RAIS Jakaya Kikwete amefanikiwa kuzima uasi uliotaka kufanywa na wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM), waliopanga kukwamisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Katiba ya mwaka 2011.
Baada ya kushindwa kukutana wabunge wote wa chama hicho, Kamati ya Uongozi ya Bunge imeteua wawakilishi watano kutoka miongoni mwa wabunge wake ambao wameunda kamati maalumu ya kukutana na Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa CCM.
Kilichoibua mawazo ya uasi miongoni mwa wabunge wa CCM kinatokana na hatua ya serikali kuamua kuwasilisha mabadiliko katika sheria hiyo siku chache baada ya Rais Kikwete kukutana kwa nyakati tofauti na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na wadau mbalimbali Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais Kikwete aliwasili Dodoma jana akitokea mkoani Mwanza alikokwenda kwa ajili ya kilele cha maadhimisho ya miaka 35 ya kuzaliwa kwa CCM, kisha akaanza kukutana na wawakilishi watano wa wabunge wa chama hicho.
Awali, Rais Kikwete alipanga kukutana na wabunge wote wa CCM, alilazimika kukutana na wawakilishi watano wa chama hicho kutokana na msimamo wa wabunge hao kukataa kuonana naye kwa madai kuwa hawana cha kujadiliana naye.
Mbali ya kukutana na wawakilishi wa wabunge hao mjini Dodoma, Rais Kikwete alibadili upepo wa kisiasa katika viunga vya Bunge kwa hotuba yake aliyoitoa juzi mjini Mwanza kwamba katika marekebisho hayo, CCM nayo ilileta mapendekezo ya marekebisho manane ya sheria hiyo.
Hata hivyo, uchunguzi wa gazeti hili ulibaini kuwa wakati kuna wabunge bado wameshikilia msimamo wa kuukwamisha muswada huo, lakini pia wapo wanaokubaliana na Rais Kikwete.
Habari ambazo gazeti hili imezipata kutoka ndani ya kikao hicho cha rais na wabunge hao zilisema kuwa rais alifafanua kwa kina sababu ya kukubadili marekebisho aliyopokea kutoka kwa ujumbe wa CHADEMA na ule wa vyama vingine kutokana na uzito wa jambo lenyewe.
Habari zinasema kuwa Rais Kikwete mbali ya kuwalainisha wabunge kuhusiana na muswada huo, pia aliweka wazi msimamo wake wa kuwataka wawakilishi hao wa wananchi kuachana na suala la posho kwa sasa kwani linawajengea taswira mbaya.
Ujumbe huo wa wabunge, ulitarajiwa kukutana na wabunge wote jana baada ya kikao chake na rais ili kuwajulisha yaliyojiri katika mazungumzo yao na kama kuna haja ya kukutana nao wote kwa pamoja kabla ya muswada huo kuwasilishwa bungeni.
Awali muswada huo wa marekebisho ya sheria ya Katiba ya mwaka 2011, ulitarajiwa kuwasilishwa bungeni jana, lakini haukuwamo katika orodha ya shughuli za Bunge jana.
Akizungumza wakati wa kuahirisha kikao cha Bunge jana, Naibu Spika, Job Ndugai, aliwataka wabunge wa CCM kuwasha simu zao muda wote kwani Mwenyekiti wao, Jenister Mhagama (Peramiho), angewapigia simu wakati wowote kwa ajili ya kikao.
Wiki iliyopita, upepo wa kisiasa kwa wabunge wa CCM ulibadilika na kusababisha kutoa kauli nzito ndani ya vikao vya ndani, wakimlaumu Rais Kikwete kwa kile walichokiita kuwageuka.
Mambo ambayo yamewakera wabunge wa CCM katika siku za hivi karibuni ni pamoja na hatua ya Rais Kikwete kukana kubariki posho mpya za wabunge wakati Waziri Mkuu Pinda na Spika Makinda, tayari walishautangazia umma kwamba rais amebariki posho hizo.
Jingine ni la marekebisho ya sheria ya Katiba ya mwaka 2011, iliyofanyiwa marekebisho baada ya Rais Kikwete kukutana na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Wakati serikali iko mbioni kuwasilisha bungeni marekebisho ya sheria ya Katiba ya mwaka 2011, kama ambavyo Rais Kikwete amekubaliana na viongozi wa CHADEMA, wabunge wa CCM, walipitisha azimo la kukataa marekebisho hayo
SOURCE:TANZANIA DAIMA