Kuwa na uwezo peke yake haitoshi kumfanya mtu apate kazi mahali fulani. Jinsi gani mtu amepata kazi hiyo ndiyo swali la msingi. Kama kwa namna yoyote ile kuna njia za mkato zimetumiwa ni halali watu kuhoji. Binafsi kuona majina ya kina Sumaye, Mkapa n.k hilo halinisumbui mbona tulikuwa na kina Mwamunyange tangu Uhuru na watoto wao nao wanapanda vyeo jeshini?
Hapa US miaka michache iliyopita wakati Collin Powell yuko State Department mtoto wake alikuwa ni mwenyekiti wa FCC.. so tusiangalie majina tu, tuangalie ni jinsi gani watu wamepata nafasi hizo.
Hata hivyo, inajulikana kwa baadhi ya watu jinsi gani watoto wa wakubwa wanapata habari ya nafasi za kazi na ni jinsi gani maombi yao ya kazi yanapatiwa "kipaumbele".
"Mzee A, mwanao K anaendeleaje bwana" anauliza Kibosile M ambaye alikuwa ni Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu.
"Ah, anaendelea vizuri ndio amerudi toka masomoni". anajibu Mheshimiwa Mbunge Utata wa jimbo la Ukata. Mkononi ameshikilia ufunguo wa gari lake la Kibunge, Toyota Prado.
"Hivi alienda kusomea nini" Anauliza tena Waziri wetu huku akiweka gilasi yake ya kinywaji baridi cha Serengeti Lager. Anamuangalia Mbunge akijikalisha vizuri kwenye kiti kile kirefu cha pale Kaunta ya Bwalo la Maafisa wa Jeshi la Polisi Oysterbay. Kwa mbali mawimbi yalikuwa yakisikika yakigonga ukingo wa bwalo hilo maarufu, huku upepo wenye harufu ya chumvi ukipulika kama kwa zamu.
Upande wa pili, kulikuwa na kikundi cha watu kama watatu hivi ambao na wenyewe walikuwa wanapata "mbili tatu". Tetesi zilisema hao walikuwa ni makomandoo wapya wa Tanzania waliorejea hivi karibuni toka Fort Bragg huko Marekani.
Kibosile anakohoa kidogo kusafisha koo, baada ya kupiga fundo moja la kinywaji baridi, "alienda kusomea mambo ya biashara, sasa hivi ana Masters bwana". Anajibu kwa fahari.
"Safi kabisa, sasa ameshaanza kutafuta kibarua bwana?" Anauliza tena Waziri mpendwa.
"hamna lolote yupo yupo tu, ila mheshimiwa kama unaweza kunisaidia nitashukuru, maana hawa vijana kukaa nyumbani tu kunawafanya wawe wavivu" Anajibu Kibosile M.
"Hamna neno, kuna kijana wa Waziri Malimau ya Konde, yuko kule Benki Kuu Human Resources ngoja nicheki halafu nitakupatia habari, nina uhakika wanaweza kupata nafasi ya mtu mmoja" Anasema kwa kujiamini.
"Nashukuru sana mheshimiwa, na wewe yule binti yako aliyekuwa Muhimbili Medicine yuko wapi sasa?" anauliza Kibosile M. Anauliza hivyo ili angalau kuonesha shukrani na uungwana.
"Nani Ndimu? au Bolibo?, maana wote wameenda Udaktari" anajibu kwa fahari.
"Yeah Ndimu" Anajibu Kibosile wetu kwani kwa sababu zake anazozijua hakutaka kulikisikia jina la "Bolibo".
"Ndimu, yeye amemaliza hapa Muhimbili, na sasa hivi ameenda mapumzikoni kwa kaka yake kule Detroit, kwenda kumsaidia wifi yake kidogo amejifungua. Atarudi kama baada ya mwezi hivi" Waziri anajibu huku akimalizia kinywaji chake kwa fundo moja. Wale jamaa watatu "makomandoo walikuwa wanaangalia TV ambapo kulikuwa na habari ya tetemeko la ardhi kule India.
"Vizuri sana Mheshimiwa, itakuwa vizuri tuwakutanishe hawa vijana wetu bwana maana wana urafiki wa zamani sana" Kibosile anasema huku ujumbe ukitumwa kwa Waziri. Waziri aliupata.
"Bila ya shaka, nina hakika watafurahi kupata muda kukumbushana vituko vyao pale Shaaban Roberts" anajibu, na wote wawili wanaangua kicheko.
Baada ya porojo za hapa na pale, wanaagana. Waziri anajiondokea taratibu hapo Bwaloni wakati Kibosile M, aliyekuwa amevaa bukta na tsheti nyeupe anachukua vifaa vyake na kwenda kwenye chumba cha kucheza squash. Moyoni amefurahi kwani kabla ya kuagana Waziri alimwambia ampatie kijana wake namba yake na kijana huyo ampigie simu kesho yake jioni.
* * *
Miezi michache baadaye, kijana wa Kibosile alikuwa ni Meneja Msaidizi wa Kitengo cha Ukaguzi katika Idara moja nyeti serikalini. Alishangaa kujikuta anakutana na watoto wa "wakubwa" wengine kwenye ofisi hiyo. Hakuna anayemuuliza mwenzie "umefikaje hapa". Miezi sita baadaye Uchumba ulitangazwa kati ya Mtoto wa Kibosile M na binti ya Waziri Ukata.
Mahali iliyotolewa ni Shilingi milioni 20 na ng'ombe wawili, mashuka, mablanketi na mbuzi mmoja.
MWISHO