JamiiTalks
JF Advocacy Team
- Aug 7, 2018
- 625
- 938
Sheria ya Utwaaji wa Ardhi ( Land Acquisition Act Cap. 118 R.E. 2002 katika kifungu chake cha 3 imempa nguvu na madaraka Rais ya kuchukua ardhi inayomilikiwa na mtu binafsi kwa ajili ya manufaa ya umma.
Rais anaweza kufanya hivi endapo tu ataona au watu wanataka ardhi hiyo kwa ajili ya manufaa ya umma kwa ujumla.
Lakini pia sheria hii imetoa ulinzi kwa watu ambao ardhi zao zitachukuliwa kwa manufaa ya umma.
Ulinzi huo ni kama ifuatavyo:
1. Lazima wapewe Taarifa ya awali (Notice) ya lengo la kuchukua ardhi yao. Kifungu cha 6 cha sheria hii inataka Waziri anayehusika na mambo ya ardhi atoe taarifa ya lengo la kuchukua ardhi kwa mtu anayemiliki ardhi hiyo. Na taarifa hiyo kutoka kwa Waziri inatakiwa itolewe si chini ya muda wa wiki 6 kabla ya kuanza mchakato wa kuchukua ardhi hiyo.
2. Lazima Fidia itolewe kwa wale wote ambao ardhi yao imechukuliwa. Kifungu cha 11 cha sheria hii inataka watu wote waliochukuliwa ardhi zao kwa lengo la manufaa ya umma wapewe Fidia juu ya ardhi yao.
Na tathimini ya Fidia itafanywa na Waziri husika au Mahakama, na kiwango cha Fidia itakuwa sawa kama ambavyo ilikuwa thamani ya ardhi husika wakati inachukuliwa na pia usumbufu alioupata mtu ambaye ardhi yake imechukuliwa.
Ingawa sheria hii haijampa mtu haki ya kujipigia tathimini juu ya Fidia anayotaka kulipwa lakini kifungu cha 13 kinampa mtu haki ya kwenda mahakamani kupinga kiwango cha Fidia atakacholipwa kama hajaridhika nacho.
Hivyo, ulinzi huu aliopewa mmiliki wa ardhi ni wa kuzingatiwa, endapo hajapatiwa kimoja wapo kati ya hivi au vyote basi uchukuaji huo wa ardhi utakuwa batili na mtu anaweza kwenda mahakamani kushitaki ili mahakama izuie zoezi hilo la uchukuaji wa ardhi au kurejesha ardhi hiyo kama tayari ilishachukuliwa.