hizi ndiyo notes nilizotumia katika warsha masasi, mbeya, dodoma na arusha. Imeripotiwa katika gazeti la uhuru (licha ya kichwa cha habari kuwa spinned, habari yenyewe ilikuwa sahihi kabisa). Baadae mheshimiwa Chacha akatoa maoni yake, ambapo yupo huru kabisa kutoa maoni yake kama Mtanzania. Leo pia nimesoma katika mwananchi kuwa mimi Chacha twaleta mgawanyo ndani ya chama.
Sihitaji kujitetea hapa, hata hivyo mimi sikutoa maoni yangu katika gazeti, ila wakati nawasilisha mada kwa vyovyote vile waandishi walikuwapo.
Mimi kama mtu niliyesomea uchumi, ninajua ukweli kuwa uchumi wetu unakua. Tatizo tulilonalo ni kwamba 'base' ya uchumi wetu ni ndogo hivyo ukuaji haui mpana ie not broadbased growth. Mbaya zaidi, sekta ya Kilimo haikui, ambayo ndiyo inasababisha broadbased growth. Sekta zinakua ni madini na utalii, ambazo mahusiano yake na sekta nyingine ni madogo ie forward and backward linkages. Changamoto tulizonazo ni haya mahusiano.
Nilitoa mfano mmoja pale Arusha: kwamba kama tuna lengo la kuleta watalii milioni moja kwa mwaka nchini, tumejiandaa vipi kuhakikisha kuwa Mkoa wa Singida unazalisha Kuku wengi na Mayai mengi zaidi? Kama kila mtalii atakula mayai 2 breakfast kwa siku na atakaa nchini siku 5 maana yake ni kuwa watu wa singida wazalishe mayai milioni 10 ya kuku wa asili. Kama kila yai ni sh 100, inaa maana umeingiza 1 bilioni katika kuku subsector mkoani Singida. Hii ndio maana ya linkages, na kwa kuwa hakuna linkages tuna import kuku na mayai kutoka Brazil!!!!
Mfano mwingine nikawaambia, kule Geita Gold Mine wafanyakazi wanakula Nyama kutoka Kenya. Kimsingi Ng'ombe hutoka usukumani na kupelekwa Kisumu. Kule wanachinja, wanapack na kuuza Geita. Hivyo Mgodi wa Geita unatengeneza ajira Kisumu Kenya. Tulipoita investors, tulipaswa kuweka mazingira haya kwani sekta za uchumi zinaingiliana ie multiplier effect. Na hapa ndio kazi ya State Intervention kwenye soko. Sisi tukawa makuadi wa soko huria.
Uchumi wetu unakua, drivers of growth ni Mining and quarrying na Trade ie tourism. Twapasa kuweka links za sekta hizi na sekta nyingine na pia kukuza rural growth ili kupunguza umasikini. Hizi ni facts, undisputable facts!
These are my talking notes, nimeshindwa kuattach, network ipo slow
===================================
TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA MKUKUTA MWAKA 2006/2007
Kabwe, Z.Z, Disemba 2007
• Taarifa ya utekelezaji wa MKUKUTA ni moja ya matokeo ya mfumo wa ufuatiliaji wa MKUKUTA. Lengo la kuzalisha ripoti hii ni kuchangia katika mfumo mzima wa kutoa taarifa kwa mawizara, serikali za mitaa na hata Asasi Zisizo za Kiserikali (AZISE). Taarifa inatoa kwa ufupi mafanikio na changamoto zilizofikiwa katika kufikia malengo ya MKUKUTA.
• MKUKUTA una lengo kubwa la kukuza uchumi na kupunguza umasikini. Hata hivyo wananchi wamekua na maswali mengi sana kuhusiana na takwimu za ukuaji wa uchumi. Kwa mfano, mbona takwimu haziendani na hali halisi za maisha ya wananchi? Mbona kila kukicha hali ya maisha inakuwa ngumu sanjari na mfumuko wa bei?
• Uvumbuzi wa maswali hayo na changamoto za kupambana na umaskini zinaweza kufaulu iwapo kila mdau atauelewa, kisha kushiriki katika utekelezaji wa Mkakati wa Kukuza Uchumi na kupunguza Umaskini Tanzania (MKUKUTA). Pia taarifa za mwaka za utekelezaji wa MKUKUTA ni muhimu sana katika kuelewa hatua ambazo zimefikiwa.
• MKUKUTA mbali na kuainisha nyenzo na rasilimali za ndani na nje za kupambana na umaskini, umebeba pia malengo ya dira ya taifa 2025 na malengo ya milenia ambayo yanadhamiria ifikapo mwaka 2015 umaskini wa kipato uwe ndoto duniani.
• Katika mwaka wa kwanza wa utekelezaji wa MKUKUTA taarifa zilizokusanywa zinaonyesha ukuaji wa uchumi unaendelea vizuri, ingawaje mwaka 2006 uchumi ulitetereka kidogo kutokana na tatizo la ukame na kuathiri Sekta za Kilimo, uzalishaji viwandani, umeme na maji.
• Rekodi ya ukuaji wa uchumi hapa nchini toka mwaka 1993 hadi 2000, inaonyesha kulikuwa na ukuaji mdogo wa uchumi toka asilimia 0.4 hadi kufikia asilimia 4.9, lakini kuanzia mwaka 2001, uchumi uliendelea kukua kwa asilimia 5.7 na hadi 2005 ukuaji wake ulifikia asilimia 6.7 na kushuka kidogo kufikia asilimia 6.2 mwaka 2006. Lengo la MKUKUTA ni kufikia ukuaji wa uchumi wa wastani wa asilimia 6-8 mpaka mwaka 2010. Ukame na tatizo la umeme ni moja ya matatizo yaliyopelekea kushuka kwa kasi ya ukuaji wa uchumi mwaka 2006.
• Ukuaji wa kisekta kuanzia mwaka 2000 ukuaji wa kisekta unaonyesha kushuka. Mchango wa kila sekta katika ukuaji wa uchumi unategemea sana ukuaji wa sekta husika. Hata hivyo, kilimo kimeendelea kuwa mchangiaji mkubwa wa uchumi. Sekta ya kilimo ilichangia asilimia 44 ya Pato la Taifa mwaka 2006
• Ukuaji wa sekta ya kilimo ni kwa wastani wa asilimia 4.7 katika kipindi cha mwaka 2000 hadi 2006, kiasi ambacho hakitoshelezi kufikia malengo ya kuondosha umaskini yaliyomo kwenye MKUKUTA. Lengo ni kuwa ifikapo 2010 kuwa na kilimo endelevu kinachokua asilimia 8 - 10. Mwaka 2005 sekta ya kilimo ilikua kwa asilimia 5.1 na mwaka 2006 ilikua kwa asilimia 4.1 na hivyo iliporomoka. Ukame ulikuwa ni sababu kubwa ya kuporomoka kwa ukuaji wa sekta ya kilimo.
• Madini ndiyo sekta inayoibuka kwa kasi, imekua haraka kwa kiwango cha asilimia 15 kati ya mwaka 2000 na 2006. Hata hivyo mchango wake katika uchumi mkuu bado ni mdogo ukuaji wa sekta ya madini bado haujachangia kwa kiasi kikubwa kupunguza umaskini kwenye maeneo ya uchimbaji. Mwaka 2006 sekta ya madini ilikua kwa asilimia 16.8. Hata hivyo mchango wa sekta hii katika Pato la Taifa ni asilimia 3.8 tu. Lengo ni kufikia mchango wa sekta ya Kilimo katika Pato la Taifa kuwa asilimia 10.
• Sekta ya uzalishaji viwandani nayo imeanza kukua, inakua kwa kiwango cha asilimia 7.5 kuanzia mwaka 2000. Hata hivyo mchango wake kwa pato la taifa bado ni mdogo, unafikia asilimia 8 tu.
• Sekta ya biashara, migahawa na hoteli ambayo inaashiria kushamiri kwa sekta ya utalii, imekuwa kwa kiwango cha asilimia 7.3. Sekta ya Utalii kwa kuwa ina mchango wa moja kwa moja katika pato la taifa, pia inachangia katika sekta nyingine za kiuchumi, lakini bado utalii haujatumika vizuri kukuza pato la taifa na hata kusaidia kuondosha umaskini wa wananchi.
Viashiria vya ukuaji wa uchumi
• MKUKUTA unakusudia kuhakikisha kuwa kuna usimamizi mzuri wa ukuaji wa uchumi endelevu. Kuanzia katikati ya mwaka 1990, kipaumbele kiliwekwa katika ukuaji wa uchumi mdogo na muundo wa usimamizi wa fedha za umma ukizingatia kudhibiti matumizi ya serikali. Hali hiyo imesaidia kupunguza mfumuko wa bei mwaka 2003. Lakini kuanzia mwaka 2004 kumekuwa na ongezeko la mfumuko wa bei ambao unaweza ukaashiria kuwa kuna ongezeko la matumizi ya serikali.
• Mwenendo wa mfumuko wa bei kuanzia mwaka 2000 hadi 2006 ni kama ifuatavyo:
Mwaka Mfumuko wa bei
2000 6.0
2001 5.1
2002 4.3
2003 5.3
2004 4.7
2005 5.0
2006 7.3
• Mwaka 2006 mfumuko wa bei uliongezeka kwa asilimia 7.3. Hali hiyo pia ilionekana katika miezi ya mwanzo ya mwaka huu (2007). Hali hiyo ilisababishwa na ukame uliotokea nchini mwaka 2005/06 ulioathiri uzalishaji wa umeme na hata uzalishaji wa chakula. Kadhalika katika kipindi hicho kulikuwa na ongezeko la mara kwa mara la bei ya mafuta ya petroli.
• Yapo maendeleo yanayoonekana ya kiuchumi ambayo yametokana na kuimarisha kwa mfumo wa utozaji kodi. Makusanyo ya kodi za ndani yameongezeka kutoka asilimia 12.2 mwaka 2000/01 hadi 15.6 mwaka 2006/07. Lengo ni kufikia mapato ya ndani kuwa 25% ya Pato la Taifa.
• Hata hivyo pamoja na kuongezeka kwa makusanyo ya kodi ya mapato lakini matumizi ya fedha za umma nayo pia yameongezeka.Kwa kawaida kuna matumizi ya aina mbili; Kwanza ni yale yanayoongeza Tija na ambayo huimarisha upatikanaji wa huduma za jamii. Hali inaonyesha kuwa kuanzia mwaka 2001 kuna upungufu katika utoaji wa huduma za jamii.
• Ili kufikia malengo ya MKUKUTA kuna haja ya kuwepo kwa uunganishaji mzuri baina ya malengo ya kuuimarisha uchumi mkuu na huduma za jamii sambamba na kupunguza matumizi ya serikali kwa kiasi kikubwa na kuwekeza katika shughuli za kiuchumi.
Uwiano wa kibiashara
• Sekta binafsi inakua vizuri tokea mwaka 2000 hii inatokana na kuwepo kwa mazingira mazuri ya kukopa kutoka katika taasisi za fedha zilizopo nchini na kufanya biashara, kwani mwaka 2006, sekta binafsi imepata asilimia 12.5 ya mikopo.
• Hata hivyo pamoja na kuwa kuna dalili nzuri za matumaini katika upatikanaji wa mikopo, mazingira haya bado hauwanufaishi wengi, wanaofaidi ni wajasiriamali wakubwa wenye mitaji imara na wengi wao wanaoishi mijini.
• Kuna matarajio makubwa ya Tanzania kuvutia wawekezaji wengi wa nje. Lakini ili hilo liwezekane, inabidi jitihada zaidi zichukuliwe kwa serikali kuendelea kuboresha vivutio na miundombinu ili wawekezaji waweze kuzalisha bila gharama kubwa .
Ukosefu wa ajira
• Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2006, inakadiriwa kuna zaidi ya watu milioni 18 wenye nguvu ya kufanya kazi hapa nchini. Ongezeko hili ni kubwa, ikilinganishwa na mwaka 2000/01 ambapo kulikuwa raslimali watu milioni 3.3.
• Hili ni ongezeko la asilimia 4.1 kwa mwaka (watu 800,000 huingia katika soko la ajira kila mwaka).Watu wapatao milioni 16.6 ambao ni asilimia 80.3 ya watu wenye uwezo wa kufanya kazi, wanafanya kazi, ingawa wengi wao wamejiajiri au wanafanya biashara ndogondogo na wengine wanafanya kazi majumbani ambazo hazina mishahara.
• Katika miaka michache iliyopita, uchumi wa Tanzania umeweza kupunguza kwa kiasi kidogo tatizo la ajira mijini MKUKUTA unadhamiria kupunguza Ukosefu wa ajira kutoka asilimia 12.9 mwaka 2000/01 hadi asilimia 6.9 mwaka 2010.
• Tatizo la ukosefu wa ajira haliwezi kushughulikiwa endapo ukuaji wa uchumi hautoshelezi. Ni makosa makubwa kuliona tatizo hilo kama mzigo kwa jamii ni vema msukumo ukawekwa katika ajira na sera za kazi na mikakati ya kuongeza ukuaji wa uchumi.
Mtandao wa barabara
• Kuwa na miundombinu imara kunaashiria kuwa na uchumi imara. Ingawa Uchumi wa Tanzania bado haujaimarika vizuri, tatizo la miundo mbinu limeainishwa katika Taarifa ya utekelezaji wa MKUKUTA.
• Ubora wa mtandao wa barabara kuu na za mikoa umeshuka kutoka asilimia 84 mwaka 2005 mpaka asilimia 78 mwaka 2006. Sababu kubwa iliyosababisha hali hii ni ufinyu wa Bajeti na kuchelewa kwa ahadi za misaada kutoka nje.
Kuboresha Maisha na Ustawi wa Jamii
Elimu
• Lengo kubwa la MKUKUTA ni kuhakikisha kuwa watoto wengi wanajiunga na shule za msingi na sekondari na pia ubora wa elimu unaimarishwa. MKUKUTA umesisitiza sana umuhimu wa watoto wa kike kuingia shuleni.
• Taarifa ya MKUKUTA inaonesha kuwa Tanzania imefanikiwa kuvuka lengo la kuandikisha wanafunzi wa darasa la kwanza kwa kufikia asilimia 114 mwaka 2006. Lengo lilikuwa asilimia 99 ifikapo mwaka 2010.
• Kwa upande wa elimu ya sekondari MKUKUTA uliweka lengo la kufikia asilimia 50 ya vijana wanaomaliza elimu ya msingi kujiunga na elimu ya sekondari ifikapo mwaka 2010. Lengo hili pia limevukwa kwani mwaka 2006 asilimia 68 ya vijana waliomaliza darasa la saba.
• Changamoto kubwa iliyopo ni ubora wa elimu. Shule nyingi hazina walimu wa kutosha na hata vifaa vya kutosha vya kufundishia.
Afya
• MKUKUTA umeweka malengo kadhaa katika sekta ya Afya. Kwa mfano, lengo la kupunguza vifo vya watoto kutoka vifo 95 mwaka 2002 mpaka vifo 50 mwaka 2010 kati ya watoto 1000 wanaozaliwa. Mwaka 2006 vifo vya watoto vilifikia 68 kati ya watoto 1000 wanaozaliwa.
• Vile vile vifo vya watoto chini ya miaka 5 vililengwa kupunguzwa kutoka vifo 154 mpaka vifo 79 ifikapo mwaka 2010. Mwaka 2006 vifo 133 vya watoto chini ya miaka 5 watoto 1000 vilirekodiwa.
• MKUKUTA pia uliweka lengo la kupunguza kudumaa (stuntedness) asilimia 43.8 mpaka asilimia 20 mwaka 2010. Mwaka 2006 kiwango cha kudumaa kilifikia asilimia 38. Changamoto ni kuongeza lishe kwa watoto ili kuondokana na tatizo hili ambalo kwa kweli ni janga kubwa sana kwa Taifa. Janga lisilozungumzwa kabisa ambalo lina madhara makubwa kwa ustawi wa Taifa. Changamoto nyingine ni kuboresha matibabu ya magonjwa ya watoto.
Utawala na Uwajibikaji
• Utawala bora ni moja ya nguzo muhimu sana katika kuhakikisha ukuaji mpana wa uchumi na uboreshaji wa maisha ya wananchi. Vigezo viwili vinaangaliwa sana, navyo ni jinsia na rushwa.
• Uwakilishi wa wanawake katika vyombo vya maamuzi umeongezeka mpaka kufikia asilimia 30.4 katika Bunge na asilimia 26.8 katika Halmashauri za Wilaya.
• Idadi ya kesi za rushwa ambazo zilizorekodiwa na PCCB zimeongezeka kutoka kesi 1244 mpaka 3121. Inawezekana kesi hizi zimeongezeka kwa sababu mwamko wa wananchi umeongezeka au kiwango cha rushwa kimeongezeka.