Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 2,813
- 11,991
Akizungumza Disemba 23, 2023 mara baada ya kuendesha zoezi la ukaguzi wa mabasi ya abiria Stendi Kuu ya Mabasi Jijini Mbeya, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mrakibu wa Polisi, Hussein Gawile amewataka madereva kujenga utamaduni wa kufanya ukaguzi wa vyombo vyao vya moto kabla ya kuanza safari.
Aidha, Mrakibu wa Polisi Gawile amesema kuwa, licha ya kufanya ukaguzi wa mabasi ya abiria pia wameendesha zoezi la kuwapima ulevi madereva wa mabasi ya abiria kwa kutumia kifaa maalum kabla ya kuanza safari zao ili kujiridhisha kama hawajatumia kilevi au la.
"Nipo na kikosi kazi cha wakaguzi wa magari wa Jeshi la Polisi pamoja na wataalam ambao watawapima madereva ulevi kabla ya kuanza safari ili kuangalia kama wapo vizuri kiafya ndipo waanze safari," alisema Mrakibu wa Polisi Hussein Gawile.
Sambamba na hilo, abiria wanaofanya safari zao kwenda maeneo mbalimbali, wamehimizwa kupaza sauti kukemea vitendo vya ukiukwaji wa Sheria za Usalama Barabarani kupitia Kampeni ya "Abiria Paza Sauti" (APS) inayoendeshwa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Mabalozi wa Usalama barabarani (RSA).