TANZANIA TUNAYOITAKA IPO
Kama kweli tunataka Tanzania imara huko tuendako naamini ipo Tanzania hiyo na inatusubiri kwa hamu kwa sababu Mungu ni mwema kwa watu wote. Ni sisi kuamua kwa pamoja.
Je,kuna Mtanzania leo hataki Tanzania yenye elimu bora?,kilimo bora?, barabara safi?, maji safi na salama?,huduma bora za afya?, na miundombinu iliyo imara?
Bila shaka kila mtanzania anataka kuliona Taifa linakuwa kwa nguvu kubwa kiuchumi huku masuala ya umasikini yakipungua kwa kasi kubwa sana. Je,tuko tayari kuitengeneza Tanzania kwa pamoja?, au wengine ni kupiga kelele wakati huo tumejiweka pembeni?.
Tuko tayari kukabiliana na changamoto zinazotukabili leo ili kuitengeneza nchi yetu kuwa imara?. Kama tuko tayari lazima tuanze kupanua bongo zetu na si kupanua midomo yetu tu. Juhudi,maarifa na ujasiri ndiyo siraha ya kuleta maendeleo.
Changamoto yetu ya kuitengeneza Tanzania tunayoitaka si kukosa mawazo ya kuifanya nchi yetu kuwa imara. Changamoto tuliyo nayo ni kukosa uwajibikaji imara uliyo na sura ya kitaifa ili kukabiliana na umasikini wa watanzania.
Changamoto yetu ya kuitengeneza Tanzania tunayoitaka si kutokuwa na ardhi yenye rutuba. Changamoto tuliyo nayo ni kupuuza kilimo na kuwapuuza wakulima wetu vijijini huku tukihubiri mijini asilimia kubwa ya watanzania wanategemea kilimo na kuja na maneno tu bila kudhamiria kuwasaidia wakulima.
Changamoto yetu ya kuitengeneza Tanzania tunayoitaka si kukosa wanasiasa wa rika mbalimbali. Changamoto tuliyo nayo ni kuwa na wanasiasa wanaosimama kuwawakilisha wananchi wakati huo huo wanaonyesha kama wanajiwakilisha wao na familia zao. Pili,kuwa na wanasiasa wanaowaza kujilimbikizia mali kwa kutumia ofisi za umma.
Changamoto yetu ya kuitengeneza Tanzania tunayoitaka si kukosa njia ya kuifanya elimu yetu iwe imara na ya ushindani. Changamoto tuliyo nayo ni kuwa na viongozi wanaopeleka watoto wao kusoma nje na kusomesha watoto wao kwenye shule bora hapa nchini na kujifanya kuzipenda na kuzisifia shule za umma. Pili,changamoto yetu kubwa ni kuwapuuza walimu wetu wanaojitolea kwa nguvu na akili nyingi kila siku.
Changamoto yetu ya kuitengeneza Tanzania tunayoitaka si kukosa njia ya kutengeneza reli yetu iwe imara na ya kuleta matumaini kwa masikini. Changamoto tuliyo nayo ni kuwa na viongozi wenye ama ubia na makampuni makubwa ya malori,ama kupata chochote au baadhi kumliki kabisa na kutokuwa na moyo dhabiti wa kukabiliana na changamoto hii.
Changamoto yetu ya kuitengeneza Tanzania tunayoitaka si kukosa njia za kupunguza umasikini. Changamoto tuliyo nayo leo ni kutoumizwa na hali ya Taifa letu na kujaa ubinafsi wa kijinga kabisa. Pili,kuwa na akili finyu kuwa wawekezaji ndiyo watapunguza umasikini wetu.
Changamoto yetu ya kuitengeneza Tanzania tunayoitaka si kushindwa kupambana na rushwa. Changamoto tuliyo nayo leo ni kupinga rushwa na wakati na sisi tunaitekeleza ipasavyo yaani tunatoa na kupokea rushwa.
Changamoto yetu ya kuitengeneza Tanzania tunayoitaka si kutokuwa na wanasayansi. Changamoto tuliyo nayo leo ni kutowasaidia watu wenye upeo wa juu kisayansi na kutegemea sayansi za kigeni. Pili,kuwakamata na ama kuwafunga wale wanaovumbua sayansi. Tatu,kukosa walimu wa sayansi kuanzia elimu ya awali,na hata wakiwepo uwezo wao wa kuwafundisha vijana wetu kuwa mdogo.
Changamoto yetu ya kuitengeneza Tanzania tunayoitaka si kukosa vijana wenye maadili mema. Changamoto tuliyo nayo leo ni kutowasaidia au kulegeza kamba ya kuwasaidia vijana wanaokosa maadili mema kuanzia ngazi ya kifamilia pamoja na taasisi zetu kama mashuleni.
Changamoto yetu ya kuitengeneza Tanzania tunayoitaka si kushindwa kupambana na wanaouza na kutumia madawa ya kulevya. Changamoto tuliyo nayo leo ni kupinga biashara na utumiaji wa madawa ya kulevya wakati wanaofanya biashara hiyo ni watu wetu wa karibu na sisi tunanufaika na biashara hiyo haramu kabisa.
Changamoto yetu ya kuitengeneza Tanzania tunayoitaka si kushindwa kuwa na wahitimu bora na walioiva kimafunzo,changamoto kubwa ni kuwa na na wahitimu wanaotegemea kuajiliwa tu kwa sababu ya mitaala ya elimu yetu. Pili, kuwa na vyuo vingi vinavyotegemea wahisani ndipo vifanye Tafiti za kijamii.
Changamoto yetu ya kuitengeneza Tanzania tunayoitaka si kushindwa kukabiliana na kundi la vijana lisilokuwa na ajira,changamoto kubwa ni kutokuwa na taasisi za kutosha,viwanda na kupuuza kilimo.
Mwisho
Kama kweli tunataka kuwa na Taifa imara lazima tuache kucheza na na sekta za elimu, kilimo pamoja na nishati na madini. Taifa likipuuza elimu haliwezi kujiamlia mambo yake leo na kesho, lazima tusimame na tuitetee elimu yetu. Elimu ikiwa imara itatusaidia kuwa na uelewa mpana kwenye sekta zingine zote.
Lazima tuwe na dira nzuri,tuijue historia yetu vizuri na tuwajibike kwa pamoja. Kelele nyingi haziwezi kututoa hapa tulipo. Tanzania imara inatusubiri,ili kuiona lazima tujitoe kweli kweli na tukumbuke kuwa tukiwa tunajitoa tujue wazi kuwa maendeleo yetu yatapatikana tu tukiwa na juhudi, maarifa na ujasiri