SUA nao watimuliwa
Hosteli Mabibo 'walizwa' mizigo yao
NA LATIFA GANZEL, MOROGORO
HATIMAYE wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) wa mwaka wa kwanza na wa pili wamesimamishwa masomo yao kwa muda usiojulikana kutokana na mgomo uliofikia siku tatu tangu Aprili 16, mwaka huu.
Wakati hayo yanatokea, baadhi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, wanaoishi katika hosteli za Mabibo, wameripotiwa kuibiwa mali zao na wenye mikokoteni, wakiwa katika pilikapilika za kuondoka baada ya kusimamishwa masomo.
Kwa upande wa wanafunzi wa SUA, walikutana na majibu hayo baada ya kuandamana kwa kutembea kwa miguu umbali wa kilomita 10 kutoka kampasi yao ya Solomoni iliyopo Mazimbu hadi eneo la utawala la chuo hicho lililopo kata ya Mbuyuni.
Kutokana na hali hiyo, wanafunzi hao walipofika eneo la utawala saa 9 alasiri huku wakiwa wamebeba mabango, walikuta Baraza la chuo hicho limeamua wawe wameondoka chuoni hapo jana saa 12 jioni huku chuo hicho kikiwa chini ya ulinzi wa polisi kuhakikisha kuwa amani haivunjwi.
Baadhi ya mabango waliyokuwa wamebeba wanafunzi hao, yalikuwa na ujumbe wa kutaka wazazi wawaunge mkono, pia kudai uchaguzi wa mwaka 2010 utakuwa mgumu, mwingine ulikuwa ukidai wazazi wao hawana uwezo wa kuwalipia asilimia 40 ya gharama.
Wanafunzi hao wakati wakitoka Mazimbu kuelekea SUA, walikuwa wapatao 2,000, lakini cha kushangaza walikuwa wakipungua kadri walivyokuwa wakikaribia eneo hilo la utawala kwa kuhofia polisi waliokuwa wametawanywa kila eneo la chuo hicho.
Rais wa serikali ya wanafunzi wa chuo hicho, Omari Ali, alisema uongozi wa wanafunzi uliamua kufanya maandamano kutokana na kwamba chuo hicho kilitoa tamko kuwa ifikapo Aprili 27, kila mwanafunzi awe amamaliza asilimia 40 kama ilivyotakiwa.
Mgomo huo wa wanafunzi ulianza Aprili 16, mwaka huu ambapo wanafunzi hao walidai sio mgomo bali ni majadiliano kuhusu maslahi yao jambo ambalo lilifanya uongozi wa chuo hicho kuona kama ni hali ya kawaida.
Juzi, wanafunzi hao walipotakiwa kuingia darasani walidai hawawezi kuingia hadi wajue hatma yao kuhusu asilimia 40 ya gharama za uchangiaji na kuongezwa kiwango cha posho za matumizi ya siku wakiwa katika mazoezi ya vitendo ambayo ni sh. 6,000 hadi ifikie sh. 10,000 kama ilivyoongezwa ya matumizi ya kila siku wakiwa chuoni kutoka sh. 2,500 hadi kufikia sh. 3,600.
Wakati huohuo, baadhi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, wanaoishi hosteli za Mabibo, wameripotiwa kuibiwa mali zao na wenye mikokoteni, wakiwa katika pilikapilika za kuondoka baada ya kusimamishwa masomo.
Uamuzi wa kuwasimamisha masomo ulifikiwa juzi na Baraza la chuo hicho, kufuatia mgomo wa wanafunzi hao uliodumu kwa siku mbili mfululizo wakitaka kuondolewa uchangiaji wa gharama za masomo.
Habari zilizopatikana katika hosteli ya Mabibo zilidai kwamba wizi huo, ulisababishwa na kutokuwepo kwa umakini wa ufuatiliaji wa mizigo hasa kwa wanafunzi waliokuwa wakitumia mikokoteni ya kukodi kuondoa vifaa vyao.
Mmoja wa walinzi wa kampuni ya Full Time Security, ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema wengi wa wanafunzi hao, walikuwa wakihaha kusaka mizigo yao, baada ya wenye mikokoteni kutoweka nayo.
Alisema wengi wao walikuwa wakifika katika eneo la lango kuu na kuulizia iwapo wamewaona vijana waliowakodisha kuchukua mizigo, hali iliyowawia vigumu askari hao kuwatambua.
Kwa mujibu wa askari huyo, pia hali ya msongamano na giza ilichangia kujitokeza kwa upotevu wa mali za wanafunzi hao.
"Kwa kweli ilikuwa inatuwia vigumu kuwasaidia maana utakuta mtu anakuuliza umemuona mtu mwenye mzigo wangu?, alisema askari huyo na kuongeza kuwa ugumu huo ulitokana na msongamano wa wanafunzi waliokuwa wakitoka na mizigo yao.
Katika eneo la kampasi ya Mlimani, Ofisa Uhusiano wa Chuo Kikuu, Julius Saule, alisema hali ni shwari na kwamba wanafunzi walengwa waliondoka kama walivyoamriwa.
Hata hivyo, hakutaka kuzungumzia zaidi hatua zinazofuatia baada ya wanafunzi hao kuondoka kwa maelezo kwamba siyo msemaji.
Wanafunzi hao pamoja na vyuo vishiriki vya Ardhi na Usanifu Majengo (UCLAS), Elimu Mkwawa (MUCE), Elimu Dar es Salaam (DUCE) na Taasisi ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (IJMC), waliamrishwa kuondoka juzi ifikapo saa 12 jioni baada kukaa kuingia madarani licha ya uongozi wa chuo kuwasihi kufanya hivyo.
Katika madai yao wanafunzi hao wanalalamikia malipo ya sh. 3,600 badala ya sh. 6,000 kwa siku kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo ambayo wanadai hailingani na mahitaji halisi.
Pia wanataka kuondolewa kwa sera ya uchangia wa asilimia 40 ya gharama za masomo ya elimu ya juu, wakidai kwamba wanafunzi wengi ni masikini na hivyo itawawia vigumu kuchangia gharama hizo.
Source: Uhuru