Naona hapa hatuna budi kuwekana sawa na kuwa wa kweli kwa nafsi zetu. Naombe nijieleze vizuri na kueleweka. Sithubutu hata kidogo kutetea, kuhalalisha, au kuendeleza kitendo ambacho wanatuhumiwa vijana wetu. Nitakuwa wa kwanza kabisa kulaani kitendo na kukilaani. Nitafanya hivyo si kwa sababu ya uanasiasa wa wanaodaiwa kuhusika bali kwa sababu ya suala zima la maadili ya mtu wa ndoa (Bi. Chifupa) na kijana mchumba wa mtu (Zitto). Kwa maneno hayo ningelikabili suala hilo kama ambavyo kaka yangu au rafiki yangu angehusishwa nalo. Nisingefikiri hata kidogo kuwa tatizo kubwa kabisa la maadili, lililowahi kutokea limetokea na linatishia kuvunja vunja jumuya au chama! Ningeliweka jambo hili katika maudhui yake sawia. Msimamo wangu uko hivi:
a. Kama ni kweli kuwa ndugu zetu (siyo maadui kwa namna yoyote ile) wamehusishwa na kitendo hiki, basi ni kosa, kukengeuka kimaadili ya kijinsia, na ni jambo la aibu. Kwa mtu wa ndoa kwenda nje ya ndoa yake kwa sababu yoyote ile ni kinyume na kiapo cha ndoa yake na kwa hilo jamii yaweza kuoneshwa kutokufurahishwa na kitendo hicho. Kwa mtu ambaye anajua mwenzie anayemtongoza ni mtu wa ndoa basi kwake huyo naye ni kosa na ni aibu kwake na hasa kama na yeye ana mtu ambaye amemuahidi penzi lake.
b. Kama (a) ni kweli basi jukumu la kwanza na kuwajibika kwa kwanza kabisa siyo kwa JF, Chadema, CCM au nchi nzima! Jukumu la hawa vijana kujieleza ni kwa wale wawapendao na familia zao. Kama AC ameshindwa kumshawishi mumewe kuwa maneno hayo ni majungu, au kama Medi ana ushahidi usiopingika kuwa kweli mkewe alikuwa na mahusiano na Zitto hilo ni suala la nyumba yao! Kama Medi ameamua kumhusisha Spika (kwa sababu anazozijua yeye mwenyewe) na hivyo kulifanya jambo hilo kuwa la hadhara, hayo ni maamuzi yake! Kwa kijana Zitto, jukumu lake la kwanza ni kwa mchumba wake, na familia yake! Kwa watu hao wa karibu ndio anatakiwa kwenda kutoa maelezo kwanza kabla ya sisi watu wa JF (au watu wa kwenye vyama vya siasa) kurukia na kutoka tuombwe radhi!!
c. Kama (a) na (b) ni vya kweli, basi AC na KZ kwa kuangalia nafasi zao katika jamii wanajukumu jingine nalo ni dogo kuliko hilo la pili. Kwa vile hawa ni viongozi itakuwa ni kosa kubwa sana kuwaangalia wao kama "mifano" ya jamii! Mtindo wa kuwaona wanasiasa kama role model ni sawa na mtindo wa kuwaona wasanii kuwa ni role model na wanapoharibu basi hisia ya kusalitiwa, kukatishiwa tamaa, na kuachwa kwenye mataa hujiri! Kwa vile vijana hawa ni wabunge wa Bunge letu na wameonesha umahiri bungeni n.k basi wengi wanawatarajia kuwa basi vijana hawa wanapaswa kuwa na maadili yaliyotukuka! Kutarajia hivyo hata kwa nia nzuri kiasi gani au kwa ajili ya chama kwa kiasi gani ni kuwa na matarajio yasiyo na msingi!!
Ni kweli tunaweza kuweka maadili kwenye ngazi ya juu lakini kutarajia kuwa watu hawatakengeuka na wakingeuka basi tuwateremshie nyundo za laana ni kutarajia maji jangwani! Tuwe wa kweli. Kitendo cha ngono na hisia ambazo huambatana nazo hakitokani na mantiki, usomi, ujuzi, umahiri wa uongozi n.k! Ni kitendo ambacho kinapita maelezo ya kitaaluma! Ni kitendo cha kinyama na kibailojia! Wengi wetu tunaweza kutawala hisia zetu na vionjo vyetu kwa muda fulani, lakini ni wachache wetu ambao wanaweza kutawala vitu hivyo wakati wote, dhidi ya watu wote, na mahali popote!! Ni kwa sababu hiyo basi, licha ya kukubali kuwa kitendo hicho kimepotoka, hata hivyo tusitoe hukumu ambayo yaweza kutumuka dhidi yetu pia! Kipimo kile kile tupimiacho ndicho kitakachotumiwa kutupimia na sisi!!
d. Nakubaliana na maoni ya baadhi ya watu kuwa maadili ni kitu muhimu sana kwa kiongozi. Katika hili nitumie maneno mawili ambayo yote kwa lugha yetu yanatafsiriwa kama "Maadili"; Morality na Ethics. Ingawa yote yanahusiana, maana yake kwa ujumla ina mstari mwembamba. Kuna maadili yanayoongoza jamii nzima katika kuamua matendo fulani ni mema au maovu, mazuri au mabaya. Kila jamii ina mambo ambayo yanakubalika kuwa ni mema na mengine ambayo yanakatazwa. Matendo haya mara nyingi hutegemea mafunzo ya dini, na tamaduni yanapotendwa. Wakati Tanzania kuoa mke zaidi ya mmoja inakubalika na kutambulika kisheria na swali la umaadili halipo, nchi kama Marekani jambo hilo ni marufuku na linaonekana ni kinyume na maadili mema (immoral). Hata hivyo kuna matendo ambayo watu fulani hutarajiwa kutenda na hukatazwa kutenda kutokana na ajira zao au nafasi zao. Mara nyingi matendo haya hayajali hasa dini au tamaduni bali yanajali zaidi athari zake katika jamii na wahusika (ethics).
Ndugu zetu wanatuhumiwa kuvunja yote mawili: Hilo la pili la (ethics) tunaweza kujadiliana uzito wake kwa wadaiwa, hilo la kwanza kwa wengi halina ubishi.
Kitu ninachokataa ni kujaribu kufanya makosa yao kuwa ni kuvunja ethics za kazi na za uongozi wa Taifa. Hivi ni wapi Chadema iliposema kuwa kitendo cha zinaa nje/kabla ya ndoa ni kosa linalohitaji kuombewa radhi? Nimeangalia kwenye Kanuni za Maadili ya CCM hakuna kosa hilo!! Haijatokea kiongozi kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa vile amelala na fulani!! Je hilo linahalalisha vitendo hivyo? La hasha! Ila jambo moja linatuambia ni kuwa vitendo hivyo havilingani na rushwa, wizi, matumizi mabaya ya madaraka, kutoa siri za chama n.k!! Ni kweli AC na KZ watakuwa wameghafilika kwa kujihusisha na vitendo wanavyodaiwa kufanya, lakini kulinganisha matendo hayo na uhalifu na matendo yanakatazwa kisheria siyo kitendo cha haki hata kidogo!!
Nimalizie kwa pointi hizi mbili:
1: Hapa niseme hivi: Msingi wa kufukuzwa AC kutoka CCM itakuwa ni madai ya kuwa kutokana na mahusiano yake (ya mapenzi au vinginevyo) na Zitto basi alikuwa anapenyeza siri za CCM kwa mbunge huyo wa upinzani. Kaeni chonjo, kwani kikao cha Kamati Kuu kinafanyika mwishoni mwa juma hili!
2: Kwa wale ambao tunamuita Zitto ni rafiki, tusimshawishi hata chembe kulizungumzia jambo hili hadharani sasa ila alishughulikie na watu wake wa karibu. Zitto ASILIZUNGUMZIE jambo hili hadi itakapojulikana Amina atasema nini na CCM itachukua hatua gani. DON'T let him play his cards, hadi atakapoona kadi za CCM zimechezwa, why you may ask;
IT IS POLITICS after all!!!