23 October 2009
Na Edmund Mihale
Majira
HATIMA ya kulipwa au kutokulipwa kwa malipo ya hisa za wamiliki wa mgodi wa Kiwira, familia ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Bw. Benjamin Mkapa na Daniel Yona itajulika katika mkutano wa 17 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania utakaoanza Jumanne ijayo huku baadhi ya wabunge wakitaka viongozi hao watoke kapa.
Taarifa kuhusu jinsi serikali ilivyoshughulikia mradi wa mgodi wa Kiwira ilikuwa ijadiliwe Dar es Salaam jana na Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, lakini ghafla uamuzi huo ulibadilishwa na kuamuriwa suala hilo lijadiliwe katika vikao vya kamati hiyo vitakavyoanza mjini Dodoma Jumanne ijayo.
Hoja hiyo ni ya pili kuahirishwa hatua za mwisho baada ya ile ya utekelezaji wa maazimio 23 ya bunge kuhusu mkataba tata wa Richmond, lakini katika hali ya kushangaza suala hilo liliahirishwa na kupangwa kujadiliwa mkoani Dodoma.
Wakati mjadala huo ukihamishiwa Dodoma, baadhi ya wabunge waliozungumza na gazeti hili bila kupenda kutajwa walisema ingependeza mgadi huo urudi mikononi mwa umma bila kuwalipa wawekezaji wake hata senti moja.
Licha ya kwamba kilichomo kwenye taarifa hiyo bado ni siri, lakini jambo moja lililowafurahisha wabunge hao ni kuwa mgodi huo umerudi mikononi mwa Watanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi ndogo ya Bunge, Waziri wa Nishati na Madini, Bw. William Ngeleja alisema hoja ya Kiwira itajadiliwa mkoani Dodoma, lakini hakutaka kuingia ndani kueleza ni kwa nini imeamuliwa hivyo.
"Niwapeni kichwa cha habari kuhusu kile nilichokabidhi kwenye Kamati ya Bunge, ni taarifa ya jinsi serikali inavyoshughulikia mgodi wa Kiwira," alisema Bw. Ngeleja na kuongeza; "Suala hili linashughulikiwa na serikali kwa kufuata na kanuni na taratibu za bunge."
Bw. Ngeleja alisema tayari mgodi huo upo mikononi mwa serikali na itaanza kuwalipa wafanyakazi wote kuanzia mwishoni mwa mwezi huu, ambapo watalipwa malimbikizo ya mishahara ya miezi 15.
Hata hivyo, Bw. Ngeleja hakuwa tayari kuzungumzia juu ulipwaji wa hisa anazomiliki Bw. Mkapa na mwenzake Bw. Daniel Yona.
Alipoulizwa na waandishi wa habari kuhusu hatima ya kulipwa hisa zao Bw. Mkapa na Bw. Yona, Waziri Ngeleja alijibu kwa kifupi; "Hayo yatajulikana bungeni."
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, Bw. William Shellukindo, alisema kamati yake imepokea taarifa na imeridhia kulipwa kwa wafanyakazi hao. "Cha kufurahisha zaidi ni taarifa ya mgodi huo kuwa mikononi mwa serikali," alisema.
Kuhusu kulipwa kwa hisa za wawekezaji wa mgodi huo, alisema kuna mambo ambayo yanafanyika. Tuhuma za Rais mtaafu, Bw. Mkapa na Bw.Yona kujimilikisha mgodi wa Kiwira ziliibuliwa na mbunge wa Vunjo, Bw. Aloyce Kimaro, katika mkutano wa 11 wa bunge.
Baada ya kuibuliwa kwa hoja hiyo, baadhi ya wabunge walitaka kiongozi huyo mstaafu aondolewe kinga na kufikishwa katika vyombo vya sheria kwa kutumia vibaya madaraka yake akiwa rais, lakini hivi karibuni Halmashauri Kuu ya CCM imemkingia kifua na kuwataka wabunge wa chama hicho pamoja na wanachama wengine wamwache apumzike.
Wakati wabunge hao wakipendekeza hivyo, tayari Bw. Yona anakabiliwa na mashitaka tofauti ya kutumia madaraka vibaya na kuliingizia taifa hasara ya sh. bilioni 11.7.