upinzani, inashangazwa na hali hii, na haitegemei kuwa maazimio ya Bunge, ambayo ndio msimamizi wa shughuli za Serikali hayatekelezwi bali yanatafutiwa “maelezo”. Hii ni hali ya hatari katika mustakabali wa uendeshaji wa nchi.
 Pamoja na Taarifa ya Ufisadi ndani ya BOT pia hakuna hatua yeyote iliyochukuliwa kuhusu maeneo mengine tuliyoyaibua mathalan Ufisadi kupitia Kampuni ya Meremeta na Tangold. Waziri wa Fedha ambaye ndiye mwenye dhamana na makampuni hayo katika majibu yake siku ya ijumaa amerusha maswala hayo kwa Mawaziri wa Kisekta. Inawezekana Serikali inasubiri Bunge liunde tena Kamati Teule nyingine kwa lengo la kupitia makampuni haya ambayo umiliki wake umegubikwa na utata mkubwa kutokana na Meremeta kuandikishwa Uingereza ikiwa na Hati ya Usajili na 3424504 ya Tarehe 19 August,1997 na kupata Hati ya Kutimiza Masharti (Certificate of Compliance) nchini Tanzania kama Tawi la Kampuni ya Kigeni yenye na 32755 ya tarehe 3 Oktoba, 1997. Kinachoshangaza katika Kampuni hii ni kuwa wenye hisa wake tofauti na Bunge lilivyoelezwa mara nyingi, ni Triennex(PTY) Ltd ya Afrika Kusini yenye hisa asilimia 50%, Msajili wa Hazina mwenye hisa asilimia 50% kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Kampuni mbili za London Law Services Ltd wa Temple Avenue, wenye hisa 1% na London Law Secretarial Services Ltd ambao anuani yao ni sawa na hao wenzao, nao pia wana hisa 1%. Hii Meremeta hasa ni ya nani, na hawa London Law Services na London Secretarial Services ni akina nani hasa. Kampuni ya Meremeta ina hisa asilimia ngapi? Haya ni mambo yanatufanya tuwe na mashaka makubwa sana. Hivi Serikali inaogopa nini kuweka mambo haya wazi hadharani, angalau kwa Kamati husika ya Bunge basi ili kama kuna sababu ya msingi wawakilishi wa Wananchi waweze kufahamu.
 Vivyo hivyo kwa Kampuni ya Tangold ambayo ilisajiliwa katika kisiwa cha Mauritius tarehe 05 April,2005 Ikiwa na Hati ya Usajili na 553334 na kupata Global Business Licence( C2/ GBL) tarehe 08 April,2005. na kupata Hati ya Kutimiza Masharti hapa nchini tarehe 20 February 2006. Hata hivyo Mhe. Spika, Taarifa zilizoko ni kuwa Tangold imekuwa na akaunti NBC Corporate Branch, no. 0lll03024840 iliyofunguliwa Tarehe 1 January, 2003, yaani miaka miwili kabla Kampuni hiyo haiijasajiliwa Mauritius na takriban miaka 4 tangu imepata Hati ya ‘Kutimiza Masharti’ Tanzania. Ni kwa vipi, kampuni hii kufanya kazi wakati Bunge lilijulishwa na Mhe. Waziri Karamagi kuwa ndiyo iliyorithi Meremeta baada ya Meremeta kufilisika? Mhe. Spika haya maswali yanahitaji kujibiwa kinagaubaga ili kuwarudishia Watanzania imani kuhusu kinachojiri na usalama wa Rasilimali na fedha zao. Waziri Mkuu ndiye mtu stahiki wa kurudisha imani hii kama Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni, baada ya Waziri wa Fedha kushindwa kutoa majibu ya kuridhisha jana. Isitoshe, Makampuni haya tangu yaliposajiliwa nchi za nje na hata hapa Tanzania japo yamekuwa na akaunti katika Benki za nje na za Ndani Hesabu zao hazijakaguliwa na chombo chochote hadi leo (hatujui kama itakuwa imekaguliwa na CAG katika Taarifa ya BOT ya 2007/2008 ambayo haijawasilishwa Bungeni bado). Wahusika wa Tangold ni Bodi ya Wakurugenzi ambayo ni viongozi au waliokuwa viongozi waandamizi katika Serikali. Wakurugenzi hao ni pamoja na hayati Daudi Balali aliyekuwa Governor wa Benki Kuu (BOT), Andrew Chenge aliyekuwa Waziri wa Miundombinu, Gray Mgonja, Katibu Mkuu-Wizara ya Fedha, Patrick Rutabanzibwa- Katibu Mkuu-Maji na Vincent Mrisho-Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika,
Ni muhimu sana kupata majibu ya maswali haya kwa mustakabali wa nchi yetu. Kupitisha bajet ni kitu kimoja na kuziba mianya ya ubadhirifu ni kitu kingine. Mheshimiwa Spika, kutokana na hayo yote yanayohusu Ufisadi ndani ya BOT, Kambi ya Upinzani, inastushwa kuwa wajumbe wa Bodi ya BOT waliokuwepo wakati wote wa sakata hilo bado wamebaki katika Bodi mpya akiwemo Katibu Mkuu wa Hazina Gray Mgonja. Hivyo basi:-

i) Kambi ya Upinzani inamtaka Mhe. Rais, amwondoe haraka iwezekanavyo Gray Mgonja katika nafasi yake ya Ukatibu Mkuu wa Hazina. Gray Mgonja amekuwa mjumbe kwa kofia yake ya Katibu Mkuu wa Hazina. Vivyo hivyo, Rais wa Zanzibar naye amwondoe ndugu K.M.Omar, Katibu Mkuu wa Hazina (Z) ambaye naye anaingia kwa kofia yake. Hatua hii itaruhusu utekelezaji wa mapendekezo ya Wakaguzi (kif.4.3) kuwa Wakurugenzi wote wa BOT waliokuwepo kati ya September 2005 na Oktoba 2006 waondolewe wote na wengine wapya kuteuliwa. Ni kwa njia hii tu Serikali itarudisha imani ya Watanzania kwa chombo hicho kikubwa katika nchi kusimamia hazina, mali na rasilimali zao.
ii) Serikali iliambie Bunge hili, ni lini uchunguzi wa kina utafanyika kuhusu ubadhirifu katika maeneo mengine yanayohusu Meremeta, Tangold, Mwananchi Gold Co. ltd na Deep Green Finance Company Ltd. Kambi ya Upinzani haikuona uchunguzi wowote katika Taarifa ya Uchunguzi wa EPA kuhusu makampuni haya, na Kamati ya Bomani nayo kwa Taarifa tuliyonayo imependekeza uchunguzi wa haraka ufanyike kunusuru rasilimali za Taifa. Kambi ya Upinzani inahitaji maelezo ya kina siyo tu jinsi fedha zilivyokuwa zinahamishwa, bali pia nani wamiliki wa makampuni hayo binafsi yaliyolipwa fedha za walipa kodi wa Tanzania, kwanini Kampuni kama ya Deep Green Finance ilikuwa inafanya kazi wakati haikuandikishwa hata BOT kama financial institution kama utaratibu unavyotaka, kwanini Tangold imefanya kazi nchini miaka 4 kabla haijasajiliwa na kwanini Msajili wa Hazina ambaye ndiye mmiliki wa mali za Taifa kwa niaba ya Serikali hajaorodheshwa mahali popote katika Hati ya Usajili ya Tangold?
iii) Serikali iwasilishe mara moja mswada wa Sheria Bungeni kuondoa utata unaosababishwa na mgongano wa nafasi za Mwenyekiti wa Bodi na Governor wa Benki Kuu, nafasi ambazo kwa sasa zote zimeshikiliwa na mtu mmoja, kuweka kisheria nafasi ya Independent Audit Committee ambapo kwa sasa kamati hii inatoka ndani ya Bodi yenyewe na kupitia upya sheria nzima kama ilivyopendekezwa na wakaguzi (Kif.4.4).
iv) Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali, bila kuchelewa kuwachukulia hatua za kinidhamu na za kisheria maofisa wote waliotajwa katika Taarifa ya Ukaguzi ya Ernst and Young, mathalan, Mkurugenzi wa Fedha wa BOT, Katibu wa Benki Kuu (SB), Mkurugenzi wa Sera za Uchumi (DEP), Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Madeni (DDDD), Kaimu Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Ndani (IA), Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Shughuli za Benki (Director of Bank Supervision). Kama hatua zimekwisha kuchukuliwa basi Waziri Mkuu alijulishe Bunge hili na Taifa kwa ujumla juu ya hatua zilizochokuliwa ili Bunge liweze kutimiza wajibu wake wa kuisimamia Serikali.
v) Kama wakaguzi walivyopendekeza Kifungu cha 4.1 Serikali ilieleze Bunge lako Tukufu ni kwanini Serikali hadi sasa imeshindwa kutekeleza pendekezo la kufungua Upelelezi rasmi wa kijinai (formal criminal investigation) na badala yake kumekuwa na utata wa kinachoendelea kwani kumetolewa taarifa zinazogongana mara kwa mara na Kamati ya Mwanyika, Waziri wa Fedha na wakati mwingine hata na Wasemaji wa CCM. Taarifa hizo zimedai kurudisha au kukusanya mapato zaidi. Watanzania wamechanganyikiwa na kinachoendelea. Wanataka kujua mapendekezo ya Wakaguzi yanatekelezwa vipi, hatua gani imefikiwa, fedha ngapi zimerejeshwa, akaunti ngapi za wahusika zimefungwa (freeze) na wahusika wangapi wamekwisha kufikishwa mahakamani kati ya makampuni 13 yanayohusika na tuhuma za ufisadi wa zaidi ya shs 90,359,078,804.13. Kama kuna fedha zimerejeshwa ni kiasi gani kimerejeshwa, na nani, na zimewekwa wapi. Haya ni maswali muhimu, ni vema Serikali ikayajibu, na kama kwa sababu yoyote itakuwa si vema kuyajibu ndani ya Ukumbi wa Bunge zima, basi majibu yatolewe kwa Kamati ya Bunge ya Kudumu inayohusika na maswala hayo. Bunge kama msimamizi kwa niaba ya Wananchi itafanya makosa kuachia majukumu yake ya “kusimamia” kwa Serikali ambayo katika hatua ya awali ndiyo imetufikisha hapa.
vi) Mheshimiwa Spika, Serikali inafanya utani katika kutotoa Tamko kuhusu kifo cha Dr.Ballali aliyekuwa Governor wa Benki Kuu. Watanzania tunashindwa kuielewa Serikali kwa kukaa kimya. Ballali siyo mtu wa kawaida tu, bali alikuwa msimamizi wa Taasisi kubwa na Nyeti sana katika nchi yetu. Balali anahusishwa na Tuhuma zote zinazohusiana na Ufisadi Mkubwa ndani ya BOT. Ballali ndiye mtu pekee aliyekuwa na ufahamu wa kina kuhusu kilichojiri katika hayo yote yanayotuhumiwa. Serikali haikumhoji japo ilifahamu Ballali alikuwa mgonjwa jambo linalohitaji maelezo ya kina. Serikali ilikuwa na hofu gani kumhoji Ballali? Serikali ilitengua uteuzi wa Ballali bila hata kumpa haki yake ya kusikilizwa, jambo linalotia utata mkubwa sana, hasa baada ya Ballali kutoa Barua yake ya kujiuzulu mwezi December, 2007. Hatimaye kitendo cha Ballali Mtanzania kuweka wosia wa kuzikwa Marekani nayo imeacha utata na maswali mengi sana vichwani mwa Watanzania. Mheshimiwa Spika, huu ni wakati mwafaka Serikali isiachie majungu na umbea kutembea kwa usalama na uhai wa Taifa letu. Itoe mara moja Taarifa ya kina kuhusu kifo cha Ballali, ikiwa ni pamoja na alivyohusika na Tuhuma hizi zote. Isitoshe Kambi ya Upinzani inataka uanzishwe mara moja mchakato wa Uchunguzi ili Taifa liweze kufahamu kinagaubaga ni nini nafasi hasa ya Ballali katika Tuhuma zote zilizomkabili, ikiwemo ya EPA. Tunajua Ballali amefariki, Mwenyezi Mungu aiweke Roho yake mahali pema peponi, lakini kwa vile kuna Taarifa kuwa Ballali ameacha wosia kuhusu nafasi yake katika Tuhuma hizi ukweli hautapatikana isipokuwa kwa Tume/Kamati maalum ya Uchunguzi.Kambi ya Upinzani haiamini kuwa Serikali kwa kila kitu itatufikisha mahali pa kuunda Select Committee ya Bunge. Tamko la Waziri Mkuu, kuwa Serikali isipotenda vizuri na kwa Uwazi Bunge litaunda Kamati Teule nyingi. Tunamtaka sasa Waziri Mkuu kusimamia kauli yake hiyo aliyotoa ndani ya Bunge lako Tukufu.Iundwe Kamati huru ya Serikali na Taarifa yake iwasilishwe Bungeni.

7.1.2: UTATA KATI YA TANGOLD/MEREMETA NA DEEP GREEN:

Mheshimiwa Spika, kuna utata mkubwa sana kuhusu matumizi ya Fedha katika Akaunti za Tangold, Meremeta na Deep Green Finance Co. Ltd. Ili kuwapa picha kamili ya sura hii ya Ufisadi ni vema Waheshimiwa Wabunge wakaona kwa macho yao kilichotokea na kinachoifanya Kambi ya Upinzani kusisitiza kupata Taarifa ya kina kuhusu mambo haya. Taarifa hiyo ni kama ifuatavyo:


7.1.2.1. DEEP GREEN FINANCE COMPANY LIMITED

Mheshimiwa Spika, Kampuni ya Deep Green Finance Ltd ilianzishwa mnamo tarehe 18 Machi 2004. Kwa mujibu wa Taarifa za Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), wakurugenzi wa Deep Green Finance walikuwa ni mabwana Mark Ross Weston wa New Zealand; Anton Taljaard wa Afrika Kusini; na Rudolph van Schalkwyk pia wa Afrika Kusini. Wote watatu ni wakazi wa Afrika Kusini na wanaelekea kuwa ni maafisa na/au wafanyakazi wa Nedbank Ltd. ya Afrika Kusini. Kufuatana na taarifa za BRELA, wanahisa wa Deep Green Finance ni mawakili Protase R.G. Ishengoma na Stella Ndikimi wa IMMMA Advocates; Nedbank Ltd., Nedbank Africa Investments Ltd. na SBM Nedcor Holdings Ltd. Tarehe 15 Aprili 2005 mawakili Ishengoma na Ndikimi walihamisha hisa zao kwa Nedbank Ltd. na Nedbank Africa Investments Ltd.

Taarifa za kibenki tulizonazo zinaonyesha kwamba tarehe 1 Mei 2004, Deep Green Finance ilifungua Akaunti Na. 011103024840 katika tawi la Corporate la Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), Dar es Salaam. Kitu cha kushangaza ni kwamba kampuni hii iliruhusiwa kufungua na kuendesha akaunti hiyo bila ya kuingiza hata senti moja kwa zaidi ya mwaka mmoja kuanzia tarehe “1 Mei” 2004 hadi tarehe 31 Julai 2005.
Hata hivyo kwa kipindi kifupi cha miezi minne kati ya Agosti 1 na Desemba 2005 kampuni hii ilipokea jumla ya shilingi 10,484,005,815.39 kutoka Wizara ya Fedha na/au BOT bila kuonyesha wazi ni biashara gani Kampuni hii imefanya na Wizara ya Fedha au BOT. Fedha hizo zilitolewa kwa utaratibu ufuatao:

(a) Tarehe 1 Agosti 2005 BOT, kwa kutumia hundi Na. 241740, ilihamisha dola za Marekani 1,354,167.26 au shilingi za Tanzania 1,546,778,770.92 kwenda kwenye akaunti ya Deep Green Finance. Siku hiyo hiyo fedha hizo zote zilitolewa kwenye akaunti ya Deep Green Finance kwa utaratibu maalum wa haraka (special clearance) na katika cash kwa Fedha za Tanzania japo zilipelekwa katika Dola za Marekani, jambo linalotia shaka kuhusu malengo ya fedha hizi, hasa ikizingatiwa kuwa waliochukua ni Wageni.

(b) Tarehe 1 Septemba 2005 BOT, kwa kutumia hundi Na. 015558, ilihamisha dola za Marekani 1,827,137.44 au shilingi za Tanzania 2,083,255,881.60 kwenda kwenye akaunti ya Deep Green Finance. Siku hiyo hiyo jumla ya shilingi 2,083,333,333.33 zilitolewa kwa mara nyingine tena kwa kutumia utaratibu maalum wa haraka tena kwa cash;

(c) Tarehe 8 Septemba 2005 Tangold Ltd ilihamisha dola za Marekani 100,256.62 au shilingi za Tanzania 114,611,746.80 kwenda kwenye akaunti ya Deep Green Finance. Itakumbukwa kwamba Tangold Ltd. ni kampuni ya kigeni iliyoandikishwa nchini Mauritius tarehe 5 Aprili 2005 na kupewa Cheti cha Kutimiza masharti ya Tanzania tarehe 20 Februari 2006. Wakurugenzi wa Tangold Ltd. Ni wale ambao tulikwisha kuwataja huko nyuma. Kufuatana na barua ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa BOT ya tarehe 21 Desemba 2006, Tangold Ltd. ililipwa na BOT dola za Marekani 13,736,628.73 kwa kupitia akaunti isiyojulikana ya Nedbank Ltd. ya Afrika Kusini na kwa madhumuni yasiyojulikana;

(d) Tarehe 16 Septemba 2005 jumla ya shilingi 129,000,000.00 zilitolewa kutoka kwenye akaunti ya Deep Green Finance na kuwekwa kwenye akaunti ya muda maalum (FDR);

(e) Tarehe 3 Oktoba 2005 hundi ya BOT Na. 16596 yenye jumla ya shilingi 2,083,333,333.33 za Wizara ya Fedha ililipwa kwa utaratibu maalum wa haraka kutoka kwenye akaunti ya Deep Green Finance. Inaelekea hundi hiyo ililipwa kabla fedha hazijaingizwa kwenye akaunti ya Deep Green Finance kwa vile tarehe 4 Oktoba 2005 BOT ilihamisha dola za Marekani 1,789,075.89 au shilingi 2,083,891,765.35 kwenda kwenye akaunti ya Deep Green Finance;

(f) Tarehe 8 Oktoba 2005 jumla ya shilingi 39,761,397.98 zilihamishwa kutoka kwenye akaunti ya Deep Green Finance kwenda Tangold Ltd.;

(g) Tarehe 31 Oktoba 2005 jumla ya shilingi za Tanzania 2,083,333,333.33 fedha za Wizara ya Fedha zilihamishiwa kwenye akaunti ya Deep Green Finance kwenda kusikojulikana;
(h) Tarehe 2 Novemba 2005 dola za Marekani 1,821,095.57 au shilingi za Tanzania 2,083,653,279.68 zilihamishwa kutoka kwenye akaunti ya Deep Green Finance kwenda kusikojulikana;

(i) Tarehe 30 Novemba 2005 BOT ilihamisha shilingi za Tanzania 2,083,333,333.33 fedha za Wizara ya Fedha kwenda kwenye akaunti ya Deep Green Finance. Siku moja baadaye, dola za Marekani 1,817,199.52 au shilingi za Tanzania 2,184,610,383.04 zilihamishwa kutoka kwenye akaunti ya Deep Green Finance kwenda kusikojulikana;

(j) Tarehe 10 Desemba 2005 shilingi 100,940,489.71 zilihamishwa kutoka Tangold Ltd. kwenda kwenye akaunti ya Deep Green Finance. Hii ilikuwa ni siku nne tu kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Desemba 14, 2005 kufanyika nchini kote;

(k) Tarehe 19 Desemba 2005, siku tano baada ya Uchaguzi Mkuu kufanyika, dola za Marekani 88,722.17 au shilingi za Tanzania 104,755,554.09 zilihamishwa kutoka kwenye akaunti ya Deep Green Finance kwenda kusikojulikana;

(l) Tarehe 9 Februari 2006 shilingi 3,836,800.00 zilihamishwa kwenda akaunti ya mawakili wa Deep Green Finance, IMMMA Advocates, iliyoko benki ya Standard Chartered. Haijulikani kama fedha hizi zilikuwa ni kwa ajili ya malipo ya mawakili hao au la;

(m) Malipo ya mwisho kutoka kwenye akaunti ya Deep Green Finance yalifanywa tarehe 22 Novemba 2006 ambapo jumla ya shilingi 14,465,000.00 zilihamishiwa katika akaunti isiyojulikana ya benki ya Standard Chartered na kwa matumizi yasiyojulikana;

Kutokana na rekodi za kibenki zilizoonyeshwa hapo juu, jumla ya shilingi 10,484,005,815.39 ziliingizwa katika akaunti ya Deep Green Finance katika kipindi cha miezi minne tu kati ya tarehe 1 Agosti na 10 Desemba 2005. Hiki kilikuwa ni kipindi cha mchakato na/au kampeni za Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 14 Desemba 2005. Aidha, kuanzia tarehe 11 Desemba 2005 hakuna fedha yoyote iliyoingizwa katika akaunti hiyo hadi tarehe 27 Februari 2007 kampuni hiyo ilipovunjwa ‘kwa hiari’ ya wanahisa wake. Ni muhimu kurudia kwamba, kwa ushahidi huu wa nyaraka za kibenki, kampuni ya Deep Green Finance haikuwa na hata senti moja kabla ya tarehe 1 Agosti 2005 na wala haikupokea hata senti tano baada ya tarehe 10 Desemba 2005 . Mheshimiwa Spika, kwa mtu yeyote makini ni lazima kupata tafsiri sahihi ya mchakato huu.

Kwa taarifa za sasa hivi, inafahamika kwamba faili la Deep Green Finance lililotakiwa kuwa BRELA limetoweka, isipokuwa Hati ya Kufunga Kampuni (Winding Up). Tuna kila sababu ya kuamini kwamba hii ilikuwa ni kampuni hewa (shell company) iliyoundwa kwa ajili tu ya kupitishia fedha za umma kutoka Benki Kuu kwenda kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2005. Ndio maana kampuni hiyo haikuwa na fedha zozote benki kutokea tarehe 1 Mei 2004 hadi tarehe 1 Agosti 2005, wiki tatu kabla ya kuanza kwa kampeni za Uchaguzi Mkuu. Na ndio maana mabilioni yaliyolipwa na Benki Kuu na Tangold Ltd yalilipwa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu na mara baada ya Uchaguzi Mkuu kupita malipo hayo ya fedha za umma yalikoma. Mhe. Waziri Mkuu Kambi ya Upinzani inakutaka utoe ufafanuzi wa kina katika jambo hili. Bunge linapaswa kuelezwa pia ni vipi kampuni ya Deep Green Finance Co.ltd imekuwa ikifanya kazi kwa kipindi chote hicho bila usajili wa Benki Kuu kama Financial Institution kama inavyotakiwa na Sheria ya Nchi.

7.1.2.2. TANGOLD LIMITED

Mheshimiwa Spika,
Tangold Limited ni kampuni ya kigeni inayomilikiwa na baadhi ya watu tuliowataja hapo juu. Kuna utata mkubwa zaidi ambao umeigubika kampuni ya Tangold Ltd. Kwanza, licha ya nyaraka kuonyesha kwamba kampuni hiyo ilipewa hati ya kutimiza masharti ya Tanzania tarehe 20 Februari 2006, nyaraka za kibenki tulizonazo zinaonyesha kwamba Tangold Ltd. ilifungua akaunti ya shilingi Na. 011103024852 NBC Corporate Branch tarehe “1 Januari 2003”. Kama ilivyokuwa kwa Deep Green Finance, siku ya TANGOLD kufungua akaunti yake ilikuwa ni siku ya Mwaka Mpya na hiyo ni siku ya Mapumziko dunia nzima. Aidha taratibu za kibenki za ufunguaji wa makampuni zinalazimu kampuni husika kuwasilisha benki nakala ya usajili, nakala ya Katiba kabla ya kuruhusiwa kufungua Akaunti, na hati ya Mlipa Kodi ( registration certificate). Taratibu za kibenki za ufunguaji wa akaunti za makampuni zinalazimu kampuni husika kuwasilisha benki nakala ya usajili wa kampuni na Katiba yake kabla ya kuruhusiwa kufungua akaunti. Swali la kujibiwa na NBC pamoja na watawala wa nchi hii ni je, ilikuwaje Tangold Ltd. waliruhusiwa kufungua na kuendesha akaunti ya benki kabla hawajaandikishwa nchini Mauritius achilia mbali kupata hati ya kutimiza masharti ya Tanzania? Kifungu cha 7 cha Memorandum and Articles of Association kinataja wazi kuwa wenye hisa wanaweza kuhamisha hisa zao kwa Baba, mke, mtoto na mpwa. Kambi ya Upinzani inataka Bunge hili lielezwe Kama kweli TANGOLD ni mali ya Serikali kwa asilimia mia moja, Baba, mke ,mtoto, na mpwa wa Serikali ni nani?

Pili, kampuni ya Tangold Ltd, iliendesha akaunti hiyo bila kuweka au kutoa fedha yoyote ile kati ya tarehe 1 Januari 2003 hadi tarehe 1 Agosti 2005 ilipoanza kunyeshewa mvua ya neema ya mabilioni ya fedha za walipa kodi wa Tanzania kutoka BOT! Mvua hiyo ni nje ya mvua ya dola za Marekani 13,340,168.37 iliyohojiwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali na iliinyeshea Tangold Ltd. kama ifuatavyo:


(a) Tarehe 1 Agosti 2005 BOT ilihamisha shilingi za Tanzania 4,703,221,229.08 kwenda kwenye akaunti ya Tangold Ltd.; Tarehe hii ni muhimu sana kwani ndiyo siku ambayo BOT ilifanya pia malipo ya kwanza kwa Deep Green Finance kama ilivyoelezwa katika Taarifa hii. Ukijumlisha kiasi hiki na kile kilichohamishwa kwenye akaunti ya Deep Green ni jumla ya Tshs 6.2 Billion. Fedha zote hizi zilichukuliwa kwa ‘cash’. Inashangaza waliozichukua fedha hizi walizebebaje kwani wataalam wanakisia kuwa sawa na Tani 50 zinazoweza kubebwa na kubebwa tu na lori 5 za Tani 10 kila moja? Hili linabaki kuwa fumbo.

(b) Tarehe 2 Septemba 2005 Tangold Ltd. ilihamisha shilingi za Tanzania 244,428,386.15 kutoka akaunti yake hiyo kwenda kwenye akaunti ya Deep Green Finance; Kama tulivyoelezea katika Taarifa hii Deep Green Finance ililipwa tarehe 1 Augusti, 2005, Tshs 2,083,255,881.60 na BOT.

(c) Tarehe 8 Oktoba 2005 shilingi za Tanzania 39,761,397.98 zilihamishiwa kwenye akaunti ya Tangold Limited kutoka kwenye akaunti ya Deep Green Finance;

(d) Tarehe 12 Oktoba 2005 Tangold Ltd. ilihamisha shilingi za Tanzania 1,690,500,000.00 kwenda Meremeta Limited;

(e) Tarehe 23 Novemba 2005 Tangold Ltd. ilihamisha shilingi za Tanzania 555,300,048.00 kwenda Meremeta Ltd.;

(f) Tarehe 10 Desemba 2005 Tangold Ltd. ilihamisha shilingi za Tanzania 100,940,489.71 kwenda kwenye akaunti ya Deep Green Finance;

(g) Tarehe 12 Desemba 2005, siku mbili kabla ya Uchaguzi Mkuu, Tangold Ltd. ilihamisha shilingi za Tanzania 551,060,000.00 kwenda kwenye akaunti ya Meremeta Ltd.

Baada ya hapo Tangold Ltd. haikupokea wala kuingiza fedha zozote kwenye akaunti yake hadi tarehe 6 Juni 2006. Tangu tarehe hiyo hadi leo hii Tangold Ltd. haijaweka wala kutoa fedha nyingine yoyote katika akaunti hiyo. Kwa maana hiyo, katika kipindi cha miezi minne Tangold Ltd. iliingiziwa na BOT jumla ya shilingi za Tanzania 4,742,982,627.06 na ilifanya malipo kwa Deep Green Finance na Meremeta Ltd. ya jumla ya shilingi za Tanzania 3,363,531,259.67.

Mheshimiwa Spika, maswali muhimu ya kujiuliza kuhusiana na Tangold Ltd. ni haya yafuatayo. Kwanza, ilikuwaje kampuni ambayo haikuwa hata imeandikishwa kisheria ikalipwa mabilioni ya fedha za walipa kodi na/au ya umma na bila maelezo yoyote?
Pili, ilikuwaje Serikali, kupitia kwa aliyekuwa Waziri Karamagi, itoe taarifa ya uongo Bungeni kwamba Tangold Ltd. ni kampuni mpya na imeanzishwa ili kurithi mali na madeni ya Meremeta Ltd. wakati makampuni yote mawili yalikuwa yakipeana mabilioni ya fedha za umma wakati wa mchakato wa Uchaguzi Mkuu katika mazingira ya kutatanisha?
Tatu, kwa nini malipo ya mabilioni haya yalikoma mara baada ya Uchaguzi Mkuu ?

Tuhuma hizi nzito zinaihusisha moja kwa moja Serikali na watendaji wake wakuu kutokana na mfumo huu wa kuhamisha fedha za umma (transaction) bila maelezo ya kutosha. Aidha tunawaomba wananchi wa Tanzania wenye mapenzi mema na Taifa letu waidai Serikali iwaeleze mabilioni haya yalilipwa kwa ajili gani.


Hivyo basi:-
Kambi ya Upinzani inamtaka Waziri Mkuu kutoa ufafanuzi wa kina kuhusu mambo yafuatayo:-
a) Makampuni haya ya TANGOLD,Meremeta na Deep Green ni ya nani, na wanahisa wake ni kina nani?
b) Serikali inatoa kauli gani kuhusu uwezekano wa uvunjifu wa Sheria ulio dhahiri jinsi makampuni haya yalivyosajiliwa, yalivyoanza kazi nchini bila usajili rasmi jambo ambalo ni kinyume na Sheria na kufungua Akaunti Benki siku za Sikukuu jambo linaloashiria kuna udanganyifu, hila za uwizi yaani ‘fraud and forgery”.
c) Serikali inaeleza nini juu ya Fedha nyingi za umma kuchukuliwa kwa cash, tena na watu ambao si raia. Fedha hizo zilihamishwa na BOT kwa Dolla za Marekani, je ni sababu zipi ziliwafanya wageni hao kuzitoa Benki kwa cash na walizipeleka wapi?)Uzito wa fedha zilizohamishwa tarehe 1Agust kwa fedha taslimu ni sawa natani 50 yaani uzito sawa na lori 5 za tani kumi kumi). Je ni utaratibu fedha za umma kuchukuliwa kwa mtindo huo?
d) Je Serikali iko tayari kufanya uchunguzi wa kina kwa kutumia Makampuni yenye sifa na kutoa Taarifa kwa Bunge hili Tukufu au ni hadi Bunge litakapounda Kamati Teule ili kupata ukweli?


7.2 KAMPUNI ZA TANPOWER RESOURCES LTD NA ANBEM:
Mheshimiwa Spika,
Kiwira Coal Mines Ltd ilikuwa mali ya Serikali kwa asilimia mia moja (100%).Kuna utata mkubwa umezuka kuhusu utaratibu uliotumika kubinafsisha Kampuni hiyo na hisa zake kuuzwa kwa Makampuni binafsi kati ya 2004 na 2005. Kwa taarifa iliyoko, Serikali imebakiziwa hisa zisizozidi asilimia 15% tu kati ya 100 % kutokana na Ubinafsishaji huo. Kampuni ya ANBEM ilisajiliwa tarehe 21 June, 1999 na wanahisa waanzilishi wakiwa ni Anna Mkapa wa S.L.P. 7652 Dar-Es-Salaam, Mjasiriamali (Entrepreneur), na Benjamin William Mkapa wa S.L.P 7652 Mjasiriamali kama ilivyo kwa Anna Mkapa. Memorandum and Articles of Association ya Kampuni ya ANBEM iliandaliwa na Wakili Maarufu,( sasa marehemu) Kapinga & Company Advocates wa Dar-Es-Salaam. Japo haikuelezwa wazi, inaeleweka wazi kuwa Benjamin William Mkapa na Anna Mkapa ni Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu hasa pale inapoelezwa kwenye nyaraka hizo hizo za Brella kuwa wanakaa Plot no 15 Luthuli Road, Wilaya ya Ilala, Dar-Es-Salaam ambayo inadhaniwa kuwa ni anuani ya Ikulu, makao ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kampuni ya ANBEM pamoja na Kampuni ya TANPOWER Resources Ltd iliyosajiliwa Tarehe 29 December 2004 na kupewa Hati ya Usajili namba 51080. Wakurugenzi wa Kampuni ya Tanpower Resources Ltd ni Hon. Anna Mkapa, Hon. Daniel Yona, Mr. Evans Mapundi, Mr. Joe Mbuna na Mr. Nicholas Mkapa.

Mhe. Spika, Kampuni ya Tanpower Resources Ltd pamoja na ‘Share holder wake ANBEM akiwemo Benjamin William Mkapa’ na makampuni binafsi mengine ya DevConsult International Ltd, Universal Technologies Ltd, Choice Industries Ltd na Forsnik Enterprises Ltd o ndizo zinazoonyeshwa kunununua hisa kwanza 70 na baadaye kuongezeka kuwa 85 za kilichokuwa Kiwira Coal Mines Ltd ambayo hadi wakati huo ilikuwa asilimia 100 mali ya Serikali ya Tanzania kwa niaba ya Watanzania wote.
Kampuni ya Tanpower Resources Ltd ndiyo inayosemekana imewekeana na TANESCO mkataba wa muda mrefu ambako inasemekana watauzia umeme Kampuni ya TANESCO kwa kiwango cha Dolla za Marekani 271 Millioni, yaani Tanasco itakuwa inalipa kiasi cha Tshs 300 Millioni kwa capacity Charge Kampuni binafsi ya Tanapower Resources Ltd, nje ya malipo ya matumizi ya Umeme. Kiwango hiki ni kikubwa kuliko hata malipo yanayolipwa na TANESCO kwa Richmond/Dowans kama inavyoonyeshwa kwenye Mkataba wa Tarehe 8 June, 2005.

Mhe. Spika, kuna mambo kadhaa hapa yanayotia wasiwasi. Wakati mikataba hii inawekwa Benjamin William Mkapa, mjasiriamali alikuwa pia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe. Daniel Yona Mkurugenzi mmojawapo wa Tanpower Resources Ltd alikuwa ndiye waziri wa Nishati na Madini. Yeye ndiye aliyekuwa anafanya mawasiliano na Kampuni ya Kiwira Coal Mines ltd wakati wa ubinafsishaji wa Kiwira Coal Mines Ltd, kama inavyoonyeshwa na nyaraka mbalimbali mathalan Barua toka kwa bwana Evans Mapunda wa Tanpower Resources Ltd yenye Kumb na TPRCL/GEN/2005/06 ya tarehe 4th January 2005/06 kwenda kwa Mhe. Daniel Yona Waziri wa Nishati na Madini, na kutoka kwa Mhe. Daniel Yona yenye Kumb.CDA 48/171/01 ya tarehe 24 March, 2004.
Mheshimiwa Spika, hapa kuna maswali mazito yanahitaji kujibiwa na Serikali:-
a) Wahusika wakubwa yaani Mhe Benjamin William Mkapa, japo kajiandika Mjasiriamali, na Mhe. Daniel Yona, japo kama Mkurugenzi hakujiainisha kama Waziri na kwenye barua hakujionyesha kama Mkurugenzi wa TPRCL suala la “Conflict of Interest” kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ilizingatiwa vipi?
b) Kwa vile hakuna ushahidi wowote wa utaratibu ulioonyeshwa wa kubinafsisha Kiwira Coal Mines Ltd, ni kitu gani kinawazuia Watanzania wasiamini kuwa hapa kulikuwa na suala la matumizi mabaya ya nafasi zao kushawishi Kiwira Coal Mines Ltd kuwauzia Kampuni ya Tanpower asilimia 85 ya mali ya Watanzania?
c) Kwa kuingia Mkataba huo wa kuiuzia TANESCO umeme unaolipiwa Capacity charge, yaani utalipiwa hata bila kutumika, ni vigezo gani vya kiushindani vilitumika, jambo ambalo ni dhahiri litawagharimu watanzania ambao hata kabla ya hapo wamekwisha kuelemewa na bei ya Umeme? Na Kama kweli ni Kampuni ya Kiwira kuwa na matatizo ya kifedha, ni kwanini hatua ya awali isiwe ni Waziri wa Nishati kufanya kila jitihada kuikoa Kampuni hiyo, na badala yake kuinunua yeye mwenyewe kwa kutumia Kampuni anayomiliki yeye na Mheshimiwa Rais aliyeko madarakani, ambaye wajibu wake wa kwanza ni kulinda na kutunza kwa uadilifu rasilimali aliyokabidhiwa na Watanzania azitunze kama mdhamini?
d) Mhe. Spika, katika hili Kambi ya Upinzani inahitaji majibu ya kina sana, kwanza kama haya tuliyoeleza ni ya kweli , Serikali inalielezaje hili la mgongano wa maslahi na kukiukwa kwa sheria ya Maadili ambayo Rais ndiye mlinzi wake, lakini badala yake yeye ndiye dhahiri anaonekana kuikiuka na hatimaye kubinafsishwa kwa Kiwira Coal Mines Ltd bila Tender? Kambi ya Upinzani kama haitapata majibu ya kuridhisha itaomba iundwe Kamati Teule ya Bunge kutazama mchakato mzima wa kuuza Kiwira Coal Mines Ltd kwa Kampuni ya Tanpower Resources Ltd. Kambi ya Upinzani pia inaitaka Serikali, ifute mara mmoja mkataba kati ya Tanpower Resources Ltd na TANESCO ili Watanzania wasije wakaumizwa na gharama kubwa ya capacity Charge ya Umeme huo utakaotokana na Tanpower Resources Ltd.
Mheshimiwa Spika, pia kumekuwepo na mjadala mkubwa kuhusu kama Rais mstaafu anaweza kushtakiwa au la kutokana na kinga zinazoelezwa na Katiba Ibara ya 46(1) na (2). Ninapenda kusema kuwa kwa maoni ya wanasheria wengi, Katiba Ibara ya 46(3) iko wazi, kwani inatamka wazi kuwa Rais mstaafu ana kinga kwa …”jambo alilofanya kama Rais wakati alipokuwa anashika madaraka ya Rais kwa mujibu wa Katiba ..” Hivyo kwa tafsiri iliyoko, Rais mstaafu hana kinga kwa.. ‘jambo alilofanya yeye kama raia binafsi wakati alipokuwa madarakani…” Isitoshe, Katiba Ibara ya 46(2) inaeleza wazi kuwa ..’haitaruhusiwa kufungua mahakamani shauri kuhusu jambo lolote alilotenda au alililokosa kulitenda yeye binafsi kama raia wa kawaida ama kabla au baada ya kushika madaraka ya Rais, ILA TU KAMA angalau siku thelathini kabla ya shauri kufunguliwa mahakamani Rais atapewa au ametumiwa kwanza taarifa ya madai….” Ni dhahiri kuwa kinga ya Rais mstaafu siyo “absolute”.
Hivyo Kambi ya Upinzani inataka Serikali kuliambia Bunge hili ni hatua gani itachukua dhidi ya Rais Mstaafu na Waziri wake wa Nishati wa Wakati ule ili kuwarudishia imani Watanzania kuwa tuliowaweka Madarakani hawatatumia tena nafasi zao kujibinafsishia mali ya Watanzania wote?

7.3 KAMPUNI YA SPM –MGOLOLO :

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inasikitishwa na hali ya Serikali kutokuchukua hatua ya kujisafisha kabla ya kuchokonolewa. Ndiyo kusema Serikali haiyajui haya yote yanayoandikwa na kusemwa na watu mbalimbali?
Mheshimiwa Spika, Kampuni ya Mgololo ilibinafsishwa kwa Kampuni ya RAI Group Ltd ya Kenya tarehe 16th January 2004 kama inavyoonekana kwenye Assets Sale Agreement kati ya United Republic of Tanzania na RAI Group Ltd (kama nilivyopokea kutoka Ofisini kwako kwa Barua yenye Kumb na. CEB/147/155/03/09 ya tarehe 19 June, 2008) inayomilikiwa na wakenya wawili bwana Jaswant Singh Rai na bwana Sarbjit Singh Rai kila moja akiwa na hisa 0.0006% kwa bei ya Dolla za Marekani 26 Millioni. Hata hivyo Mheshimiwa Spika Mkataba huu wa mauziano unatisha sana na Kambi ya Upinzani inataka ufafanuzi wa kina katika maeneo yafuatayo:

a) Kifungu cha 3.1 cha Mkataba wa Mauziano unatamka kuwa Bei ya mauzo ni Dolla za Marekani 26 Millioni. Cha kushangaza ni kuwa mkataba huo huo unaeleza italipwa $ za Marekani 1 Million siku ya kuwekeana saini. Na $ za Marekani 3,000,000 zitawekwa kwenye Escrow Account ambazo Mwekezaji atazichukua atakapokuwa anatimiza masharti fulani fulani kwa ukarabati wa kiwanda “chake”. Fedha zingine $ za marekani 22 Millioni atazitumia Mwekezaji kwa kufanyia kiwanda Ukarabati. Mhe. Spika, hivi anadanganywa nani? Kama Bei ni $ 1 Millioni kwanini isielezwe hivyo wazi wazi? Hili fumbo maana yake ni nini. Isitoshe hata kodi ya Serikali imewekwa kwani mkataba unasema dhahiri kuwa kwa kutimiza matakwa ya Ushuru wa Stamp Duty kiwango kitakachotumika ni $ za Marekani 1 Millioni? Hii maana yake ni nini kama si kutoa sadaka Rasilimali za Watanzania?
b) Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani ilikuwa inajiuliza hivi hawa wawekezaji wenye Hisa 0.006% kila mmoja ni kweli wawekezaji, na wanaweza kukifufua kiwanda kama kweli kiko kwenye hali mbaya kama Serikali inavyosema. Utafiti wetu umeonyesha kuwa kumbe mwenye mali halisi wala siyo Rai Brothers kama walivyo kwenye Sale agreement, bali ni Angel Hurst Industries ya Uingereza yenye hisa 99.988% kama ilivyosajiliwa kwenye Kituo cha Uwekezaji kama inavyoonekana kwenye Certificate of Incentives no 00021049 iliyotolewa TIC tarehe 19 April, 2004 kwa Mufindi Paper Mills Ltd ambayo ndiyo Kampuni iliyosajiliwa baada ya kununua Kampuni ya Southern Paper Mills (SPM) ambayo ilikuwa asili mia 100% mali ya Serikali na hivyo mali ya Watanzania wote na kusimamiwa na NDC ikiwa na Hati ya Industrial Licence na .0907. Isitoshe, kiwango cha Fedha kilichotajwa kwa TIC ni Dola za Marekani 52 Millioni (Foreign) na Tshs billion 9.251 fedha za ndani yenye jumla ya Dola za Marekani 61.251 na siyo 25.Millioni walioyotaja kwenye Nyaraka mbalimbali za Sale Agreement. Kwanini kuwe na udanganyifu huu mkubwa?
c) Mheshimiwa Spika, Mahakama ya kazi katika hukumu yake ya Uchunguzi wa Mgogoro wa Kazi na 80/2006 ya TUICO vs PSRC na wenzake ilitamka wazi kuwa “si rahisi kuamini kuwa mali zote za Southern Paper mills Ltd, za thamani ya soko la mabilioni ,si chini ya 500 Billioni kwa makisio yangu na si ile thamani ya tshs 85 Billioni iliyotumika kuuzia .. ambayo nionavyo ni “token/book price value” tu ambayo mathalan flat rate ya Trailer Scania linalofanya kazi lilithaminiwa kwa Tshs 300,000 kwa kila Traillor ambayo ni chini ya Bei halisi hata ya tairi lake moja tu…”
d) Hii ni hali ya kutisha Mhe. Spika, kwani hata kama tatizo ni hapakuwa na mnunuzi wa SPM Ltd basi wangeliuza vifaa hivyo kimoja kimoja wangelipata mara kadhaa ya bei waliyopata. Rasilimali zilizouzwa ni pamoja na Nyumba zikiwemo za Grade A, Kijiji kizima cha Wafanyikazi kama ilivyorikodiwa kwenye Mkutano wa Mashauriano wa Kamati ya FAST TRACK ya Baraza la Mawaziri la tarehe 4 August,2003 inayosomeka ..”kinachouzwa ni kiwanda, kijiji na eneo la Ardhi ambalo bado kuendelezwa la hekta 28,000.
e) Mheshimiwa Spika, Serikali yetu imekuwa si makini katika ubinafsishaji huu, kama ilivyo kwa mengine mengi. Watumishi zaidi ya 760 bado wanadai haki zao pamoja na hukumu iliyotolewa na mahakama wanadai zaidi ya Tshs 2,647,255,816. Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali isimamie utaratibu unaoeleweka wa kulipwa Watanzania hawa maskini ambao wamejikuta wao na familia zao katika maisha magumu kutokana na maamuzi yasiyo makini ya Serikali.
Kutokana na hayo yote Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali yafuatayo;
i) Bunge hili lielezwe Angel Hurst Industries ni nani hasa na kwanini hawako popote kwenye Mkataba rasmi ?
ii) Mkataba kati ya Serikali na RAI Group utazamwe upya kuondoa utata huu wa Mali ya Watanzania, ikiwemo vifaa vya kiwanda, nyumba, kijiji cha Wananchi Watanzania, na eneo la Hekta 28,000 ambazo hazikulipiwa kitu kabisa, ikiwa lazima tathmini ifanyike upya kuangalia bei halisi ya yote hayo, na au Mkataba uvunjwe. Serikali iangalie ni kwanini Watendaji wetu Serikalini hawakulinda maslahi ya nchi yetu, badala yake waliegemea kwa mwekezaji ikiwa ni pamoja na kuweka Jeshi la Polisi kulinda kiwanda hicho kwa miaka yote kwa kodi ya Watanzania, wakati polisi hao wangeliweza kufanya kazi ya ulinzi na usalama wa Raia. Kuegemea huku kunaonekana hasa katika Barua ya Waziri wa wakati huo wa Viwanda na Biashara Mhe.Juma Ngasongwa yenye Kumb CCD/111/450/01 ya 14 August, 2005 na tena Barua yanye Kumb. Na CCD/111/450/01/33 ya tarehe 8 September, 2005.

7:4 COMMODITY IMPORT SUPPORT:

Mheshimiwa spika, Kama nilivyokwisha wahi kusema ndani ya Bunge hili, kuwa kuna ufisadi mkubwa kupitia mpango wa Commodity Import Support. Huu ni mpango wa kuipa Serikali uwezo wa kuimarisha uchumi wake kwa kuzipatia taasisi, makampuni, viwanda na biashara mbalimbali katika kipindi cha miaka ya 1980 hadi 2004. Katika mpango huo, Wahisani mbalimbali wakiwemo Serikali ya Japan ilitoa fedha nyingi za kigeni kwa mpango huu na BOT/Hazina kusimamia fedha hizo, na wajasiriamali kuruhusiwa kuagiza bidhaa au huduma kutoka nje ya nchi na Serikali kupitia BOT/Hazina kulipia kwa fedha za kigeni. Wajasiriamali walitakiwa kukopa bila riba, ila iwapo atashindwa kulipia atatakiwa kulipia asilimia 17 kama riba ya thamani ya mali au huduma walizokuwa wanaaigiza nje.

Fedha zilizokuwa zinalipwa na wajasiriamali zilitakiwa kuingia kuimarisha Bajeti ya Serikali, pamoja na miradi maalum ya maendeleo kama ilivyokubaliwa katika mkataba kati ya Serikali na Wafadhili waliochangia mpango huo. Matatizo ya Mpango huu ni kama ifuatavyo:-

i) Mheshimiwa Spika ,Kimsingi mimi sina Tatizo na waliokopa fedha kupitia mpango huu. Kukopa ni deni na mkopaji anatakiwa kulipa, kama si leo kesho kwa utaratibu wowote wa kisheria kama ni lazima. Hivyo sina Tatizo kuwa hizi fedha ni za mkopo hivyo Serikali itaendelea kuwadai wahusika.
ii) Tatizo langu la msingi ni Taarifa kuwa kuna Utapeli na Ufisadi mkubwa jinsi fedha hizi zilivyokopeshwa na au kuidhinishwa, na au kutolewa. Nyaraka nilizonazo zinaoonyesha kuwa:
a) Kati ya makampuni 980 mengi yalianzishwa tu kama chambo cha kupatia fedha hizo, na mengi ya kampuni hizo au yamekwisha kufungwa na hayako tena, au yamefilisika, na au yalikuwa hewa. Jambo ambalo linaonyesha kuwa kulikuwa na uzembe mkubwa sana katika Serikali kwani mikopo hiyo au ilitolewa bila uchambuzi wa kutosha, au kulikuwa na ushirikiano kati ya viongozi wa Serikali hasa Hazina na BOT walioidhinisha ukopaji huo, na au uwizi wa moja kwa moja, kupitia kampuni moja ya Ushauri.
b) Taarifa zinaonyesha maajabu kuwa kwa mfano Kampuni moja ilipata mikopo kupitia makampuni hewa 35 . Fedha za umma zilichukuliwa kupita makampuni haya hewa na hivyo kufanya fedha hizo zisilipike kabisa au kuwa ngumu kabisa kulipika.
c) Majina mengine yakiwemo ya wabunge, au walianzisha makampuni au walipata vibali na kuviuza vibali vyao kwa wajasiriamali wajanja na wao kulipwa kiasi fulani tu cha fedha, au kwa kuelewana, au kwa kudanganywa na kuhujumiwa.
iii) Matokeo ya haya yote, ni fedha za Umma zaidi ya 900 Billioni zilichukuliwa kwa njia hii na waroho hawa wachache kwa njia hii ya ufisadi. Taifa limepata hasara kubwa kwa vile fedha hazikufanya kazi zilizokusudiwa, hazilipiki kwa vile makampuni mengi ni hewa na au utaratibu haukuwa makini kwa makusudi au kwa uzembe. Kambi ya Upinzani inamtaka Mheshimiwa Waziri Mkuu kutoa Taarifa ya kina kuhusu hatima ya fedha hizi zilizochotwa kupitia utaratibu huu, ikitenganisha zilizokopwa kwa utaratibu halali na zile zilizokopwa kupitia makampuni hewa, ambayo inasemekana makampuni zaidi ya 400 kati ya 980 yalikuwa hewa.



7.5: TAARIFA ZA KAMATI MBALIMBALI:

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inastushwa na Usiri ulioko Serikalini na hasa usiri unaohusiana na Taarifa mbalimbali za Kamati zinazoundwa na Serikali ( Waziri Mkuu) na Mhe. Rais. Mhe Spika, Ibara ya 63(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ilipotoa jukumu la “kusimamia” Serikali kwa Bunge haikuweka mpaka wowote. Hii ni kwa sababu kazi zote anazofanya Mhe. Rais zinafanyika kwa kutumia fedha za Wananchi kutoka kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali, yaani Consolidated Fund. Hivyo, Bunge linapaswa kujua matokeo ya Tume na Kamati hizo ili kuleta ufanisi. Kwa mfano Mhe Spika, katika Miaka 6 iliyopita zimeundwa Kamati 5 kuchunguza Madini. Hadidu rejea za Kamati hizo karibu zote zinafanana kwa mfano Kamati ya Kipokola, Kamati ya Masha, Kamati ya Generali Mboma na sasa Kamati ya Bomani. Ripoti ya Kamati zote zimewasilishwa kwa Mhe. Rais, na hakuna Taarifa kwa umma wa Tanzania, wala kwa Bunge. Taarifa zote hizo hazijafanyiwa kazi na hakuna anayejua kama ziko kwenye Shelf za Rais, au zimejaa buibui mahali fulani kwenye kona ya Ikulu. Taarifa ya kamati iliyoundwa na Mhe. Lowassa kuchunguza ujenzi wa maghorofa DSM, baada ya Hotel ya Chang'ombe Village kuanguka nayo haijatolewa Taarifa. Taarifa hii haijulikani nini mapendekezo yake. Hakuna utekelezaji uliofanyika wa mapendekezo ya Kamati hizo, huku majengo mengine yakiendelea kuporomoka kama ilivyotokea Kisutu juzi tarehe 21/06/2008 Jijini Dar es salaam. Kambi ya Upinzani inaona haya ni matumizi mabaya ya Kodi za Umma na hakuna Kamati inayofanya kazi bila kutumia mabilioni ya Fedha. Huu ni ulaji mwingine.

Mheshimiwa Spika, kwa vile hakuna Taarifa rasmi tunawajibika kufanya makisio tu. Kamati ya Bomani imeenda Zambia, Australia, Canada, Ghana kwa taarifa tulizopata kwenye vyombo vya Habari. Kamati imezunguka karibu nchi nzima, mathalan maeneo yote yenye madini. Kwa tafsiri rahisi haya ni mabilioni ya fedha ambayo yangeweza kutumika kujenga shule, zahanati, mabweni na au kutoa chakula kwa watoto wetu ambao sasa wengi wamefunga shule kwa kukosa chakula.
Ni vema basi, Mheshimiwa Spika, Waziri Mkuu akaliarifu Bunge lako Tukufu Kamati ya Bomani imetumia shillingi ngapi na Wakaguzi wa EPA wamelipwa kiasi gani. Hizi ni fedha za Wananchi ni lazima zitolewe taarifa kwa chombo chao ambacho ni Bunge.



Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani imetishwa zaidi na Taarifa iliyosambaa katika Mtandao inayoonyesha kuwa Taarifa hizo za Kamati ya Rais, ambayo ni Siri kubwa kwa Wabunge na kwa Watanzania tayari inajulikana na watu wa nje wakiwemo wawekezaji. Kambi ya Upinzani imefadhaishwa sana na Taarifa aliyotoa CEO wa Kampuni ya Tanzanian Royalty Exploration Corporation bwana James E. Sinclair Mwenyekiti na CEO, ya Tarehe 30 May, 2008 yenye kichwa cha habari “changes To Tanzanian Mining Law Certain to benefit Mineral Exploration” na pia ya tarehe 11 June, 2008 yenye kichwa cha Habari “ A special note to Shareholders”. Taarifa ya Bwana Sinclair ya 30 May, 2008 inatamka wazi kuwa “ I have had the privilege of reviewing the Committees Recommendations-along with comments from the Chamber of Mines –and have no serious issues with them…What is important to know, however is that the man who will make the final decision on the recommendation is the President not the Committee…” na “As one might expect, any legislation involving such an important segment …has generated heated debate. In my opinion, a small percentage of this rhetoric is instigated by special interest groups in the west whose commentary reads like … a standard play book”.
Mhe Spika, Kambi ya Upinzani inadhani haya ni madharau makubwa kwa Watanzania, matusi kwa Wabunge, na pia inajenga picha kuwa Wabunge wanaopiga “kelele” kuhusu mali na rasilimali zao sio watu wanaoweza kufikiri wenyewe bali “wanatumika” …… Matusi haya hayawezi kuvumilika hivyo basi, tunamtaka Bwana Sinclair aombe Radhi kwa Bunge hili na watanzania wote kwa ujumla. Mheshimiwa Spika, kiburi hiki amekipata baada ya Bunge lako Tukufu kudharauliwa kwa kunyimwa Taarifa muhimu kama hii. Hivyo Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kuacha mara moja tabia ya kuthamini vyombo na watu wa nje.

Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali iwasilishe mara moja Bungeni katika kipindi hiki cha Bunge Taarifa ya Kamati ya Bomani, pamoja na Taarifa zote za Kamati za awali ili wabunge waweze kutimiza majukumu yao ya ‘Kuisimamia’ Serikali. Mhe. Spika, tumekwisha kusema mara nyingi, Wabunge ni watu wazima, waliokula kiapo, wanajua kutunza siri kwa vile na wao ni wazalendo, hivyo suala la Siri haliwezi kuwepo kwa Wabunge vinginevyo Kiapo wanachokula hakina maana yeyote.

8: Mheshimiwa Spika,
Kwa mtu yeyote mnyofu, mkweli na anayefanya upembuzi yakinifu wa hali ya siasa ya Tanzania atakubali leo kuwa hali ya siasa ni tete. Tusijidanganye kwa kusema kila mara kuwa hali ya kisiasa nchini ni ‘shwari’. Tusipojiangalia na kuwa makini tutakuwa tunacheza mchezo wa Mbuni wa ‘kuficha kichwa kwenye mchanga’.

Mheshimiwa spika, kila kukicha kuna taarifa ya mgomo kwenye shirika hili au lile kutokana na wafanyikazi au kunyanyasika, au kunyimwa haki zao, au kubaguliwa kama ilivyo kwa hoteli ya Wildlife Lodge kule Ngorongoro ambako wafanyakazi wanatengwa na mwajiri kwa msingi wa kwamba kama aliyeajiriwa ni baba basi mama na watoto hawatambuliwi, hivyo hawatakiwi katika kambi ya hoteli.

Kutoka maeneo mbalimbali ya nchi kuna taarifa ya wananchi kuvamia vituo vya polisi na wakati mwingine kuondoka na wahalifu, au kuwapiga hadi kufa. Pamoja na kuwa Kambi ya Upinzani haikubaliani na hali hii ya jamii kujichukulia sheria mikononi lakini hii ni kielelezo cha wazi kuwa hali si shwari nchini kama tulivyozoea. Watanzania walio wengi takriban asilimia 18 hawana uhakika wa mlo wao wa siku. Baba na Mama Lishe kila kona ya nchi wananyanyasika kwa vyakula vyao kumwagwa kinyume na utaratibu, na au watu kubomolewa makazi yao bila utaratibu makini. Mahakamani na polisi, na hospitalini kuna taarifa za haki kununuliwa kama karanga kutokana na matendo ya rushwa yaliyokithiri. Matukio ya wanafunzi kugoma au kupiga waalimu na kufanya uharibifu kwa mali za shule yanazidi kuongozeka mambo ambayo tulikuwa tukiyasikia kwa nchi jirani. Haya yote kwa vyovyote hayafanyi hali ya Siasa kuwa shwari.
Kila kukicha matabaka yanazidi kujengeka au ya walio nazo na wasio nazo; watu wanazungumza zaidi na zaidi kwa misingi ya kikanda au ya kiudini. Hii si hali tuliyo zoea watanzania.

Mheshimiwa Spika, sikio la kufa huwa halisikii dawa. Serikali inaelekea kufanya mzaha na hali ya mpasuko wa kisiasa Zanzibar. Kidole kikiumwa mwili mzima huathirika. Mpasuko wa Zanzibar kwa vyovyote vile unaathari kubwa kwa jamii nzima ya Watanzania. Kwa Mhe. Rais kutokuchukua nafasi yake katika kutafuta suluhu ya kudumu kwa mpasuko wa Zanzibar ni kutokutaka kutambua hali halisi ya Siasa Zanzibar na athari yake kwa jamii yote. Kitendo cha kuachia mazungumzo kwa vikao 21 katika miezi 14 wakati Mabilioni ya fedha za Wananchi zimeteketea kwa vikao ambavyo CCM toka mwanzo haikuwa na nia ya kuvifikisha kwenye hatima kama inavyothibitishwa na hoja ya “ kura ya Maoni” kama ilivyowasilishwa kwenye NEC Butiama na hasa Kamati ya Mwafaka inapopeleka hoja kuwa kwa…. CCM “ imeipiku CUF..” ni jambo la kusikitikiwa na wote wenye uchungu na nchi hii.

9: Mheshimiwa Spika,
Moja ya malengo makuu kwa mwaka wa Fedha 2008/2009 ni pamoja na “Kuwezesha na kudumisha hali ya Utawala Bora wenye kuzingatia Demokrasia, usawa na Haki” . Waziri Mkuu ndiye msimamizi mkuu wa shughuli zote za Serikali na mratibu wa Wizara, Idara na vyombo vyote vya Serikali za Mitaa. Kambi ya Upinzani inadhani Ofisi ya Waziri Mkuu ina nafasi kubwa sana katika kusimamia, kuimarisha, kukemea na hata kurekebisha pale ambapo kuna dosari katika masuala yote ya Utawala Bora na Haki za binadamu katika nchi yetu. Mheshimiwa Spika, utawala bora ni pamoja namna yetu ya kutenda kazi na kutoa huduma. Siku hizi hata barua hazijibiwi na Wizara au idara mbalimbali za serikali idara mbalimbali. Kama wanajibu ni kwa kuchelewa sana na hii ni pamoja na kuwa na “Clients charter” na hata pale sheria zinapotoa muda maalum mathalan sheria ya uwekezaji. Utawala Bora na Haki za Binadamu zisipoheshimiwa na kusimamiwa kikamilifu yote tunayofanya yanapoteza maana, kwani maendeleo yote ni kwa ajili ya Binadamu. Hivyo basi Serikali itoe ufafanuzi katika maeneo yafuatayo:-

(i) Mauaji ya Maalbino na wazee ni baadhi ya mambo yanayoaibisha Tanzania katika karne hii ya Sayansi na Teknolojia. Hata hivyo cha kushangaza ni kuwa iwapo ndani ya Bunge lenyewe mjadala wa “uchawi’ ulishika kasi takriban kwa wiki nzima!hali ikoje huko nje? Mheshimiwa Spika, kumteua “mwakilishi” wa Maalbino Bungeni ni kitu kimoja na kuchukua hatua na au kusimamia kwa umakini sheria zinazolinda haki za binadamu ni kitu kingine. Kambi ya Upinzani inaamini Serikali haijasimamia kikamilifu sheria zilizoko kukomesha kabisa mauaji ya wazee na Albino. Inatisha kusoma Taarifa ya RPC, Mwanza, Zeloth Stephen kuwa katika miaka miwili iliyopita wazee 238 wameuawa kwa imani ya ‘kichawi’ (LHRC/2007 pg 21). Mauaji haya yako zaidi Mikoa ya Kagera, Shinyanga, Mara na Tabora. Kulikoni? Mhe. Waziri Mkuu ni vema akalieleza Bunge hili Tukufu ni mkakati gani wa dhati wa kutokomeza janga hili linaloendelea kumaliza maisha ya wananchi wetu!

(ii) Taarifa mbalimbali zinaonyesha kuna unyanyasaji unaotokana na maamuzi mabovu katika ngazi ya Halmashauri za miji, manispa na wilaya, kama vile utekelezaji usio na mpango wa kuwaondoa Wamachinga na Mama na Baba lishe ambayo imewasababishia upotevu wa mali, na kuwarudisha katika lindi kubwa la umasikini na upotevu wa mali pamoja na wengi kukosa kazi na hivyo familia zao kuathirika sana .


(iii) Unyanyasaji wa Wafugaji uliotokea Ihefu mwezi March, 2006 kwa kuwaondoa bila utaratibu wala mipango mathubuti, wananchi hawa kutoka bonde la Usangu/Ihefu wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya bado umeacha makovu mengi kwa wananchi wengi waliopoteza mali zao, mifugo, familia na kuumia kisaikolojia. Tume ya Rais, iliyotumia mamilioni ya fedha za Watanzania iliyoongozwa na Mhe. Jaji Chande hadi leo taarifa yake imewekwa makabatini, na wala Watanzania hawakujulishwa kilichojiri na wala hatua iliyochukuliwa kwa wale waliotekeleza vibaya agizo la Serikali. Mkuu wa Wilaya ya Mbarali peke yake anasemekana kuhusika na matumizi yasiyo na maelezo ya zaidi ya shs 1 Billioni. Kambi ya Upinzani inamtaka Mhe. Waziri Mkuu atoe Tamko la Serikali kuhusu Taarifa ya Tume/Kamati ya Rais iliyochunguza matukio ya Ihefu ili Watanzania waamini kuwa Serikali yao inawajali.


10: Mheshimiwa Spika,

Liko pia Suala la Adhabu ya Kifo (Death Penalty), bado halijafanyiwa kazi ya kutosha na Serikali yetu. Hadi mwaka 2007 nchi 133 duniani zilikuwa zimekwisha kufuta adhabu ya kifo, na nchi 64 ikiwemo Tanzania bado haijachukua hatua yeyote kufuta adhabu hiyo. Bunge hili lilijulishwa kuwa Serikali inakusanya bado maoni ya Watanzania. Kambi ya Upinzani inaitaka sasa Serikali kuliarifu Bunge hili sasa matokeo ya Utafiti huo. Sababu nilizotoa kufuta Adhabu hiyo katika Hotuba yangu ya mwaka jana bado ziko pale pale.

11: Mheshimiwa Spika,
Mwezi Decemba, 2008 tutakuwa tumekamilisha miaka mitatu kamili tangu Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani uliofanyika mwaka 2005. Mwaka kesho, 2009 tunaingia kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Kambi ya Upinzani inamtaka Waziri Mkuu kutoa ufafanuzi wa mambo yafuatayo:-
i) Nafasi nyingi katika Serikali za Mitaa zimeripotiwa kuwa Wazi na Wasimamizi wa uchaguzi ngazi hiyo, yaani Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri wamekuwa hawachukui hatua za kujaza nafasi zilizo wazi katika ngazi ya wenyeviti wa vijiji kama vile Kijiji cha Kambi ya Simba Wilayani Karatu, vijiji kadhaa vya Mpanda Kati, wenyeviti wa mitaa, na hata wajumbe wa Serikali, Kambi ya Upinzani inaitaka Ofisi ya Waziri Mkuu kuliarifu Bunge hadi leo ni nafasi ngapi kwa kila ngazi ziko wazi, na ziko wazi kwa muda gani hadi sasa. Je ni sababu zipi za msingi zimewafanya wasimamizi hao kutojaza nafasi hizo?

ii) Kuna Taarifa kuwa hata pale uchaguzi ulipofanyika, Wasimamizi kama vile Msimamizi wa kijiji cha Ido, Wilayani Mpwapwa, Pashungu Mbeya vijijini ambapo Upinzani ulipata viti 7 na 1 CCM. Lakini baada ya miezi minne Mkurugenzi akaenda kufuta matokeo, japo hana mamlaka ya kisheria.Vitongoji vya Nanjilinji A na Nanjilinji B Wenyeviti wa Vitongoji walifutwa na hadi leo nafasi zao ziko wazi. Kijiji cha Nakiu Serikali yote ya kijiji nayo imefutwa na hadi leo kijiji hakina uongozi uliochaguliwa. Mheshimiwa Spika Wakurugenzi wamekuwa wakifuta matokeo ya uchaguzi kinyume na utaratibu wa Sheria. Mahali pengine vijiji vya upinzani vimekuwa vikizuiliwa maendeleo yao kwa misingi ya kisiasa kama ilivyotokea Kijiji cha Gongali, wilayani Karatu, au Nanyanje Wilayani Lindi ambapo Shule ya Sekondari iliyokuwa imeanza watoto wamehamishwa kwa vile tuimejengwa katika eneo la upinzani. Ofisi ya Waziri Mkuu imechukua hatua gani kuzuia hali hiyo inayochafua misingi ya utawala bora na imewachukulia hatua gani Wakurugenzi hao wanaojichukulia sheria mikononi mwao? Kahama nako Serikali ya Kijiji cha Kakola imetafuta fedha zake, wamejenga Soko la kisasa. Mara baada ya kukamilika DC amefika na Polisi kuikabidhi kwa CCM, Wilaya kama mali ya CCM. Hivi ni vituko.

(i) Kwa vile Uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka 2009 hauko mbali tena, maandalizi yapi yanafanyika na wadau mbalimbali wameshirikishwa kwa kiasi gani ?
(ii) Kwa vile kuna maeneo mengi yenye utata kwenye Katiba, je Serikali inafikiria nini kuhusu kuanzisha mchakato wa Kufanyia Katiba yetu marekebisho makubwa kwa kushirikisha wadau wote, hasa ikizingatiwa kuwa ni jambo la kawaida siku hizi kusikia hata Idara za Serikali zikilalamikia mapungufu ya Katiba, mathalan CAG.

Mhe. Spika, Tanzania waliweka saini Azimio la AU kuhusu Wanawake kuwa Asilimia 50 katika nafasi za maamuzi na uongozi. Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kuliarifu Bunge lako Tukufu hatua iliyofikiwa katika maandalizi ya Bunge letu kufikia 50/50 katika Uchaguzi Mkuu wa 2010? Wadau wameshirikishwa kwa kiasi gani katika maandalizi hayo?

12: Mheshimiwa Spika,
Kwa vile Kambi ya Upinzani imeufanya mjadala wa kuhamisha Makao Makuu Dodoma ni mjadala wa kila mwaka, Kambi ya Upinzani inataka kujua mwaka huu pia, ni hatua zipi mahususi zimefanya kuhamishia Makao Makuu Dodoma. Je kwa hatua hiyo, Serikali itakuwa imefikia asilimia ngapi ya malengo ya Kuhamisha Makao Makuu?

13: Mheshimiwa Spika,
Serikali za Mitaa ni vyombo muhimu sana katika uongozi wa nchi kwa vile vyombo hivi viko karibu na watu na ndiyo ngazi inayokutana na wananchi kuliko ngazi nyingine zote. Katika hotuba yangu ya mwaka jana nilizungumzia mambo mengi ikiwa ni kuhusu namna ya kuimarisha vyombo hivi. Ninaomba nirudie tena machache mwaka huu, kwa lengo la kutoa mchango wa Kambi ya Upinzani katika kujenga Serikali imara za Mitaa na hivyo kujenga Demokrasia ya kweli nchini mwetu. Mambo haya ni kama yafuatayo:-
a. Mhe. Spika, kama tulivyosema, Wenyeviti wa vitongoji, wenyeviti wa Vijiji, Madiwani na viongozi ambao mchana kutwa na usiku kucha wako kazini kusimamia programu zote zinazobuniwa na Serikali Kuu na Halmashauri. Bado wanatakiwa kubuni mipango na miradi inayohusiana na maeneo yao. Hawa ndio walinzi wa amani na usalama katika maeneo yao. Ni dhahiri basi, hawa ni viongozi muhimu sana katika nchi yetu.
b. Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kubuni ‘mpango maalum’ wa kuwawezesha viongozi hawa kujengewa uwezo ili waweze kusimamia vizuri zaidi rasilimali nyingi zilizopelekwa chini na Serikali kuu kupitia Programu hizi za kitaifa. Si mara nyingi kusikia viongozi hawa wakienda Semina, Warsha au kongamano, lakini sisi viongozi wa juu kila wakati tuko kwenye Semina, kuanzia Mawaziri, Makatibu wakuu na Wabunge. Ni vema sasa tukapunguza Semina katika ngazi ya juu na tukazielekeza chini.
c. Wenyeviti wa Vitongoji, vijiji, na Madiwani wawekewe mpango mzuri wa kuwapatia kipato cha uhakika, angalau kwa kiwango cha kima cha chini cha Mshahara Serikalini. Haiwezekani mtu anayesimamia fedha na rasilimali nyingi kama zinavyopelekwa fedha za Program zilizotajwa na yeye maisha yake yawe ya kubangaiza. Ni lini Matokeo ya Kamati ya Mhe. Lubeleje,(mb) wa Mpwapwa iliyokuwa inaandaa mapendekezo ya maboresho ya maslahi ya Madiwani itatangazwa rasmi?
d. Mhe.Spika, siku za karibuni magazeti mengi yameripoti ubadhirifu unaofanywa katika ngazi za Vijiji. Yote haya kimsingi ni kwa sababu nafasi za vishawishi zimekuwa nyingi zaidi, tofauti na huko nyuma ambapo programu zilikuwa zinatekelezwa na kusimamiwa na ngazi za wilaya. Vijiji viko chini ya 13,000 kata ziko kama 2,500. Tukiwa na nia hatutashindwa kuwalipa angalau mshahara wa kima cha chini viongozi hawa ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu.
e. Tukisimamia vizuri fedha nyingi kama zinavyoainishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu kila mwaka, na kubuni vianzio vipya kama vilivyoonyeshwa na Waziri Kivuli wa Fedha, Kambi ya Upinzani inaamini kabisa kuwa tutapata fedha za kutosha kuwalipa hawa viongozi wetu kwa kuanzia bila hata kwenda kuomba fedha kwa mfadhili. Wafadhili wakitusaidia itakuwa ni nyongeza. Mhe. Spika, dhamira na uzalendo ndicho kitu kinachotakiwa.
f. Watendaji wa Kata ambao ni waratibu wakubwa wa maendeleo, wanaosimamia ‘Amani’ katika maeneo yao, wanamsaidia Mkurugenzi wa Wilaya (DED) katika utekelezaji wa majukumu yake. Hawa, wanahitaji vyombo vya uhakika vya usafiri mathalan pikipiki. Ni vema Serikali ikabuni mpango wa kudumu (sustainable programme) wa kuwasaidia Watendaji hawa kupata vifaa hivi, hata kama ni kwa kuwakopesha kama tunavyofanya kwa Wabunge na kukata kwenye mishahara yao. Kimsingi hawa ndio wanaofanya kazi nyingi zaidi kuliko hata Makatibu Tarafa ambao tumewapatia pikipiki tayari. WEO wako karibu zaidi na maeneo ya kazi, na Makatibu tarafa wana umuhimu wa uratibu tu. Uratibu hauna tija iwapo mzalishaji hana tija.
g. Serikali itazame upya sheria na 7 na 8 ya Mwaka 1982 na kuweka wazi zaidi majukumu ya Wakuu wa Wilaya, kama kufuta nafasi hizo zimeshindikana, ili kuleta tija zaidi kati ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Wilaya (DED) ambaye ndiye mwenye Wataalam na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ambaye kimsingi ina viongozi wakuu wasiozidi watatu. Sheria zinazoongoza Serikali za Mitaa pamoja na Sheria ya Regional Administration inayounda Ofisi ya Mkuu wa Mkoa zirekebishwe haraka sana kuendana na mabadiliko makubwa yanayotokea sasa na kwa kuzingatia Mpango wa Maboresho.
h. Mhe. Spika, Mapendekezo ya Wadau kwa siku nyingi ni kuwa ili uchaguzi katika ngazi ya Vijiji, vitongoji na mitaa uonekane na utendeke kwa haki na huru, ni kurudishwa chini ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi na utumie pia Daftari la Kudumu katika kujiandikisha badala ya kuwa na utaratibu wa sasa ambao unaruhusu udanganyifu mkubwa.
Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani inataka kufahamu kwa kina kauli ya Serikali juu ya mapendekezo haya.

14:: Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani inatoa rai kuwa ili tufanikiwe katika mipango yetu ya maendeleo yetu, ni lazima tuondokane na dhana ya itikadi katika masuala yanayogusa maslahi na ustawi wa Taifa. Maendeleo Mhe. Spika hayajui itikadi.
15:Mheshimiwa Spika,
Barabara ni barabara tu haijali chama na watu wa vyama vyote wanapita. Maji hayana sura, na wananchi hawatajali chama bali wataangalia nani kawaongoza kupata maji. Hivyo, Ofisi ya Waziri Mkuu, ambayo ndiyo Mratibu wa Vyama vya Siasa, ni vyema ikaandaa utaratibu wa kujenga imani kwa Watanzania kufanya kazi pamoja bila ya kuangalia itikadi za kisiasa. Utamaduni wa amani na mshikamano hujengwa hauji tu kwa miujiza.
16:Mheshimiwa Spika,
Ni imani yetu, kuwa Waziri Mkuu atakuwa kiungo kati ya Serikali na Vyama kama malengo ya Ofisi yake yanavyoeleza, na atapanga mapema iwezekanavyo kukutana na vyama vya Siasa ili kubadilishana mawazo na viongozi wa Vyama mbalimbali vya siasa



17: Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani inapenda kupata Taarifa na majibu ya kina kuhusu hoja hizi. Mwenyezi Mungu atupe busara zake kama tunavyoomba kwenye Dua kila siku asubuhi. Naomba nikushukuru tena kwa kunipa fursa hii, na pia nawashukuru waheshimiwa Wabunge wenzangu kwa kunisikiliza.

Mheshimiwa Spika, Nawasilisha.

…………………………………………………
Dr. Willibrod Peter Slaa (MB),
Jimbo la Karatu,
MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI-
OFISI YA WAZIRI MKUU/TAMISEMI.
23 June, 2008, Dodoma.
 
MUNGU akubariki na kukulinda Dr Slaa dhidi ya mafisadi na wahujumu wa taifa letu. Asante kwa kufungua macho watanzania kwa mara nyingine tena.
 
Mpita Njia, asante kwa bandiko hili zuri na lililokwenda shule!!!! Nimeisoma hotuba hii kwa makini na kuitafakari aya baada ya aya. Hii kweli ni presentaion nzuri ambayo naamini imegusa mambo yote yanayotuudhi sisi wapenda nchi yetu. Yetu masikio na macho kumsikiliza Waziri Mkuu atavyojibu hoja hotuba hii. Hongera Dr. Slaa, Mwenyezi Mungu azidi kukupa afya njema na upeo mkubwa. Twamuomba Mwenyezi Mungu ampe ujasiri Waziri Mkuu Pinda kuweza kujibu hoja baada ya hoja kwa kuzingatia ukweli wa mambo bila kuwalinda mafisadi na wahavidhina. Mungu Libariki Bunge Letu, Mungu Ibariki Tanzania.
 
Mimi naloweza kusema ni kuwa nimemvulia kofia ndume huyu! The truth must be said however painful it is. Mpita njia tunashukuru sana kwa thread hii!
 
tunakuombea mungu akulinde, tuko pamoja.
Hopefully sikio lakufa safari hii litasikia dawa.
Yetu macho
 
Mkuu hii ngoma imetulia ngoja nile nishibe niipitie kwa makini. ila tujitahidi kuwatafuta wakina Slaa wengine kama huyu.
 
Mpita njia, Njia zako moto. Asante sana. Dr. Slaa tuko pamoja katika harakati za kupambana na Mafisadi na kulikomboa taifa.
 
Asanteni Dr. Slaa, hili ni somo la kutosha. nafikiri Serikali itaacha kujiuma uma na kutoa majibu na kuwafikisha wanaohusika katika vyombo vya sheria hili haki itendeke.
 
Kweli dr kamkoma Nyani kisawasawa, hivi ndivyo inavyotakiwa, lakini wakati huo huo
inabidi wapinzani wajiandae vyema, uchaguzi wa serikali za mitaa ndo huo unakuja, na uchaguzi mkuu pia, inabidi waweke stratergy kali ili waongezeke bungeni
 
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani imetishwa zaidi na Taarifa iliyosambaa katika Mtandao inayoonyesha kuwa Taarifa hizo za Kamati ya Rais, ambayo ni Siri kubwa kwa Wabunge na kwa Watanzania tayari inajulikana na watu wa nje wakiwemo wawekezaji. Kambi ya Upinzani imefadhaishwa sana na Taarifa aliyotoa CEO wa Kampuni ya Tanzanian Royalty Exploration Corporation bwana James E. Sinclair Mwenyekiti na CEO, ya Tarehe 30 May, 2008 yenye kichwa cha habari “changes To Tanzanian Mining Law Certain to benefit Mineral Exploration” na pia ya tarehe 11 June, 2008 yenye kichwa cha Habari “ A special note to Shareholders”. Taarifa ya Bwana Sinclair ya 30 May, 2008 inatamka wazi kuwa “ I have had the privilege of reviewing the Committees Recommendations-along with comments from the Chamber of Mines –and have no serious issues with them…What is important to know, however is that the man who will make the final decision on the recommendation is the President not the Committee…” na “As one might expect, any legislation involving such an important segment …has generated heated debate. In my opinion, a small percentage of this rhetoric is instigated by special interest groups in the west whose commentary reads like … a standard play book”.
Mhe Spika, Kambi ya Upinzani inadhani haya ni madharau makubwa kwa Watanzania, matusi kwa Wabunge, na pia inajenga picha kuwa Wabunge wanaopiga “kelele” kuhusu mali na rasilimali zao sio watu wanaoweza kufikiri wenyewe bali “wanatumika” …… Matusi haya hayawezi kuvumilika hivyo basi, tunamtaka Bwana Sinclair aombe Radhi kwa Bunge hili na watanzania wote kwa ujumla. Mheshimiwa Spika, kiburi hiki amekipata baada ya Bunge lako Tukufu kudharauliwa kwa kunyimwa Taarifa muhimu kama hii. Hivyo Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kuacha mara moja tabia ya kuthamini vyombo na watu wa nje.
 
Kuna mswada ulipita mwaka jana au juzi wa kufuta hati chafu za CAG, kwa mihadi kwamba zitafuatiliwa, lakini sijaona Mzee wetu akiziulizia, maendeleao yake.
Mambo mengine kweli yametulia. Tumsubiri Pinda na majibu ya serekali.
 
hivi hili bunge litaisha kweli kabla hatujampata hata fisadi mmoja?
 
Kuna mswada ulipita mwaka jana au juzi wa kufuta hati chafu za CAG, kwa mihadi kwamba zitafuatiliwa, lakini sijaona Mzee wetu akiziulizia, maendeleao yake.
Mambo mengine kweli yametulia. Tumsubiri Pinda na majibu ya serekali.

Mkuu kwa somo hili sidhani kama Waziri mkuu ana cha kujibu maswali ni mazito mno yanayohitaji kamati za bunge si chini ya kumi. Mimi nafikiri tungeitisha uchaguzi upya.
 
Back
Top Bottom