Nov 26, 2023 02:26 UTC
Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesema, utawala wa Kizayuni umelazimika kukubali usitishaji vita baada ya kushindwa kumkomboa hata mateka wake mmoja kupitia mashambulio ya ardhini dhidi ya Ukanda wa Gaza.
Usitishaji vita wa siku nne kati ya utawala wa Kizayuni na Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS katika Ukanda wa Gaza ulianza kutekelezwa juzi Ijumaa saa moja asubuhi kwa wakati wa eneo hilo.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Lebanon, Sheikh Naim Qassem, Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah amesisitiza kuwa "baada ya siku 49, imeamuliwa kwamba usitishaji vita wa muda uliofikiwa unaweza kurefushwa. Israel haikutaka kusitisha vita, bali imelazimika kuukubali kwa sababu utawala huo wa Kizayuni ulikuwa umepiga upatu wa kuwakomboa mateka wake kwa kufanya mashambulio ya ardhini, lakini baadaye ikabainika kuwa haukuweza kukomboa hata mateka mmoja kupitia mashambulio yake hayo.
Sheikh Naim Qassem
Sheikh Qassem amebainisha kuwa, mmoja wa viongozi wa Hamas ametueleza kwamba, katika muda wote huu, miundomsingi ya Muqawama ya chini ya ardhi haijaharibiwa hata kidogo na baada ya kumalizika usitishaji vita, ikiwa adui atarudi, na sisi tutarudi na wataona harakati za kuwashangaza ambazo hawajawahi kuziona maisha mwao.
Sheikh Naim Qassem amesisitiza kwa kusema, "sisi tunapigana vita vya haki dhidi ya batili kupitia Muqawama; vita vya ukombozi wa ardhi kutoka kwa wavamizi na maghasibu na vita vya kuirejesha Quds. Vita hivi haviwahusu Wapalestina peke yao, bali ni vita vya usalama wa kiutamaduni, kijamii, kimaadili na kisiasa".
Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesema, Kimbunga cha Al-Aqsa ni operesheni kubwa na ni mradi unaoonyesha imani iliyopo juu ya Muqawama na akaongeza kuwa operesheni hiyo ni mafanikio ya kihistoria ambayo yatabaki kuwa ya kudumu.
Kimbunga cha Al-Aqsa ni ushindi ambao umesajiliwa juu ya ardhi ya Palestina na nyoyo za Wapalestina; na kushindwa kwa Wazayuni pia kumesajiliwa juu ya nyoyo zao; na matokeo ya vita hivyo yatabainika katika siku au miaka ijayo.