Chenge kujiuzulu ni hatua nzuri, tumedai sana hapa kuwa aachie ngazi, lakini bado hata sasa baada ya kujiuzulu bado tuna wasiwasi kuwa huenda hii ikawa ni fursa kwake kuendelea kujitumbulia mabilioni yetu ambayo kwake ni "vijisenti" tu! Inapaswa hatua za kisheria dhidi yake zifuate, lakini sioni matumaini ya hili kutokea wakati waliomtangulia kina Lowassa, Karamagi na Msabaha wanaendelea kutumbua huku wakisifiwa na chama chao kuwa ni "mashujaa" kwa kujiuzulu! La pili ni kuwa huyu fisadi amesubiri hadi kutuhumiwa na SFO ya UK ndipo akachukua hatua ya kujiuzulu. Ikumbukwe kuwa SFO hawakuwa wanachunguza habari za Chenge, wao walikuwa wanafuatilia ufisadi wa kampuni ya BAE iliyouzia Tanzania radar, ndipo wakagundua pia kuwa Chenge alilambishwa mshiko katika dili hilo. Kampuni hiyo ya BAE pia inatuhumiwa kuiuzia serikali ya Saudi Arabia vifaa vya kijeshi vya zaidi ya pound 40bn, ambako madalali fisadi walilamba rushwa ya kueleweka. Tony Blair alipokuwa waziri mkuu alizuia ucunguzi dhidi ya BAE katika dili la Saudi Arabia usifanyike, akitoa sababu feki za kuogopa kukosa ushirikiano wa waarabu hao katika vita ya Iraq, lakini Gordon Brown alipoingia madarakani akaruhusu uchunguzi uendelee, na ndio uliotuwezesha kuyapata haya ya Chenge. Kwa hiyo hii ya Chenge imekuja kama "side effect" ya uchunguzi wa SFO dhidi ya BAE ya UK. Swali ni kuwa sisi tutaendelea kuishi kwa kudandia hadi lini? Yaani system zetu hazina uwezo wa kufichua mafisadi hadi "waibuliwe kwa bahati" kwenye uchunguzi wa wengine? Kumbukeni hata masuala ya kina Balali na EPA huko BoT yaliibuliwa na kampuni ya kigeni ya auditors, Deloitte and Touche (ambayo hata hivyo ilitimuliwa na waziri aliyekuwepo) nakuja kuthibitishwa na kampuni nyingine ya kigeni pia iliyopewa tenda hiyo na CAG. Kwa hiyo kumbe sisi wenyewe hatuna uwezo wa kudhibiti mifumo yetu ya uwajibikaji, ama saratani ya ufisadi imeenea kila mahali, hakuna wa kuaminiwa tena! Labda sasa JK aiombe SFO ya Uingereza ije kumchunguzia serikali yake yote, pengine ataamini ripoti yao kuliko vyombo vyake vya ndani!