Mchango wa DR.Slaa -Bungeni juzi.
MHE. DR. WILBROD P. SLAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, niungane na wenzangu kuchangia bajeti hii. Nianze kwanza kwa kusema kwamba nimeshtushwa sana na maandalizi ya bajeti ya mwaka huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bahati mbaya, Watanzania wengi na tukiwemo baadhi yetu sisi Wabunge, tunafikiria bajeti ni hotuba ya Waziri. Bajeti ni vitabu vinne, hotuba ya Waziri, ni ufafanuzi tu wa maeneo. Vitabu vinne visipooana hasa mapato na matumizi, bajeti ile haipo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania wengi wakiwemo hata wa barabarani, Waandishi wa Habari labda hawajatusaidia sana hapa, baada ya kusikia hotuba ya Waziri, hawajaona takwimu, hawajaona vitabu, wanaisifu bajeti lakini kumbe ni sawa na mtu asiyejua barua iliyowekwa ndani ya bahasha ina nini kumbe imeandikwa unaenda kunyongwa, ndivyo Watanzania tulivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nianze kuchangia kama ifuatavyo:-
Kwanza sina sababu ya kurudia tofauti ambayo iko kwenye vitabu hivi hasa Kitabu cha Mapato, Kitabu cha Kwanza, tofauti katika ujumla wake imeorodheshwa na Mheshimiwa Zitto na Mheshimiwa Cheyo, mimi sitarudia eneo hilo, ni zaidi ya bilioni karibu 120, kama hesabu yangu ni sahihi, nikikosea, Waziri aniambie baadaye.
Mheshimiwa Naibu Spika, nasahihishwa, naambiwa wala siyo 120 ni 136 bilioni. Tofauti ya zaidi ya bilioni 130, ni hesabu kubwa mno.
Waheshimiwa Wabunge, kazi tunayofanya ni kazi ya Kikatiba, Ibara 63(3)(c) inasema:-
Kujadili na kuidhinisha mpango wowote wa muda mrefu na wa muda mfupi unaokusudiwa kutekelezwa katika Jamhuri ya Muungano, na kutunga Sheria ya kusimamia utekelezaji wa mpango huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi hiyo ya kutunga Sheria, tunaikamilisha kwa kupitisha Finance Bill siku za mwisho. Ndiyo maana kuna Finance Bill na Appropriation Bill. Kwa utaratibu huo, kazi tunayofanya, ni kazi ya kutunga Sheria, ni kazi ya Kikatiba, siyo ya ushabiki wala ya kuona tu kwamba hapa tunaweza kuisifia. Tusifie tunachokijua, tulichokisoma, tulichokiona na kilicho sahihi chenye maslahi kwa Watanzania wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tofauti ya bilioni 130, haikubaliki popote kwamba haiko kwenye vitabu. Naomba kwa hilo, nitangaze siungi mkono bajeti hii na Waziri akitaka ana njia moja tu, kwenda kurekebisha hivi vitabu na siku ya kupiga kura, hivi vitabu ambavyo ndiyo tunavipitisha viwe vimerekebishwa na viletwe Bungeni tuweze kuvipigia kura. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, nimeangalia vile vile kwenye Finance Bill, nimekuta kuna upungufu mwingi. Waheshimiwa Wabunge, tusipokuwa waangalifu, kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu, tunaweza tukacheza mchezo mbaya sana. Huu ni mchezo wa hatari hasa Wabunge tukiwa na ushabiki tu kwa kupongeza hotuba badala ya kuangalia vitu vilivyoko ndani ya bajeti. Sitaki kwenda zaidi ya hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, unapokuta kwenye bajeti unaletewa kwenye Finance Bill maeneo karibu matano, sita yanasema the Minister may determine hapo tuko kwenye hali ya hatari sana katika nchi hii. Imefika mahali Bunge linaacha kazi ya kupitisha bajeti, linampa sasa Waziri, ukisema the Minister may determine kiwango atakachochukua EWURA, maana yake Waziri ataenda kuchukua kile kiwango, lakini EWURA nao watapitisha kwa watumiaji wa maji au kwa wasafirishaji kwenye nauli au sijui kwenye kitu gani. Huu ndio utaratibu wa kodi. Kodi hailipwi na yule anayeitoa, yule anaitoa ni chombo cha Serikali cha kuweza kukusanyia kodi mlipa kodi ni mtumia huduma. Sasa mtumia huduma wa EWURA, mtumia huduma wa Civil Aviation, wa Port Authority, wale wote ni watumiaji Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa maana nyingine tumefanya double taxation bila kuelewa yaani tumemlipisha Mtanzania kodi mara mbili, actually mara tatu. Ile anayolipa ya indirect kwenye huduma mbalimbali kama soda, bia na kadhalika na nguo ya pili ni ile ambayo anadaiwa alipe kwa Regulatory Authority, ile mamlaka yenyewe na ya tatu ile ambayo inachukuliwa sasa kwa mamlaka ambayo na yenyewe itaihamisha baadaye. Hii ni hali ya hatari sana Wabunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda Wabunge tuelewe kabisa kwamba maamuzi yetu yanaweza kuwa kitanzi kwa Watanzania. Bunge linaweza kuwa kitanzi kwa Watanzania tusipokuwa makini na tusipokemea matendo ya aina hii. Sasa Waziri atuambie anaposema anaenda ku-determine, sisi katika Bunge hili kwenye Finance Bill tunapitisha nini? Tunapitisha ku-determine? Tunapitisha viwango vilivyokubalika au tunapitisha
MHE. DR. WILBROD P. SLAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakubali lakini unapounganisha vitabu vinne, huwezi kujadili kitu kimoja kwa sababu ni saa hizi ndiyo wanaenda kufanyia kazi. Kwa uzoefu wetu, Finance Bill inajadiliwa kwa nusu saa. Kwa hiyo, sibishani na wewe, nakubali hilo lakini ukweli ni kwamba ni lazima tuangalie mtiririko katika yote kwa sababu yaliyoko kwenye Finance Bill ndiyo yaliyoko kwenye kitabu cha kwanza, kitabu cha pili na kitabu cha tatu. Sasa huwezi kuacha kujadili kwa sababu tu tutajadili mwishoni, mtiririko unaweza kuwa mgumu na yale yote ninayoyasema yako katika kitabu cha kwanza, yamekuwa reflected humo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani niseme tu jambo lingine la mwisho katika hilo. Nimeshtushwa sana na kipengele kimoja hapa. Juzi Waziri alijibu ndani ya Bunge hili kuhusu kodi inayotozwa kampuni moja kule Kilimanjaro Airport kwamba inalipa nini? Sasa ninashangaa hii kampuni inatulipa hela kidogo sana. Nadhani Waziri alisema haizidi milioni tatu. Leo naishangaa kampuni hii tunaenda kuikopa sisi Serikali, hivi unapokopa kampuni ambayo inakulipa kidogo sana halafu wewe unatakiwa kuisimamia, hivi utawezaje kuisimamia hiyo kampuni? Mimi mantiki ya aina hii, nimeshindwa kuielewa, nitaomba Waziri anithibitishie baadaye maana yake ni nini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la mwisho, vitabu vyenyewe pia vina vitu ambavyo havieleweki. Hivi ukituambia Mheshimiwa Waziri Tanzania Harbours Corporation, ni kitu gani katika Tanzania ya leo? Iko kwa Sheria ipi? Ukiniambia kwamba kuna Tanzania Harbours, ipo kwa Sheria ipi? Hivi ni kweli Serikali haijui vyombo vyake? Tukifikia hapa tumefika wapi katika nchi hii?
Mheshimiwa Naibu Spika, namalizia, hayo yako mengi, yasinichukulie muda bure, kwa sababu nataka kusema mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini maana yake ni kwamba vitabu hivi vinatakiwa vitupwe na tena haraka iwezekanavyo, tupate vingine, tuwe na muda wa kusoma vitabu hivi ili tupitishe bajeti.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme mambo mawili tena. La kwanza, bajeti ni lazima imguse mwananchi wa kawaida. Kwa bahati mbaya, kwenye vitabu hivi, mwaka huu na hata kwenye hotuba ya Waziri, amefumbafumba, hotuba haionekani hasa mapato, jumla yake yote ni wapi na kutoka kwenye kifungu kipi?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tumeshtushwa, tukirudi kwenye vitabu hivi, unapokuta sukari inakuja kuwekewa VAT maana yake ni kwamba, mwananchi ambaye tayari saa hizi amezidiwa, unamwondoa kwenye listi ya watu watakaokunywa chai Tanzania. Kwa hiyo, tujue kwa bajeti hii, tumepunguza wanywa chai, hii ndiyo maana yake hapa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapokuta kwamba katika hali ya sasa pembejeo, japo hatukuiongezea kodi lakini kodi za nyuma zilikuwepo na kwa bajeti hii, hatujaifanyia adjustment na mbolea leo ni shilingi 75,000 kule Kusini, shilingi 50,000 kule kwangu Karatu, maana yake ni kwamba mwananchi wa kawaida hawezi kutumia mbolea. Kwa hiyo, bajeti haija-reflect, tumekwenda kugusa maeneo ya kodi madogo sana. Motopoa ni kitu gani kwa Mtanzania wa kijijini, hivi anaielewa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukisema unaondoa kodi kwenye magunia, kiwanda chenyewe sijui kiko wapi, sijui kama kiko hai, cha Moshi kimefungwa siku nyingi. Hivi effect yake kwa mwananchi wa kawaida iko wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, Mtanzania alitegemea kwenye bajeti hii, bei ya cement itashuka, bei ya bati itashuka, lakini kwa jinsi ilivyo, kwa kuwa umepandisha vitu vingine, kwa mfano magari ya CC5000, maana yake bei ya vitu hivyo nayo itapanda. Kwa sababu magari ya CC5000, ni malori na mabasi, ukishayagusa hayo, umegusa nauli, utagusa vitu vyote ambavyo vinaendana navyo na vyenyewe vitapandisha bei ya vitu vingine vyote. Kwa hiyo, nilidhani hapa tuna wajibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kilichonishtua katika ukurasa wa 86, Vote 50, nimeona kodi moja ambayo ni ya ajabu na ninaomba Waziri baadaye anisaidie. Tunapotoza kodi kwa mfano kwenye magari, kwenye kipengele kidogo cha 050903, Motor Vehicle Registration Fee, halafu pale chini unarudi tena unasema Motor Vehicle Number Plate, hivi uli-register nini kama hakuna number plate kwenye hiyo gari? Una-register nini kama siyo number plate? Sasa unapokuja kufanya hivyo maana yake ni nini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika nchi zote ninazozifahamu, ukiacha hii ya kwetu, number plate inakuwa control measure, haiwi ni revenue measure, sisi tunageuza kuwa revenue measure. Hili ni jambo ambalo linaongeza gharama bila sababu na tunafikiri haya magari ni ya watu wakubwa, anayepanda taxi siyo mtu mkubwa. Kule vijijini, wala tusifikirie msongamano wa Dar es Salaam kwamba tunaweka hii ili tupunguze msongamano wa magari kule Dar es Salaam, inaweza, lakini kwenye miji yote siku hizi Watanzania wanatumia kama usafiri, kama ambulance kupeleka mgonjwa hospitali kwa sababu magari madogo (taxi) zimejaa kwenye miji yote, nani hajui hili? Anayepanda ni yule mtu wa kawaida. Kwa hiyo, ukiongeza hizi maana yake unamwongezea nauli na taxi sasa hivi hazipandiki tena, nadhani wote tunafahamu hiyo. Kwa hiyo, tunaongeza gharama bila sababu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kuwa muda si mrefu, nina mambo mawili madogo. La kwanza, nimempelekea Mheshimiwa Waziri hoja zangu nyingine kwa madokezo madogo madogo kwa utaratibu wa kawaida wa Bunge zaidi ya matatu au manne. Nitapenda nipate ufanunuzi wa kina wa masuala hayo. Mengine mwisho wa yote, nadhani ninaweza nikaomba kuunda Kamati Teule ya Bunge tena kama sitapata majibu, sasa namwachia hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ningependa nipate ufafanuzi katika maeneo ya ubadhirifu hasa TANGOLD na MEREMETA. Ninaomba kitu kimoja kikubwa hapa. Tunafahamu sasa na tuna kumbukumbu, tuna nyaraka za Serikali kwamba TANGOLD na MEREMETA zote mbili zimeandikishwa nje ya nchi kama makampuni ya kigeni. TANGOLD imeandikishwa Mauritius nyingine imeandikishwa Uingereza na nimeomba details huko kwako. Naomba zile details zijibiwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa hapa ninachoomba, ninahitaji kujua accounts zao za nje zinakaguliwa na nani? Tungependa kupata hizo fedha tangu walipoanza mpaka leo walipofunga kama ni MEREMETA na kama ni TANGOLD najua bado ipo, kwa hiyo tungependa kujua wanakaguliwa na nani na kwa nini hizi hela hazionekani na kwa nini kwa mfano account ya TANGOLD iliyoko Dar es Salaam ambayo iko hapa hapa nchini kwetu haikuwa imekaguliwa labda kama imekaguliwa, ni mwaka huu kwa mara ya kwanza. Kwa nini miaka yote haijakaguliwa na sasa ina fedha kiasi gani lakini kwa nini haikuwa inakaguliwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho nimempelekea Mheshimiwa Waziri. Vile vile tumeipongeza TRA na mimi naipongeza lakini Kambi ya Upinzani tulisema kuna unyanyasaji, nimempelekea ushahidi wa aina ya unyanyasaji uliokuwa umetokea. Hatujui ni wangapi wamenyanyaswa kwa kiwango hiki. Haiwezekani kampuni ya Kitanzania tunayotakiwa kui-promote tunainyanyasa halafu tunasema hakuna rushwa, wakati mwingine inaweza kuleta mashaka kumbe mapato, makusanyo yanaongezeka. Kwa matukio ya aina hii, nitapenda nipate maelezo ya kina kuhusu suala la aina hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili nisigongewe kengele kwa kuwa mimi ni wa mwisho, naomba kurudia kusema kwamba mimi sitaunga mkono hoja hii ya bejeti na ninaomba Waziri anipe taarifa ya kina ni kwa nini vitabu hivi vinatofautiana. Kama atakubaliana, aende kutengeneza vingine ili budget debate iende vizuri kwa sababu Wabunge tunatakiwa kuwa na information sahihi ili tunapopitisha tuwe tunapitisha kitu ambacho tuna uhakika nacho.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. (Makofi)