Hatua ya Kusitishwa kwa JamiiForums: Uchambuzi wa Kisheria na Haki za Wananchi

Hatua ya Kusitishwa kwa JamiiForums: Uchambuzi wa Kisheria na Haki za Wananchi

Abdul Said Naumanga

JF-Expert Member
Joined
Jan 28, 2024
Posts
745
Reaction score
1,470
Disclaimer:
Uzi huu umeandaliwa kwa madhumuni ya kutoa elimu na kuibua mjadala wa kitaalamu na kiraia kuhusu uamuzi wa TCRA dhidi ya JamiiForums. Yalichopishwa hapa hayapaswi kutafsiriwa kama ushauri rasmi wa kisheria, bali ni uchambuzi wa kisheria na kikatiba kwa lengo la kuelimisha na kujadili kwa pamoja masuala yanayogusa haki, wajibu na utawala wa sheria.

Habarini wanajamvi,

Nikiwa kama mmoja wa wanachama wa JF ambao hatujaridhishwa kabisa na uamuzi wa TCRA kulifungua jukwaa hili pendwa haswa kwa intelligent, smart and reasonable people, naona wazi haki yangu na mmeber wenzangu ya kutoa maoni ikibagazwa waziwazi. Sisemi JF wapo sahihi wala sisemi Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) wapo sahihi, ninachojaribu kusema ni kwamba haya mambo yanayogusa haki za watu moja kwa moja yanatakiwa kuangaliwa kwa jicho pana kuliko walilolitumia TCRA.

Kwa kuwa suala hili ni refu na linagusa sheria na katiba, nitaligawa katika sehemu nne: sehemu ya kwanza hii itaeleza msingi wa kisheria wa TCRA, sehemu ya pili madai yao dhidi ya JF, sehemu ya tatu mapungufu ya kisheria na taratibu, na ya nne itakuwa mapendekezo ya nini JF na sisi wananchi tunaweza kufanya.

Okay, nadhani wote tumeshuhudia siku za hivi karibuni TCRA ikitoa uamuzi wa kusimamisha leseni ya maudhui mtandaoni ya JF (Vapper Tech Ltd) kwa muda wa siku tisini. Uamuzi huu umeibua mjadala mkubwa miongoni mwa wananchi na wadau wa habari kuhusu uhalali wake, taratibu zilizofuatwa, na athari zake kwa haki za kikatiba za uhuru wa kujieleza na kupata habari. Ila kabla ya yote ni muhimu kwanza kufahamu msingi wa kisheria wa mamlaka ya TCRA, taratibu zinazopaswa kufuatwa, na hatimaye kutathmini hoja za TCRA dhidi ya JF.​
IMG_6502.jpeg

Kiufupi Mamlaka ya TCRA kufanya walichoifanyia JF yametokana kwa mujibu wa sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Post, yaani Electronic and Postal Communications Act, Cap.306. Sheria hii inawapa nguvu ya kusimamia sekta ya mawasiliano na hasa kutoa na kusimamia leseni za huduma za maudhui mtandaoni. Kwa mujibu wa kifungu cha 103 cha sheria hiyo, Waziri wa Mawasiliano anayo mamlaka ya kutunga kanuni ndogo (subsidiary legislation) za kusimamia maudhui. Ndipo ilipozaliwa Electronic and Postal Communications (Online Content) Regulations, 2020 (GN No. 538/2020) na marekebisho yake ya mwaka 2022 (GN No. 136/2022) pamoja na ya mwaka 2025 (GN No. 57/2025). Kanuni hizi ndizo zilizobainisha majukumu ya “online content service providers” kama JF, “internet service providers” na hata wamiliki wa mitandao ya kijamii.

Pia kwa mujibu wa Kanuni ya 8(1) ya kanuni za 2020, TCRA inaweza kusimamisha au kufuta leseni iwapo masharti yaliyotolewa kwaajili ya matumizi ya leseni hiyo yatakiukwa. Pia Kifungu cha 22 cha sheria ya Mawasiliano Cap. 306 TCRA inaweza kufungia ama kusimamisha leseni na hatua hiyo inapaswa kuchukuliwa tu endapo kuna material breach , na TCRA lazima imjulishe mtoa huduma kwa maandishi na kueleza sababu.​

Nitaendelea 🚶🏿🚶🏿🚶🏿
 
SEHEMU YA PILI:
Madai ya TCRA dhidi ya JF

Katika barua yao na taarifa kwa umma, TCRA imetaja misingi miwili mikuu ya kisheria iliyopelekea uamuzi wa kusimamisha leseni ya JF.

Kwanza, TCRA imedai kuwa JF imekiuka Kanuni ya 9(a) ya Kanuni za Maudhui Mtandaoni za mwaka 2020 (kama zilivyorekebishwa na GN No. 136/2022). Kanuni hii inawataka watoa huduma wa maudhui mtandaoni kuhakikisha wanadhibiti na kusimamia (monitor and moderate) maudhui yanayozalishwa na watumiaji wao (user generated content) ili kuzuia kuchapishwa kwa maudhui yaliyopigwa marufuku (prohibited content). Kwa tafsiri ya TCRA, JF ilipaswa kuzuia kuenea kwa kauli na picha ambazo ziliibua mijadala ya kashfa na kejeli dhidi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano.

Pili, TCRA imejenga hoja chini ya Kanuni ya 12(a)(i), inayowataka watoa huduma wa “Online Content Services – Category A” kuzingatia maadili ya uandishi wa habari na taaluma (journalism ethics and professional requirements as per the Media Services Act). TCRA imeona kwamba mara tu JF ilipoamua kuchapisha au kurudia chapisha kauli za kisiasa zinazohusu masuala ya kitaifa, ilijikuta katika nafasi sawa na chombo cha habari (news outlet kama zilivyo ITV, TBC na zinginezo), na hivyo ilikuwa na wajibu wa kisheria kuhakikisha mizania ya habari kwa kuwasiliana na upande wa pili, kuhakiki vyanzo na kuepuka lugha ya kejeli.

Kwa maelezo ya TCRA, JF ilichapisha maneno ya Humphrey Polepole akimtuhumu Rostam Aziz kununua mgodi mkubwa wa makaa ya mawe kwa shilingi bilioni tano pekee, huku serikali ikiwa haipati mapato halisi kutoka humo. Aidha, JF iliripoti kauli za Polepole akimuhusisha Rais na Bw. Wicknell Chivayo, raia wa Zimbabwe, kwa madai kuwa kuna rekodi za kihalifu za raia huyo.

Kwa maneno mengine TCRA imeona tatizo kuu liko katika mambo mawili: kwanza, JF haikutoa nafasi kwa Rostam, wala msemaji wa Rais au Serikali, kujibu tuhuma hizo, jambo lililokiuka dhana ya balance chini ya Kanuni ya 12(a)(i); na pili, picha zilizochapishwa zikimuonyesha Rais na Bw. Wicknell hazikuthibitishwa uhalisia wake, jambo lililojenga misingi ya kueneza taarifa zisizohakikiwa na hatimaye kusababisha upotoshaji kwa umma uliochangia lugha za matusi na kejeli miongoni mwa wachangiaji.
IMG_6503.jpeg


Nitarejea🚶🏿🚶🏿🚶🏿​
 
SEHEMU YA TATU:
Dosari za Kitaratibu na Kimsingi katika Uamuzi wa TCRA

Uchambuzi wa kisheria unaonyesha kwamba pamoja na TCRA kutumia kanuni ya 9(a) na ya 12(a)(i) kama msingi wa kusimamisha leseni ya JF, bado uamuzi wao unakabiliwa na dosari kubwa za kitaratibu (procedural flaws) na kimsingi (substantive flaws).

Kwanza, tukianzia na kutazama Kanuni ya 21 ya Kanuni za Maudhui Mtandaoni (GN No. 538/2020) inayohusiana na adhabu, imeweka utaratibu mahsusi wa kushughulikia malalamiko ya maudhui. Kanuni hii inaelekeza kwamba malalamiko yanapowasilishwa TCRA, ama TCRA wanapoona kuna ukiukwaji wa kanuni hizo bas TCRA inapaswa kumfikisha mtoa huduma husika mbele ya Content Committee kwa ajili ya kusikilizwa. Utaratibu huu unalenga kuhakikisha kwamba mtoa huduma anapata fair hearing (right to be heard) kama ilivyoelekezwa na Ibara ya 13(6)(a) ya katiba ya Nchi na kuhakikisha kwamba uamuzi unafanywa kwa kuzingatia ushahidi na hoja za pande zote mbili.

Aidha, Kanuni ya 21(2) specifically, inasisitiza kwamba iwapo ukiukwaji wa kanuni hizo umefanywa na mtoa huduma mwenye leseni kama ilivyo Vapper LTD (JF), TCRA inapaswa kumfikisha mbele ya Content Committee ambayo yenyewe ndio yenye mamlaka kisheria ya kusikiliza na kutoa adhabu kwa yeyote aliyevunja kanuni hizo za Maudhui mtandaoni. Kisha, kwa mujibu wa kanuni ya 21(3), baada ya kusikiliza pande zote mbili, Committee hiyo itatoa maamuzi, ambapo inaweza kuchukua hatua kadhaa, zikiwemo: kutoa onyo kwa mtoa huduma; kuamuru mtoa huduma kuomba radhi kwa umma na mhusika aliyeathirika; kuamuru kuondolewa kwa maudhui yanayolalamikiwa; au kutoza faini kwa mujibu wa sheria. Kwa maneno mengine, hatua ya kusimamisha leseni nzima si hatua ya kwanza iliyokusudiwa na kanuni, bali ni hatua ya mwisho kabisa (extreme sanction) ambayo ilipaswa kuzingatia taratibu na ushirikishwaji wa Content Committee.​
IMG_6516.jpeg

Sina uhakika kama TCRA walifata hatua hii, nadhani waliiruka hatua hii na kuchukua hatua moja kwa moja ya “suspension of licence.” Kitendo hiki kinachukuliwa kama mfano wa wazi wa procedural impropriety yani ukiukaji wa taratibu zilizowekwa kisheria ambazo zinahakikisha haki ya kusikilizwa na due process. Kwa lugha ya kisheria tunasema, once a statute prescribes a specific procedure, that procedure must be followed. Failure to do so renders the decision procedurally unlawful.

Pili, katika sakata hili ni wazi kwamba hakuna proportionality kati ya kosa la JF na adhabu iliyotolewa na TCRA. Hata kama tukisema JF walikiuka kanuni ya 9(a) na ya 12(a)(i), bado adhabu ya kusimamisha leseni nzima kwa siku tisini ni nzito mno ukilinganisha na kosa linalodaiwa. Kanuni zenyewe (Kanuni ya. 21(3)) zilitaja hatua ndogo zaidi ambazo zingetosha kurekebisha hali mfano onyo, kuondoa maudhui, au kuomba radhi. Hivyo basi, tunaweza sema TCRA walitumia “hammer to kill a fly,” jambo linalopingana na kanuni ya uwiano (principle of proportionality) inayotaka kila adhabu iwe na uhusiano wa moja kwa moja na uzito wa kosa.

Tatu, kwa mtazamo wa substantive review, uamuzi huu unaweza kuangukia katika kile kinachoitwa Wednesbury unreasonableness dhana ya kisheria inayotokana na kesi ya Associated Provincial Picture Houses v. Wednesbury Corporation (1948). Kwa mujibu wa kipimo hiki, uamuzi wa kiutawala unakuwa unreasonable iwapo hakuna chombo cha utawala chenye akili timamu kingeweza kuufanya katika mazingira yale. Katika suala hili la JF, kitendo cha TCRA kuhesabu kauli za kisiasa na kiuchumi kama “prohibited content,” kisha kuruka hatua za Content Committee na kuchagua kusimamisha jukwaa lote, kinaweza kuonekana kama uamuzi ambao ni so unreasonable that no reasonable authority would ever consider imposing it.

Lakini zaidi ya hapo, uamuzi huu unakinzana pia na misingi ya natural justice, hususan kanuni ya audi alteram partem (the right to be heard). Kwa sababu sina hakika kama JF walipata nafasi ya kusikilizwa ipasavyo na chombo huru (Content Committee), hapa haki yao ya kimsingi ya kujitetea ilivunjwa wazi wazi kinyume na ibara ya 13(6)(a) ya katiba ya Nchi.

Kwa jumla, dosari hizi za kuruka utaratibu wa kisheria (procedural impropriety), kutoa adhabu isiyo na uwiano (disproportionate sanction), na kufanya uamuzi ambao hauwezi kuhesabiwa reasonable (Wednesbury unreasonableness), na kukosekana kwa fair hearing zinatosha kuufanya uamuzi wa TCRA kuwa ultra vires na hivyo kukosa mashiko kisheria.

Nitamalizia 🚶🏿🚶🏿🚶🏿​
 
Back
Top Bottom