Mkapa si fisadi - Pinda
Afunga mjadala kwa kumtetea, kumsafisha na kumsifu
na Martin Malera, Dodoma
Tanzania Daima~Sauti ya Watu
WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, jana aliingia katika orodha ya viongozi wa serikali na wanasiasa waliojitoa mhanga kumtetea Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, dhidi ya tuhuma mbalimbali za ufisadi ambazo amekuwa akihusishwa nazo kwa muda mrefu sasa.
Pinda ambaye ndiye kiongozi wa juu wa serikali anayeongoza kwa kutoa kauli tatanishi tangu alipoteuliwa kushika wadhifa wake huo, Februari mwaka jana, alitoa utetezi wake huo jana ndani ya Bunge mjini Dodoma wakati alipokuwa akifanya majumuisho ya hotuba ya bajeti ya wizara yake aliyoiwasilisha Jumatatu wiki hii.
Akizungumza huku akipigiwa makofi na kushangiliwa na wabunge wa CCM ambao baadhi yao walimtetea kwa nguvu kubwa Mkapa wakati wa mjadala wa bajeti hiyo, Pinda alimuelezea kiongozi huyo mstaafu kuwa ni mcha Mungu, muadilifu, muwazi na mtu aliyefanya kazi kubwa kulinusuru taifa hili kiuchumi.
Nimesikia maoni ya wabunge wengi waliokuwa wakimtetea Mkapa, nami naungana nao kumtetea mzee huyo. Maana tujiulize, kama kweli Mkapa ni fisadi, basi tuangalie ufisadi wake uko wapi? Je, anamiliki akaunti zenye dola nje ya nchi? Ana ndege zake zinazoruka hapa nchini? Sasa ufisadi wake uko wapi? alihoji Pinda.
Alisema anakubaliana na wabunge wanaomtetea kwa kusema kuwa mwelekeo huu wa kuwasakama viongozi wa kitaifa kwa tuhuma za ufisadi, si mzuri. Viongozi hawa wa kitaifa ili uwe fisadi kama yule wa DRC, sitaki kumtaja jina hapa, lazima uwe dikteta sana ili ujilimbikizie mali, lakini kwa mfumo wetu, huwezi, alisema Pinda.
Mbali ya hilo, Pinda ambaye alionyesha dhahiri kukerwa na tuhuma ambazo zimekuwa zikielekezwa kwa Mkapa, aliwataka wanasiasa wanaofikiria kuwagusa viongozi wakuu wastaafu kwa masuala ya ufisadi, kujiuliza wao wenyewe mara mbili mbili kabla ya kuibua tuhuma zao, hoja ambayo ilionekana kuwalenga watu kama Mbunge wa Vunjo, Aloyce Kimaro (CCM), ambaye ndiye aliyekuwa mbunge wa kwanza kumshambuliwa rais huyo mstaafu ndani ya Bunge mwaka jana.
Akizungumzia kuhusu hoja katika mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira ambao unaaminika familia za Mkapa na ile ya aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona zina hisa, waziri mkuu alisema yeye mwenyewe atahakikisha jitihada za serikali kuumiliki mgodi huo kikamilifu zinafanikiwa.
Chonde chonde wabunge wenzangu, tukifikia hatua ya kuwagusa viongozi hao wastaafu wa kitaifa, tufikirie mara mbili, nimeamua kama tatizo ni mgodi wa Kiwira, zile hisa zote nitazirudisha serikalini ili tuanze upya, alisema Waziri Pinda.
Uamuzi wa Pinda kuzungumzia suala la mgodi wa Kiwira na kumtetea Mkapa unatokana na kuwapo kwa baadhi ya wanasiasa, hasa wa kambi ya upinzani kutaka kiongozi huyo mstaafu aondolewe kinga ili aweze kufikishwa mahakamani dhidi ya tuhuma mbalimbali, zikiwamo za matumizi mabaya ya madaraka na uwekezaji katika mgodi wa Kiwira.
Katika kuchangia hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu iliyohitimishwa jana, kuna baadhi ya wabunge walijitokeza kumtetea Mkapa wakidai kiongozi huyo hapaswi kuhusishwa na ufisadi, kwa kuwa alitenda mambo mengi mazuri yaliyosaidia ukuaji wa uchumi.
Mmoja wa wabunge hao ni pamoja na Mbunge wa Kwela, Chrisant Mzindakaya (CCM), ambaye aliwabeza baadhi ya wabunge wanaotaka kumfikisha mahakamani Rais Mkapa.
Wengine waliochangia mjadala huo na kumtetea Mkapa kwa tuhuma zinazoelekezwa kwake ni Mbunge wa Mchinga, Mudhihir Mudhihir, Musa Hassan Zungu (Ilala) na Esther Nyawaza (Viti Maalumu CCM).
Hatua hiyo ya Pinda na wabunge kumtetea Mkapa inatafsiriwa kuwa ni majibu kwa kina Kimaro, Mbunge wa Karatu, Dk. Wilibrod Slaa (CHADEMA) na wabunge wengine ambao wamekuwa wakimhusisha Mkapa na tuhuma za ufisadi na hususan ule unaomhusisha na umiliki wa mgodi wa Kiwira.
Aidha, katika hatua nyingine, Pinda alisema mapambano dhidi ya rushwa ni suala la kila Mtanzania na kuwataka wananchi kushirikiana na serikali kukabiliana na vita hiyo.
Vita hii ni ya kila Mtanzania. Nawapongeza wabunge walio mstari wa mbele, nampongeza Mama Anne Kilango ambaye amepewa tuzo ya kuwa mwanamke jasiri katika vita hii, lakini navipongeza pia vyombo vya habari kwa mchango mkubwa wanaoutoa katika vita hii, tukiendelea hivi naamini Tanzania bila rushwa inawezekana, alisema Waziri Pinda.
Wabunge jana walipitisha bajeti ya sh trilioni 2.6 alizoziomba kwa ajili ya ofisi yake kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2009/2010.