WATANZANIA leo wanaadhimisha miaka 45 ya Uhuru wa Jamhuri ya Tanganyika (Tanzania Bara).
Miaka 45 si haba. Ni umri wa mtu mzima, tena mwenye wajukuu. Waliozaliwa Desemba 9, 1961, wako kwenye utu uzima.
Uhuru ni kitu muhimu katika maisha ya kiumbe chochote kilicho hai. Kama wanyama wanafurahia uhuru, seuze binadamu?
Kwa vyovyote iwavyo, leo ni siku muhimu katika historia ya nchi yetu. Ndiyo siku ambayo wakoloni wa Kiingereza walifunga virago na kurejea kwao.
Waliondoka baada ya kupora utajiri wetu mwingi. Walituonea kwa mengi. Wakatuletea dini zao na kuua dini zetu, waliua utamaduni wetu, wakatufanya kila jambo letu tulione kuwa ni la kishenzi. Athari za ukoloni, zipo hadi leo hii.
Miaka 45 baada ya uhuru, tujiulize maswali. Je, Tanzania na Watanzania tuko huru? Je, malengo ya kujitawala tumeyafikia? Je, tumelifanyia nini taifa letu?
Baada ya kuuondoa ukoloni mkongwe, sasa Tanzania na mataifa mengine ya dunia ya tatu, inakabiliwa na ukoloni mpya. Utandawazi ni ukoloni mpya. Utandawazi umeshaiathiri mno Tanzania. Utandawazi ni mbinu mpya ya mataifa ya kibeberu, kuendelea kuitawala dunia.
Wazee wetu walidai uhuru na hatimaye kuupata ili lijengwe taifa la watu huru. Lakini kwa bahati mbaya, Watanzania wengi hawajawa huru. Bado kuna uonevu ndani ya jamii yetu, kuna sheria zinazozuia uhuru wa Watanzania, na kuna mengi yaliyorithiwa kwa wakoloni, ambayo kwa kweli miaka 45 baadaye, hatukupaswa kuendelea nayo.
Lakini lililo kubwa ni je, Watanzania wamelifanyia nini taifa lao? Tunaona kuwa miaka 45 baada ya uhuru, moyo wa Watanzania kujituma, kufanya kazi kwa bidii ili kulijenga taifa lao, umekuwa ukipungua siku hadi siku.
Katika miaka ya 1960 hadi mwanzoni mwa miaka ya 1980, Watanzania walikuwa hodari katika kulijenga taifa lao. Walikuwa tayari kulitumikia taifa lao katika nyanja mbalimbali, na kwa kweli maendeleo yalionekana.
Hali ni tofauti sasa. Ubinafsi umewatawala wananchi wengi. Mashirika ya umma yamefilisiwa, mali zimeibwa, utajiri wa nchi umeangukia mikononi mwa wachache, hakuna anayejali tena kulinda mazingira au kuwa na uchungu na nchi yake.
Mambo yamekwenda mrama kiasi kwamba sasa baadhi ya watu wanachowaza ni kugawana nchi.
Watanzania wamekuwa hodari sana wa kuwashutumu viongozi. Wanataka wafanyiwe kila kitu. Wanataka wabebwe kila mahali. Wanataka wahudumiwe hata kwa yale wanayoweza kujihudumia. Hawajitumi, na hawaonyeshi dalili ya kubadilika.
Kila uchao, lawama ni kwa viongozi. Sawa viongozi ndio waliopewa dhamana ya kuongoza, lakini wanaochagua viongozi hao ni kina nani? Je, viongozi tulionao wanaingia madarakani kwa mapinduzi? Kwa udikteta? Au ni kwa kupitia sanduku la kura.
Kama wanatokana na masanduku ya kura, nani wa kulaumiwa? Ni wanaopigiwa kura au ni wale wanaopiga kura?
Wakati tukisherehekea sherehe hizi kubwa na muhimu kwa taifa letu, Watanzania tunapaswa kubadilika. Tutambue kuwa bila kulitumikia taifa letu, kamwe hatutaendelea.
Marekani, Ulaya au Asia inayoonekana leo, haikujengwa kwa kusubiri viongozi wafanye hili au lile. Wananchi, kwa kuongozwa na viongozi shupavu, walisimama kidete kuhakikisha wanajenga nchi zao.
Hali ni tofauti na sisi ambao kila kitu tunataka serikali itufanyie. Kwa kuendekeza tabia hii ya ajabu, uhuru wetu utakuwa hauna maana, kwani hatukujikomboa kutoka kwa wakoloni, ili mzigo wa maendeleo tuwaachie viongozi.
Tunapaswa tukumbuke maneno ya busara ya Uhuru na Kazi. Tusibweteke. Tanzania inapaswa ijengwe na Watanzania. Kuwashutumu viongozi, sawa; lakini wananchi nasi tujiulize, tumeifanyia nini Tanzania kwa miaka 45?
Freemedia