Kifo cha Wangwe utata (Majira)
*Gari lapondekapondeka vibaya, halitamaniki
*Mwili wake wakutwa na majeraha kichwani pekee
*Mwenzake hakuonekana na majeraha, alipiga simu
Waandishi Wetu, Dodoma na Dar es Salaam
WATANZANIA wamepokea kwa masikitiko makubwa habari za kifo cha Mbunge wa Tarime, Bw. Chacha Wangwe (CHADEMA) kilichotokea kwa ajali ya gari juzi usiku huku habari huzo zikigubikwa na utata wa chanzo cha kifo.
Baadhi ya watu waliotoa maoni yao kutokana na tukio hilo, walihusisha kifo hicho na mgogoro ndani ya CHADEMA, huku wakihis kuwapo mkono wa mtu, huku wengine wakiamini ni ajali iliyopangwa na Mungu.
Viongozi na wananchi waliozungumza na gazeti hili walisema walipokea kwa mshituko kifo cha mbunge huyo.
Huzuni na simanzi iliyoambatana na idadi kubwa ya wabunge kububujikwa na machozi, ni miongoni mwa mambo yaliyotawala ndani na nje ya ukumbi wa Bunge jana, kutokana na kifo cha Bw. Wangwe.
Habari kuhusu kifo cha marehemu Wangwe, zilitangazwa rasmi jana asubuhi na Spika wa Bunge, Bw. Samuel Sitta, ambaye naye alishindwa kujizuia na hatimaye kulia kwa sauti.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu Bw. Mizengo Pinda, alionekana akitumia kitambaa kujifuta macho, kitendo ambacho kilifanywa na wabunge wengi ndani ya ukumbi wa Bunge.
Kwa mujibu wa Spika, Bw. Wangwe alikufa baada ya gari alilokuwa akisafiria kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam, kupinduka katika eneo la Pandambili, Dodoma.
Bw. Sitta alisema ajali hiyo ilitokea saa 2.55 usiku na kwamba katika gari hilo, marehemu alikuwa na rafiki yake Bw. Deus Malya. Walikuwa wanakwenda kushiriki katika msiba wa marehemu Bhoke Munanka.
Alisema katika ajali hiyo, gari liliacha njia, kupinduka na baadaye kupoteza mwelekeo uliofanya kwenda porini huku likiwa linakata miti.
Habari za awali zilisema gari hilo lilirushwa kwa umbali wa meta 50 kutoka barabara kuu ya Dodoma-Morogoro.
Kutokana na kifo hicho, Bw. Sitta alitangaza kuahirishwa kwa shughuli za Bunge, ili kutoa nafasi kwa wabunge kuomboleza kifo cha mbunge huyo machachari na aliyekuwa kipenzi cha wengi.
Hata hivyo ilipofika saa 6 mchana, Spika wa Bunge alitangaza kuwa marehemu Wangwe, atazikwa kesho adhuhuri kijijini kwake wilayani Tarime. Hakutaja kijiji hicho,lakini alisema kiko kilometa 12 kutoka Tarime.
Mwili wa marehemu ambao ulikuwa umehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma na baadaye kufanyiwa uchunguzi wa kitaalamu, uliagwa rasmi jana jioni.
Rais Jakaya Kikwete, aliwaongoza wabunge kuuaga mwili huo ambao jeneza lake, lilifunikwa bendera ya Taifa. Waziri Mkuu, Bw. Pinda alimfuatia Rais katika tukio hilo.
Mwili huo utasafirishwa asubuhi hii kwa ndege kwenda Tarime na utaondoka na msafara utakaohusisha watu 18 ambao ni ndugu wa marehemu na wabunge wawili.
Kwa mujibu wa Spika, wabunge 20 wataondoka kesho asubuhi kwa ndege maalumu, kuliwakilisha Bunge katika mazishi ya marehemu Wangwe.
Alisema wabunge hao ni pamoja na wote wa mkoa wa Mara, watatu wa kambi ya upinzani na wengine walioteuliwa kwa kuzingatia uwiano wa uwakilishi wa jinsia na pande za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wabunge wamlilia
Lakini hayo yakitangazwa, mapema asubuhi jana mara baada ya kusitishwa kwa shughuli za Bunge, baadhi ya wabunge walielezea kusikitishwa kwao juu ya kifo hicho.
Wabunge hao ni pamoja na Naibu Spika Bibi Anne Makinda, ambaye alisema kifo hicho kimeacha pengo kubwa si tu katika kambi ya upinzani, lakini pia katika Bunge.
Bibi Makinda ambaye alimwelezea marehemu kuwa mtetezi mkubwa wa wapiga kura wake, alisema alikufa wakati akiwa mbioni kutaka kuwasilisha hoja binafsi kuhusu wizi wa mifugo na mapigano ya koo wilayani Tarime.
Alisema marehemu Wangwe, alitaka kuwasilisha hoja hiyo Ijumaa iliyopita, lakini hakupata nafasi.
Bibi Makinda ambaye pia ni Mbunge wa Njombe Kusini (CCM), alisema baada ya kukosa nafasi katika siku hiyo, alimshauri avute subira, ili awasilishe hoja hiyo juzi jioni ambapo kulikuwa na nafasi.
"Nilimwambia avute subira ili awasilishe hoja yake jana, lakini baadaye nilimtafuta hakupatikana. Hoja hiyo inaonesha namna marehemu Wangwe alivyokuwa mtetezi mkubwa wa watu wake na tumekubaliana kuwa itasomwa," alisema Bibi Makinda huku akionesha simanzi kubwa.
Alisema marehemu pia alikuwa mtu aliyependa kushirikiana na wabunge wenzake katika mambo mbalimbali ndani na nje ya Bunge na kwamba hoja zake zilikuwa zinasisimua Bunge.
Mbunge wa Bariadi Mashariki (UDP), Bw. John Cheyo, alisema kambi ya upinzani ilipata pigo kubwa lililotokana na kifo cha Wangwe, ambaye alimwelezea kuwa mtu muhimu si tu kwa kambi hiyo, lakini pia kwa wananchi wa Tarime na chama chake.
"Alikuwa mtu aliyependa watu wake Tarime na Taifa kwa jumla, ameacha pengo kubwa katika kambi ya upinzani bungeni maana idadi yetu inazidi kupungua," alisema Bw. Cheyo.
Mbunge wa Mchinga (CCM), Bw. Mudhihir Mudhihir, alisema amepokea habari hizo kwa mshituko mkubwa hasa ikizingatiwa kuwa saa kadhaa kabla ya kuondoka kwake (Wangwe) bungeni, alitaniana naye.
"Unajua Wangwe alikuwa mtu wa masihara na mimi ni mtu wa masihara, jana wakati anatokana bungeni nilitaniana naye, utani wake ulihusu tukio la Yanga kutokwenda uwanjani na mimi nikamwambia mbona hujui kuvaa koti maana amefunga hadi kifungo cha mwisho, akasema ni kweli tukacheka akaondoka," alisema.
Mbunge wa Simanjiro (CCM), Bw. Christopher ole Sendeka, alisema kifo cha Bw. Wangwe, kilisababisha pengo kubwa kwa wananchi wa Tarime ambao alikuwa akiwawakilisha na kuwatetea vilivyo.
"Wangwe alikuwa mtetezi wa watu wake na asiyetetereka kwa msimamo hasa katika mambo ya msingi...hoja zake zilikuwa za kusisimua," alisema Bw. Sendeka.
Alisema mbunge huyo alikuwa kipenzi cha wengi ndani ya nje ya Bunge.
Kwa upande wake, Mbunge wa Same Mashariki (CCM), Bibi Anne Kilango, alisema kifo cha mbunge huyo ni pigo kubwa si tu kwa familia yake, lakini pia kwa Bunge.
Alisema wakati wa uhai wake, marehemu alishirikiana na kila mtu bila kujali itikadi za kisiasa.
"Mimi nilipigiwa simu na wenzangu kunieleza habari za kifo cha Wangwe, kwa kweli nilishituka sana kusikia habari hizi," alisema Bi. Kilango.
Akizungumzia hali halisi aliyokuwa nayo marehemu siku hiyo, Mbunge wa Viti Maalumu, Bibi Joyce Masunga (CCM), ambaye ni jirani ya marehemu Dodoma, alisema alishtushwa na taarifa ya kifo hicho kutokana na mazingira ya ajali yenyewe.
Alisema anaamini huenda Bw. Wangwe alitabiri kifo chake kutokana na matendo aliyokuwa akiyafanya kwa mujibu wa maelezo ya familia yake.
Aliongeza kuwa baada ya kifo hicho alizungumza na familia yake ambayo ilimweleza hali halisi aliyokuwa nayo marehemu siku hiyo.
Akizungumza katika kipindi maalumu kilichorushwa na Televisheni ya Taifa (TBC) jana asubuhi, Bibi Masunga alisema kwa taarifa ambazo alizipata kwa watoto wake marehemu kabla ya tukio, alikuwa akijisikia vibaya kiasi cha kushindwa hata kuweka maji bafuni kuoga.
Aliongeza kuwa watoto wake walimpa msaada kwa kumwekea maji bafuni baada ya kushindwa kufanya hivyo na marehemu aliingia kuoga na alipomaliza kujiandaa, alitoka nje na kuingia ndani ya gari kisha kwenda bungeni.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Bw.Omar Yufusu Mzee, alisema Bunge limempoteza mtu ambaye alikuwa akilichangamsha hasa kutokana na jinsi alivyokuwa akijua kujenga hoja.
Mbunge wa Mbozi Mashariki (CCM), Bw. Godfrey Zambi, naye aliungana na wabunge wenzake katika kuelezea masikitiko yao juu ya kifo cha marehemu Wangwe.
"Kwa kipindi cha miaka miwili tuliyokuwa naye bungeni, alikuwa kivutio kikubwa kwa michango yake. Kwa jumla alikuwa mpiganaji na mtetezi wa haki za watu wake Tarime," alisema.
Naye Mbunge wa Karatu, Bw. Wilbroad Slaa ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CHADEMA alisema amesikitishwa na mazingira ya ajali ya Bw. Wangwe na kudai kuwa yana utata.
Alisema utata wa ajali hiyo ulitokana na dereva ambaye alidaiwa kuwa ni marehemu Wangwe mwenyewe, kiti chake hakikuwa na damu na badala yake kiti cha abiria ndicho kilitapakaa damu.
Alisema hata mazingira ya ajali yenyewe yana utata, hivyo kushindwa kuelewa nini kilitokea na dereva alikuwa nani na kwa nini abiria alinusurika wakati kiti chake kikilowa damu.
"Sisi tunaliachia Jeshi la Polisi juu ya ajali hii, kwani ina mazingira ya utata ambayo yanatuachia maswali na kushindwa kuelewa dereva alikuwa nani na abiria alikaa wapi na kutoka bila majeraha makubwa huku kiti chake kikiwa na damu nyingi," alisema Bw. Slaa.
Aliongeza na kusema jinsi gani lilivyoharibika hawakutarajia kama wangekuta mwili wa Bw. Wangwe, ilivyo japo mwili wake umeharibika kichwani kiasi cha kushindwa kumtambua kama alikuwa ni Bw. Wangwe anayefahamika na wengi.
"Kwa kweli msiba huu tuliupokea kwa sura ngumu hasa ukizingatia uchache wa wabunge wa upinzani ndani ya Bunge hasa wa CHADEMA sasa tumepungua na kubaki 43 badala ya 45 kama ilivyokuwa mwanzo, baada ya Mbunge wa TLP, Biharamulo Bw. Falis Kabuye, kuenguliwa katika ubunge," alisema Bw. Slaa.
Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Bi Suzan Lyimo (CHADEMA) alisema huenda marehemu Wangwe alifahamu fika kuwa siku zake za kuishi duniani zimekwisha, kutokana na kauli alizokuwa akizitoa kwa ndugu na jamaa zake wa karibu.
Kwa mujibu wa watu walio jirani na marehemu Wangwe, alishawahi kutamka kuwa ana dalili nyingi za kuuawa na huenda kwa siku ya jana ndiyo ilikuwa hitimisho la kauli zake.
Mbunge wa Gando, Bw. Halifa Suleiman (CUF), alisema amepokea kwa mshituko taarifa hizo kwa kuwa jana saa 5 asubuhi, alikuwa na mazungumzo naye ya faragha.
Alisema walikutana nje ya ukumbi wa Bunge na kuzungumza naye kwa muda mrefu, lakini hali yake ilikuwa tofauti na alivyomzoea.
"Kwa siku ya jana Wangwe alikuwa tofauti na nilivyomzoea labda huenda ndiyo umauti ulikuwa ukimnyemelea na ilikuwa ngumu kwangu kumuuliza kwa nini amebadilika hivyo," alisema Bw. Halifa.
Alisema marehemu Wangwe alikuwa mcheshi, muwazi na daima alikuwa akishauriana naye katika masuala mbalimbali, hivyo pengo aliloliacha ndani ya kambi ya upinzani ni kubwa hasa katika kipindi hiki kigumu.
Kiongozi wa Upinzani bungeni, Bw. Hamad Rashid Mohamed (CUF) alisema kuwa msimamo wa marehemu Wangwe aliokuwa nao unapaswa kuigwa na wabunge wengine.
Alisema alikuwa na msimamo na kipiganaji ambapo akitoa hoja yake ilikuwa vigumu kumbadilisha kimawazo zaidi ya kuongezea anachokihitaji yeye na wapiga kura wake.
Wanawe wasimulia
Watoto watu wa marehemu wakiongozwa na mkubwa wao Zakayo Chacha (18), waliezea kuhuzunishwa kwao, juu ya kifo cha mzazi wao wa kiume.
Kwa mujibu wa Zakayo kifo cha baba yao kimetokea wakati mama yao yuko Dar es Salaam.
Katika simulizi zake, mtoto huyo alisema kabla ya kifo chake, baba yake alikuwa anasumbuliwa na malaria.
"Tuliondoka naye Dar es Salaam Alhamisi iliyopita, akiwa na makusudio ya kuja kuwasilisha bungeni hoja yake binafsi kuhusu mambo ya Tarime," alisema.
Alisema kwa mujibu wa maelezo ya baba yake, hoja hiyo alitarajia kuiwasilisha Ijumaa, lakini alikosa nafasi.
"Lakini kuanzia Ijumaa jioni baba alikuwa anajisikia vibaya, akanywa dawa, pia Jumamosi. Jumapili usiku alitueleza kuwa alikuwa hajisikii vizuri, akaniambia nimtafutie dawa (Panadol), nikatafuta lakini sikupata," alisema kijana huyo huku akionesha masikitiko makubwa.
Alisema aliwasiliana na mama yake kwa njia ya simu kumweleza kuhusu hali ya marehemu na kutoonekana kwa dawa zilizokuwa zimehifadhiwa kabatini.
Bw. Chacha alisema baadaye, mama yake alimshauri aende kununua dawa hizo katika duka la jirani na kwamba alipokwenda, duka lilikuwa limefungwa kwa kuwa ilikuwa usiku wa manane.
Alisema hata hivyo, muuzaji wa duka hilo alikubali kuwapa dawa alizokuwa amezihifadhi kwa matumizi binafsi.
Alisema baada ya kunywa dawa hizo, alilala usingizi mzito," alisema.
Mtoto huyo alisema ilipofika saa 11 alfajiri mtu aliyetamtaja kuwa ni Bw. Deus Malya, ambaye ni rafiki wa marehemu, alikwenda katika makazi hayo na kumtaka marehemu waondoke.
"Nilimgongea sana mlango wa chumba chake, hakujibu baadaye nikampigia simu akajibu na baadaye wakaondoka na kurudi," alisema.
Alisema juzi marehemu aliamka akiwa amebanwa na mafua makali na kwamba kwa kumwona akiwa katika hali hiyo, alisihi baba yake apumzike badala ya kwenda bungeni.
"Lakini alinijibu kuwa hoja yake ilikuwa ni ya muhimu sana na kwa hiyo lazima aende kuiwasilisha, akaondoka lakini pia nilimshauri apitie hospitalini," alisema Zakayo.
Alisema baadaye baba yake alirejea nyumbani na kumweleza kuwa hoja yake imeshindikana kuwasilishwa.
Kwa mujibu wa kijana huyo, marehemu Wangwe pia alimwambia kuwa alipitia hospitalini ambako alipimwa na kukutwa na wadudu watatu wa malaria na kwamba alipewa dawa za mseto ili azitumie.
"Baadaye tulimka ale chakula halafu apumzike, akasema hajisikii kula, lakini alikuwa ameleta matunda akataka tumtengenezee matunda ambayo alisema angeweza kula," alisema.
Bw. Chacha alisema baada ya muda, alimpa baba yake dawa za mseto na kumtaka apumzike na kwamba alipokwenda kumjulia hali alikumtaka anakoroma.
"Saa 11 jioni alikuja Deus na kumtaka baba waondoke, lakini kabla hawajaondoka kuelekea Dar es Salaam, nilimweleza Deus kuhusu hali ya gari.
"Gari lilikuwa na matatizo nati za matairi ya mbele zilikuwa zimelegea tukajitahidi kuzifunga upya. Baada ya hapo nililijaribu lakini ghafla nati zilichomoka, jambo ambalo kwa kweli nilisema lilikuwa la hatari kama wangesafiri nalo," alinena.
Alisema baadaye alimpa taarifa baba yake ambaye alimshukuru na kumtaka yeye na Deus wakashughulikie gari hilo, ili liwe imara kwa kusafiria.
"Gari lilitengenezwa na wakaondoka likiwa linaendeshwa na Deus. Lakini baada ya muda, baba alinipigia siku kuwa gari limewaharibikia Ihumwa na kwamba wanarejea mjini kwenda kulitengeneza. Nikawa nawatafuta sikuwapata.
"Saa mbili usiku nilichukua simu nikaiweka kwenye chaji na baada ya muda, nilipokea simu kutoka kwa mama akiniarifu kuwa baba amepata ajali na amekufa," alisema kijana huyo.
Alisema baada ya taarifa hiyo, alipiga simu ya baba yake ambayo ilipokewa na Deus na kwamba alimuuliza kuhusu habari za kifo cha baba yake, Deus alimjibu kuwa wao walikuwa wamejeruhiwa na walikuwa wanapata matibabu.
Kwa mujibu wa Zakayo, mama yake alipata taarifa hizo kupitia Polisi.
Mmoja wa waandishi wa habari hii aliyefika katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Mkoa Dodoma jana, alishangaa kuushuhudia mwili wa mbunge huyo ukiwa na majeraha kichwani na mwili mwingine ukiwa shwari.
Hata hivyo alishuhudia damu nyingi kwa imeganda usoni ingawa alimshuhudia Bw. Malya akiwa hana jeraha lolote kunwa la kutisha hasa ikizingatiwa jinsi gari lilivyoharibika.
Hadi tunakwenda mitamboni bado hakukuwa na taarifa yoyote ya uchunguzi uliofanywa na wataalamu kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Polisi, Hospitali ya Mkoa Dodoma, ndugu wa marehemu na mwakilishi wa wabunge iliyokuwa imetolewa.
Watoto wengine wawili waliokuwapo katika makazi yao ni Bob na Abdunedo Chacha.
Wasifu wake
Marehemu Wangwe alizaliwa Julai 15, 1956. kijijini kwao Kyamakorere, umbali wa kilomita 20 kutoka Tarime Mjini.
Alipata elimu ya msingi katika shule za Rosana na Magoto kati ya mwaka 1962 na 1968 kabla ya kujiunga na elimu ya sekondari katika shule ya Nyaroha.
Baadaye alihamia Dar es Salaam na kujiunga na Sekondari ya Kinondoni Muslim ambako alimaliza kidato cha nne mwaka 1974. Alisoma kidato cha tano na sita katika shule ya Mkwawa kati ya 1975 na 1976.
Alijunga na masomo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1978 lakini hakumaliza. Aliwahi kufanya kazi Benki ya NBC, Shirika la Kujitolea la Ujerumani, Kampuni ya Lacop na mgodi wa dhahabu wa Afrika Mashariki.
Kisiasa aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali ukiwamo uenyekiti wa tawi la vijana wa TANU katika sekondari ya Mkwawa, Mwenyekiti wa Wilaya CHADEMA Tarime, kati ya 1994 na 1998 kabla ya kujiunga na NCCR-Mageuzi ambako alikuwa Mwenyekiti wa Mkoa kati ya 1998 hadi 2002, lakini akarejea CHADEMA mwaka 2002 na kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Mkoa wa Mara wa chama hicho.
Marehemu ambaye hadi wakati anakufa alikuwa na umri wa miaka 52, ameacha watoto kumi; wa kwanza akiwa ni wa kike anayeishi Marekani.