Mzee Mwanakijiji
Platinum Member
- Mar 10, 2006
- 33,478
- 40,000
Na Hassan Abbas
UONGOZI wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) leo huenda ukajitia kitanzi utakapotoa hatma ya viongozi wa Serikali ya Wanafunzi (DARUSO) ambao ni miongoni mwa 56 waliokuwa wamesimamishwa awali.
Wakati 'vinara' hao wa mgomo wakianza kuhojiwa asubuhi hii, hali ya mambo katika chuo hicho inaonesha dhahiri kuwa wanafunzi wamejipanga kupinga uamuzi wowote wenye madhara kwa wenzao, uongozi wa chuo utakapotoa uamuzi wake leo mchana.
Jana wakati wanafunzi waliosimamishwa wakiendelea kukamilisha taratibu za utetezi wao, ziliibuka fununu chuoni hapo kuwa huenda baadhi yao wakasamehewa na wengine kukumbwa na 'fagio la chuma.'
"Hizo taarifa zimeenea hapa chuoni, lakini hakuna mwenye uhakika nazo," alisema mmoja wa wabunge wa chuo hicho na kuongeza:
"Sisi tunasubiri hatma itakayotangazwa na mara tu tutakapopata taarifa rasmi, Bunge letu litakaa kujadili kitakachokuwa kimeamuliwa."
Jana mamia ya wanafunzi wa kampasi ya Mlimani wakiwa na baadhi ya viongozi wao wa DARUSO waliosimamishwa walikusanyika kwenye uwanja maarufu chuoni hapo wa Rodney Revolution Square, ambapo lilipitishwa azimio la kukutana tena kesho, mara baada ya hatma ya wenzao kutangazwa.
Akizungumza na Majira, Makamu wa Rais wa DARUSO, Bi. Renedata Rushau, alisema wanafunzi wote ndio watakaokutana hapo Rodney Square kesho saa tisa alasiri na kuamua wafanye nini iwapo kutakuwa na uamuzi unaowaumiza wenzao.
"Azimio lililofikiwa leo ni wanafunzi wote kesho kukusanyika, ili watoe maoni yao na kisha Bunge la Wanafunzi litakaa kutangaza kile kitakachopaswa," alisema.
Juzi akizungumza na gazeti hili, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Rwekaza Mukandala, alisema chuo kinatarajia kulimaliza suala hilo katika namna ambayo itarejesha amani na utulivu.
Wakati huo huo, Agness Mayagila, anaripoti kutoka Arusha, kwamba
Kurugenzi ya Vijana Taifa ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) imepongeza uamuzi wa uongozi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam kuwarejesha wanafunzi wote waliokuwa wamesimamishwa masomo yao kutokana na mgomo wakiishinikiza Serikali kuwakopesha asilimia 100 ya ada na mahitaji mengine.
Taarifa ya Uongozi wa Chuo Kikuu hicho, ilisema kuwa idadi ya waliotimiza masharti ya kurejea chuoni ni asilimia 41 jambo linaloonesha kuwa Watanzania wengi hawana uwezo wa kujilipia gharama za masomo.
Aidha, taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na kusainiwa na Mkurugenzi wa Vijana wa CHADEMA, Bw. John Mnyika, ilisema waliotimiza masharti walifanya hivyo kwa kujibana sana, ikiwa ni pamoja na kuuza mali, vifaa vya ndani, kwa lengo la kuhakikisha wanarejea chuoni.
Iliiomba Serikali kutotumia asilimia 41 ya waliolipa kama kiwango cha Watanzania wanaoweza kujilipia, kwani wengi wamelipa kwa shinikizo na hofu ya kupoteza masomo na wamelipia kwa matarajio ya kupatikana ufumbuzi baadaye.
Ilieleza kuwa kwa upande wa pili, wananalaani uamuzi wa Chuo Kikuu kusimamisha wanafunzi 56 wakiwamo viongozi wa DARUSO kwa madai kuwa walitumia nguvu ikiwa ni pamoja na viboko kuwashinikiza wanafunzi wengine wagome.
NB:
Napenda kuwatangazia mapema kuwa endapo uongozi utawapa viongozi wa DARUSO masharti ya kujinyonga ili warudi chuoni, msiwe na shaka HAWATATUABISHA!