SoC01 Kushuka kwa kiwango cha Elimu nchini na hatua za kuchukua

Stories of Change - 2021 Competition
Dec 10, 2020
15
14
Katika maendeleo ya jamii elimu ni nguzo muhimu sana, thamani ya elimu ni kubwa mno kiasi kwamba mtu hawezi akajua thamani ya elimu papo hapo.

Waliofanikiwa na wakapata mafanikio kama ajira wanajivunia thamani ya elimu na wale baadhi ambao bado wanahangaika mitaani baadhi yao hao hawaoni mwanga wowote wa elimu kukomboa maisha yao na hii wanachukulia kuwa pengine elimu imepoteza muda wao mwingi na wanatamani bora wangetumia muda huo waliokuwa masomoni kutafuta chochote kitu Kwa ajili ya maisha yao ya leo lakini je, ni kweli elimu haina manufaa, jibu tunaloweza kupata ni hapana isipokuwa labda tuzishushie lawama kidogo mamlaka za elimu.

Elimu ya wahitimu wa fani mbalimbali hasa fani ya ualimu ndiyo changamoto kubwa sana ambayo kama utapita katika wahitimu watano au sita wa fani hii basi watatu au wanne ambao bado hawajaariwa wanaweza kukwambia kuwa hamna maana ya elimu ile, imefikia hadi kuna wengine wanasema ambao wameacha shule wengi wamefanikiwa kimaisha je, bora aliyeacha? Japo si kila aliyesoma hajafanikiwa lakini kwa nini kunakuwa hivi? Kama tulivyosema awali kuwa labda tuilamu mamlaka kidogo. Na pia tujiulize kwa nini lawama iende Kwa mamlaka? Majibu ni haya.

Kwanza kabisa lawama zinaenda Kwa mamlaka za elimu Kwa sababu ya kutokuweka malengo thabiti ya uhitaji na kwa muda upi, hapa ndipo tunapata chanzo cha lawama zote. Lawama zinaenda kwao kwa sababu ya msingi kuwa katika ngazi ya maendeleo kuna sera, mipango na miradi mbalimbali. Kimsingi mamlaka ya elimu tuseme wizara ya elimu ndiyo yenye kubeba lawama.

Katika kutetea pointi hii nitatumia mfano wa mwalimu mmoja ambaye nikiwa kidato cha sita nikiwa na wenzangu tulikuwa tukifanya kitu kinachoitwa project yaani mradi na sisi tulijikita katika kuangalia ubora wa elimu na tulipita shule tatu shule mbili zikiwa za msingi na shule moja ikiwa ya sekondari, nakumbuka moja ya changamoto ambayo mwalimu wa shule moja ya msingi ambaye tunaweza kusema alitoa madini mengi kwetu ni pale alipotaja kuwa moja ya changamoto kubwa ya elimu ni kukosa shabaha. Kwa maelezo ya mwalimu huyu mahili kabisa ambaye umri wake ulionekana kusogea kama si kati ya miaka 49 basi hamsini na hivi alieleza kusikitishwa kwake Kwa elimu yetu kukosa shabaha.

Mwalimu yule aliweza kuona kuwa moja ya mambo ambayo yanachangia elimu kuwa mbovu ni kutokana na kutokuwa na malengo thabiti ya nini kinatarajiwa hasa ambacho kinaweza kumwezesha kijana wa kitanzania kuweza kujiandaa na kuweza kuyakabili mazingira yake.

Moja ya msistizo wake ulikuwa ni hii elimu inayoendeshwa kinadharia kuweza kuondoshwa na kufutiliwa mbali. kwa kusisitiza zaidi aliweza kutolea mfano kwa kujikita katika historia ya elimu ya Tanzania kuanzia kipindi cha baada ya ukoloni yaani kuanzia mwaka 1961 na kuendelea mpaka mwaka huo ambao ulikuwa ni mwaka 2016.

Moja ya vitu ambavyo yeye aliona kuwa na athari chanya ni kile alichokiona katika kipindi cha baada ya Azimio la Arusha ambapo azimio hilo lilikuja na falsafa kombozi ya elimu iliyojulikana kama Elimu ya Kujitegemea (Education for Self Reliance) alisisitiza hakika mtaala wa elimu ile ulikuwa ni mtaala haswa wenye ujenzi ambapo, vijana walioko shuleni walifundishwa nadharia na baada ya nadharia walienda katika vitendo yaani kazi mbalimbali kama kilimo na kweli vijana walitoka wakimaliza darasa la saba tu tayari wangeweza kufanya kazi na kujipatia kipato na kuendeleza maendeleo ya jamii na taifa Kwa ujumla. Lawama yake ilienda moja kwa moja na kusema iko wapi elimu hii? Na Elimu Kazi au EK iko wapi na msistizo mbona nadharia imetawala? naam shabaha, shabaha ya elimu ya sasa si nzuri.

Kwa kuendelea, ni ukweli unaoumiza kuwa shabaha ya elimu ya sasa ndiyo changamoto kubwa sana, hasa tukiangalia kwa kutumia mwongozo wa takwimu katika kuleta maendeleo ya elimu, hapa turudi katika elimu ya vyuo hasa vyuo vikuu, je, idadi ya wahitimu iliyopo na ukilinganisha nafasi za ajira na uhitaji iliangaziwa na mamlaka kwa kutumia takwimu, sera na mipango?

Mtu anaweza kujibu ndiyo, walitumia sera zilizokuwepo ama zipo na mipango iliyopo lakini swali je ni kweli kama zilitumika sera hizo na mipango hiyo ilikuwa nzuri au ni mizuri? jibu litakuja kusema bado haikuwa na haikuandaliwa katika mazingira yanayokidhi kuleta mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kujiajiri na kuajiriwa kwa wahitimu.

Sababu kubwa ni kuwa hakuna shabaha ya kitakwimu inayotumika vizuri na kipimo cha makadirio ya muda mrefu ili kuweza kuleta kitu fulani na badala yake matokeo yamekuwa mabaya kutokana na kuweka mipango, sera na miradi inayokidhi mahitaji ya serikali ya awamu fulani bila kujali maslahi mapana, yaliyojikita katika tafiti na muda mrefu.

Kutokana na kuwepo kwa takwimu za sensa za watu na makazi inaonekana bado hazijatumika vizuri kuweza kukabili changamoto za kujiajiri na kuajiriwa ukijumlisha na kukosa shabaha ndiyo maana utakuta kuna kutofautiana kwa matamko ya viongozi, wengine wanasema jiajirini na mwingine anasema tunaajiri na mwingine anasema tunatengeneza ajira.

Hii inaonesha kabisa kuwa kukosekana kwa msingi bora wa namna ya kuangazia mambo kwa takwimu tafiti na sera nzuri za muda mrefu ndiyo maana kumetawala matamko ya viongozi na kikawaida nchi haiwezi kuishi katika matamko ya kila siku na ukizingatia si kila wakati kiongozi huyo huyo atakuwepo.

Labda tutolee mfano mmoja ili kueleweka zaidi katika kukosekana kwa shabaha nzuri katika elimu, kuna wahitimu wengi sana wa taaluma ya ualimu wa shahada, astashahada, na cheti, wakati huo huo kuna bodi ya vyuo vikuu mfano TCU yaani Tanzania Commission for Universities na kuna NACTE na pia Wizara ya Elimu, bado hapo hapo idadi ya shule zilizopo binafsi na serikali ipo, na hata uhitaji nadhani unajulikana kuwa wapi panahitajika walimu wangapi na pia kuna nafasi za kila mwaka katika udahili wa wanafunzi ukijumlisha na mikakati, mipango, na miradi mbalimbali ya elimu ya mbeleeni bado utakuta kuna takwimu ambazo zingesaidia kuwa kwa kipindi hiki tunadahili idadi fulani na kufikia kipindi fulani tutakuwa na uhitaji fulani na hii idadi itakuja kuingizwa moja kwa moja kwenye ajira kwa muda fulani na ili isije ikaleta usumbufu basi ziada yake itakuwa kiasi ambacho wahitimu wanaweza kuajiriwa na serikali na ama sekta binafsi.

Kwa hali iliyopo sasa ni kwamba vitu havifanyiki hivyo, kwani kuna mrundikano wa wahitimu ambao hadi imekuwa tatizo na viongozi wanataka kulijibu haraka haraka kwa kusema mjiajiri. Je waliandaliwa mazingira ya kuweza kujiajiri? Ikumbukwe kuwa yule aliyesomea taaluma ya ualimu alitaka aje kufanya kazi ya ualimu na hivyo hawezi kujiajiri tena kama mwalimu maana hana shule yake hivyo huenda asingesomea fani hiyo kama kungekuwa na mpaka wa udahili kutokana na mahitaji.

Kiufupi shabaha haipo tu. Kwani kama kungekuwa na shabaha hata idadi ya wahitimu ingekuwa inafiti idadi ya uhitaji wa muda fulani na wale wengine wangesomea taaluma ambazo nazo zingekuwa zimewekewa shabaha ya ama hapa kuna hawa wataajiriwa na hapa hawa watasomea kitu hiki na wanaweza kujiajiri popote na hiyo isingeleta tatizo lolote.

Hakika, maelezo ni baguzi haitawezekana kuandika kila kitu hapa, basi, shabaha ya elimu ni muhimu mno hata ubora wa elimu unaletwa na shabaha nzuri, hivyo niwasihi viongozi waweze kukaa na kutafakari na kutengeneza mazingira mazuri ya elimu na iwe yenye kulenga kuajiri na kujiari na pia, ni jambo la lazima sana kutengeneza kitu cha kutatua changamoto ya sasa yenye wahitimu wengi wasio na ajira Kwa kutafuta ama namna ya kuwawezesha huku mkitengeneza namna nzuri ya muda wote ya kuifanya elimu iendane na uhitaji kwa fani mbalimbali, ikizingatia mabadiliko, takwimu, sera na mipango ya muda mrefu na ziwe nzuri zipimwe vizuri na si kupitisha pitisha tu na ikiwezekana wataalamu mbalimbali na maoni kutoka kwa wananchi na wahitimu yakusanywe na baada ya hapo ndipo iweze kupitishwa kwa kuzingatia vitu vingi na muhimu vyenye kuweza na kukubaliana na mabadiliko ya wakati na mahitaji, na ni lazima tathmini ifanyike mara kwa mara kuepusha matatizo (uncertainty) Kwa mbele.

Halikadhalika ni ukweli mgumu na unaoumiza kuwa elimu kwa sasa haina tija kwa wahitimu hasa kwa fani ambazo hazina ajira na ni maumivu makubwa na matumizi mabaya ya fedha kuona kitu alichokisomea mtu wala hakina manufaa kwake na aje kuambiwa ajiajiri Kwa kitu kingine ni bora tu angesomea hicho ambacho anaambiwa ajiajiri nacho. Na hiyo haitokani na matatizo ya wahitimu bali matatizo ya mfumo wa elimu kwa ujumla na chanzo chake ni kutokuona mbali na kutokuweka mazingira mazuri ya elimu hasa serikali.

Pia ni vyema serikali inapopima kuongezeka kwa wanaopata elimu na wanaoingia ikajitahidi sana kupima ubora na manufaa yanayotoka baada ya, kama elimu kuwa chombo chenye kufanikisha uchumi wa watu na maendeleo mengine yote ikiwa ni pamoja na uwezo wa wahitimu kujiajiri katika fani zinazowezekana kujiajiri na zimewekwa katika elimu na zinasomewa na zinawezesha kweli.

Na tena, suala la elimu ni jambo linaloleta matokeo ya baada ya muda mrefu ni muhimu sana kuzingatia hilo hata katika utekelezaji wake na katika kuunda sera, na mitaala. Tofauti na miradi kama ujenzi na mingine ambayo inaweza kukamilika na kuleta matokeo kwa muda mfupi hivyo hata viongozi wa kiserikali ni vyema wakazingatia katika awamu zao kuwa suala la elimu haliwezi kukamilika kwa awamu moja ni endelevu ni lazima kuwe na msingi mzuri na kujitahidi kuondoa kasoro nyingi kwa lengo la muda mrefu na si katika kuangalia awamu fulani pekee.

Muhimu, shabaha ya elimu ya muda mrefu na isiyobadilishwabadilishwa na matakwa ya viongozi wa kisiasa kila ajae eti anakuja na hili.
 
Back
Top Bottom