ahsante mkuu kwa maelekezo as asked:
MIGOMO CHUO KIKUU INAEPUKIKA
written by
www.saidiyakubu.blospot.com
Chuo Kikuu cha Dar es salaam, katika siku za hivi karibuni kimekuwa katika chati kubwa sio kwa sababu zinazofurahisha, hivi niandikavyo Chuo hicho kimefungwa na wanafunzi wamewekewa masharti mazito wanayotakiwa kuyatimiza ili waweze kurejea. Kwa kadri nionavyo, kuna walakini mkubwa kwenye suala zima la mikopo ya wanafunzi. Kwa tafsiri na nadharia nyepesi, mkopo ni msaada anaopewa mtu kwa lengo la kuurudisha baadae lakini tunavyoona sasa hakuna mazingira kama hayo kwenye utaratibu wetu. Leo nimeona tujadili suala hili kwa kirefu ili kuweza kuishauri serikali ya sasa na kusaidia kuepuka migomo hii inayotokea mara kwa mara:
Vyuo vikuu duniani kote inafahamika ndio msingi mkuu wa uchumi wa nchi husika kwani kwa kiasi kikubwa wahitimu wa vyuo husika huingia katika uchumi wa nchi ama kwa ajira katika idara na makampuni au kujiajiri wenyewe.
Kwa mazingira ya sasa, takriban kila mwanafunzi aliesoma Chuo Kikuu cha Dar es salaam katika miaka ya hivi karibuni, historia yake ya chuo haiwezi kukamilika bila kukutajia ushiriki wake katika mgomo! Kwa asilimi kubwa mikopo na fedha za wanafunzi ndio imekuwa ni tatizo kuu.
Kama hatua madhubuti hazitachukuliwa, kuna hatari ya kuwa na wahitimu nusu nusu kutokana muda mwingi kupotea kwa wanafunzi kuwa katika migomo. Kwa vile tatizo ni mikopo nadhani ni bora kuangalia mfumo mzima kwa lengo la kuutafutia marekebisho maridhawa.
Wanafunzi wengi wamekuwa ''wakikopeshwa'' na serikali ili kumudu gharama za maisha wanapokuwa masomoni lakini kuna tatizo kubwa kwa vile hakuna utaratibu maalum au unaoeleweka wa kukusanya fedha za wanaohitimu, kwa kifupi hivi sasa mwanafunzi akimaliza shule basi ndio anapotea katika rekodi za chuo kwa vile hakuna mtandao wowote madhubuti wa kujua mhitimu husika yupo wapi seuze kumdai fedha alizokopeshwa.
Athari ya hii ni kuwa kumekuwa utumbukizwaji wa fedha za serikali bila ya kuwa na mfumo muafaka wa kukusanya fedha zilizotolewa huko nyuma, serikali zote zilizopita na hata hii ya sasa zimekuwa zikifadhili wanafunzi in disguise manake kama hakuna utaratibu wa kukusanya fedha zilizokwishatolewa huo tena si mkopo!
Kwa hiyo picha inayojitokeza ni kujikanganya kwa idara zinazohusika. Binafsi nikiangalia mfumo wa ukopeshaji wanafunzi hapa Uingereza napata picha kwamba mfumo wa mikopo kwa wanafunzi wa Vyuo vikuu Tanzania unahitaji mabadiliko makubwa sana.
Uingereza hapa mwanafunzi anakopeshwa fedha kwa ajili ya elimu ya juu kutokana na uwezo wake {income based assistance}, lazima mzazi wa mwanafunzi husika au mlezi kujaza fomu maalum akielezea kipato chake na kuna viwango maalum vimewekwa kuwa kwa mapato ya kila mwaka ya mzazi au mlezi husika basi mwanafunzi atapewa msaada kwa kiwango fulani. Kama mzazi wa mwanafunzi husika hana mapato yanayovuka kiwango cha chini kilochowekwa basi mwanafunzi atakopeshwa kwa asilimia mia moja.
Mkopo wenyewe mwanafunzi haanzi kulipia mpaka amemaliza masomo na kuanza kazi, kiwango cha kulipia ni kidogo sana, na si hivyo tu bali serikali kupitia mashirika yasiyo ya kiserikali inatambua hali ya maisha ilivyo hivyo mwanafunzi mpaka aanze kupata kiasi fulani ndio ataanza kulipa deni hilo, huwezi kumaliza chuo ukawa unapata malipo ya kima cha chini ukalazimishwa kulipia.
Deni la Chuo Kikuu Uingereza mwanafunzi hawezi kukwepa! Rekodi za deni husika zimeunganishwa na mamlaka ya kodi na kukatwa moja kwa moja kwa mwajiri kutokea Mamlaka ya kodi, kama kodi ya tatu anayolipa mdau husika. Hili linawezekana licha ya kuwa Uingereza bado hawajaanzisha utaratibu wa vitambulisho kwani wana kadi za bima zinazotumiwa katika kupata ajira.
Kwa Tanzania hili tunaliweza, wengi wa wafanyakazi wa Tanzania ni wahitimu wa vyuo vikuu vyetu vya pale pale nyumbani tunaweza kuwa na utaratibu wa revolving fund, yaani wanafunzi wanakopeshwa kulingana na uwezo na kisha wakiajiriwa hela zinakatwa kama inavyokatwa kodi ya mapato na mamlaka ya kodi Tanzania {TRA} inakuwa ikifanya kazi kwa karibu na mamlaka ya mikopo ya Elimu ya Juu ili kuweza kuwa na 'revolving fund' itakayotosheleza mahitaji ya wanafunzi wote.
Inaweza kusemwa kuwa ni vigumu kuwa na rekodi hizi, lakini mimi sifikiri hivyo kwani kila mwajiriwa hujaza fomu za maombi, hivyo kwa urahisi kabisa muomba kazi akiwa ni mhitimu chuo kikuu basi kuwe na kipengele maalum katika fomu hizo kwa mujibu wa sheria kukubali kukatwa fedha za kurejesha mkopo, kama waajiri wanaweza kulipia mifuko ya jamii na kodi za kichwa naamini wanaweza kusaidiwa na kushirikishwa katika ukusanyaji wa fedha husika na hivyo kiwango kikubwa zaidi kutumika kusaidia vijana na wasomi wetu.
Lakini hapa pia inabidi kuchangia kidogo kuhusu mchango wanaotakiwa kutoa wanafunzi wetu, kwa hivi sasa mwanafunzi anatakiwa kuchangia asilimia arobaini na serikali kumkopesha mwanafunzi husika asilimia sitini. Kwanza kabisa sijui ni vigezo gani vimetumiwa kufikia hiyo asilimia arobaini, kwa utafiti upi, na pili wanafunzi hawa wanatoka katika familia zenye vipato tofauti lakini kwenye kuchangia woote kwa pamoja wanatakiwa kuchangia asilimia arobaini, hii inamuumiza zaidi mwanafunzi anaetoka kwenye familia zenye vipato vya chini.
Hapa ipo haja ya kuiangalia upya sheria inayotaka wanafunzi kuchangia kiwango hicho, ingekuwa mzazi wa mwanafunzi anaepata kuanzia kiwango X kwenda juu anatakiwa kuchangia asilimia arobaini ingekuwa sawa lakini kuweka 'umbrella cap' kwa wote ni kuwanyanyasa zaidi wasio nacho ambao bila shaka ndio wanahitaji zaidi elimu kujikwamua kimaisha.
Njia nyingine ambayo nadhani tunaweza kujifunza kutoka Uingereza ni kuwa na misamaha ya kodi kwa kiwango fulani kwa mashirika na makampuni pale wanapofadhili wafanyakazi wao kusoma elimu ya juu. Hapa Uingereza shirika ambalo linahimiza wanafunzi wake kusoma elimu ya juu kwa kutoa ufadhili hupatiwa 'tax incentives' ambazo kwa hakika zinasaidia wadau wote, serikali kwa kuwa na mzigo mdogo wa kumsomesha mwanafunzi husika, mwanafunzi kwa kujua kampuni inamthamini na hivyo kuongeza ufanisi kazini, kampuni kwa kupata misamaha ya kodi.
Kama tumeweza kutoa misamaha ya kodi kwa makampuni yanayowekeza Tanzania tunaweza kusaidia makampuni ya nyumbani kufadhili wanafunzi kwa kuwapa misamaha hiyo. Huu naamini ndio UWEZESHAJI KWA WATANZANIA.
Nadhani kwa maoni yangu, migomo katika elimu ya juu inaepukika iwapo serikali itakuwa na sera madhubuti zinazoonekana kuwajali wananchi wake ambao wanafunzi ni sehemu muhimu sana. Tusipowathamini na kuwasaidia wanafunzi wawapo katika vituo vyao vya kusoma tutakuwa tunarudi nyuma badala ya kusonga mbele.
Naomba kutoa hoja, nakaribisha maoni kutoka kwa wadau...