Juliana - Erick Shigongo

Juliana - Erick Shigongo

SEHEMU YA 18...

Gideon akatoka kuoga, akalivua taulo lake na kukaa kitandani. Alimwangalia mpenzi wake, Juliana, kwa jinsi alivyoonekana, hakuonekana kama alivyokuwa ameelekea bafuni, alibadilika na kwa jinsi uso wake ulivyokuwa, ilionyesha kabisa kwamba kulikuwa na kitu.

Hakujua ni kitu gani kilitokea, ila cha kwanza kabisa akaiangalia simu yake, alitaka kujua kama ilikuwa salama. Akatoa password na kuingia huku akizuga kuangalia kama kuna ujumbe au kupigiwa simu.

Akaenda kotekote, hakukuta ujumbe wowote wala simu iliyopigwa kwani wakati Juliana ametuma ujumbe kwa Halima, aliufuta ujumbe wake. Gideon akajiridhisha kwamba hakukuwa na kitu kibaya, sasa kwa nini mpenzi wake alibadilika hivyo?

“Kuna nini? Mbona upo hivyo?” aliuliza Gideon huku akimwangalia Juliana.
“Hakuna kitu! Kichwa kinaniuma sana, kimeanza ghafla, yaani sina raha mpenzi,” alisema Juliana huku akikishika kichwa chake.
“Pole sana jamani! Hebu sogea huku kwanza,” alisema Gideon, Juliana akasogea na kisha kumkumbatia.

Alilihisi joto la mwili wa msichana huyo, lilikuwa kali lililomfanya kujisikia vizuri kabisa kutokana na uwepo wa mvua zilizokuwa zikiendelea kunyesha. Walikumbatiana kwa dakika kadhaa na msichana huyo kuaga, siku hiyo hata kusindikizwa hakutaka.

Njiani alikuwa na mawazo tele, moyo wake ulimuuma, kitu kilichokuwa akilini mwake ni kwamba Gideon alikuwa akitoka kimapenzi na Halima. Kwa nini amsaliti? Kwa nini mchukue msichana huyo na wakati alikuwa naye kipindi hicho.

Akafungua WhatsApp kupitia kwa namba yake nyingine ambayo alimpa Halima. Alitaka kuangalia kama kungekuwa na ujumbe wowote ule, kabla ya kufanya chochote akabadilisha picha na kuweka ya Gideon.

Alikaa na kuangalia huko, hakukuwa na ujumbe wowote ule lakini baada ya dakika chache akapokea ujumbe kutoka kwa msichana huyo ambaye alikuwa akilalamika.

“Kwa nini umenifanyia hivi?” aliuliza Halima kwa kupitia ujumbe mfupi WhatsApp, tena aliweka na emoj ya kulia.
“Nimekufanyaje jamani?” aliuliza Juliana kwa namba ile aliyojifanya Gideon.
“Hebu niambie kitu kimoja! Unanipenda?” aliuliza Halima.

Itaendelea.
 
SEHEMU YA 19...

“Daah! Unanipa wakati mgumu sana! Kwani wewe unanipenda?” aliuliza Juliana.
“Ndiyo! Tena sana lakini sijui kwa nini umekuwa ukinikataa!” alijibu Halima.
“Kwani nilikwambiaje?”

“Najua una mpenzi! Unampenda sana lakini naomba unipe nafasi. Ninakupenda mno, kinachoniumiza, nimekutumia picha zangu za utupu, umenitukana, mbaya zaidi umekwenda kumpa rafiki yako! Kwa nini unanifanyia hivi jamani Gideon?” aliuliza Halima huku akilalamika.

Mpaka kufika hapo, tayari Juliana alipata picha juu ya kila kitu kilichokuwa kimetokea. Akashusha pumzi nzito, akashukuru Mungu kwani ni kweli msichana huyo alimpenda mpenzi wake lakini Gideon alimuonyeshea msimamo thabiti kwa kumwambia kwamba alikuwa na mtu na asingeweza kuwa naye.

Moyo wake ukazidi kumpenda mwanaume huyo, alionekana kuwa imara, mwenye msimamo ambaye hakuwa akiteteleka hata kama alipendwa na msichana mrembo kiasi gani.
“Kama nilivyokwambia! Siwezi kumuacha mpenzi wangu kwa ajili yako,” aliandika Juliana.

“Sawa. Ila ulichonifanyia sijapenda,” aliandika Halima.
Juliana akaamua kuachana na msichana huyo na kuendelea na mambo yake. Bado moyo wake ulikuwa kwa Gideon, alijua fika kwamba mpenzi wake huyo alikuwa mzuri wa sura, aliwatetemesha wanawake wengi hivyo kitendo cha kutokuwa naye karibu kilimaanisha kwamba angewapa nafasi wanawake wengine kumfuatafuata.

Mapenzi yakaendelea mpaka walipomaliza chuo. Kitu cha kwanza kabisa alichokifanya Gideon ni kwenda nyumbani kwa kina Juliana na kuzungumza na wazazi wake. Aliwaambia ukweli jinsi alivyokuwa akimpenda msichana huyo na alikuwa na malengo naye ya kumuoa na kuwa mke wake maisha yake yote.

“Una uhakika unampenda binti yangu?” aliuliza Mzee Marcel huku akimwangalia Gideon.
“Ninampenda mzee! Nisingekuwa nampenda, nadhani nisingefika mahali hapa,” alijibu Gideon huku akitoa tabasamu pana.

“Basi sawa. Kama mmependana mimi nitasema nini sasa! Sina msemo au mama hapa,” alisema Mzee Marcel na kumgeukia mkewe.
“Hata mimi sina! Cha msingi ni kumuomba Mungu mpaka watakapofunga ndoa,” alisema mama yake Juliana.

Itaendelea.
 
SEHEMU YA 20...

Baada ya miezi minne, wawili hao wakafunga ndoa na kuwa mume na mke. Kwa kuwa Gideon hakuwa akijiweza sana, akapewa milioni hamsini kwa ajili ya kufanya biashara. Hiyo ilikuwa nafasi kubwa kwa mwanaume huyo, hakutaka kuona akishindwa, akaingia katika kazi ya kilimo, akakodi mashamba na kuanza kulia mahindi na nafaka nyingine.

Hiyo ndiyo ikawa biashara iliyomuinua kutoka pale alipokuwa. Akaanza kutengeneza pesa pamoja na mkewe. Muda wote walishirikiana wao wawili, biashara ikakua, wakaingiza mamilioni ya shilingi na kufanikiwa kuwa matajiri wakubwa.

Ndani ya kipindi kifupi, wakajenga jumba lao kubwa na la kifahari na kununua nyumba nyingine. Wakawekeza katika ardhi na kila kitu walichokuwa wakikifanya, Mungu akawabariki zaidi na kuyafanya maisha yao kuwa na furaha, amani na mapenzi tele.
“Nikwambie kitu mume wangu?” aliuliza Juliana.

“Niambie!”
“Sikuona siku zangu! Nina uhakika kwamba nina mimba,” alisema Juliana huku akimwangalia mumewe kwa uso uliokuwa na tabasamu pana.
“Kweli?”
“Kweli tena!”

Gideon akamsogelea mkewe na kumkumbatia. Moyo wake ukawa na furaha tele, hakuamini kama mkewe alikuwa na mimba kwani kitu pekee alichokuwa akikihitaji sana kipindi hicho kilikuwa ni mtoto tu.

Alikuwa na kila kitu, utajiri, alikwenda alipotaka kwenda lakini suala la kutokuwa na mtoto ndilo lililokuwa likimtesa usiku na mchana, kitendo cha mkewe kusema kwamba alihisi alikuwa na mimba, kikampa fura tele.
Baada ya wiki mbili, akaenda kupima, akaambiwa kwamba alikuwa mjauzito kitu kilichompa furaha.

Mapenzi yakaongezeka, kila wakati Gideon alikuwa akimpigia simu mkewe kumjulia hali. Alimuomba Mungu kila siku kwamba siku ya kujifungua mkewe ajifungue salama kabisa.
“Hamjambo!” alisalimia Gideon huku akimwangalia mkewe.
“Hatujambo?”

“Ndiyo! Si mpo wawili! Wewe na huyo hapo,” alisema Gideon huku akicheka.
“Hahah! Hatujambo! Tumekumisi tu!”
“Kweli?”
“Yeah! Hasahasa huyu hapa,” alisema Juliana huku akimuonyeshea mumewe tumbo lake.

Itaendelea.
 
SEHEMU YA 21...

Gideon akamsogelea, akalishika na kisha kuweka sikio lake katika tumbo lile. Lilikuwa dogo, halikuanza kuonekana lakini kwake hakutaka kushindwa, alihitaji kuonyesha mbwembwe zote hata kabla mtoto hajazaliwa.

Kutokana na furaha kubwa aliyokuwa nayo, Gideon akaanza kuwaambia marafiki zake wengi kuhusu ujauzito ule, kila alipotembea alijiona kuwa kidume kwani kulikuwa na wanaume wengi ambao hawakuwa na watoto, kwake, alijiona kuwa na nguvu kuliko wote.

Malenzi mema kwa mkewe yakaongezeka, akazidi kumjali, mapenzi yakanoga sana mpaka alipotimiza miezi tisa na hatimaye kwenda kujifungua, akafanikiwa kupata mtoto wa kike waliyempa jina la Jesca.
“Ni mtoto mzuri sana,” alisema rafiki yake huku akimwangalia mtoto huyo.
“Kweli?”

“Yeah! Kachukua kila kitu kutoka kwa mama! Ila hivi vikono hivi ni vya baba pyua,” alisema rafiki huyo na kuanza kucheka.
Hiyo ndiyo ikawa furaha yao, ndiyo ikawa mwanzo wa kupendana zaidi na zaidi. Gideon hakuwa akitulia kazini, kila siku alikuwa akirudi nyumbani mapema kabisa, alipofika, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kumbeba mtoto wake, kwake alikuwa kila kitu, alikuwa tayari kupoteza kila alichokuwa nacho lakini si mtoto huyo.

Wakawa karibu zaidi na mtoto wao, walimpenda na kumpa kila kitu alichotakiwa kupewa. Miezi ikakatika, siku zikaenda mbele, waliendelea kumpenda kila siku huku wakiahidi kumfanyia mambo mengi katika maisha yake.

Alipofikisha umri wa miaka miwili, akaanza chekechea katika Shule ya Watoto ya Livingstone Day Care ambayo ilikuwa ikisomwa na watoto wa matajiri tu. Walitaka kumpa elimu bora, hawakupenda kumuona akipokea elimu ya kawaida kwa kuamini kwamba hakukuwa na kitu ambacho kingemkomboa zaidi ya kuwa na elimu tu.

Mtoto alipofikisha miaka minne, wakapanga kupata mtoto mwingine kwa kuwa tayari Jesca alikuwa mkubwa. Wakajadiliana na kukubaliana kwamba kusingekuwa na tatizo lolote lile kama tu wangepata mtoto wa pili.

Itaendelea!
 
SEHEMU YA 22...

Zoezi lao lilichukua miezi mitatu lakini hakukuwa na majibu yoyote yale. Kila mmoja alishangaa, walijitahidi sana, walikuwa vyakula vingi vya kuirutubisha afya zao na vizazi vyao lakini Juliana hakufanikiwa kushika ujauzito.
Walipoona kila kitu kimeshindikana ndipo wakaamua kwenda hospitalini kuona kama kulikuwa na tatizo lolote lile.

Walipofika huko, daktari akawapima na baadaye kuwapa matokeo ambayo yaliwashtua wote wawili.
“Hamtoweza kupata mtoto,” alisema daktari huku akiwaangalia wote wawili.
“Kwa nini?”
“Mkeo ana kansa ya kizazi,” alijibu daktari huyo huku uso wake ukionyesha huzuni kubwa.

Hawakuamini kile walichokisikia, walimwangalia daktari yule, mioyo yao ilichoma kupita kawaida. Juliana akahisi moyo wake ukichoma kuliko kawaida, akayafumba machoo yake na kuanza kulia.
Hakuamini kwamba alikuwa na kansa ya kizazi, daktari akawaambia kwamba haikuwa imekomaa hivyo kulikuwa na nafasi ya kuiwahi kitu kilichowafanya kuanza kuhangaikia tiba.

Walikwenda kila kona, Juliana alitumia dawa za kila aina lakini kitu cha ajabu ni kwamba hakufanikiwa kupona kansa ile ambayo ilikuwa ikiendelea kumtafuna kila siku.
Ugonjwa ukampa mawazo, kila alipokuwa akikaa, mawazo yake yalikuwa katika ugonjwa huo uliokuwa ukimtesa kila siku. Moyo wake ulimuuma mno, hakukuwa na mtu wa kumfariji zaidi ya mume wake mpendwa.

Gideon alihuzunika, kila alipomwangalia mke wake, moyo wake ulimuuma mno. Juliana alimsikitisha, alikuwa akikonda, mawazo yalimtesa na kila wakati aliona kabisa kwamba angekufariki dunia.
Alimuonea huruma mume wake, alikuwa akihangaika mno, kila kulipokuwa na tetesi kwamba dawa ilikuwa ikipatikana, alikwenda huko. Alinunua dawa za kila aina, kwa Wachina, Wakolea na nyingine za asili ilimradi mke wake apone kansa ile lakini haikusaidia kitu.

Alihuzunika, wakati mwingine alipokuwa ofisini, aliufunga mlango na kuanza kulia. Moyo wake ulichoma mno, wakati mwingine alimwambia Mungu kwamba lile jaribu alilompa lilikuwa kubwa mno na asingeweza kulibeba peke yake.
“Mungu! Hili ni jaribu kubwa sana! Nitawezaje kulibeba?” alimuuliza Mungu huku akiwa ofisini kwake.

Itaendelea!
 
SEHEMU YA 23...

Kila alipokuwa alimfikiria mke wake, Juliana. Aliona kabisa hizo ndizo zilikuwa dakika za mwisho kumuona mke wake huyo akiendelea kupumua. Hakuacha kuomba, alisali kwa nguvu zote, aliamini kwamba kuna siku Mungu angetenda muujiza na mke wake kurudi kwenye hali ya kawaida.

“Mke wangu! Una imani kwamba utapona?” aliuliza Gideon huku akimwangalia mke wake.
“Nina imani nitapona, ila….” Alisema Juliana.
“Unaposema ila inaonyesha huna imani! Naomba uwe na imani mke wangu!

Mungu wetu ni mponyaji, kama alimponya mwanamke mwenye baada ya kushika vazi la Yesu Kristo, kama aliwaponya vipovu, kansa ni nini mbele yake? Amini kwamba Mungu ni mponyaji, unachotakiwa ni kuamini kwani mungu hufanya kazi na wanaoamini,” alisema Gideon huku akimwangalia mke wake huyo.

Japokuwa aliambiwa maneno mengi na mume wake kwamba alitakiwa kuamini lakini moyoni mwa Juliana hali ilikuwa tofauti kabisa. Kichwani mwake zikaja picha za watu mbalimbali waliokuwa wakiugua kansa na mwisho wa siku kufariki dunia, hakuona kama angepona, aliamini kwamba mumewe alikuwa akimwambia maneno mengi kama kumtia moyo lakini ukweli ni kwamba asingeweza kupna.

Alilia mchana kutwa, moyo wake uliendelea kulia. Kila alipomwangalia mtoto wake, Jesca moyo wake ulimuuma, alikuwa mtoto mdogo ambaye bado alihitaji malezi kutoka kwake, hakujua angefanyaje kama angekufa, hakujua ni kwa jinsi gani mtoto wake huyo angeumia usiku na mchana.

Miaka ikakatika, hali yake ikazidi kuwa mbaya, ugonjwa ule ulimtesa na mwisho wa siku kuanza kutafuna nywele zake. Zinaanza kunyonyoka, akaanza kubaki na upara kichwani. Alitia huruma, aliumia mno kwani hizo zote zilikuwa ni dalili kwamba asingeweza kupona tena.
“Mke wangu! Amini kwamba Mungu anaweza kukuponya,” aliisikia sauti ya mumewe moyoni mwake.

Itaendelea!
 
SEHEMU YA 24...

Akahisi akipata nguvu kubwa, akaanza kuingiwa na kumbukumbu za watu waliokuwa wakiumwa sana na mwisho wa siku kuponywa. Kama Mungu aliiumba dunia, kama Mungu aliumba binadamu wote duniani, ilikuwaje kuhusu ugonjwa wa kansa, angeshindwa vipi kumponya mtu aliyekuwa na ugonjwa huo?

“Mungu naomba uniponye,” alisema Juliana huku akiwa amepiga magoti.
Alimuomba Mungu kila siku, alimuamini kwamba kuna siku angemponya tena lakini hilo lilionekana kuwa gumu kutokea. Mwili wake ulizidi kudhoofika, kansa iliendelea kusambaa na mbaya zaidi wakati mwingine alikuwa akitoka damu nyingi sehemu za siri kama mwanamke aliyeingia kwenye simu zake.

Hilo ndilo lililomtesa zaidi, likamfanya kukaa ndani, akajifungia, hakutaka kutoka kwani muda wowote ule damu zilikuwa zikimtoka sehemu za siri. Huo ndiyo ulikuwa msiba mkubwa, aliomboleza kila siku, wakati hali ikiwa imekuwa hivyo, wakati ambao alikuwa akihitaji sana msaada na faraja kutoka kwa mume wake, hapo ndipo Gideon akaanza kubadilika.

Hakuwa karibu naye kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma, alichelewa kurudi nyumbani kitu kilichomfanya kuwa na maswali mengi juu ya kitu kilichokuwa kikiendelea kwa mumewe.
Alitamani sana kuzungumza naye lakini mwanaume huyo hakuwa na muda. Moyo wa Juliana ulimchoma, japokuwa alikuwa na maumivu makali katika mwili wake lakini kufanyiwa vitu kama hivyo na mwanaume aliyempenda kwa moyo wa dhati kwake ilikuwa ni zaidi ya maumivu.


Alilia, hakuna aliyemfuta machozi, alihuzunika, hakukuwa na wa kumfariji. Wakati mwingine aliisikia sauti moyoni mwake ikimwambia kwamba aachane na mumewe kwa kuwa alikuwa amepata mwanamke mwingine lakini Juliana hakutaka kukubaliana na hilo.
“Gideon! Hapana! Hawezi kuwa na mwanamke mwingine,” aliibishia sauti aliyokuwa akiisikia moyoni mwake.

“Aya! Utakapoletewa mwanamke ndani ya nyumba ndipo utakapoamini kwamba amepata mwanamke mwingine, tena mzuri zaidi yako, na ana afya nzuri sio kama wewe goigoi ambaye muda wowote ule unakufa,” aliisikia sauti hiyo maneno ambayo yaliuchoma moyo wake vilivyo.

Itaendelea!
 
SEHEMU YA 25...

Kansa iliendelea kumtesa Juliana, hakuwa na furaha, muda wote alikuwa akilia, alimuomba Mungu kumponya kansa ile au kubadilisha kila kitu na mwisho wa siku kugundua kwamba kila kilichoendelea kilikuwa ndoto.

Alimpenda sana mume wake, Gideon lakini kwa kipindi hicho mwanaume huyo alikuwa bize na mambo yake, upendo uliondoka, akawa anachelewa kurudi nyumbani, hakutaka kabisa kuona akiendelea kuwa na mwanamke mgonjwa kama alivyokuwa Juliana.

Moyo wa mwanamke huyo ulimuuma kupita kawaida. Bado aliendelea kutoka damu sehemu za siri, aliumia, alihitaji msaada kutoka kwa mume wake lakini mwanaume huyo hakuwa na muda naye.
Wakati mwingine akawa anampigia simu, hakuwa akipokea na hata alipomtumia ujumbe kwenye simu yake mwanaume huyo hakuwa anajibu kitu kilichomfanya kujisikia vibaya mno.

Wakati Juliana akiteseka kitandani, Gideon alikuwa kwenye penzi la mwanamke mwingine aliyeitwa Juliet. Lilikuwa penzi jipya, penzi lililochipukia kwa kasi kubwa, penzi ambalo lilimfanya kuanza kumsahau mke wake.

Alihitaji faraja, alihitaji kulala na mwanamke, mkewe hakuwa akiweza kufanya kitu chochote kile, alionekana kama sanamu hivyo kwa hali aliyokuwa akipitia ilikuwa ni lazima kutafuta mwanamke mpya ambaye angeufanya moyo wake kuwa na furaha muda wote.
Akawa akitoka na Juliet kwenda sehemu mbalimbali, alikuwa na pesa, alitumia pesa zake kumfurahisha msichana huyo pasipo kumkumbuka mwanamke ambaye alichuma naye.

Kila alipokuwa na Juliet, Juliana alikuwa akipiga simu, aliichukua simu yake na kuangalia, alipoona jina la mke wake, alicheka sana na kumuonyeshea Juliet ambaye alimwambia amsahau mwanamke huyo kwani hakuwa chochote kile.
“Achana naye!” alisema Juliet.
“Ndiyo ninachofanya. Unajua namchukia sana yule mwanamke,” alisema Gideon huku akionekana kuwa na hasira.
“Jamani! Basi tukampoteze,” alishauri Juliet.

“Tumpotezaje?”
“Tumuue!”
“Sawa. Ngoja nikafanye mipango, mwanamke yule hatakiwi kuishi. Kwanza pale alipokuwa tayari maiti,” alisema Gideon.

Itaendelea.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom