Mengi ataka DPP aifichue Kagoda
Theopista Nsanzugwanko
Daily News; Tuesday,November 18, 2008 @21:15
Mwenyekiti wa Shirikisho la Wenye Viwanda Nchini (CTI) Reginald Mengi, amemwomba Mkurugenzi wa Mashitaka ya Jinai (DPP) kutoa ufafanuzi kuhusiana na kampuni ya Kagoda ambayo ni miongoni mwa kampuni 22 zilizochota Sh bilioni 133 Benki Kuu.
"Tunataka tuelezwe Kagoda ni kitu gani?" Alihoji Mengi wakati akimshukuru Makamu wa Rais, Dk Mohamed Shein Mara baada ya kufungua Maadhimisho ya 19 ya Viwanda ya Afrika na sherehe ya miaka 10 ya Taasisi ya Sekta binafsi Dar es Salaam jana.
Kampuni ya Kagoda inadaiwa kuchota Sh bilioni 40 lakini hadi sasa wamiliki wake hawajafikishwa mahakamani. Inadaiwa kuwa baadhi ya vigogo wa kisiasa na wafanyabiashara wakubwa ndio wamiliki wa kampuni hiyo.
Mengi alimuomba Makamu wa Rais kufikisha pongezi kwa Rais Jakaya Kikwete kwa jinsi alivyoshughulikia suala la Madeni ya Akaunti ya Nje (EPA) kitu kilichoonyesha jinsi nchi hii ilivyo na utawala wa sheria.
Lakini pia aliomba Mkurugenzi wa Mashitaka kuondoa kiu kwa wananchi kwa kuwaeleza kuwa Kagoda ni mdudu gani? Au ni kitu gani? Kutokana na wananchi wengi kwa sasa kutokuwa na uelewa. "Naomba kwa kumalizia DPP utusaidie kutuelezea kuwa Kagoda ni mdudu gani na wa aina gani na ikiwezekana kutueleza hii Kagoda ni nini ili kutuondolea kiu tuliyonayo sisi wenye viwanda pamoja na wananchi"anasema.
Mengi alisema ingawa si sehemu yake ya kuzungumzia suala hilo; lakini kwa kuwa amepata nafasi ya kuzungumza alisema ni bora kutoa pongezi kwa Rais alivyolishughulikia vyema suala hilo kwani watu wengi walijua baada ya fedha kurudishwa ingekuwa mwisho wa suala hilo.
Alisema kitendo cha majalada yote kupelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kimeonyesha jinsi nchi ilivyo chini ya utawala wa sheria na kumtaka DPP kuharakisha katika kutolea uamuzi suala hilo. Tayari Mkurugenzi wa Mashitaka ya Jinai (DPP) Eliezer Feleshi amewataka wananchi waiachie ofisi yake kushughulikia kesi za ufisadi wa mabilioni ya fedha yaliyochotwa katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA).
Feleshi katika taarifa yake kwa vyombo vya habari hivi karibuni, alifafanua kuwa licha ya kuwa ofisi yake ni ya umma lakini inafanya kazi bila kuingiliwa na mtu au mamlaka yoyote."Kwa msingi huo ninawaomba wananchi kuwa na subira na kuiacha ofisi kufanya kazi yake kwa mujibu wa sheria," alisema Feleshi.
Alisema majalada yote yanayohusiana na EPA yamewasilishwa kwake na yanaendelea kufanyiwa kazi. "Kama mnavyoshuhudia baadhi ya watuhumiwa wamepelekwa mahakamani." Aliongeza kuwa kwa majalada ambayo yanahitaji uchunguzi zaidi yanaendelea kufanyiwa kazi kama alivyoelekeza vyombo vya uchunguzi.