SIKU moja baada ya Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), Hamad Masauni Yussuf kuachia ngazi wadhifa huo, baadhi ya vijana wa jimbo la Kikwajuni warejesha kadi za CCM kutokana na kutoridhishwa na suala hilo.
Viongozi wa CCM Jimbo la Kikwajuni jana walikataa kusema lolote kwa madai kuwa wao hawajui kinachoendelea zaidi ya kupata taarifa hizo kwenye magazeti na walipotakiwa kuelezea uamuzi wa Vijana kurejesha kadi walisema "hatujawaona, lakini kwa vijana hilo linawezekana" Alisema Kiongozi Mmoja wa Jimbo hilo ambayer hakutaka kutajwa hata cheo chake.
Baadhi ya viongozi hao walionekana wakisoma gazeti la Mwananchi na kusema kwamba ndio kwanza wamepata gazeti hivyo hawezi kutoa ufafanuzi wowote kuhusiana na suala hilo lakini wanachokijua huo ni uamuzi kutoka ngazi ya juu ya vijana.
"Sasa hivi ndio nilikuwa na gazeti hapa lakini sijawahi hata kulisoma nimenyanganywa kuna vijana wanalisoma huko kwa hivyo hatujajua chochote hadi sasa lakini hata kama ndio amejiuzulu huo uamuzi ni wa vijana sisi kama chama hatujaletewa taarifa zozote zinazomhusu yeye ni mambo yao vijana" alisema Katibu wa jimbo hilo la kikwajuni.
Mbali na suala hilo, pia imebainika kuwa mabadiliko mbali mbali yaliyofanywa na Masauni ikiwemo uhamisho wa mke wa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Shara Saleh Ferouz uliwachukiza baadhi ya vigogo wa CCM Visiwani humo.
Mke wa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar ni Afisa Mwandamizi wa UVCCM Afisi Kuu Visiwani hapa ambaye hata hivyo amerudishwa Afisi Kuu, ingawa si kwa nafasi yake ya awali.
Habari zaidi zilizopatikana jana Mjini hapa zinaeleza kwamba jambo kubwa lililomponza Masauni ni pamoja na kutajwa kwake kuwania Jimbo la Kikwajuni sanjari na hasimu wake, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Saleh Ramadhan Ferouz ambaye ni mtu wa karibu na Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM aliyeachia ngazi, Mohammed Nassor Moyo.
Imeelezwa pia baadhi ya vigogo wa CCM Visiwani wanatajwa kuhusika na vuguvugu la kumwondosha Masauni, ingawa wao walikaa kando wakiwachochea na kuwasukia mkakati ‘vibaraka' wao ndani ya Umoja huo ambao wameathirika na uongozi wa Masauni.
Jana katika maeneo mbalimbali ya Jimbo la Kikwajuni vijana walionekana wakiwa kwenye vikundi vikundi wakitafakari hali iliyotokea ambapo katika Afisi za CCM hali ilikuwa ni tofauti na siku nyengine viongozi walikuwa katika wakati mgumu wa kutoa ufafanuzi.
"Tatizo hapa ni Ubunge Kikwajuni…huyu Masauni anachuana na Ferouz (Saleh Ramadhan Ferouz), lakini hata kama Masauni ameacha Uenyekiti haitofanya mabadiliko yoyote Jimboni" Kilisema chanzo kimoja Jimboni humo.
Katika hatua nyengine, zipo taarifa kwamba Vijana wa Zanzibar wameandaa mapokezi makubwa kwa Mwenyekiti aliyejiuzulu atakapowasili Visiwani hapa akitokea Iringa kwenye mkutano wa Baraza Kuu.
"Huu ni msiba wa Zanzibar nzima kwa kweli ni pigo hawa vijana alikuwa ni hodari kwenye kazi za Chama na nje ya Chama, lakini kwa kila aliyefanya fitina hii Mungu atamlipa" Alisema Kada mmoja wa CCM.
Katika mitaa mbalimbali ya Unguja, wengi walisikika kusikitishwa na hali iliyotokea ndani ya Umoja wa Vijana wa CCM ambapo waliwashambulia wale wanaotajwa kuchochea vurugu katika Umoja huo.
Masauni alikuwa Mwenyekiti wa pili Mzanzibari kukalia kiti cha UVCCM, mtangulizi wake Mzanzibari mwengine ni Muhammed Seif Khatib ambaye kwa wakati mmoja alikuwa Mwenyekiti na Katibu Mkuu.
Taarifa zaidi zilizoenea hapa zinadai kwamba makundi ya wagombea Urais Zanzibar nao wanatajwa huenda wamehusika katika mbinu za kumwondoa Masauni ambaye walimuona kuwa na msimamo usiotabirika kwao.
Source: Zanzibar yetu web blog