Date::11/7/2009
Vigogo CCM wauweka pabaya urais wa Kikwete
Na Mwandishi Wetu
Mwananchi
MALUMBANIO yanayoendelea miongoni mwa wabunge CCM unamweka katika wakati mgumu, Rais Jakaya Kikwete kutetea nafasi yake katika Uchaguzi Mkuu wa 2010.
Hali hiyo inayoonyesha wazi kuwepo kwa ukiukwaji mkubwa wa maadili ya uongozi kwa baadhi ya mawaziri wake na kuuweka katika hali tete uongozi wa kitaifa.
Wachambuzi wa siasa nchini, wanaona kuwa hali hiyo imechangiwa na mbinu zinazotumiwa na Rais Kikwete kuyapatia ufumbuzi masuala nyeti ya kitaifa na chama.
Wanasema kushindwa kueleweka kwa msimamo wa Rais kuhusu masuala muhimu yayohitaji maamuzi magumu, kumechangia mpasuko mkubwa ndani ya CCM na serikali yake.
Wakizingumza na Mwananchi Jumapili kwa nyakati tofauti jana, wananchi wa kada mbalimbali wakiwemo wasomi walisema kutojulikana kwa msimamo wa Rais Kikwete dhidi ya makundi yanayopingana ndani ya CCM na uimara wake katika kuongoza ni tatizo kubwa.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Ezavel Lwaitama alisema hatma ya malumbano pamoja na mpasuko unaondelea kujitokeza ndani ya CCM utategemeana na Rais Kikwete ataegemea katika kundi lipi kati ya mawili yaliyopo hivi sasa ndani ya chama hicho.
Dk Lwaitama alifafanua kwamba, kwa sasa CCM anakabiliwa na tatizo kubwa la uadilifu kwa viongozi wake hivyo kusababisha kuzuka kwa makundi mawili ambayo ni lile linalojipambanua kuwa linapingana na ufisadi na linaloona ufisadi sio tatizo
"Mustakabali wa taifa pamoja na urais wa Kikwete katika uchaguzi ujao wa mwaka 2010 utategemeana atajiunga na kundi gani kati ya haya mawili," alisema Dk Lwaitama na kuongeza; "Haya yote yanayotokea kwa sababu ya kutokuwepo kwa maadili ya uadilifu ndani ya viongozi wetu na hasa wa CCM".
Dk Lwaitama alisema kutokana na hali ya kisiasa iliyopo ndani CCM ni vigumu kwa makundi hayo kuwa pamoja hadi hapo Rais Kikwete atakapokuwa na ujasiri wa kupigania misingi iliyowekwa tangu enzi za chama cha TANU.
"Haya mambo yanaweza kuisha tu endapo Rais Kikwete atakuwa na ujasiri wa kupigania kurudi kwa misingi ya chama cha TANU ambayo ilikataza kabisa rushwa na ni adui wa haki na kutekeleza kauli hiyo kwa vitendo," alisema Dk Lwaitama.
Hata hivyo, Dk Lwaitama alisema jitihada zinazofanywa na Rais Kikwete kunusuru hali hiyo hazijafanikiwa kutokana na nguvu ya kisiasa zilizopo baina ya makundi hayo.
"Rais Kikwete alihisi kuanzishwa kwa kamati maalum iliyochini ya Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi ingeweza kutatua na kuondosha tofauti zote zilizopo, lakini imeshindwa kufanya hivyo kutokana na nguvu za kisiasa walizonazo wabunge," alisema.
Dk Lwaitama alisema kimsingi kamati hiyo ndiyo imekuja kuzidisha mapasuko na malumbano zaidi ndani ya CCM.
Mhadhiri huyo alifafanua kwamba, kamati hiyo iliundwa ili kupatanisha makundi hayo, lakini matarajio yamekuwa tofauti na hivyo ameitaka NEC kuivunja haraka kamati hiyo.
Kupitia vikao vya kamati hiyo vilivyokuwa vikifanyika mjini Dodoma hivi karibuni, wabunge wa CCM na baadhi wanachama wamekuwa katika malumbano makali yanayosababishwa na tuhuma za ufisadi hadi kufikia hatua ya kurushiana maneno ya kudhalilishana.
Naye Mhadhiri Mstaafu wa UDSM, Profesa Mwesiga Baregu alisema kuna kila dalili katika uchaguzi wa 2010, CCM ikachagua kiongozi mpya wa kugombea nafasi ya urais.
Alisema hali hiyo inatokana na Rais Kikwete kushindwa kusimamia kidete kukemea masuala mbambali yanayoendelea kujitokeza ndani ya chama hicho.
Profesa Baregu alisema Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, bado hajapata ujasiri wa kukemea na hata kuonyesha msimamo wake kuhusu hali Inayoendelea, ndio maana tofauti ndani ya chama hicho inazidi kuwa kubwa.
"Kuyumba kwa CCM kunaashiria kuwa huenda mwakani wakachagua mgombea mpya wa nafasi ya urais na hii ni kuwa hadi sasa Rais Kikwete bado hajaonyesha uimara katika uongozi wake," alisema Profesa Baregu.
Profesa huyo alisema chama hicho kinayumba kutokana na kuwepo kwa makundi matatu ya CCM Mtandao, CCM Mpasuko na CCM asili.
Alifafanua kuwa kati ya makundi hayo, kundi la CCM Mtandao na lile la CCM mpasuko ndiyo yanapambana kwa kuwa yamejitenga na misingi ya zamani ya chama hicho huku la Asili ndilo linailoenzi na kufuata.
"Ukiangali kwa umakini utagundua kuwa makundi la mpasuko na lile la mtandao ndiyo yanayoatarisha mustakabali wa CCM kwa kuwa yamejitenga na misingi ya azimio ya Arusha," alisema.
Profesa Baregu alisema kinachomponza Rais Kikwete ni kutoonyesha ujasiri katika kutatua matatizo mbalimbali hali inayomfanya kuelemewa na makundi hayo.
Alisema siku zote kiongozi ni lazima awe wa jumla mwenye ujasiri na asiyesukumwa na makundi.
"Inawezekana matatizo yanayokumba CCM yakapungua na hata kuondoka endapo Rais Kikwete kama atapata ujasiri wa kuongoza kuwa imara na kupata shinikizo kutoka kundi lolote," alisema Profesa Baregu.
Juzi Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema Rais Jakaya Kikwete ndiyo chanzo cha malumbano yanayoendelea baina ya wabunge wa chama hicho.
Profesa Lipumba alisema tabia ya Rais Kikwete kutaka kuwa mwema kwa makundi yote hasimu ya chama hicho na kushindwa kutoa msimamo wake kama kiongozi mkuu, ndio chanzo cha tishio hilo la kusambaratika kwa CCM.
Hata hivyo, Ikulu imekuwa ikijitetea kwamba Rais Kikwete hajawahi kubariki mkataba wa Richmond na ni mtu wa kwanza kuzuia malipo kwa kampuni hiyo.
Tangu kamati ya mzee Mwinyi ianze kuwahoji wabunge mjini Dodoma kuhusu mgawanyiko ndani ya chama hicho, kumeibuka malumabano makali yakiambatana na kutoleana lugha chafu.
Waziri Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Sophia Simba ambaye alidai kuwa Waziri Mkuu Mstaafu, John Malecela na mkewe Anna Kilango si safi kwa kuwa walipokea fedha za harusi yao na kampeni za uchaguzi 2005 kutoka kwa Jeetu Patel; huku akiwasafisha Waziri Mkuu wa zamani,Edward Lowassa kuwa ni mtu safi ila walimwonea wivu.
Pia alimsafisha Mbunge wa Bariadi Mashariki, Andrew Chenge ambaye anatuhumiwa na kashfa ya rada kwa ni ni mtu safi ambao wanaonewa wivu.
Waziri Simba pia alidai kuwa Kilango ni mnafiki na si msafi kiasi cha kuwanyooshea wenzake vidole na kwamba, kelele zake zote zimetokana na kukosa kuwa mke wa rais baada ya Malecela kuenguliwa mapema na CCM kwenye mchakato wa kumpata mgombea wake.
Hata hivyo, Kilango alisema hatakatishwa tamaa na tuhuma hizo nzito, ambazo alisema bado anazitafakari, ili kubaini kiini chake na sababu za kutolewa sasa katika kipindi ambacho vita dhidi ya ufisadi imepamba moto.
Naye Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Dk Makongoro Mahanga na Mbunge viti maalumu, Bernadeta Mushahushu waliponda ripoti ya Richmond kuwa iliandaliwa kummaliza Lowassa kwa wivu na uchu wa madaraka wa baadhi ya wana-CCM.
Dk Mahanga ambaye ni Mbunge wa Ukonga, alisema ripoti hiyo kuwa ni feki huku na kupendekeza Rais Kikwete aunde tume huru kupata ukweli akidai kuwa Lowassa alionewa.
Naye Christopher Ole Sendeka wa jimbo la Simanjiro alitaka Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz, Mbunge wa Bariadi Magharibi Andrew Chenge na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa wawajibishwe kutokana kuhusishwa na tuhuma mbalimbali za ufisadi.