SEHEMU YA 35...
Kwa kuvumilia maumivu, Juliana akakubaliana na mumewe, wakaingia ndani ya gari na kuondoka mahali hapo. Hawakuchukua muda mrefu wakafika katika hoteli hiyo ambapo akachukua chumba na kwenda na mkewe.
Wakatulia huko, muda mwingi alikuwa akimpigia simu Juliet kwa lengo la kumsisitiza kwamba alitakiwa kuonana naye haraka sana. Hilo halikuwa tatizo, baada ya dakika ishirini, msichana huyo akafika na kwenda ndani ya chumba hicho alichoambiwa kwamba Gideon alikuwepo akimsubiri.
Alipoingia na macho yake kutua kwa mwanaume huyo, akamfuata na kumkumbatia kwa furaha. Gideon hakuonyesha tofauti yoyote ile, naye akamkumbatia huku mke wake, Juliet akiwa bafuni akisubiri muda wa kuambiwa atoke.
“Hongera sana kwa kazi nzito!” alisema Juliet huku akiachia tabasamu.
“Nashukuru! Ila ningependa kwanza nikwambie kitu kimoja,” alisema Gideon.
“Kitu gani hubby?”
“Ninampenda mke wangu!” alisema Gideon.
“Unampenda mke wako? Kashakufa tayari! Tuanze maisha mapya hubby!” alisema Juliet.
“Hapana! Mke wangu hajafa.”
“Hajafa?”
“Juliet! Ninampenda mke wangu. Hujui tulipotoka, nilimpenda kwa kipindi kirefu sana, tangu tulipokuwa shuleni. Nilikuwa masikini, mwanamke yule alinipenda hivyo hivyo, sikuwa na kitu, alinionyeshea mapenzi ya dhati. Nilimthamini sana.
Uliponiambia nimuue, nilikubaliana nawe, sikukumbuka kitu chochote kile kuhusu mimi na yeye,” alisema Gideon na kuendelea:
“Ni mwanamke mzuri, hajawahi kunikosea, ananipenda. Juliet! Mke wangu ni mke mwema, sikuweza kumuua mwanamke yule, ni mzuri sana, mcha Mungu! Nitamuua vipi? Siwezi!
Nikwambie tu Juliet, ninampenda mke wangu, ninampenda sana, haijalishi ni mgonjwa, ninampenda mno, ninampenda kwa kiasi kwamba siwezi kuelezea. Kama ulitarajia nimuue, hicho ni kitu ambacho hakiwezi kutokea, siwezi kumuua mwanamke ninayempenda toka moyoni mwangu,” alisema Gideon huku machozi yakimtiririka mashavuni mwake.
Juliet alivimba kwa hasira, hakuamini kile alichokisikia, alimwamini Gideon na kuona kwamba angefanya kile alichomwambia akifanye lakini matokeo yake akamwambia kwamba hakukifanya kwa kuwa tu alikuwa akimpenda mke wake.
Je, nini kitaendelea?