Jeshi la Polisi latoa somo kwa Madereva wa Malori Mkoani Mbeya

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,812
11,987
Kuelekea mwisho wa mwaka 2023, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kupitia kikosi cha usalama barabarani limewataka madereva wa malori kuwa na udereva wa kujihami ili kuepuka ajali zinazoweza kuepukika.

Akizungumza Desemba 11, 2023 katika eneo la maegesho ya malori Jijini Mbeya, Mkuu wa Kikosi cha usalama barabarani Mkoa wa Mbeya, Mrakibu wa Polisi Hussein Gawile amewataka madereva hao kuzingatia sheria za usalama barabarani sambamba na kuwa na udereva wa kujihami ili kuepuka ajali.

Aidha, Mrakibu wa Polisi Gawile amesisitiza suala la ukaguzi wa gari kwa kila dereva kabla ya kuanza safari ili kuweza kujua mapungufu na changamoto zilizopo katika chombo chake.

Naye, Mwenyekiti wa Mabalozi wa Usalama barabarani Mkoa wa Mbeya (RSA) ndugu Furaha Malele ametoa wito kwa madereva kuzingatia sheria, alama na michoro ya usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazoweza kuepukika.

Sambamba na hilo, ndugu Malele amesema kuwa, wataendelea kutoa elimu kwa wananchi, madereva na pia kuendelea kushauri mamlaka husika katika kurekebisha sheria, kuweka alama za usalama barabarani katika maeneo yanayohitaji kuwa na alama pamoja na kutoa taarifa za madereva wasiofuata na kutii sheria za usalama barabarani.
 
Back
Top Bottom